Mkutano Mkuu
Kufundisha Kujitegemea kwa Watoto na Vijana
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


Kufundisha Kujitegemea kwa Watoto na Vijana

Acha tumfuate Mwokozi wetu, Yesu Kristo na injili Yake kwa kuwa wenye kujitegemea katika maisha yetu yote na kufundisha hili kwa watoto na vijana wetu.

Nitazungumza kuhusu kujitegemea na jinsi kunavyoweza kufundishwa kwa watoto na vijana. Kujitegemea kunaweza kufikiriwa kama mada kuu kwa ajili ya watu wazima. Nimepata kufahamu kwamba watu wazima wanaweza kuwa vizuri zaidi kwenye njia ya kuelekea kujitegemea wakati wanapokua wamefunzwa injili ya Yesu Kristo na wamefanyia mazoezi mafundisho na kanuni zake tangu utotoni na kama vijana nyumbani.

Kielelezo kizuri zaidi ni mfano mkuu wa maisha halisi. Wilfried Vanie, ndugu zake saba pamoja na mama yake walijiunga na Kanisa huko Abidjan, Ivory Coast, wakati alipokuwa na miaka sita. Alibatizwa alipokuwa na miaka minane. Baba yake, mtunza familia mkuu, alifariki wakati Wilfried akiwa na miaka kumi na moja.

Japokuwa alihuzunishwa na hali ya familia, Wilfried aliamua kuendelea na shule, kwa kutiwa moyo na mama yake na kwa msaada wa Kanisa. Alihitimu shule ya sekondari na kuhudumu misheni huko Ghana Cape Coast, ambapo alijifunza Kingereza. Baada ya misheni yake, alikwenda chuo kikuu na kupata diploma ya uhasibu na fedha. Japo ilikuwa vigumu kupata ajira kwenye sekta hii, alipata kazi kwenye sekta ya utalii na ukarimu.

Alianza kama mhudumu kwenye hoteli ya nyota tano, lakini matamanio yake ya kuwa bora yalimsukuma ajifunze zaidi mpaka akawa mpokea wageni anayezungumza lugha mbili mahala pale. Wakati hoteli mpya ilipofunguliwa, aliajiriwa kama mkaguzi wa usiku. Baadaye, alijiunga na BYU–Pathway ya Ulimwenguni kote na kwa sasa anajifunza kozi ili kupata cheti kwenye utalii na hoteli. Hamu yake ni siku moja kuwa meneja wa hoteli kubwa sana. Wilfried anaweza kumpa mahitaji mwenza wake wa milele na watoto wawili, vilevile kumsaidia mama yake na ndugu zake. Kwa sasa anahudumu Kanisani kama mshiriki wa baraza kuu la kigingi.

Kujitegemea maana yake ni “uwezo, msimamo na juhudi ya kukimu mahitaji muhimu ya kiroho na ya kimwili ya maisha kwa ajili ya mtu binafsi na familia.”1 Kujitahidi kuwa mwenye kujitegemea ni sehemu ya kazi yetu kwenye njia ya agano ambayo inatuongoza kurudi kwa Baba wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo. Itaimarisha imani yetu katika Yesu Kristo na kwa shangwe kutuunganisha Kwake kupitia maagano na ibada za wokovu na kuinuliwa. Kujitegemea ni fundisho la injili ya Yesu Kristo na si programu. Ni mchakato ambao hudumu maisha yote, wala si tukio.

Tunakuwa wenye kujitegemea katika maisha yetu yote kwa kukua katika nguvu ya kiroho, kuboresha afya ya mwili na hisia, kutafuta elimu na ajira yetu na kuwa waliojitayarisha kimwili.2 Je, jukumu hili limewahi kukamilika wakati wa maisha yetu? Hapana, ni mchakato wa maisha yote wa kujifunza, ukuaji na kufanya kazi. Kamwe haukomi; ni mchakato endelevu, wa kila siku.

Ni jinsi gani tunaweza kufundisha mafundisho na kanuni za kujitegemea kwa watoto na vijana wetu? Njia moja muhimu ni kutumia kanuni za programu ya maendeleo ya Watoto na Vijana. Wazazi na watoto hujifunza injili ya Yesu Kristo, hushiriki kwenye huduma na shughuli na hufanya kazi pamoja katika maeneo manne ya ukuaji binafsi ambayo ni ya kipekee kwa kila mtoto. Siyo tena programu ya maelekezo inayofanana kwa wote.

Kitabu cha Mwongozo cha Watoto kinasema: “Yesu alipokuwa na umri kama wako, Alijifunza na kukua. Wewe pia unajifunza na kukua. Maandiko yanasema: ‘Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.’ (Luka 2:52).”3 Andiko hili linamaanisha ukuaji na kujifunza katika kipengele cha kiroho, akimpendeza Mungu; kipengele cha kijamii, akiwapendeza wanadamu; kipengele cha kimwili, kimo; na kipengele cha akili, hekima. Maeneo haya ya ukuaji yanahusika kwetu sote bila kujali umri wetu. Ni wakati gani tunayafundisha? Katika Kumbukumbu la Torati 6:6–7 tunasoma:

“Na maneno haya, ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako:

“Nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.”

Tunayafundisha mambo haya kwa watoto kwa mifano yetu mizuri, tukifanya kazi na kuhudumu pamoja nao, tukijifunza maandiko na kufuata mafundisho ya Yesu Kristo kama yalivyofundishwa na manabii.

Nimesema kwamba kwenye programu ya maendeleo ya Watoto na Vijana, watoto huchagua malengo tofauti katika kila moja ya maeneo manne ya ukuaji. Ni muhimu kwamba wabuni malengo yao wenyewe kwenye kila eneo. Wazazi na viongozi wanaweza kufundisha, kushauri na kusaidia.

Kwa mfano, mjukuu wetu Miranda amehamasika kukua kiroho kwa kushiriki kwenye madarasa ya kila siku ya seminari ya mapema asubuhi. Alivutiwa kwa kusikia mawazo chanya kutoka kwa wanafunzi wengine wa seminari kwenye kata yake. Mama yake hana haja ya kumwamsha kwa ajili ya darasa. Peke yake, anaamka na kujiunga na mkutano kwa njia ya video kwa muda uliopangwa wa saa 12:20 asubuhi kwa sababu amekuza tabia njema ambazo zimemsaidia kufanya hivyo. Wazazi wangu waliniambia hivi karibuni kwamba Miranda sasa anazungumza sana wakati anapowatembelea, kwani amekua kwenye ujasiri binafsi. Haya ni masomo kwa ajili ya maisha na ukuaji yenye matokeo ya kuonekana.

Wazazi, bibi na babu, viongozi na marafiki wanasaidia kwenye ukuaji na maendeleo ya watoto. Akina kaka na dada waliojikita kwenye uhudumiaji, pamoja na viongozi wa ukuhani na vikundi saidizi vya kata, hutoa usaidizi. “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” linasema: “Kwa mpango mtakatifu, akina baba wanapaswa kusimamia familia zao katika upendo na utakatifu na wana jukumu la kukimu mahitaji ya maisha na ulinzi kwa familia zao. Akina mama wana jukumu la kimsingi kwa utunzaji wa watoto wao. Katika majukumu haya matakatifu, akina baba na mama wana wajibu wa kusaidiana mmoja kwa mwingine kama washiriki sawa. Ukoo unapaswa kutoa usaidizi pale unapohitajika.”4 Mstari huo wa mwisho unamaanisha bibi na babu, kati ya wengine.

Tunapohudumu Afrika Magharibi, mke wangu, Nuria, amefanya kazi kubwa kuhudumu na kubaki na muunganiko wa familia yetu na wajukuu kuvuka bahari. Anafanya hili kwa kutumia teknolojia. Anawasomea vitabu wajukuu wadogo. Anawafundisha wajukuu wakubwa wa kike mada kama vile hadithi ya familia yetu, sayansi, historia ya Puerto Rico, Makala za Imani na injili ya Yesu Kristo. Umbali siku hizi hauzuii kuunganika, kuwa sehemu ya, kuhudumu kwa, na kukifundisha kizazi kinachoinukia kuhusu familia zetu. Mimi pia hujumuika na Nuria pale ninapoweza ili kuwafundisha wajukuu zetu wa thamani, kuwapenda na kuwadekeza na kuwafanya wacheke.

Unapaswa kugundua mifanano yenye uvuvio kati ya programu ya Watoto na Vijana na kukuza kujitegemea. Maeneo manne ya ukuaji katika kila moja yanafanana. Nguvu ya kiroho kwenye kujitegemea inahusiana na kipengele cha kiroho kwenye Watoto na Vijana. Afya ya mwili na akili kwenye kujitegemea huunganika na vipengele vya kimwili na kijamii kwenye Watoto na Vijana. Elimu, ajira na kujiandaa kimwili kwenye kujitegemea hufanana na kipengele cha kiakili kwenye programu ya Watoto na vijana.

Katika kuhitimisha, acha tumfuate Mwokozi wetu Yesu Kristo na injili Yake kwa kuwa wenye kujitegemea katika maisha yetu yote na kufundisha hili kwa watoto na vijana wetu. Tunaweza kufanya hili vyema zaidi kwa

  1. kuwa mifano mizuri ya kuwahudumia wengine,

  2. kuishi na kufundisha mafundisho na kanuni za kujitegemea, na

  3. kutii amri ya kukuza kujitegemea kama sehemu ya injili ya Yesu Kristo.

Mafundisho na Maagano 104:15–16 inasema:

“Na ni madhumuni yangu kuwa niwapatie mahitaji watakatifu wangu, kwani vitu vyote ni mali yangu.

“Lakini haina budi kufanyika katika njia yangu mwenyewe; na tazama hii ndiyo njia ambayo Mimi, Bwana, nimeazimia kutoa mahitaji ya watakatifu wangu, ili maskini wapate kuinuliwa, na kwa njia hiyo matajiri hushushwa.”

Hili ni Kanisa la Yesu Kristo. Injili yake hubariki familia hapa duniani na milele yote. Inatuongoza katika maisha yetu pale tunapojitahidi kuwa familia za milele. Mimi najua hili ni kweli. Katika Jina la Yesu Kristo, amina.

Chapisha