Kumfuata Yesu: Kuwa Mpatanishi
Wapatanishi si watu wa kukaa kimya; wanashawishi katika njia ya Mwokozi.
Akina kaka na dada zangu wapendwa, tunapopitia siku za kufadhaisha za vurugu, mabishano, na, kwa wengi, mateso makali, mioyo yetu inajawa na shukrani nyingi kwa Mwokozi wetu na baraka za milele za injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Tunampenda na tunamtumaini Yeye, na tunaomba kwamba daima tutamfuata Yeye.
Changamoto ya Vyombo vya Habari vya Kijamii
Athari kubwa ya intaneti ni baraka na changamoto, ya kipekee kwa wakati wetu.
Katika ulimwengu wa vyombo vya habari vya kijamii na njia kuu za habari, sauti ya mtu mmoja inaweza kuzidishwa kwa kasi kubwa. Sauti hiyo, iwe ya kweli au ya uwongo, iwe ya haki au ya ubaguzi, iwe ya ukarimu au ya kikatili, inasikika kwa kasi ulimwenguni kote.
Posti za vyombo vya habari vya kijamii za kujali na wema mara nyingi huwa chini ya rada kimya kimya, wakati maneno ya dharau na hasira yanasikika mara kwa mara masikioni mwetu, iwe kwa falsafa ya kisiasa, watu kwenye habari, au maoni juu ya janga. Hakuna mtu yeyote au mada yoyote, ilijumuisha Mwokozi na injili Yake iliyorejeshwa, ina kinga kutokana na shani hii ya kijamii ya sauti za kukingamiza.
Kuwa Mpatanishi
Mahubiri ya Mlimani ni ujumbe kwa wote lakini yalitolewa mahususi kwa wanafunzi wa Mwokozi, wale waliochagua kumfuata Yeye.
Bwana alifundisha jinsi ya kuishi hapo kale na sasa katika ulimwengu wenye dharau. “Heri wapatanishi,” Yeye alitangaza, “maana hao wataitwa wana wa Mungu.”1
Kwa ngao ya imani yetu katika Yesu Kristo, tunakuwa wapatanishi, tukizimisha—ikimaanisha kutuliza, kupoza, au kuzuia—mishale yote ya moto ya adui.2
Tunapofanya sehemu yetu, ahadi Yake ni kwamba tutaitwa “wana wa Mungu.” Kila mtu duniani ni “uzao”3 wa Mungu, lakini kuitwa “wana wa Mungu” kunamaanisha mengi zaidi. Tunapokuja kwa Kristo na kufanya maagano Naye, tunakuwa “uzao wake” na “warithi wa ufalme,”4 “watoto wa Kristo, wana wake, na binti zake.”5
Je, mpatanishi anawezaje kutuliza na kupoza mishale yenye moto? Hakika si kwa kusitasita mbele ya wale wanaotudharau. Badala yake, tunabaki jasiri katika imani yetu, tukishiriki imani yetu kwa ari, lakini siku zote bila hasira au chuki.6
Hivi karibuni, baada ya maoni yenye maneno makali ambayo yalikosoa Kanisa, Mchungaji Amos C. Brown, kiongozi wa kitaifa wa haki za kiraia na kasisi wa Kanisa la Third Baptist huko San Francisco, alijibu:
“Ninaheshimu uzoefu na mtazamo wa mtu aliyeandika maneno hayo. Kwa kweli, sioni anachokiona.”
“Ninaichukulia kama mojawapo ya furaha kuu kwangu kuwajua viongozi hawa [wa Kanisa], akiwemo Rais Russell M. Nelson. Wao, kwa makadirio yangu, ni kielelezo cha uongozi bora ambao nchi yetu inao.”
Kisha akaongeza: “Tunaweza kulalama jinsi mambo yalivyokuwa. Tunaweza kukataa kukiri mema yote yanayoendelea sasa. Lakini mbinu hizi hazitaponya migawanyiko yetu ya kitaifa. Kama Yesu alivyofundisha, hatuondoi uovu kwa uovu zaidi. Tunapenda kwa ukarimu na tunaishi kwa rehema, hata kwa wale tunaowafikiria kuwa adui zetu.”7
Mchungaji Brown ni mpatanishi. Alipoza mishale yenye moto kwa utulivu na kwa heshima. Wapatanishi si watu wa kukaa kimya; wanashawishi katika njia ya Mwokozi.8
Ni nini hutupatia nguvu za ndani za kupoza, kutuliza, na kuzima mishale yenye moto inayolenga kweli tunazozipenda? Nguvu huja kutoka kwa imani yetu katika Yesu Kristo na imani yetu katika maneno Yake.
“Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi … na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu.
“… Kwani thawabu yenu ni kubwa mbinguni: kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.”9
Umuhimu wa Haki ya Kujiamulia
Kanuni mbili muhimu huongoza hamu yetu ya kuwa wapatanishi.
Kwanza, Baba yetu wa Mbinguni amempa kila mtu haki yake ya kujiamulia kimaadili, na uwezo wa kuchagua njia yake mwenyewe.10 Haki hii ya kujiamulia ni mojawapo ya karama kuu za Mungu.
Pili, kwa haki hii ya kujiamulia, Baba yetu wa Mbinguni aliruhusu “upinzani katika mambo yote,”11 “Tunaonja uchungu, ili [sisi] tupate kujua kuthamini chema.”12 Upinzani haupaswi kutushangaza. Tunajifunza kutofautisha mema na mabaya.
Tunafurahia baraka ya haki ya kujiamulia, tukielewa kwamba kutakuwa na wengi ambao hawaamini kile tunachoamini. Kwa hakika, ni wachache katika siku za mwisho watakaochagua kufanya imani yao katika Yesu Kristo kuwa kiini cha yote wanayofikiri na kufanya.13
Kwa sababu ya majukwaa ya vyombo vya habari vya kijamii, sauti moja ya kutoamini inaweza kuonekana kuwa sauti nyingi hasi,14 lakini hata kama ni sauti nyingi, tunachagua njia ya wapatanishi.
Viongozi wa Bwana
Wengine wanaona Urais wa Kwanza na Akidi ya Kumi na Wawili kuwa na nia za kiulimwengu, kama vile viongozi wa kisiasa, kibiashara, na kitamaduni.
Hata hivyo, tunakuja kitofauti sana na majukumu yetu. Hatujachaguliwa au kuteuliwa kutokana na kutuma maombi. Bila maandalizi yoyote maalum ya kitaaluma, tunaitwa na kutawazwa kutoa ushuhuda wa jina la Yesu Kristo ulimwenguni kote hadi pumzi yetu ya mwisho. Tunatafuta kwa bidii kuwabariki wagonjwa, wapweke, waliovunjika mioyo na maskini na kuimarisha ufalme wa Mungu. Tunatafuta kujua mapenzi ya Bwana na kuyatangaza, hasa kwa wale wanaotafuta uzima wa milele.15
Ingawa tamanio letu la dhati ni kwamba mafundisho ya Mwokozi yathaminiwe na wote, maneno ya Bwana kupitia manabii Wake mara nyingi ni kinyume na mawazo na mitindo ya ulimwengu. Imekuwa hivyo siku zote.16
Mwokozi aliwaambia Mitume Wake:
“Iwapo ulimwengu [unawachukia], mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. …
“… Haya yote watawatenda … kwa kuwa hawamjui yeye aliyenipeleka.”17
Kuwajali Wote
Kwa heshima tunawapenda na kuwajali jirani zetu wote, bila kujali ikiwa wanaamini kama sisi au la. Yesu alitufundisha katika mfano wa Msamaria Mwema kwamba wale wa imani tofauti wanapaswa kujitahidi kwa unyoofu kuwasaidia wote wenye uhitaji, wakiwa wapatanishi, wanaotafuta mambo mema na mazuri.
Mnamo Februari, kichwa cha habari katika Jamhuri ya Arizona kilisema, “Muswada wa pande mbili unaoungwa mkono na Watakatifu wa Siku za Mwisho ungelinda watu mashoga na waliobadili jinsia wa Arizona.”18
Sisi, kama Watakatifu wa Siku za Mwisho “tunafurahia kuwa sehemu ya muungano wa imani, biashara, LGBTQ na viongozi wa jumuiya ambao wamefanya kazi pamoja katika roho ya uaminifu na kuheshimiana.”19
Rais Russell M. Nelson wakati fulani aliuliza kwa kufikiri, “Je, mistari ya mipaka haiwezi kuwepo bila kuwa safu za vita?20
Tunatafuta kwa bidii kuwa “wafuasi wapatanishi wa Kristo.”21
Nyakati za Kutojibu
Baadhi ya mashambulizi dhidi ya Mwokozi yalikuwa mabaya sana hata Yeye hakusema chochote. “Wakuu wa makuhani na waandishi … wakamshitaki kwa nguvu sana … na kumdhihaki,” lakini Yesu hakuwajibu [wao] lolote.”22 Kuna nyakati ambapo kuwa mpatanishi ina maana kwamba tunakataa msukumo wa kujibu na badala yake, kwa heshima, tunabaki kimya.23
Inahuzunisha kwetu sote wakati maneno makali au ya kejeli kuhusu Mwokozi, wafuasi Wake na Kanisa Lake yanaposemwa au kuchapishwa na wale ambao wakati fulani walisimama nasi, wakapokea sakramenti pamoja nasi, na kushuhudia pamoja nasi kuhusu jukumu takatifu la Yesu Kristo.24
Hili lilitokea pia wakati wa huduma ya Mwokozi.
Baadhi ya wanafunzi wa Yesu waliokuwa pamoja Naye wakati wa miujiza Yake mikuu walikusudia “[kutoandamana] naye tena.”25 Cha kusikitisha, si wote watakaobaki imara katika upendo wao kwa Mwokozi na azimio lao la kushika amri Zake.26
Yesu alitufundisha kujiondoa katika mzunguko wa hasira na ubishi. Katika mfano mmoja, baada ya Mafarisayo kumkabili Yesu na kushauriana jinsi ambavyo wangeweza kumwangamiza, maandiko yanasema kwamba Yesu alijitenga nao,27 na miujiza ilifanyika kwani “makundi ya watu yalimfuata, naye akawaponya wote.”28
Kubariki Maisha ya Wengine
Sisi pia tunaweza kujiondoa kwenye mabishano na kubariki maisha ya wengine29 huku tukiwa hatujitengi katika kona yetu wenyewe.
Huko Mbuji-Mayi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mwanzoni baadhi walikuwa wakilikosoa Kanisa, bila kuelewa imani yetu au kuwajua waumini wetu.
Wakati fulani uliopita, mimi na Kathy tulihudhuria ibada ya pekee sana ya Kanisa huko Mbuji-Mayi. Watoto walikuwa wamevalia mavazi nadhifu, wakiwa na macho angavu na tabasamu pana. Nilitarajia kuzungumza nao kuhusu elimu yao lakini niligundua kwamba wengi hawakuwa wakihudhuria shule. Viongozi wetu, wakiwa na fedha kidogo sana za msaada wa kibinadamu, walipata njia ya kusaidia.30 Sasa, zaidi ya wanafunzi 400—wasichana kwa wavulana, waumini pamoja na wale wasio wa imani yetu—wanakaribishwa na kufundishwa na walimu 16 ambao ni waumini wa Kanisa la Yesu Kristo.
Kalanga Muya mwenye umri wa miaka kumi na minne alisema, “[Nikiwa na pesa kidogo,] miaka minne ilipita bila kuhudhuria shule. Ninashukuru sana kwa kile ambacho Kanisa limefanya. Sasa naweza kusoma, kuandika, na kuzungumza Kifaransa.”31 Akizungumzia mpango huu, meya wa Mbuji-Mayi alisema, “Nimetiwa moyo na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa sababu wakati makanisa [mengine] yakijigawa kila moja kwenye kona yake … [ninyi mnafanya kazi] pamoja na [ wengine] kusaidia jamii yenye shida.”32
Kupendana Mmoja na Mwingine
Kila wakati ninaposoma Yohana sura ya 13, ninakumbushwa kuhusu mfano mkamilifu wa Mwokozi kama mpatanishi. Yesu kwa upendo aliwaosha miguu Mitume. Kisha, tunasoma “alifadhaika rohoni,”32 alipofikiri juu ya mtu Yeye aliyempenda akijitayarisha kumsaliti. Nimejaribu kufikiria mawazo na hisia za Mwokozi wakati Yuda alipoondoka. Cha kushangaza, wakati wa mashaka, Yesu hakuzungumza tena kuhusu hisia Zake za “kufadhaika” au kuhusu usaliti. Badala yake, Yeye alizungumza na Mitume Wake kuhusu upendo, maneno Yake yakileta ushawishi kwa karne nyingi.
“Amri mpya nawapa, Mpendane, kama vile nilivyowapenda ninyi. …
“Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”34
Na tumpende Yeye na kupendana mmoja na mwingine. Na tuwe wapatanishi, kwamba tuweze kuitwa “wana wa Mungu,” Ninaomba katika jina la Yesu Kristo, amina.