Mkutano Mkuu
Upendo Mtakatifu katika Mpango wa Baba
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


14:47

Upendo Mtakatifu katika Mpango wa Baba

Dhumini la mafundisho na sera za Kanisa hili la urejesho ni kuwatayarisha watoto wa Mungu kwa ajili ya wokovu katika ufalme wa selestia pamoja na kuinuliwa katika daraja la juu kabisa.

Mpango wa injili unaonyesha upendo wa Baba yetu wa Mbinguni kwa watoto Wake wote. Ili kuelewa hili, tunapaswa kutafuta kuelewa mpango Wake na amri Zake. Anawapenda sana watoto Wake kiasi kwamba alimtoa Mwanaye wa pekee, Yesu Kristo, kuwa Mwokozi na Mkombozi wetu, kuteseka na kufa kwa ajili yetu. Katika Kanisa la urejesho la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za mwisho, tuna uelewa wa kipekee wa mpango wa Baba yetu wa Mbinguni. Hii inatupatia njia tofauti ya kuangalia azma ya maisha haya ya duniani, hukumu takatifu ambayo inafuata, na hatma ya majaliwa ya watoto wote wa Mungu.

Ninawapenda, kaka na dada zangu. Ninawapenda watoto wote wa Mungu. Wakati Yesu alipoulizwa, “Ni amri gani iliyo kuu katika sheria?” Alifundisha kwamba kumpenda Mungu na kuwapenda jirani zetu ni amri za kwanza kuu za Mungu.1 Amri hizo ni za kwanza kwa sababu zinatualika sisi kukua kiroho kwa kutafuta kuiga upendo wa mungu kwa ajili yetu. Natamani sote tungekuwa na uelewa mzuri wa mafundisho ya upendo na sera ambazo Baba yetu wa Mbinguni na Mwanaye, Yesu Kristo, wamezianzisha katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Kile ninachosema hapa kina kusudi la kufafanua jinsi upendo wa Mungu unavyoelezea mafundisho hayo na sera hizo za Kanisa zenye uvuvio.

I.

Uelewa wa kawaida wa hukumu ambayo hatimaye inafuatia maisha ya kufa ni kwamba watu wema wanakwenda sehemu inayoitwa mbinguni na watu wabaya wanakwenda kwenye sehemu ya kudumu inayoitwa jehanamu. Dhana hii isiyo sahihi ya hatma mbili tu za mwisho inadokeza kwamba wale wasioweza kutii amri zote zinazohitajika kwa ajili ya kwenda mbinguni watalazimika kwenda jehanamu milele.

Baba wa Mbinguni mwenye upendo ana mpango mzuri zaidi kwa ajili ya Watoto Wake. Mafundisho yaliyofunuliwa ya Kanisa la Urejesho la Yesu Kristo yanafundisha kwamba watoto wote wa Mungu—pamoja na wachache sana kuwafikiria hapa—hatimaye wataishia katika ufalme wa utukufu.2 “Nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi,”3 Yesu alifundisha. Kutokana na ufunuo wa siku za leo tunajua kwamba makao hayo yapo katika falme tatu tofauti za utukufu. Katika hukumu ya mwisho kila mmoja wetu atahukumiwa kulingana na matendo na matamanio ya mioyo yetu.4 Kabla ya hiyo, tutahitajika kuteseka kwa ajili ya dhambi zetu tusizotubu. Maandiko yako wazi juu ya hilo.5 Kisha Hakimu wetu mwenye haki ataturuhusu kukaa katika mojawapo ya falme hizo za utukufu. Hivyo, kama tunavyojua kutokana na ufunuo wa siku za leo, sote “tutahukumiwa … na kila mtu atapokea kulingana na matendo yake, utawala wake, katika makao yaliyotayarishwa.”6

Bwana amechagua kufunua kwa kulinganisha kidogo kuhusu mbili za falme hizi za utukufu. Kinyume chake, Bwana amefunua mengi kuhusu ufalme wa juu kabisa wa utukufu, ambao Biblia inauelezea kama “utukufu wa jua.”7

Katika utukufu wa “selestia”8 kuna falme au madaraja matatu.9 Iliyo juu zaidi ya hizi ni kuinuliwa kwenye ufalme wa selestia, ambapo tunaweza kuwa kama Baba yetu na Mwanaye, Yesu Kristo. Ili kutusaidia kukuza sifa za kiungu na kubadilika katika asili iliyo muhimu kutambua uwezekano wetu mtakatifu, Bwana amefunua mafundisho na ameanzisha amri zenye msingi wa sheria ya milele. Hiki ndicho tunachofundisha katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa sababu azma ya mafundisho na sera za Kanisa hili la urejesho ni kuwatayarisha watoto wa Mungu kwa ajili ya wokovu katika utukufu wa selestia na, zaidi hasa, kwa ajili ya kuinuliwa katika daraja la juu kabisa.

Maagano yaliyofanywa na baraka zilizoahidiwa kwa waaminifu katika mahekalu ya Mungu ni msingi. Hii inafafanua ujengaji wetu wa mahekalu ulimwenguni kote, ambayo kwaya imeimba vizuri kuyahusu. Baadhi wameshangazwa kwa mkazo huu, bila kuelewa kwamba maagano na ibada za hekaluni zinatuongoza kuelekea kufikia kuinuliwa. Hii inaweza tu kueleweka katika muktadha wa ukweli uliofuniliwa wa madaraja matatu ya utukufu. Kwa sababu ya upendo mkuu wa Baba yetu wa Mbinguni kwa watoto Wake wote, Yeye ametoa falme zingine za utukufu—kama Mzee Quentin L. Cook alivyofafanua jana—zote ambazo ni za kupendeza zaidi kuliko tunavyoweza kudhani.10

Upatanisho wa Yesu Kristo unafanya haya yote yawezekane. Amefunua kwamba Yeye “anamtukuza Baba, na kuokoa kazi zake zote za mikono yake.”11 Wokovu huo umetolewa katika falme tofauti za utukufu. Tunajua kutokana na ufunuo wa siku za leo kwamba “falme zote zinayo sheria zilizotolewa.”12 Kwa umuhimu:

“Kwani yule ambaye hawezi kuishi kwa sheria ya ufalme wa selestia hawezi kustahimili katika utukufu wa selestia.

“Na yule asiyeweza kuishi kwa sheria ya ufalme wa terestria hawezi kustahimili utukufu wa terestria.

“Na yule asiyeweza kuishi kwa sheria ya ufalme wa telestia hawezi kustahimili utukufu wa telestia.”13

Kwa maneno mengine, ufalme wa utukufu tunaoupokea katika Hukumu ya Mwisho unaamuliwa na sheria tunazochagua kuzishika katika mpango wa upendo wa Baba yetu ya Mbinguni. Ndani ya mpango huo kuna falme nyingi ili kwamba watoto Wake wote waweze kupangiwa kwenye ufalme ambao wanaweza “kuishi.”

II.

Mafundisho na sera za Kanisa la urejesho la Bwana hutumia kweli hizi za milele kwa njia ambayo inaweza kueleweka kikamilifu katika muktadha pekee wa mpango wa upendo wa Baba yetu wa Mbinguni kwa ajili ya watoto Wake wote.

Hivyo, tunaheshimu haki binafsi ya kujiamulia. Wengi wanafahamu kuhusu juhudi kubwa za Kanisa hili kusaidia kuwepo kwa uhuru wa kidini. Juhudi hizi ni katika kusongesha mpango wa Baba yetu wa Mbinguni. Tunatafuta kuwasaidia watoto Wake wote—si tu waumini wetu pekee—kufurahia tunu ya haki ya kujiamulia.

Vile vile, wakati mwingine huwa tunaulizwa ni kwa nini tunawatuma wamisionari katika mataifa mengi, hata miongoni mwa idadi kubwa ya Wakristo. Pia tunaulizwa kwa nini tunatoa misaada mikubwa ya kibinadamu kwa watu ambao si waumini wa Kanisa letu bila kuunganisha hili kwenye juhudi zetu za umisionari. Tunafanya hivi kwa sababu Bwana ametufundisha kuwachukulia watoto Wake wote kama kaka zetu na dada zetu, na tunataka kushiriki utajiri wetu wa kiroho na kimwili kwa kila mmoja.

Mafundisho ya milele pia yanatoa mtazamo wa kipekee kwa watoto. Kupitia mtazamo huu tunaona uzazi na ulezi wa watoto kama sehemu ya mpango mtakatifu. Ni jukumu la furaha na takatifu kwa wale waliopewa uwezo wa kushiriki katika hilo. Kwa hivyo, tumeamriwa kufundisha na kutetea kanuni na matendo ambayo yanatoa hali bora zaidi kwa ajili ya maendeleo na furaha ya watoto chini ya mpango wa Mungu.

III.

Mwishowe, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linajulikana vyema kama Kanisa lenye kiini chake kwenye familia. Lakini kile kisichoeleweka vyema ni ukweli kwamba kiini chetu kwenye familia hakiishii kwenye mahusiano ya maisha ya hapa duniani. Mahusiano ya milele pia ni msingi katika thiolojia yetu. Kazi ya Kanisa la urejesho ni kuwasaidia watoto wote wa Mungu kustahili kwa kile Mungu anachotamani kama hatma yao ya mwisho. Kwa ukombozi unaotolewa kupitia Upatanisho wa Kristo, wote waweze kupata uzima wa milele (kuinuliwa katika ufalme wa selestia), ambao Mama Hawa alitangaza “Mungu huutoa kwa wote walio watiifu.”14 Hii ni zaidi ya wokovu. Rais Russell M. Nelson ametukumbusha kwamba “katika mpango wa milele wa Mungu, wokovu ni suala binafsi, [lakini] kuinuliwa ni suala la familia.”15

Muhimu kwetu sisi ni ufunuo wa Mungu kwamba kuinuliwa kunaweza kufikiwa kupitia tu uaminifu kwenye maagano ya ndoa ya milele kati ya mwanamume na mwanamke.16 Mafundisho hayo matakatifu ndiyo sababu tunafundisha kwamba “jinsia ni hulka muhimu ya utambuzi wa milele wa maisha kabla ya maisha ya duniani, maisha ya duniani na utambulisho na lengo la milele.”17

Hiyo ndiyo sababu Bwana pia ametaka Kanisa Lake la urejesho kupinga mashinikizo ya kijamii na kisheria ya kukimbia kutoka mafundisho ya Bwana ya ndoa kati ya mwanamume na mwanamke, kupinga mabadiliko ambayo yanakanganya au kubadili jinsia au kuondoa tofauti kati ya wanamume na wanawake.

Misimamo ya Kanisa lililorejeshwa juu ya kweli hizi mara kwa mara huchochea upinzani. Tunalielewa hilo. Mpango wa Baba yetu wa Mbinguni huruhusu “upinzani katika vitu vyote,”18 na upinzani mkali wa Shetani umeelekezwa kwenye kile kilicho muhimu zaidi kwenye mpango huo. Kwa hiyo, anatafuta kupinga maendeleo kuelekea kuinuliwa kwa kukanganya jinsia, kuharibu ndoa, na kupinga uzaaji wa watoto. Hata hivyo, tunajua kwamba mwishowe, azma takatifu na mpango wa Baba yetu wa Mbinguni mwenye upendo hautabadilishwa. Hali binafsi zinaweza kubadilika, na mpango wa Mungu unahakikisha kwamba mwishoni, waaminifu ambao wanashika maagano yao watakuwa na fursa za kustahili kila baraka iliyoahidiwa.19

Mafundisho ya thamani ya kipekee ya kutusaidia kujitayarisha kwa ajili ya uzima wa milele, “kipawa ambacho ni kikuu katika vipawa vyote vya Mungu,”20 ni tangazo kwa familia la mwaka 1995.21 Matamko yake, hakika, ni tofauti na sheria, mila, na utetezi wa sasa, kama vile kuwekana kinyumba na ndoa ya jinsia moja. Wale ambao hawauelewi kikamilifu mpango wa upendo wa Baba kwa ajili ya watoto Wake wanaweza kufikiria tangazo hili la familia si zaidi ya maelezo ya sera ambazo zinapaswa kubadilishwa. Kinyume chake, tunathibitisha kwamba tangazo kwa familia, lililopatikana kutokana na mafundisho yasiyobadilika, linafafanua aina ya mahusiano ya familia ambapo sehemu muhimu sana ya maendeleo yetu ya milele inaweza kutokea.

Huo ndio muktadha kwa ajili ya mafundisho ya kipekee na sera za Kanisa la urejesho la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

IV.

Katika mahusiano mengi na hali nyingi za mambo katika maisha ya duniani, kila mmoja wetu lazima aishi kwa tofauti mbalimbali. Kama wafuasi wa Kristo tunaopaswa kuwapenda binadamu wenzetu, tunapaswa kuishi kwa amani na wale ambao hawaamini kama tunavyoamini. Sisi sote ni watoto wa Baba wa Mbinguni mwenye upendo. Kwetu sisi sote , Amekusudia maisha baada ya kifo na hatimaye, ufalme wa utukufu. Mungu anatamani sisi sote tujitahidi kwa ajili ya baraka zake za juu zinazowezekana kwa kutii amri Zake, maagano, na ibada za juu, vyote ambavyo vinafikia kilele katika mahekalu Yake matakatifu yanayojengwa ulimwenguni kote. Ni lazima tutafute kushiriki kweli hizi za milele pamoja na wengine. Lakini pamoja na upendo tunaodaiwa kwa majirani zetu wote, siku zote tunakubali maamuzi yao. Kama nabii wa Kitabu cha Mormoni alivyofundisha, lazima tusonge mbele, tukiwa na “upendo kwa Mungu na kwa wanadamu wote.”22

Kama Rais Russell M. Nelson alivyotangaza katika mkutano wetu mkuu uliopita, “Hakujawahi kuwepo na kipindi katika historia ya ulimwengu wakati elimu ya Mwokozi wetu ni yenye umuhimu binafsi na yenye kufaa kwa kila nafsi ya mwanadamu kama sasa. Injili halisi ya Kristo ina nguvu. Inabadilisha maisha ya kila mtu ambaye anaielewa na kutafuta kuitekeleza katika maisha yake.23

Ili kwamba sote tuweze kutekeleza mafundisho hayo matakatifu katika maisha yetu wenyewe, ninaomba katika jina la Yesu Kristo, amina.