Hubiri Injili ya Amani
Tuna jukumu takatifu la kushiriki nguvu na amani ya Yesu Kristo na wale wote ambao watasikiliza.
Akina kaka na dada zangu wapendwa, karibuni kwenye mkutano mkuu! Nimetazamia siku hii kwa matarajio makubwa. Mimi husali kwa niaba yao kila siku. Pia nimesali kwamba mkutano huu utakuwa muda wa uhuishwaji wa kiroho kwa kila mmoja wenu.
Tangu mkutano uliopita, magumu ulimwenguni yameendelea. Janga la ulimwenguni kote bado linaathiri maisha yetu. Na sasa ulimwengu umeyumbishwa na vita ambavyo vinaleta hofu kwa mamilioni ya wanaume, wanawake, na watoto wasio na hatia.
Manabii waliona siku zetu ambapo kungekuwa na vita, na minong’ono ya vita, kwamba ulimwengu wote utakuwa katika ghasia.1 Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tunawasihi viongozi wa mataifa watafute suluhu za amani katika tofauti zao. Tunawaomba watu kila mahali waombe kwa ajili ya wale walio na huhitaji, kufanya kile wanachoweza kuwasaidia wenye dhiki, na kutafuta msaada wa Bwana kumaliza migogoro yoyote mikubwa.
Akina kaka na dada, injili ya Yesu Kristo kamwe haijahitajika zaidi kama ilivyo leo. Migogoro, mabishano vinakinzana na kila kitu ambacho Mwokozi alikisimamia na kukifundisha. Ninampenda Bwana Yesu Kristo na kushuhudia kwamba injili Yake ni suluhisho pekee la kudumu la amani. Injili Yake ni injili ya amani.2
Injili yake ndiyo jibu pekee wakati mioyo ya watu wengi wametishika kwa hofu.3 Hili inasisitiza haja ya haraka kwetu ya kufuata maelekezo ya Bwana kwa wafuasi Wake ya “kwenda … ulimwenguni mwote, na kuhubiri injili kwa kila kiumbe.”4 Tuna jukumu takatifu la kushiriki nguvu na amani ya Yesu Kristo na wale wote ambao watasikiliza na kuacha Mungu ashinde katika maisha yao.
Kila mtu ambaye ameshafanya maagano na Mungu ameahidi kuwatunza wengine na kuwatumikia wale walio na huhitaji. Tunaweza kuonesha imani katika Mungu na daima kuwa tayari kutoa jibu kwa wale wanaouliza kuhusu “tumaini lililo ndani [yetu].”5 Kila mmoja wetu ana jukumu katika kuikusanya Israeli.
Leo, ninahakikisha kwa dhati kwamba Bwana ameamuru kila mvulana mstahiki, na mwenye uwezo ajiandae kwa ajili ya na kutumikia misheni. Kwa wavulana Watakatifu wa Siku za Mwisho, huduma ya kimisionari ni jukumu la kikuhani. Ninyi wavulana mmeletwa katika muda huu wakati kusanyiko lililoahidiwa la Israeli linafanyika. Mnapotumikia misheni, mnashiriki katika jukumu muhimu katika tukio hili ambalo halijawahitokea!
Kwenu ninyi akina dada wenye uwezo, misheni pia ni kitu chenye nguvu, lakini ni fursa isiyo lazima kwenu. Sisi tunawapenda akina dada wamisionari na tunawaalika kwa moyo wote. Kile mnachochangia katika kazi hii ni kikubwa sana! Sali kujua kama Bwana angetaka utumikie misheni, na Roho Mtakatifu atakujibu katika moyo wako na akilini mwako.
Rafiki wapendwa, ninyi ni wa thamani kwa Bwana. Amewahifadhi mpaka sasa ili kusaidia kuikusanya Israeli. Maamuzi yako ya kutumikia misheni, iwe ni misheni ya kuhubiri au ya huduma, yatakubariki wewe na wengine wengi. Pia tunawaalika wanandoa wazee kutumikia wakati hali zinaporuhusu. Juhudi zao haziwezi kushushwa thamani.
Wamisionari wote wanafundisha na kushuhudia juu ya Mwokozi. Giza la kiroho katika ulimwengu hufanya nuru ya Yesu Kristo kuhitajika zaidi kuliko hapo awali. Kila mmoja anastahili fursa ya kujua kuhusu injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Kila mtu anastahili kujua wapi wanaweza kupata tumaini na amani ambayo “[inapita] uelewa wote.”6
Na mkutano huu uwe muda wa amani na karamu ya kiroho kwenu. Na mtafute na kupokea ufunuo binafsi wakati wa vipindi hivi, ni sala yangu katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.