Njoo kwenye Zizi la Mungu
Ndani ya zizi la Mungu, tunapata uzoefu wa uangalizi wa Mchungaji Mwema, malezi Yake na tunabarikiwa kuhisi upendo Wake wenye kukomboa.
Kama wazazi vijana, Kaka na Dada Samad walijifunza injili ya Yesu Kristo katika nyumba ndogo ya vyumba viwili huko Semarang, Indonesia.1 Wakiwa wameketi kuzunguka meza ndogo, na taa isiyo angavu ambayo ilionekana kuleta mbu wengi kuliko mwanga, wamisionari wawili vijana waliwafundisha kweli za milele. Kupitia maombi ya dhati na mwongozo wa Roho Mtakatifu, walikuja kuamini kile walichofundishwa na kuchagua kubatizwa na kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Maamuzi hayo, na mpangilio wao wa kuishi tangu wakati huo, umewabariki Kaka na Dada Samad na familia yao katika kila kipengele cha maisha yao.2
Wao ni miongoni mwa Watakatifu waanzilishi wa awali katika Indonesia. Baadaye walipokea ibada za hekaluni, Kaka Samad alitumikia kama rais wa tawi na kisha kama rais wa wilaya, akiendesha gari kote katika Java ya Kati ili kutimiza majukumu yake. Kwa muongo uliopita, yeye ametumikia kama patriaki wa kwanza wa Kigingi cha Surakarta Indonesia.
Kama mmoja wa wamisionari katika nyumba hiyo ndogo, iliyojawa na imani miaka 49 iliyopita, nilishuhudia kile Mfalme Benyamini alichofudisha katika Kitabu cha Mormoni: “Ningetamani mtafakari juu ya hali ya baraka na yenye furaha ya wale wanaotii amri za Mungu. Kwani tazama, wanabarikiwa katika vitu vyote, vya kimwili na vya kiroho.”3 Baraka ambazo hutiririka katika maisha ya wale ambao wanafuata mfano na mafundisho ya Yesu Kristo, wale wanaochagua kuhesabiwa miongoni mwa wanafunzi Wake, ni nyingi sana, za furaha na za milele.4
Zizi la Mungu
Mwaliko wa Alma wa agano la ubatizo kwa wale walikusanyika katika Maji ya Mormoni huanza na kifungu hiki cha maneno: “kwa vile mnatamani kujiunga na zizi la Mungu.”5
Zizi au zizi la kondoo ni boma kubwa, mara nyingi lililojengwa kwa kuta za mawe, ambapo kondoo wanalindwa usiku. Lina mlango mmoja tu. Mwisho wa siku, mchungaji huwaita kondoo. Wanaijua sauti yake, na kupitia katika lango wanaingia katika usalama wa zizi.
Watu wa Alma wangejua kwamba wachungaji husimama kwenye mlango mwembamba wa zizi ili wakati kondoo wanapoingia wanahesabiwa6 na vidonda na maradhi yao yanaonekana na kushughulikiwa mmoja mmoja. Usalama na afya ya kondoo hutengemea utayari wao wa kuja katika zizi na kubaki katika zizi.
Miongoni mwetu yawezekana kuwa na baadhi yetu ambao wanahisi wako kando ya kundi, pengine wanafikiria hawahitajiki sana au hawana thamani kubwa au wao si wa zizi hilo. Na, kama katika zizi la kondoo, katika zizi la Mungu sisi wakati mwingine tunakanyagana vidole na tunahitaji kutubu au kusamehe.
Lakini Mchungaji Mwema7—mchungaji wetu wa kweli—ni mwema daima. Ndani ya zizi la Mungu, tunapata uzoefu wa uangalizi Wake na malezi Yake na tunabarikiwa kuhisi upendo Wake wenye kukomboa. Yeye alisema, “Nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu; kuta zako ziko mbele zangu daima.”8 Mwokozi wetu amechora katika vitanga vya mikono yake dhambi zetu, maumivu yetu, masumbuko yetu,9 na yote yasiyo haki katika maisha.10 Wote wanakaribishwa kupokea baraka hizi, kama “wanatamani kuja”11 na kuchagua kuwa katika zizi. Kipawa cha haki ya kujiamulia siyo haki tu ya kuchagua; ni fursa ya kuchagua kilicho sahihi. Na kuta za zizi sio kizuizi bali ni chanzo cha usalama wa kiroho.
Yesu alifundisha kwamba kuna “kundi moja, na mchungaji mmoja.”12 Yeye alisema:
“Aingiaye mlangoni ni mchungaji wa kondoo. …
“Na kondoo humsikia sauti yake … ,
“… na wale kondoo humfuata, kwa maana waijua sauti yake.“13
Yesu kisha akatangaza, “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka,”14 akifundisha wazi kwamba kuna njia moja tu kuingia katika zizi la Mungu na njia moja tu ya kuokolewa. Ni kwa na kupitia Yesu Kristo.15
Baraka Huja kwa Wale walio katika Zizi la Mungu
Tunajifunza jinsi ya kuja katika zizi kutokana na neno la Mungu, ambalo ni mafundisho yanayofundishwa na Yesu Kristo na manabii Wake.16 Tunapofuata mafundisho ya Kristo na kuja ndani ya zizi kupitia imani katika Yesu Kristo, toba, ubatizo na uthibitisho, na uaminifu endelevu,17 Alma aliahidi baraka nne mahususi, za kibinafsi. Wewe unaweza (1) “kukombolewa na Mungu,” (2) “kuhesabiwa pamoja na wale wa ufufuko wa kwanza,” (3) “kuwa na uzima wa milele,” na (4) Bwana “atamimina kwa wingi Roho yake juu yako.”18
Baada ya Alma kufundisha kuhusu baraka hizi, watu walipiga makofi ya furaha. Hapa ni kwa nini:
Kwanza: Kukomboa humaanisha kulipa deni au wajibu au kufanya huru kutokana na kitu kinachokusumbua au kuumiza.19 Hakuna kiasi cha uboreshaji binafsi wa sehemu yetu kinachoweza kututakasa kutokana na dhambi tulizofanya au kuponya vidonda tunavyougua bila Upatanisho wa Yesu Kristo. Yeye ni Mkombozi wetu.20
Pili: Kwa sababu ya Ufufuko wa Kristo, watu wote watafufuliwa.21 Baada ya roho zetu kutengana na miili yetu yenye kufa, sisi bila shaka tutatazamia ule wakati sisi tutakapoweza tena kuwa na mwili uliofufuka ili kuwakumbatia wale tunaowapenda. Tunatazamia kwa hamu kuwa miongoni mwa wale wa Ufufuko wa Kwanza.
Tatu: Uzima wa milele humaanisha kuishi pamoja na Mungu na kama Yeye anavyoishi. Ni “kikuu katika vipawa vyote vya Mungu”22 na shangwe yao itakuwa tele milele.23 Ni kusudi na lengo la msingi la maisha yetu.
Nne: Wenzi wa mshiriki wa Uungu, Roho Mtakatifu, hutoa mwongozo unaohitajika sana na faraja wakati wa maisha ya duniani.24
Fikiria baadhi ya sababu za kutokuwa na furaha: taabu huja kutokana na dhambi,25 huzuni na upweke kutokana na kifo cha mpendwa, na hofu kutokana na kukosekana kwa uhakika wa kile kinachotokea tunapokufa. Lakini tunapoingia katika zizi la Mungu na kuyashika maagano yetu na Yeye, tunahisi amani ya kujua na kutumaini kwamba Kristo atatukomboa sisi kutokana na dhambi zetu, kwamba kutenganishwa kwa mwili wetu na roho kutaisha upesi sana, na kwamba tutaishi na Mungu milele katika namna ya utukufu sana.
Kumtumainia Kristo na Kutenda kwa Imani
Akina kaka na akina dada, maandiko yamejaa mifano ya ukuu wa nguvu za Mwokozi na huruma Yake yenye rehema na neema. Wakati wa huduma yake duniani, baraka Zake za uponyaji ziliwajia wale walio mtumainia Yeye na kutenda kwa imani. Kwa mfano, mtu asiyejiweza katika bwawa la Betheseda alitembea wakati, kwa imani yeye alifuata amri ya Mwokozi ya “simama, jitwike godoro lako, uende.”26 Wale waliokuwa wagonjwa au waliosumbuka kwa aina yo yote katika nchi ya Neema waliponywa wakati “kwa hiari” wao “walisonga mbele.”27
Vile vile, ili kupokea baraka hizi za ajabu zilizoahidiwa kwa wale ambao wanakuja ndani ya zizi la Mungu hutuhitaji sisi kufanya hivyo tu—tunahitaji kuchagua kuja. Alma Mdogo alifundisha, “Na sasa ninawaambia kwamba mchungaji mwema anawaita; na ikiwa mtaisikiliza sauti yake atawaleta katika zizi lake.”28
Miaka kadhaa iliyopita rafiki yangu mpendwa alifariki dunia kutokana na saratani. Wakati mke wake, Sharon, alipoandika kwa mara ya kwanza kuhusu uchunguzi wake wa ugonjwa, alisema: “Sisi Tulichagua Imani. Imani katika Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Imani katika mpango wa Baba yetu wa Mbinguni, na imani kwamba Yeye anajua mahitaji yetu na anatimiza ahadi Zake.”29
Nimekutana na Watakatifu wa Siku za Mwisho wengi kama Sharon ambao wanahisi amani ya ndani ya kuwa salama ndani ya zizi la Mungu, hasa wakati majaribu, upinzani, au dhiki inapokuja.30 Wao wamechagua kuwa na imani katika Yesu Kristo na kumfuata nabii Wake. Nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson amefundisha, “Kila kitu kizuri maishani—kila baraka inayowezekana ya umuhimu wa milele—huanza na imani.”31
Njoo Kikamilifu kwenye Zizi la Mungu
Babu wa babu wa babu yangu James Sawyer Holman alikuja Utah mwaka 1847, lakini yeye hakuwa miongoni mwa wale waliowasili mwezi Julai pamoja na Brigham Young. Alikuja baadaye mwaka huo na, kulingana kumbukumbu za familia, alikuwa na jukumu la kuwaleta kondoo. Hakufika Bonde la Salt Lake mpaka Oktoba, lakini yeye na kondoo walifika.32
Kuzungumza kiistairi, baadhi yetu bado tuko kwenye nyanda za tambarare. Si kila mtu anawasili katika kundi la kwanza. Marafiki zangu wapendwa, tafadhali endeleeni na safari—na wasaidieni wengine—kuja kikamilifu katika zizi la Mungu. Baraka za injili ya Yesu Kristo hazina kipimo kwa sababu ni za milele.
Ninayo shukrani kuu kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ninatoa ushahidi juu ya upendo wa Baba yetu wa Mbinguni na Mkombozi wetu, Yesu Kristo, na juu ya amani ambayo huja kutoka Kwao tu—amani ya ndani na baraka zinazopatikana katika zizi la Mungu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.