Mkutano Mkuu
Sasa Ndiyo Wakati
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


5:57

Sasa Ndiyo Wakati

Sasa ndio wakati tunaoweza kujifunza. Sasa ndio wakati tunaoweza kutubu. Sasa ndio wakati tunaoweza kuwabariki wengine.

Wapendwa akina kaka na dada zangu, mkutano huu umekuwa wa kihistoria katika njia nyingi. Tumebarikiwa kwa sala, jumbe na muziki. Tumefundishwa vyema na watumishi wa Bwana.

Tumepokea maelekezo muhimu kwa ajili ya siku za baadaye. Sala yangu ni kwamba Roho amezungumza nawe moja kwa moja kuhusu mambo ambayo Bwana angetaka wewe ufanye.

Siku za baadaye daima hazitabiriki. Hali ya hewa hubadilika. Hali za kiuchumi hazitabiriki. Majanga ya asili, ajali na magonjwa yanaweza kubadilisha maisha kwa haraka. Matukio haya kwa sehemu kubwa yako nje ya uwezo wetu. Lakini yako mambo tunayoweza kuyadhibiti, ikijumuisha jinsi tunavyoutumia muda wetu kila siku.

Ninapenda shairi hili la Henry Van Dyke, lililowekwa kwenye saa ya machweo ya jua huko Wells College New York. Linasomeka:

Kivuli kwa kidole changu

Huzitenga siku zijazo kutoka zile zilizopita:

Kabla yake, inalala saa ambayo haijazaliwa

Gizani, na mbali na nguvu zako:

Nyuma ya mstari wake usiorudi,

Saa iliyopotea, sio yako tena:

Saa moja pekee iko mikononi mwako,—

SASA ambayo kwayo kivuli kinasimama.1

Ndiyo, tunapaswa kujifunza kutoka kwa yaliyopita na ndiyo, tunapaswa kujitayarisha kwa ajili ya siku za baadaye. Lakini ni sasa pekee tunaweza kufanya hivyo. Sasa ndiyo wakati tunaoweza kujifunza. Sasa ndiyo wakati tunaoweza kutubu. Sasa ndiyo wakati tunaoweza kuwabariki wengine na “kuinyoosha mikono iliyolegea.”2 Kama vile Mormoni alivyomshauri mwanawe Moroni, “Acha tuwafundishe kwa bidii; … kwani tuna kazi ya kufanya [wakati tungali] katika hekalu hili la udongo, kwamba tuweze kumshinda adui wa haki yote, na kupumzisha nafsi zetu katika ufalme wa Mungu.”3

Adui kamwe halali. Daima kutakuwepo na upinzani kwenye ukweli. Ninarudia kusihi kwangu tangu asubuhi ya leo fanya mambo yale ambayo yatakuongezea msukumo chanya wa kiroho, msukumo ule ambao Mzee Dieter F. Uchtdorf aliuzungumzia ambao utakufanya usonge mbele kupita changamoto na fursa zozote zinazokuja.

Msukumo chanya wa kiroho unaongezeka tunapoabudu hekaluni na kukua katika uelewa wetu juu ya upana na kina cha baraka tunazopokea huko. Ninawasihi kukinzana na njia za kiulimwengu kwa kufokasi kwenye baraka za milele za hekaluni. Muda wenu huko huleta baraka kwa milele yote.

Kadiri Kanisa linavyokua, tunajitahidi kupiga hatua kwa kujenga mahekalu zaidi. Mahekalu mapya arobaini na manne kwa sasa yapo kwenye ujenzi. Mengi zaidi yako kwenye marekebisho. Ninaomba kwa ajili ya mafundi wataalamu wanaofanya kazi kwenye miradi hiyo kote ulimwenguni.

Katika roho ya sala na shukrani, ninafurahi kutangaza mipango yetu ya kujenga hekalu jipya katika kila moja ya maeneo yafuatayo: Wellington, New Zealand; Brazzaville, Jamhuri ya Kongo; Barcelona, Hispania; Birmingham, Uingereza; Cusco, Peru; Maceió, Brazili; Santos, Brazili; San Luis Potosí, Mexico; Mexico City Benemérito, Mexico; Tampa, Florida; Knoxville, Tennessee; Cleveland, Ohio; Wichita, Kansas; Austin, Texas; Missoula, Montana; Montpelier, Idaho; na Modesto, California.

Mahekalu haya 17 yatabariki maisha ya watu wengi katika pande zote za pazia. Ninawapenda, kaka zangu na dada zangu wapendwa. La muhimu zaidi, Bwana anawapenda. Yeye ni Mwokozi wenu na Mkombozi wenu. Anaelekeza na kuliongoza Kanisa Lake. Na tuwe watu wenye kumstahili Bwana, ambaye alisema, “Mtakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wenu.”4

Juu ya hili ninaomba katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.