Hisia Zetu Zote za Moyoni
Ikiwa tunataka Mwokozi atuinue juu, basi msimamo wetu Kwake na kwa injili Yake hauwezi kuwa wa kawaida au wa kipindi fulani tu.
Dhabihu Kwake
Siku chache tu kabla ya kutoa uhai wake kwa ajili yetu sisi, Yesu alikuwa hekaluni huko Yerusalemu, akitazama watu wakitia pesa kwenye sanduku la hazina hekaluni. “Matajiri wengi wakatia mengi,” lakini kisha, akaja mjane maskini, “akatia senti mbili.” Kilikuwa kiasi kidogo sana, isingefaa hata kuiwekea kumbukumbu.
Na bado kiasi hiki kilichoonekana kama mchango usio na matokeo yoyote kilimvutia Mwokozi. Kweli, kilimvutiwa sana kiasi kwamba “Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amini, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina:
“Maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.”1
Kwa zingatio hili moja rahisi, Mwokozi alitufundisha sisi jinsi matoleo yanavyopimwa katika ufalme Wake—na ni tofauti sana na njia tunayotumia kupima vitu. Kwa Bwana, thamani ya mchango haikupimwa kwa matokeo uliyonayo kwenye sanduku la hazina bali matokeo uliyonao kwenye moyo wa mtoaji.
Katika kumsifia huyu mjane mwaminifu, Mwokozi alitupatia sisi kiwango cha kupimia ufuasi wetu katika vyote vihusianavyo na hili. Yesu alifundisha kwamba matoleo yetu yaweza kuwa makubwa au yaweza kuwa madogo, lakini kwa namna yoyote ile, lazima yote yatoke moyoni.
Kanuni hii hutoa mwangwi katika ombi la nabii wa Kitabu cha Mormoni Amaleki: “Mje kwa Kristo, ambaye ni Mtakatifu wa Israeli, na mpokee wokovu wake, na nguvu za ukombozi wake. Ndio, njooni kwake, na mumtolee nafsi zenu zote kama sadaka kwake.”2
Lakini hili linawezekanaje? Kwa wengi wetu, kiwango hicho cha dhamira ya nafsi yetu yote kinaonekana vigumu kufikia. Tayari tumekwishajitahidi sana. Tunawezaje kuweka uwiano wa mahitaji mengi ya maisha yetu na matamanio yetu ya kutoa nafsi zetu zote kwa Bwana?
Pengine changamoto yetu ni kwamba tunafikiria uwiano inamaanisha kuugawa muda wetu sawa miongoni mwa mahitaji yetu yanayotuhitaji sana. Ukitazama kwa njia hii, kujitoa kwetu kwa Yesu Kristo kungekuwa moja ya mambo mengi tunayopaswa kuyapachika katika ratiba yetu yenye shughuli nyingi. Lakini pengine kuna njia nyingine ya kulitazama hili.
Uwiano: Kama Kuendesha Baiskeli
Mke wangu, Harriet, na mimi tunapenda kwenda kuendesha baiskeli kwa pamoja. Ni njia nzuri ya kufanya mazoezi pamoja lakini pia mkitumia muda kuwa pamoja. Wakati tunaendesha, wala sipumui kwa nguvu na sijisifii kupita kiasi, tunafurahia uzuri wa ulimwengu unaotuzunguka na tunakuwa na maongezi mazuri. Mara chache sana huwa tunajali kuweka uwiano kwenye baiskeli zetu. Tumekuwa tukiendesha kwa muda mrefu kiasi kwamba hatuhitaji kufikiria kuhusu hilo—imekuwa kawaida na halisi kwetu.
Lakini wakati nimtazamapo mtu akijifunza kuendesha baiskeli kwa mara ya kwanza, inanikumbusha kwamba siyo rahisi kujiweka katika uwiano wewe mwenyewe juu ya matairi yale mawili membamba. Inachukua muda. Inahitaji mazoezi. Inahitaji uvumilivu. Pengine hata kuanguka chini mara moja au mbili.
Zaidi ya yote, wote wanaofuzu kuwa na usawa kwenye baiskeli wanajifunza vidokezo hivi muhimu:
Usiangalie miguuni mwako.
Angalia mbele.
Macho yako yawe kwenye barabara mbele yako. Fokasi unakokwenda. Na endelea kunyonga. Kubaki kwenye uwiano ni kuhusu kwenda mbele.
Kanuni sawa na hizo hutumika inapokuja kwenye kutafuta uwiano katika maisha yetu kama wafuasi wa Yesu Kristo. Kugawa muda wako na nguvu miongoni mwa kazi zako nyingi muhimu itatofautiana kati ya mtu mmoja hadi mwingine na kutoka kipindi kimoja cha maisha hadi kingine. Lakini lengo letu kuu la pamoja, ni kufuata Njia ya Bwana wetu, Yesu Kristo, na kurejea kwenye uwepo wa mpendwa Baba Yetu wa Mbinguni. Lengo hili sharti libakie lisilobadilika na endelevu, bila kujali sisi ni akina nani na kile kinachotokea maishani mwetu.3
Inua: Kama Kurusha Ndege
Sasa, kwa wale waendesha baiskeli wenye uchu, kulinganisha ufuasi na kuendesha baiskeli kunaweza kuwa mfanano wenye kusaidia. Kwa wale ambao sio, msihofu. Ninao mfano mwingine ambao, nina hakika, kila mwanaume, mwanamke na mtoto wataweza kujifananisha nao.
Ufuasi, kama vitu vingi katika maisha, vinaweza pia kulinganishwa na kurusha ndege.
Je, umewahi kufikiria ilivyo ya kushangaza kwamba ndege kubwa ya abiria kweli inaweza kuondoka ardhini na kupaa? Je, ni kitu gani hasa kinachoziweka mashine hizi za kupaa ziendelee kupaa kwa madaha angani, zikivuka bahari na mabara?
Jibu rahisi ni, ndege inapaa tu wakati hewa inapotembea juu ya mabawa yake. Mwendo huo wa hewa huleta tofauti katika msukumo wa hewa ambao huipaisha ndege. Na ni kwa jinsi gani unapata hewa ya kutosha kutembea juu ya mabawa ili kuipaisha? Jibu ni msukumo wa mbele.
Kwa vyovyote ndege haitainuka ikiwa imesimama tu juu ya barabara ya kukimbilia. Hata katika siku ya upepo mwingi, upaaji hautokei hadi ndege iwe inaenda mbele, ikiwa na msukumo wa kutosha ili kukinzana na nguvu zinazoizuia isiende mbele.
Kama vile tu nguvu mwendo ya kwenda mbele inavyoiweka baiskeli kwenye uwiano na wima, kwenda mbele kunaisaidia ndege kushinda kuvutwa na mvutano na kuzuiwa.
Hii ina maana gani kwetu sisi kama wafuasi wa Yesu Kristo? Inamaanisha kwamba kama tunataka kupata uwiano katika maisha, na kama tunataka Mwokozi atuinue kuelekea mbinguni, basi dhamira zetu Kwake na kwa injili Yake haviwezi kuwa vya kawaida tu au muda. Kama yule mjane huko Yerusalemu, ni lazima tumtolee nafsi zetu zote. Matoleo yetu yaweza kuwa madogo, lakini ni lazima yatoke moyoni na nafsini mwetu.
Kuwa mfuasi wa Yesu Kristo siyo tu ni moja ya vitu vingi tunavyofanya. Mwokozi ndiye nguvu ituhamasishayo nyuma ya vyote tunavyofanya. Yeye siyo kituo cha kupumzika katika safari yetu. Yeye siyo mandhari nzuri njiani au alama kubwa. Yeye ni “njia, kweli na uzima: mtu haji kwa Baba”, bali kwa njia ya [Yesu Kristo].”4 Hiyo ndiyo njia na hatma yetu ya milele.
Uwiano na kupaa huja sisi tunapokuwa “tunasonga mbele kwa bidii katika Kristo, tukiwa na tumaini angavu, na upendo wa Mungu na watu wote.”5
Dhabihu na Wakfu
Na vipi kuhusu kazi nyingi na majukumu ambayo hufanya maisha yetu kuwa na shughuli nyingi? Kutumia muda na wapendwa wetu, kwenda shule au kujiandaa kwa ajili ya ajira, kupata riziki, kutunza familia, kuhudumu katika jumuiya—hivi vyote vinaingia wapi? Mwokozi anatuhakikishia:
“Kwani Baba yenu wa mbinguni anajua kwamba mna mahitaji ya hivi vitu vyote.
“Lakini utafuteni kwanza ufalme wa Mungu na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa.”6
Lakini hii haimaanishi kwamba ni rahisi.7 Inahitaji vyote dhabihu na wakfu.
Inahitaji kuachia baadhi ya vitu viende na kuruhusu baadhi ya vitu vikue.
Dhabihu na Wakfu ni sheria mbili za mbinguni ambazo tunaagana kuzitii katika hekalu takatifu. Sheria hizi mbili zinafanana lakini haziko sawa. Kutoa dhabihu inamaana kuachana na kitu fulani kwa ajili ya kitu chenye thamani kubwa zaidi. Hapo kale, watu wa Mungu walitoa dhabihu ya wanyama wazaliwa wa kwanza wa mifugo yao kwa heshima ya Masiya ajaye. Katika historia yote, Watakatifu waaminifu wametoa dhabihu ya matamanio binafsi, faraja na hata maisha yao kwa ajili ya Mwokozi.
Sote tunavyo vitu, vikubwa na vidogo, tunahitaji kuvitoa dhabihu ili kumfuata Yesu Kristo kikamilifu zaidi.8 Dhabihu zetu zinaonyesha kwa hakika kile tunachokithamini. Dhabihu ni takatifu na zinaheshimika na Bwana.9
Wakfu ni tofauti na dhabihu kwa angalau njia moja muhimu. Wakati tunapoweka wakfu kitu, hatukiachi ili kiliwe madhabahuni. Badala yake, tunakiweka kitumike katika huduma ya Bwana. Tunakiweka kitu hicho wakfu kwa Bwana na makusudi Yake matakatifu.10 Tunapokea talanta ambazo Bwana ametupatia na tunajitahidi kuzikuza, kuzifunua, kuwa hasa wenye kusaidia katika kujenga ufalme wa Bwana.11
Wachache sana kati yetu wataombwa kutoa dhabihu maisha yetu kwa ajili ya Mwokozi. Lakini sisi sote tumealikwa kuweka wakfu maisha yetu kwa ajili Yake.
Kazi Moja, Shangwe Moja, Kusudi Moja
Tunapotafuta kutakasa maisha yetu na kumwangalia Kristo katika kila wazo,12 kila kitu kingine kinaanza kuwa sawa. Maisha hayaonekani tena kuwa kama orodha ndefu ya juhudi tofauti zilizoshikiliwa kwenye uwiano dhaifu
Baada ya muda, zote zinakuwa kazi moja.
Shangwe Moja.
Kusudi moja takatifu.
Ni kazi ya kumpenda na kumtumikia Mungu. Ni kuwapenda na kuwatumikia watoto wa Mungu.13
Tunapotazama maisha yetu na kuona mamia ya vitu vya kufanya, tunahisi kuzidiwa. Tunapoona kitu kimoja—kumpenda na kumtumikia Mungu na watoto Wake, katika njia mia moja tofauti—kisha tunaweza kufanyia kazi vitu hivyo kwa shangwe.
Hivi ndivyo tunavyotoa nafsi zetu zote—kwa kutoa dhabihu kitu chochote kinachotuzuia sisi na kuweka wakfu vinavyobakia kwa Bwana na makusudi Yake.
Neno la Kutia Moyo na Ushuhuda
Kaka na dada zangu wapendwa na marafiki zangu wapendwa, kutakuwa na nyakati ambapo ungetamani kufanya zaidi. Mpendwa Baba yako wa Mbinguni anajua moyo wako. Yeye anajua huwezi kufanya kila kitu moyo wako unachotaka ufanye. Lakini unaweza kumpenda na kumtumikia Mungu. Unaweza kufanya kadiri uwezavyo kutii amri zake. Unaweza kuwapenda na kuwatumikia watoto Wake. Na jitihada zako zinautakasa moyo wako na kukutayarisha wewe kwa ajili ya kesho tukufu.
Hiki ndicho yule mjane kwenye sanduku la hazina ya hekaluni alionekana kuelewa. Hakika alijua kwamba matoleo yake yasingebadili utajiri wa Israeli, lakini yangembadilisha na kumbariki yeye—kwa sababu, ingawa ni kidogo, ilikuwa riziki yake yote.
Hivyo, marafiki zangu wapendwa na wafuasi wenzagu wa Yesu Kristo, “tusichoke kutenda mema,” kwa kuwa “tunaijenga misingi ya kazi kubwa.” Na kutokana na mambo yetu madogo huja “yale yaliyo makuu.”14
Ninashuhudia kwamba hii ni kweli, kama vile ninavyoshuhudia pia kuwa Yesu Kristo ni Bwana Wetu, Mkombozi wetu na Njia yetu pekee ya kurudi kwa mpendwa Baba yetu wa Mbinguni. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.