Mkutano Mkuu
Kristo Huponya Kile Kilichovunjika
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


10:39

Kristo Huponya Kile Kilichovunjika

Anaweza kuponya uhusiano na Mungu uliovunjika, uhusiano na wengine uliovunjika, na sehemu zetu sisi wenyewe zilizovunjika.

Miaka michache iliyopita, nikiwa kwenye mkusanyiko wa familia, mpwa wangu William wakati huo akiwa na umri wa miaka minane alimuuliza mwana wetu mkubwa, Briton, kama angependa kucheza mpira naye. Briton alijibu kwa shauku, “Ndiyo ! Ningependa!” Baada ya kuwa wamecheza kwa muda mrefu, mpira ulipigwa na Briton na kwa bahati mbaya akavunja vyungu ya kale vya babu na bibi yake.

Briton alihisi vibaya. Alipoinama na kuanza kuokota vipande vya vyungu vilivyovunjika, William alimsogelea binamu yake na kumpigapiga mgongoni kwa upendo. Kisha akamfariji, “Usijali, Briton. Nilivunja kitu kwenye nyumba ya Bibi na Babu wakati mmoja, na Bibi akanikumbatia na kusema, ‘Ni SAWA, William. Wewe una umri wa miaka mitano tu.’”

Ambayo Briton alijibu, “Lakini, William, mimi nina umri wa miaka 23!

Tunaweza kujifunza mengi kutoka kwenye maandiko kuhusu jinsi Mwokozi wetu, Yesu Kristo, atakavyotusaidia kuendesha kwa mafanikio mambo katika maisha yetu ambayo yamevunjika, bila kujali ya umri wetu. Anaweza kuponya uhusiano na Mungu uliovunjika, uhusiano na wengine uliovunjika, na sehemu zetu sisi wenyewe zilizovunjika.

Uhusiano na Mungu Uliovunjika

Wakati Mwokozi alipokuwa akifundisha hekaluni, mwanamke aliletwa Kwake na waandishi na Mafarisayo. Hatujui hadithi yake kamili, ila tu kwamba alikuwa “aliyefumaniwa katika uzinzi.”1 Mara nyingi, maandiko yanatoa sehemu ndogo tu ya maisha ya mtu, na kwa mujibu wa sehemu hiyo, wakati mwingine tunaelekea kuinua au kulaani. Hakuna maisha ya mtu yanayoweza kueleweka kwa wakati maarufu mmoja tu au kwa kisa cha hadharani cha kujutia. Kusudi la simulizi hizi za kimaandiko ni kutusaidia sisi kuona kwamba Kristo alikuwa ndiye jibu wakati huo, na Yeye ndiye jibu hivi sasa. Anajua hadithi yetu kamili na yale hasa tunayoteseka, na pia uwezo wetu na udhaifu wetu.

Jibu la Kristo kwa binti huyu wa thamani wa Mungu lilikuwa “Wala mimi sikuhukumu: enenda zako; wala usitende dhambi tena.”2 Njia nyingine ya kusema “enenda, wala usitende dhambi tena” inaweza kuwa “nenda ukabadilike.” Mwokozi alikuwa akimualika kutubu, kubadili tabia yake, mahusiano yake, jinsi alivyohisi juu yake yeye mwenyewe, moyo wake.

Kwa sababu ya Yesu Kristo, uamuzi wetu wa “kwenda na kubadilika” unaweza pia kuturuhusu “kwenda na kupona,” kwa kuwa Yeye ndiye chanzo cha uponyanji wa yote ambayo yamevunjika maishani mwetu. Akiwa Mpatanishi mkuu na Mwombezi kwa Baba, Kristo hutakasa na kurejesha uhusiano uliyovunjika—muhimu zaidi uhusiano wetu na Mungu.

Tafsiri ya Joseph Smith inaweka wazi kwamba mwanamke huyo alifuata ushauri wa Mwokozi na kubadilisha maisha yake: “Na yule mwanamke akamtukuza Mungu tangu saa ile, na kuamini katika jina lake.”3 Ni bahati mbaya kwamba hatujui jina lake, au maelezo mengine kuhusu maisha yake baada ya wakati huu, kwa sababu ingehitaji jitihada kubwa, unyenyekevu, na imani katika Bwana Yesu Kristo kwake yeye ili atubu na kubadilika. Tunachojua ni kwamba alikuwa mwanamke ambaye “aliamini katika jina lake” pamoja na ufahamu kwamba hakuwa nje ya upeo wa kufikiwa na dhabihu Yake isiyo na mwisho na ya milele.

Uhusiano na Wengine Uliovunjika

Katika Luka mlango wa 15 tunasoma fumbo la mtu aliyekuwa na wana wawili. Yule mdogo akamwomba baba yake urithi wake, na akasafiri kwenda nchi ya mbali, akatapanya mali yake kwa maisha ya uasherati.4

“Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kubwa iliingia katika nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji.

“Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe.

“Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu.

“Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa!

“Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako,

“Sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako.

“Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana.”5

Ukweli kwamba baba alimkimbilia mwanawe, naamini, ni muhimu. Maumivu ya kibinafsi ambayo mwana huyo alikuwa amemletea baba yake bila shaka yalikuwa mazito na makubwa. Vivyo hivyo, huenda baba aliaibishwa kiuhalisia na matendo ya mwanawe.

Basi, kwa nini baba hakungoja mwanawe aombe msamaha? Kwa nini hakusubiri utoaji wa matoleo ya urejesho na upatanisho kabla ya kutoa msamaha na upendo? Hili ni jambo ambalo mara nyingi nimelitafakari.

Bwana anatufundisha kwamba kusamehe wengine ni amri ya ulimwengu wote: “Mimi, Bwana, nitamsamehe yule nitakaye kumsamehe, lakini ninyi mnatakiwa kuwasamehe watu wote.”6 Kutoa msamaha kunaweza kuchukua ujasiri na unyenyekevu mkubwa. Kunaweza pia kuchukua muda. Inatuhitaji sisi kuweka imani na tumaini letu katika Bwana tunapochukua uwajibikaji kwa hali ya mioyo yetu. Hapa ndipo penye umuhimu na nguvu ya haki yetu ya kujiamulia.

Kwa taswira ya baba huyu katika fumbo la mwana mpotevu, Mwokozi alisisitiza kwamba msamaha ni mojawapo ya karama bora sana ambazo tunaweza kupeana mmoja na mwingine na hasusani sisi wenyewe. Kuifungua mioyo yetu kupitia msamaha si rahisi kila mara, lakini kupitia nguvu za kuwezesha za Yesu Kristo, inawezekana.

Sehemu Zetu Zilizovunjika

Kwenye Matendo ya Mitume mlango wa 3 tunajifunza kuhusu mtu fulani ambaye alizaliwa kilema na “ambaye walimweka kila siku katika mlango wa hekalu uitwao Mzuri, ili aombe sadaka kwa watu waingiao ndani ya hekalu.”7

Yule mwombaji mwenye ulemavu alikuwa na umri wa zaidi ya miaka 408 na alikuwa ameishi maisha yake yote katika hali inayoonekana kutokuwa na mwisho ya kutaka na kungoja, kwa kuwa alitegemea usaidizi na ukarimu wa wengine.

Siku moja aliwaona “Petro na Yohana wakiingia hekaluni [na] aliwaomba wampe sadaka.

“Na Petro, akimkazia macho pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi.

“Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao.

“Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende.

“Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu.

“Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akirukaruka, na kumsifu Mungu”9

Mara nyingi tunajipata wenyewe, kama vile mwombaji kiwete kwenye lango la hekalu, kwa subira—au wakati mwingine bila subira—“[tuki]mngojea Bwana.”10 Kungojea kuponywa kimwili au kihisia. Kungojea majibu ambayo hupenya sehemu ya ndani kabisa ya mioyo yetu. Kungojea muujiza.

Kumsubiria Bwana kunaweza kuwa mahali patakatifu—mahali pa kung’arishwa na kutakaswa ambapo tunaweza kumjua Mwokozi kwa njia ya kibinafsi na ya kina. Kumsubiria Bwana pia kunaweza kuwa mahali tunajipata tukiuliza, “Ee Mungu uko wapi?”11—mahali ambapo ustahimilifu wa kiroho hutuhitaji tufanye imani katika Kristo kwa kusudi kumchagua Yeye tena na tena na tena. Ninapafahamu mahali hapa, na ninaelewa aina hii ya kusubiri.

Nilikaa masaa mengi kwenye kituo cha matibabu ya saratani, nikiungana katika mateso yangu na wengine wengi ambao walikuwa wakitamani kuponywa. Wengine waliishi; wengine hawakuishi. Nilijifunza kwa njia ya kina kwamba ukombozi kutokana na majaribu yetu ni tofauti kwa kila mmoja wetu, na kwa hivyo fokasi yetu inapaswa kwa kiasi kidogo sana kuhusu njia ambayo tunakombolewa na zaidi iwe kuhusu Mkombozi Mwenyewe. Mkazo wetu daima unapaswa kuwa juu ya Yesu Kristo!

Kutumia imani katika Kristo kunamaanisha kutumainia siyo tu mapenzi ya Mungu bali pia katika ratiba Yake. Kwa kuwa Yeye anajua hasa kile tunachohitaji na wakati maalumu tunapohitaji. Tunapojisalimisha kwenye mapenzi ya Bwana, hatimaye sisi tutapokea kwa kiasi kikubwa zaidi ya yale tuliyotamani.

Rafiki zangu wapendwa, sote tuna kitu maishani mwetu ambacho kimevunjika ambacho kinahitaji kurekebishwa, kutatuliwa, au kuponywa. Tunapomgeukia Mwokozi, tunapolinganisha mioyo yetu na akili zetu pamoja Naye, tunapotubu, Yeye huja kwetu “na uponyaji mabawani Mwake,”12 huweka mikono Yake kutuzunguka kwa upendo, na kusema, “Ni SAWA. Una umri wa miaka 5 tu—au 16, 23, 48, 64, 91. Tunaweza kurekebisha hii kwa pamoja.”

Ninashuhudia kwenu kwamba hakuna kitu chochote maishani mwako ambacho kimevunjika ambacho ni zaidi ya nguvu za uponyaji, ukombozi na za kuwezesha za Yesu Kristo. Katika jina tukufu na takatifu la Yeye aliye hodari wa kuponya, Yesu Kristo, amina