Njia ya Agano: Njia ya Uzima wa Milele
Njia kuelekea ukamilifu ni njia ya agano, na Yesu Kristo ndiye kiini cha ibada na maagano yote.
Mfalme mwenye nguvu alitamani mwanawe atawale mojawapo ya falme zake. Mwana mfalme ilibidi ajifunze na kukua katika hekima ili kukalia kiti cha enzi. Siku moja, mfalme alikutana na mwana mfalme na kumwelezea mpango wake. Walikubaliana mwana mfalme angeenda katika mji tofaui na kupata uzoefu. Angekabiliwa na changamoto vile vile kufurahia vitu vingi vizuri huko. Mfalme kisha akampeleka kwenye ule mji, ambapo mwana mfalme alitarajiwa kuthibitisha uaminifu wake kwa mfalme na kuonyesha kwamba alikuwa anafaa kupokea heshima na majukumu mfalme aliyokuwa ameyahifadhi kwa ajili yake. Mwana mfalme alipatiwa uhuru wa kuchagua kupokea fursa hizi na majukumu haya au la, kulingana na matamanio na uaminifu wake. Nina hakika unataka kujua kile kilichotendeka kwa mwana mfalme. Je, alirudi kuurithi ule ufalme?
Akina kaka na akina dada wapendwa, kila mmoja wetu ni mwana mfalme au binti mfalme. Tumetumwa duniani na Baba wa Mbinguni mwenye upendo ili kufurahia baraka za mwili ambao ungekuja kuwa usiokufa kupitia Upatanisho na Ufufuko wa Yesu Kristo. Tunatarajiwa kujiandaa kurudi katika uwepo wa Mungu kwa kuthibitisha kwamba “tutafanya mambo yote yale Bwana Mungu [wetu] atakayotuamuru [sisi]” (Ibrahamu 3:25).
Ili kutusaidia, Mwokozi alikuja kutukomboa na kutuonyesha njia ya kurudi kwa Mungu. Watoto wa Mungu wamealikwa kuja kwa Mwokozi na kukamilishwa ndani Yake. Katika maandiko, tunapata mwaliko kwa ajili yetu wa kuja kwa Bwana ukirudiwa zaidi ya mara 90, na zaidi ya nusu ya hii ni mialiko binafsi kutoka kwa Bwana Mwenyewe. Kukubali mwaliko wa Mwokozi humaanisha kupokea ibada Zake na kuyashika maagano yetu pamoja Naye. Yesu Kristo ndiye “njia, kweli, na uzima” (Yohana 14:6), na Yeye hutualika sisi “sote kuja kwake na kupokea wema wake; na hamkatazi yeyote anayemjia” (2 Nefi 26:33).
Kujifunza kwetu na kufundisha kwetu injili ni kuongeza uongofu wetu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na kutusaidia sisi kuwa zaidi kama Wao. Ingawa si vitu vyote vimeshafunuliwa kuhusu “wakati kamili na namna ambayo kwayo baraka za kuinuliwa zitatolewa,” hata hivyo tumehakikishiwa baraka hizo (M. Russell Ballard, “Tumaini katika Kristo,” Liahona, Mei 2021, 55).
Alma kuhani mkuu, akifundisha katika nchi ya Zarahemla, alisimulia mwaliko muhimu wa Yesu Kristo kwamba:
“Tazama, yeye huwatumia wanadamu wote mwaliko, kwani mikono ya huruma imenyoshwa kwao, na anasema: Tubuni, na nitawapokea.
“Ndiyo, anasema: Njooni kwangu na mtakula matunda ya mti wa uzima”(Alma 5:33–34).
Mwokozi Mwenyewe hutualika sisi kuja Kwake na kuchukua nira Yake juu yetu ili kwamba tuweze kupata pumziko kutokana na ulimwengu wa ghasia (ona Mathayo 11:28–29). Tunakuja kwa Kristo kwa “kuonesha imani yetu [Kwake], kutubu kila siku, kufanya maagano na Mungu wakati tunapopokea ibada za wokovu na kuinuliwa, na kuvumilia hadi mwisho kwa kuyashika maagano hayo” (Kitabu cha Maelekezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa bSiku za Mwisho, 1.2.1, ChurchofJesusChrist.org). Njia kuelekea ukamilifu ni njia ya agano, na Yesu Kristo ndiye kiini cha ibada na maagano yote.
Mfalme Benjamini alifundisha kwamba kwa sababu ya maagano tunayofanya, tunakuwa wana na mabinti wa Kristo, ambaye ametuzaa kiroho, na chini ya uongozi wake tunafanywa huru, kwani “hakuna jina lingine ambalo kwalo huleta wokovu” (ona Mosia 5:7–8). Tunaokolewa tunapovumilia hadi mwisho kwa “kufuata mfano wa Mwana wa Mungu aliye hai”(2 Nefi 31:16). Nefi alishauri kwamba yote hayafanyiki kwa kuingia tu katika njia nyembamba iliyosonga; “lazima tusonge mbele tukiwa na imani imara katika Kristo, tukiwa na mng’aro mkamilifu wa tumaini, na upendo kwa Mungu na wanadamu wote”(ona 2 Nefi 31:19–20).
Mafundisho ya Kristo hutusaidia kuipata na kubakia kwenye njia ya agano, na injili imepangiliwa ili kwamba baraka alizoahidi Bwana zinapokelewa kupitia ibada na maagano matakatifu. Nabii wa Mungu, Rais Russell M. Nelson, alitusihi katika matangazo ya televisheni ya Januari 16, 2018, kwamba “tuendelee katika njia ya agano. Dhamira yako ya kumfuata Mwokozi kwa kufanya maagano pamoja Naye na kisha kuyashika maagano haya itafungua mlango kwa kila baraka ya kiroho na fursa zilizopo kwa wanaume, wanawake na watoto kila mahali. Mwisho ambao kila mmoja wetu hujitahidi kuufikia ni kupata endaumenti ya nguvu katika Nyumba ya Bwana, kuunganishwa kama familia, kuwa waaminifu katika maagano yaliyofanywa katika hekalu ambayo hutufanya tustahili baraka kubwa zaidi ya Mungu—ile ya uzima wa milele” (“Tunaposonga Mbele Pamoja,” Liahona, Apr. 2018, 7).
Mungu hatatupilia mbali uhusiano Wake na, au kuzuia baraka zilizoahidiwa za uzima wa milele kutokwa kwa mtunza maagano yeyote mwaminifu. Na tunapoheshimu maagano matakatifu, tunasogea karibu na Mwokozi. Mzee David A. Bednar alitufundisha jana kwamba maagano na ibada za injili hufanya kazi katika maisha yetu kama vile dira ili kutupatia maelekezo muhimu ya kuja kwa Kristo na kuwa zaidi kama Yeye.
Maagano huonesha njia ya kurudi kwa Mungu. Ibada za ubatizo na kupokea kipawa cha Roho Mtakatifu, kutawazwa kwenye ukuhani, na sakramenti hutuongoza hadi kwenye hekalu la Bwana ili kupokea ibada Zake za kuinuliwa.
Ningependa kutaja mambo mawili Mwokozi wetu aliyoyasisitiza ili kutusaidia sisi kushika maagano kwa uaminifu:
-
Roho Mtakatifu anaweza kutufundisha, kutukumbusha juu ya mafundisho ya Mwokozi, na kubaki nasi milele (ona Yohana 14:16, 26). Yeye anaweza kuwa mwenza wetu daima ili kutuongoza kwenye njia ya agano. Rais Russell M. Nelson amefundisha kwamba “katika siku zijazo, haitawezekana kunusurika kiroho bila mwongozo, maelekezo, faraja na ushawishi endelevu wa Roho Mtakatifu.” (“Ufunuo kwa Kanisa, Ufunuo kwa Ajili ya Maisha Yetu,” Liahona,” Mei 2018, 96).
-
Mwokozi alianzisha ibada ya sakramenti ili kwamba daima sisi tuweze kumkumbuka Yeye na Roho Wake apate kuwa pamoja nasi. Ubatizo hufungua lango la uzima wa milele, na sakramenti hutusaidia kwa uthabiti kusonga mbele katika njia ya agano. Tunapopokea sakramenti, itakuwa ushuhuda kwa Baba kwamba daima tunamkumbuka Mwanawe. Na tunapomkumbuka Yeye daima na kutii amri Zake, Roho Wake atakuwa pamoja nasi. Nyongeza katika ahadi hii, Bwana hufanya upya ondoleo la dhambi lililoahidiwa pale tunapotubu dhambi zetu kwa unyenyekevu.
Katika kubaki waaminifu kwenye maagano yetu, tunapaswa kujitahidi daima kuwa na Roho ili atuandae sisi kuwa wanaostahili kupokea sakramenti, na, vivyo hivyo, sisi kila mara tunapokea sakramenti ili daima Roho awe pamoja nasi.
Wakati binti yetu alipokuwa na umri wa miaka mitano, alikuwa na mfano wa gari lenye betri na alipenda kuliendesha ndani ya nyumba. Jioni moja, alinijia na kusema, “Baba, gari langu haliendi tena. Je, tunaweza kupata petroli kutoka katika gari lako tuweke katika gari langu ili liweze kutembea tena? Pengine linahitaji petroli kama gari lako ili liweze kutembea.”
Baadaye niligundua kwamba nguvu za betri zilikuwa zimeisha, kwa hiyo nilisema tungeweza kulitengeneza kwa takriban saa moja. Kwa msisimko mkubwa, alisema, “ndiyo! Tutalipeleka kwenye kituo cha mafuta.” Niliunganisha tu betri kwenye soketi ya umeme ili kuchaji, na baada ya saa moja aliweza kuendesha gari, lililopata nguvu za beteri iliyochajiwa. Baada ya hapo alijifunza kwamba ni muhimu daima kuchaji beteri kwa kuunganisha kwenye soketi.
Pale binti yetu alipojifunza uhusiano kati ya betri na nguvu za kuendesha gari lake, ndivyo nasi tunavyojifunza kuhusu Yesu Kristo, sakramenti, na Roho. Tunamhitaji Roho ili atusaidie kupita katika maisha ya duniani tunaposhika maagano kwa uaminifu, na sakramenti ili kutia nguvu utu wetu wa kiroho. Kufanya upya agano letu la ubatizo na kupokea sakramenti kunaingiza uaminifu kwenye maagano mengine yote. Hatima ya furaha inahakikishwa wakati tunapojifunza kwa sala na kuheshimu mwaliko wa Mwokozi na kufurahia baraka zake zilizoahidiwa. Yeye alisema, “Na ili ujilinde na dunia pasipo mawaa, utakwenda kwenye nyumba ya sala na kutoa sakramenti zako katika siku yangu takatifu” (Mafundisho na Maagano 59:9).
Ninashuhudia kwamba washika maagano wanaahidiwa “amani katika ulimwengu huu na uzima wa milele katika ulimwengu ujao” (Mafundisho na Maagano 59:23). Ninatoa ushahidi kwamba unapopokea kila mara ishara za Mwokozi kupitia sakramenti, utakuwa na Roho Wake ili kukuongoza kwenye njia ya agano na kubaki mwaminifu kwenye maagano yako. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.