Mkutano Mkuu
Badiliko Kuu la Moyo: “Sina Cha Kukupa Zaidi”
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


10:57

Badiliko Kuu la Moyo:

“Sina Cha Kukupa Zaidi”

Badiliko hili la moyo sio tukio; huhitaji imani, toba, na kazi ya kila mara ya kiroho kufanyika.

Utangulizi

Mnamo Ijumaa, Oktoba 28, 1588, ikiwa imepoteza usukani wake kwa kutawaliwa tu na makasia, meli hiyo La Girona, mali ya Meli kubwa ya Kihispania, iligongana na miamba ya Lacada Point huko Ireland Kaskazini.1

Meli hiyo ilizama. Mmoja wa wahanga waliokuwa wakihangaika kuishi alivaa pete ya dhahabu aliyopewa miezi michache mapema na mkewe iliyokuwa na maandishi, “Sina cha kukupa zaidi.”2

“Sina cha kukupa zaidi,” kirai, na pete yenye muundo wa mkono unaoshikilia moyo, onyesho la upendo kutoka kwa mke kwa mumewe.

Muunganisho wa Maandiko

Niliposoma hadithi hii, ilinigusa sana, na nikafikiria juu ya ombi lililotolewa na Mwokozi: “Nanyi mtatoa dhabihu kwangu moyo uliovunjika na roho iliyopondeka.”3

Pia nilipofikiria majibu ya watu kwa maneno ya Mfalme Benyamini: “Ndiyo, tunaamini maneno yote ambayo umetuzungumzia … , ambayo yameleta mabadiliko makuu ndani yetu, au mioyoni mwetu, hata kwamba hatuna tamaa ya kutenda maovu tena, lakini kutenda mema daima.”4

Muunganiko wa Kibinafsi

Acha nishiriki nanyi uzoefu niliopata nilipokuwa na umri wa miaka 12, na athari ambazo zimedumu mpaka leo.

Mama yangu alisema, “Eduardo, fanya haraka. Tumechelewa kwa mikutano ya kanisa.”

“Mama, nitabaki na baba leo,” nilijibu.

“Una hakika? Unapaswa uhudhurie mkutano wako wa akidi ya ukuhani,” alisema.

Nilijibu, Maskini Baba! Ataachwa peke yake. Nitabaki naye leo.”

Baba hakuwa mshiriki wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho

Mama na dada zangu walienda kwenye mikutano ya Jumapili. Kwa hiyo, nilikwenda kukutana na Baba kwenye karakana yake, ambako alipenda kuwa siku ya Jumapili, na kama nilivyomwambia mama yangu, nilikaa naye muda, yaani, dakika chache naye, kisha nikamuuliza, “Baba! kila kitu sawa?”

Aliendelea na shughuli yake ya kutengeneza redio na saa, na alinitabasamu tu.

Kisha nikamwambia, “Nitaenda kucheza na marafiki zangu.”

Baba, bila kuangalia juu, aliniambia, “Leo ni Jumapili. Je, hutakiwi kwenda kanisani?”

“Ndiyo, lakini leo nimemwambia mama sitaenda,” nilimjibu. Baba aliendelea na shughuli zake, na kwangu, hiyo ilikuwa ruhusa ya kuondoka.

Asubuhi hiyo kulikuwa na mchezo muhimu wa soka, na marafiki zangu walikuwa wameniambia singeweza kukosa, na kwamba tulipaswa kushinda mchezo huo.

Changamoto yangu ilikuwa kwamba nililazimika kupita mbele ya kanisa ili kufika uwanja wa soka.

Nikiwa nimedhamiria, nilikimbia kuelekea uwanja wa soka na kusimama mbele ya kikwazo kikubwa, kanisa. Nilikimbia kuelekea upande wa pili wa barabara, ambapo kulikuwa na miti mikubwa, na niliamua kukimbia katikati yake ili mtu hasinione kwani ni muda ambao waumini walikuwa wanafika kwenye mikutano.

Nilifika kwa wakati wa kuanza kwa mchezo. Niliweza kucheza na kurudi nyumbani kabla ya mama yangu kufika nyumbani.

Kila kitu kilikuwa kimeenda vizuri; timu yetu ilikuwa imeshinda, na nilifurahi. Lakini mbio hizo zilizotekelezwa vyema uwanjani hazikupuuzwa na mshauri wa akidi ya mashemasi.

Kaka Félix Espinoza alikuwa ameniona nikikimbia upesi kutoka mti hadi mti, nikijaribu nisionekane.

Mwanzoni mwa juma, kaka Espinoza alikuja nyumbani kwetu na kuomba kuzungumza nami. Hakusema lolote kuhusu yale aliyokuwa ameona Jumapili, wala hakuniuliza kwa nini nilikuwa nimekosa mkutano wangu.

Alinipatia kitabu cha kiada na kusema, “Ningependa ufundishe darasa la ukuhani siku ya Jumapili. Nimetia alama somo hilo kwa ajili yako. Si gumu sana. Ninataka wewe usome, na nitakuja baada ya siku mbili kukusaidia na maandalizi ya somo. Baada ya kusema haya, alinipa kitabu cha kiada na kuondoka.

Sikutaka kufundisha darasa, lakini nisingeweza kumwambia hapana. Nilikuwa nimepanga Jumapili hiyo nikae na baba tena—maana, kulikuwa na mchezo wa soka mwingine muhimu.

Kaka Espinoza alikuwa mtu ambaye vijana walimpenda.5 Alikuwa amepata injili iliyorejeshwa na kubadilisha maisha yake au, kwa maneno mengine, moyo wake.

Jumamosi alasiri ilipofika, nilifikiri, “Vema, labda kesho nitaamka nikiwa mgonjwa, na sitalazimika kwenda kanisani.” Haukuwa mchezo wa soka ambao ulinitia wasiwasi tena; lilikuwa ni darasa nililopaswa kufundisha, hasa somo kuhusu siku ya Sabato.

Jumapili ilikuja, na niliamka nikiwa na afya njema kuliko hapo awali. Sikuwa na kisingizio—wala pa kutorokea.

Ilikuwa mara ya kwanza ningefundisha somo, lakini Kaka Espinoza alikuwa karibu nami, na hiyo ilikuwa siku ya badiliko kubwa la moyo kwangu.

Kuanzia wakati huo na kuendelea, nilianza kuitakasa siku ya Sabato, na baada ya muda, katika maneno ya Rais Nelson, siku ya Sabato imekuwa ya furaha.6

“Bwana, ninakupa kila kitu; sina cha kukupa zaidi.”

Kupata

Je, tunapataje badiliko hilo kuu la moyo? Huanzishwa na hatimaye hutokea

  1. tunapojifunza maandiko ili kupata maarifa ambayo yataimarisha imani yetu katika Yesu Kristo ambayo yataleta hamu ya kubadilika.7

  2. tunapokuza tamaa hiyo kwa maombi na kufunga.8

  3. tunapotenda, kulingana na neno lililosomwa au tulilopokea, na tunafanya agano la kusalimisha mioyo yetu Kwake, kama tu kwa watu wa Mfalme Benyamini.9

Utambuzi na Agano

Tunajuaje kwamba moyo wetu unabadilika?10

  1. Tunapotaka kumpendeza Mungu katika mambo yote.11

  2. Tunapowatendea wengine kwa upendo, heshima, na wema.12

  3. Tunapoona kwamba sifa za Kristo zinakuwa sehemu ya tabia zetu.13

  4. Tunapohisi mwongozo wa Roho Mtakatifu zaidi kila mara.14

  5. Tunaposhika amri ambayo imekuwa ngumu kwetu kutii na kisha kuendelea kuiishi.15

Tunaposikiliza kwa makini ushauri wa viongozi wetu na kuamua kuufuata kwa moyo mkunjufu, je, hatujapata mabadiliko makubwa ya moyo?

“Bwana, ninakupa kila kitu; sina cha kukupa zaidi.”

Udumishaji na Faida

Je, tunadumishaje hili badiliko kuu?

  1. Tunaposhiriki sakramenti kila juma na kufanya upya agano la kuchukua juu yetu jina la Kristo, daima kumkumbuka, na kuzishika amri Zake.16

  2. Tunapogeuza maisha yetu kuelekea hekalu.17 Kuhudhuria hekaluni kila mara kutatusaidia kudumisha moyo mpya na kufanywa upya tunaposhiriki katika ibada.

  3. Tunapowapenda na kuwatumikia jirani zetu kwa shughuli za uhudumiaji na kazi ya ummisionari.18

Kisha kwa furaha yetu kuu, hilo badiliko la ndani linaimarishwa na kuenea mpaka linazidi katika matendo mema.19

Badiliko hili kuu la moyo hutuletea hisia ya uhuru, uaminifu, na amani.20

Badiliko hili la moyo sio tukio; huhitaji imani, toba, na kazi ya kila mara ya kiroho kufanyika. Huanza tunapotamani kuwasilisha mapenzi yetu kwa Bwana, na hutokea tunapoingia na kuweka maagano Naye.

Hatua hiyo ya mtu binafsi ina matokeo chanya kwetu na kwa watu walio karibu nasi.

Kwa maneno ya Rais Russell M. Nelson, “Fikiria jinsi upesi haya mapigano ya uharibifu ulimwenguni kote—na yale katika maisha yetu binafsi—yangetatuliwa kama sisi sote tukichagua kumfuata Yesu Kristo na kusikiliza mafundisho Yake.”21 Tendo hili linalofuata mafundisho ya Mwokozi linaongoza kwa badiliko kuu la moyo.

Wapendwa akina kaka na akina dada, vijana, na watoto, tunaposhiriki katika mkutano mkuu wikendi hii, acha maneno ya manabii wetu, ambayo yatakuja kutoka kwa Bwana, yaingie mioyoni mwetu ili tupate badiliko kuu.

Kwa wale ambao bado hawajajiunga na Kanisa la Bwana lililorejeshwa, ninawaalika kuwasikiliza wamisionari kwa hamu ya kweli ya kujua kile ambacho Mungu anatarajia kutoka kwako na kupata mabadiliko hayo ya ndani.22

Leo ni siku ya kuamua kumfuata Bwana Yesu Kristo. “Bwana, ninakupa wewe, moyo wangu; sina cha kukupa zaidi.”

Kama vile pete iliyopatikana kutoka kwa ajali hiyo ya meli, tunapotoa mioyo yetu kwa Mungu, tunaokolewa kutoka kwa machafuko ya bahari ya maisha haya, na katika mchakato huo, tunasafishwa na kutakaswa kupitia kwa Upatanisho wa Kristo na kuwa “watoto wa Kristo” kwa kuwa “tumezaliwa Naye” kiroho.23 Juu ya hili ninashuhudia katika jina la Yesu Kristo, amina.