Mkutano Mkuu
Masomo kutoka Kisimani
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


11:29

Masomo kutoka Kisimani

Tunaweza kumgeukia Mwokozi kwa ajili ya nguvu na uponyaji vitakavyotusaidia kutimiza yale yote tuliyotumwa kuyatimiza hapa.

Ni furaha iliyoje kukusanyika na kila mmoja wenu kwenye kikao hiki cha wanawake cha mkutano mkuu!

Nimekulia magharibi mwa New York na kuhudhuria tawi dogo la Kanisa takribani maili 20 (km 32) kutoka nyumbani kwetu. Nilipoketi katika darasa la Shule ya Jumapili katika jengo la chini la kukodi la kanisa pamoja na rafiki yangu Patti Jo, nisingeweza kudhani kuwa sehemu ya udada wa ulimwengu wa mamilioni ya wanawake.

Miaka mitano iliyopita, mume wangu, Bruce, aliugua sana tulipokuwa tukitumikia pamoja na Watakatifu waliwekwa wakfu katika Eneo la Mashariki ya Ulaya. Tulirejea nyumbani na alifariki wiki chache baadaye. Maisha yangu yalibadilika ndani ya usiku mmoja. Nilihuzunishwa na kuhisi dhaifu na muhanga. Nilimlilia Bwana kuongoza njia yangu: “Ungependa nifanye nini?”

Wiki chache baadaye, nilikuwa nikipitia barua zangu wakati picha ndogo kwenye orodha ilipovutia macho yangu. Nilipoangalia kwa ukaribu, nilitambua ilikuwa tafsiri ya mchoraji ya mwanamke Msamaria pamoja na Yesu mtoni. Kwa wakati huo, Roho alizungumza nami kwa dhahiri: “Hilo ndilo unapaswa kulifanya.” Baba wa Mbinguni mwenye upendo alikuwa akinialika kuja kwa Mwokozi na kujifunza.

Ningependa kushiriki nanyi masomo matatu ninayojifunza ninapoendelea kunywa kutoka kwenye kisima Chake cha “maji ya uhai.”1

Kwanza: Hali Zetu za Kale na Sasa Haziamui Kesho Yetu

Akina dada, najua kwamba wengi wenu wanahisi kama nilivyohisi, kutokuwa na hakika ya jinsi ya kukabiliana na changamoto ngumu na upotevu—upotevu kwa sababu maisha yako hayaendi katika njia uliyotarajia, uliyoiomba na uliyopanga.

Bila kujali hali zetu, maisha yetu ni matakatifu na yana maana na lengo. Kila mmoja wetu ni binti mpendwa wa Mungu, tuliozaliwa na utakatifu nafsini mwetu.

Mwokozi wetu, Yesu Kristo, kupitia dhabihu yake ya upatanisho, alifanya iwezekane kwetu kusafishwa na kuponywa, kutusaidia kukamilisha lengo letu duniani bila kujali maamuzi ya wanafamilia, hali ya ndoa, afya ya kimwili au kiakili au hali nyingine yoyote.

Mfikirie mwanamke kisimani. Maisha yake yalikuwaje? Yesu aliona kwamba aliwahi kuwa na wanaume watano na kwa sasa alikuwa hajaolewa na mwanaume aliyekuwa akiishi naye. Na bado, bila kujali magumu ya maisha yake, moja ya tangazo la kwanza la Mwokozi kwamba Alikuwa Masihi lilitoka kwake. Mwokozi alisema, “Mimi ninayezungumza nawe mimi ndiye.”2

Mwanamke alikuwa shahidi mkubwa, akitangaza kwa watu wa mji wake kwamba Yesu alikuwa Kristo. “Na katika mji ule Wasamaria wengi walimwamini kwa sababu ya neno la yule mwanamke.”3

Hali yake ya kale na sasa hazikuamua kesho yake. Kama yule mwanamke, tunaweza kuchagua kumgeukia Mwokozi leo kwa ajili ya nguvu na uponyaji utakaotusaidia kutimiza yale yote tuliyotumwa kuyatimiza hapa.

Pili: Uwezo Upo Ndani Yetu

katika mstari mashuhuri kwenye Mafundisho na Maagano, Bwana anawahimiza wanawake na wanaume “kujishughulisha kwa shauku katika kazi njema, na kufanya mambo mengi kwa hiari yao wenyewe, na kutekeleza haki nyingi; kwani uwezo u ndani yao.”4

Akina dada, uwezo upo ndani yetu wa kutekeleza haki nyingi!

Rais Russel M. Nelson alishuhudia, “Kila mwanamke na kila mwanaume anayefanya maagano na Mungu na kutunza maagano hayo, na anayeshiriki kwa kustahili katika ibada za ukuhani, ana fursa ya moja kwa moja kwenye nguvu za Mungu.”5

Nimekuja kutambua kwamba tunapojitahidi kuheshimu maagano matakatifu yaliyofanywa wakati wa ubatizo na katika mahekalu matakatifu, Bwana atatubariki “kwa nguvu Yake ya uponyaji, ya kuimarisha” pamoja na “utambuzi wa kiroho na uamsho ambao kamwe hatujawahi kuwa nao.”6

Tatu: “Kutokana na Mambo Madogo Huja Yale Yaliyo Makuu”7

Katika Mahubiri ya Mlimani, Yesu aliwafundisha wafuasi wake, “Ninyi ni chumvi ya ulimwengu”8 na “Ninyi ni nuru ya ulimwengu.”9 Baadaye alifananisha ukuaji wa ufame wa mbinguni na chachu, “aliyoitwaa mwanamke, akaisitiri ndani ya pishi tatu za unga, hata ukachachwa wote pia.”10

  • Chumvi

  • Chachu

  • Nuru

Hata kwa viwango vidogo, kila kimoja huathiri vingine vyote. Mwokozi anatualika kutumia nguvu Yake kuwa kama chumvi, chachu, na nuru.

Chumvi

Inashangaza ni tofauti kiasi gani kiasi kidogo cha chumvi huleta katika ladha ya kile tulacho. Na bado, chumvi ni kiungo cha gharama nafuu na kawaida sana.

Katika kitabu cha 2 Wafalme, tunasoma kuhusu “kijana mwanamke,”11 ambaye alikamatwa na Washami na kuwa mtumishi kwa mke wa Namaani, mkuu wa jeshi la Shamu. Alikuwa kama chumvi; alikuwa kijana, asiye maarufu na maisha yake kama mtumwa kwenye nchi ya kigeni kwa dhahiri yalikuwa sicho alichotarajia.

Hata hivyo, alizungumza sentensi mbili kwa nguvu za Mungu, akimshuhudia mke wa Naamani: “Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.”12

Maneno yake ya imani yalifikishwa kwa Naamani, ambaye aliyatendea kazi, yakamruhusu yeye kuponywa kimwili na kiroho.

Mara kwa mara tunafokasi kwa watumishi ambao walimsadikisha Naamani kuoga katika mto Yordani, kama nabii Elisha alivyoamuru, lakini Naamani asingekuwepo hata kwenye mlango wa Elisha bila ya “kijana mwanamke.”

Unaweza kuwa mdogo au kuhisi kutokuwa wa muhimu, lakini unaweza kuwa kama chumvi katika familia yako, shuleni na jamii yako.

Chachu

Je, umewahi kula mkate usiotiwa chachu? Unaweza kuuelezeaje? Umegandamana? Mzito? Mgumu? Kwa kiasi kidogo cha hamira, mkate huumuka, huongezeka kuwa mwepesi na laini.

Tunapoalika nguvu ya Mungu katika maisha yetu, tunaweza kubadilisha “roho nzito”13 kwa maoni ya kuvuviwa ambayo huwainua wengine na kuandaa chumba kwa ajili ya mioyo kuponywa.

Hivi karibuni rafiki yangu mmoja alilala kitandani asubuhi ya Krismasi, akiwa amesongwa na huzuni. Watoto wake walimwomba aamke; hata hivyo, alijazwa na maumivu ya talaka iliyokuwa ikimsubiria. Akiwa amelala kitandani akilia, alimimina nafsi yake katika sala kwa Baba yake wa Mbinguni, akimuarifu kuhusu kukata kwake tamaa.

Alipohitimisha sala yake, Roho alinongoneza kwamba Mungu alifahamu maumivu yake. Alihisi huruma Yake Uzoefu huu mtakatifu ulihalalisha hisia zake na kumpa tumaini kwamba hakuwa akiomboleza peke yake. Aliamka, akatoka nje nje na kujenga mtu wa theluji pamoja na watoto wake, akiondoa uzito wa asubuhi kwa kicheko na shangwe.

Nuru

Je, inachukua nuru kiasi gani kuangaza giza ndani ya chumba? Mwale mmoja mdogo. Na mwale huo wa nuru katika sehemu ya giza unaweza kutokana na nguvu ya Mungu ndani yako.

Japo unaweza kuhisi mpweke kadiri dhoruba za maisha zinavyoongezeka, unaweza kuangaza nuru katika giza la kutoelewa, kuchanganyikiwa na kutoamini. Nuru yako ya imani katika Kristo inaweza kuwa imara na thabiti, ikiwaongoza wale wanaokuzunguka kwenye usalama na amani.

Akina dada, mioyo inaweza kubadilishwa na maisha kubarikiwa tunapotoa kiasi kidogo cha chumvi, kijiko cha hamira na mwale wa nuru.

Ninashuhudia kwamba Mwokozi ni chumvi katika maisha yetu, akitualika sisi kuonja shangwe na upendo Wake.14 Ni Yeye ambaye ni chachu wakati maisha yetu ni magumu, akituletea sisi tumaini15 na kunyanyua mizigo yetu16 kwa kupitia nguvu zake zisizo na kifani na upendo wa kuokoa.17 Yeye ni nuru yetu,18 akiangaza njia yetu ya kurejea nyumbani.

Ninaomba kwamba tuweze kusonga kwa Mwokozi, kama mwanamke kisimani, na kunywa maji Yake ya uhai. Pamoja na watu wa Samaria, kisha tunaweza kutangaza, “Sasa tunaamini, … maana sisi tumesikia wenyewe, tena twajua ya kuwa hakika huyu ndiye Mwokozi wa ulimwengu.”19 Katika Jina la Yesu Kristo, amina.