Sabato ni Siku ya Furaha
Unaweza kuhakikisha vipi kwamba tabia yako katika Sabato italeta furaha na shangwe?
Wapendwa akina kaka na dada, siku hizi mbili za mkutano zimekuwa nzuri. Tumeinuliwa kwa muziki mzuri na maombi mazuri. Roho zetu zimekuzwa kwa ujumbe wenye nuru na kweli. Katika Jumapili hii ya Pasaka, tunaungana kumshukuru Mungu kwa ajili ya nabii!
Swali kwa kila mmoja wetu ni: kwa sababu ya yale niliyoyasikia na kuhisi wakati wa mkutano huu, nitabadilikaje? Bila kujali jibu lako, naomba nikualike kutafakari hisia zako juu ya, na tabia zako katika, siku ya Sabato.
Ninafurahishwa na maneno ya Isaya, aliyeiita Sabato siku ya “ furaha.”1 Hata hivyo nashangaa, ni kweli Sabato ni furaha kwako na kwangu?
Kwanza nilipata furaha katika siku ya Sabato miaka mingi iliyopita wakati, nikiwa daktari mpasuaji, siku ya Sabato ilikuwa ni siku yangu ya kupumzika. Mwishoni mwa kila wiki, mikono yangu ilikuwa ikiuma kwa sababu ya kuisugua kwa sabuni, maji na burashi kila mara. Pia nilihitaji kupumzika toka kwenye kazi nzito. Jumapili ilileta nafuu niliouhitaji sana.
Mwokozi alikuwa na maana gani pale Aliposema “sabato iliwekwa kwa ajili ya mwanadamu, na si mwanadamu kwa ajili ya sabato”?2 Ninaamini Alitutaka sisi tuelewe kwamba Sabato ilikuwa zawadi yake kwetu, akitoa mapumziko ya kweli kutoka kwa kazi ngumu za kila siku na kutoa nafasi kwa kujiweka upya kiroho na kimwili. Mungu ametupa siku hii maalum, siyo kwa ajili ya starehe au kufanya kazi bali kwa ajili ya mapumziko ya kazi, tukipata pumziko la kimwili na kiroho.
Katika Kiebrania, neno Sabato lina maana “pumziko.” Lengo la Sabato lilikuwepo tangu kuumbwa kwa ulimwengu, baada ya siku sita za kazi, Bwana alipumzika toka kwenye kazi ya uumbaji.3 Baadaye alipoleta Amri Kumi kwa Musa, Mungu aliamuru kwamba “tuikumbuke siku ya sabato, na kuitakasa.”4 Baadaye, Sabato iliheshimiwa kama kumbukumbu ya kukombolewa kwa Iraeli toka utumwani huko Misri.5. Huenda kilicho muhimu zaidi ni kuwa Sabato ilitolewa kama ishara ya agano la milele, ukumbusho wa kila mara ili Bwana aweze kuwatakasa watu Wake.6
Zaidi ya hayo, sasa tunapokea sakramenti katika siku ya Sabato tukikumbuka Upatanisho wa Yesu Kristo.7. Tena, tunaahidi kwamba tupo tayari kujichukulia jina Lake takatifu.8.
Mwokozi alijitambulisha Mwenyewe kama Bwana wa Sabato.9. Ni siku Yake! Kila mara, Ametuomba tuishike Sabato 10 au tuitukuze siku ya Sabato.11 Tupo chini ya maagano kufanya hivyo.
Tunaweza kutukuza siku ya Sabato vipi? Nikiwa katika miaka ya ujana wangu, nilijifunza kazi za wengine ambazo ziliorodhesha vitu vya kufanya na vya kutofanya katika Sabato. Ilikuwa baadaye ndipo nikajifunza kutoka kwa maandiko kwamba mwenendo wangu na mtazamo wangu juu ya Sabato ilikuwa ishara kati ya nyangu na Baba wa Mbinguni.12 Kwa kuelewa huo, sikuhitaji tena orodha za kufanya na kutofanya. Nilipohitaji kufanya maamuzi ya kujua kama kazi zilikuwa sahihi kwa ya Sabato, nilijiuliza mwenyewe, “Ni ishara gani ninataka kumwonyesha Mungu?” Swali hilo lilifanya uchaguzi wangu kuhusu siku ya Sabato kuwa wa wazi zaidi.
Japo mafundisho kuhusu siku ya Sabato ni ya asili ya kale, yamefanywa upya katika siku hizi za mwisho kama sehemu ya agano jipya lenye ahadi. Sikiliza uwezo wa agizo hili mtakatifu:
“Na ili ujilinde na dunia pasipo na mawaa, utakwenda kwenye nyumba ya sala na kutoa sakramenti zako katika siku yangu takatifu;
“Kwani amini hii ndiyo siku iliyoteuliwa kwako kupumzika kutokana na kazi zako, na utoe dhabihu zako za shukrani kwa Aliye Juu sana. …
“Na katika siku hii … acha chakula chako kitengenezwe kwa moyo mmoja ili kufunga kwako kuweze kukamilika, … ili shangwe yako iweze kuwa kamilifu. …
“Na kadiri mtakavyofanya mambo haya kwa shukrani, pamoja na mioyo na nyuso zenye furaha, … vijazavyo dunia ni mali yenu.”13
Fikiria ukuu wa kauli hii! Utimilifu wa dunia umeahidiwa kwa wale wanaoishika siku takatifu ya Sabato.14 Ndiyo maana Isaya aliita Sabato siku “ya furaha.”
Unawezaje kuhakikisha kwamba tabia yako katika Sabato itakuongoza katika furaha na kufurahishwa? Zaidi ya kwenda kanisani, kupokea sakramenti, na kuwa na bidii katika wito maalum wa kutumikia, ni kazi gani nyingine zinazoweza kuifanya siku ya Sabato kuwa nzuri kwako? Ni ishara gani utakayoitoa kwa Bwana kuonyesha upendo wako Kwake?
Sabato inatoa nafasi nzuri ya kuimarisha uhusiano wa familia. Zaidi ya yote, Mungu anataka kila mmoja wetu, kama watoto Wake, turudi Kwake kama Watakatifu waliofanya endaumenti, familia iliyounganishwa hekaluni, na mababu zetu, na vizazi vyetu vya baadaye.15
Tunaifanya Sabato kuwa nzuri pale tunawapofundisha injili watoto wetu injili. Jukumu letu kama wazazi liko wazi. Bwana alisema, “Ilimradi wazazi wanao watoto katika Sayuni, au katika kigingi chake chochote ambacho kimeundwa, ambao hawawafundishi wao kuelewa mafundisho ya toba, imani katika Kristo Mwana wa Mungu aliye hai, na ubatizo na kipawa cha Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mkono, wafikapo miaka minane, dhambi zao zitakuwa juu ya vichwa vya wazazi.”16
Miaka iliyopita Urais wa Kwanza ulisisitiza umuhimu wa kuwa na muda mzuri wa familia. Waliandika:
“Tunawataka wazazi kujitolea nguvu zao katika kuwafundisha na kuwakuza watoto wao katika kanuni za injili ambazo zitawafanya wawe karibu na Kanisa. Nyumbani ndipo sehemu muhimu ya maisha mema, na hakuna sehemu yoyote inayoweza kuchukua nafasi yake au kutimiza majukumu yake katika kutimiza majukumu tuliyopewa na Mungu.
“Tunawashauri wazazi na watoto kutoa nafasi ya juu katika sala ya familia, jioni ya familia, mafunzo na mwongozo wa injili, na shughuli za familia. Chochote chema na kizuri kinachohitajika au kazi inayoweza kufanyika, hazitakiwi kuchukua nafasi ya kazi zilizowekwa ambazo ni wazazi na familia tu wanaoweza kutekeleza.”17
Ninapotafakari ushauri huu, ninatamani ningekuwa tena kijana. Sasa wazazi wana nyenzo nzuri zilizopo ili kuwasaidia kuufanya muda wa familia uwe na maana zaidi, katika siku ya Sabato na siku nyingine pia. Wana LDS.org, Mormon.org, the Bible videos, the Mormon Channel, the Media Library, the Friend, the New Era, the Ensign, the Liahona, na zaidi---zaidi sana. Nyenzo hizi zinasaidia sana wazazi katika kutimiza wajibu wao mtakatifu wa kuwafundisha watoto wao. Hakuna kazi nyingine zaidi ya ile ya wema, ya ulezi hai!
Unapofundisha injili, utajifunza zaidi. Hii ndiyo njia ya Bwana ya kukusaidia kuielewa injili Yake. Alisema:
“Na ninatoa kwenu amri ya kuwa mfundishane mafundisho ya ufalme.
“Fundisheni kwa bidii … , ili mpate kuelekezwa kikamilifu zaidi … katika mafundisho, katika sheria ya injili, katika mambo yale yote yahusuyo ufalme wa Mungu.”18
Kujifunza injili kwa aina hii kunaifanya Sabato siku ya furaha. Ahadi hii haijalishi ukubwa wa familia, utungo, au eneo.
Katika nyongeza ya muda wa familia, unaweza kuwa na furaha ya kweli katika Sabato kutoka katika kazi ya historia ya familia. Kutafuta wanafamilia ambao wameshaondoka duniani---wale ambao hawakupata nafasi ya kuikubali injili wakiwa hapa---kunaweza kuleta furaha ya ajabu.
Nimeyaona haya kwa macho yangu. Miaka kadhaa iliyopita, mke wangu mpendwa, Wendy, aliamua kujifunza jinsi kufanya utafiti wa historia ya familia. Maendeleo yake mara ya kwanza yalikuwa ya taratibu, kidogo kidogo, alijifunza jinsi ilivyokuwa rahisi kufanya kazi takatifu. Na sijawahi kumwona na furaha kama wakati ule. Nawe pia hauhitaji kusafiri kwenda nchi nyingine au hata kwenye kituo cha historia ya familia. Nyumbani, ukiwa na msaada wa kompyuta au simu ya rununu, unaweza kuzitambua nafsi zinazotamani ibada zao. Ifanye Sabato siku ya furaha kwa kuwatafuta wahenga wako na kuwaokoa kutoka katika gereza la roho!19
Ifanye Sabato siku ya furaha kwa kutoa huduma kwa wengine, hususani wale wasiojisikia vizuri au wale walio wapweke au wenye kuhitaji msaada.20 Kuziinua nafsi zao kutainua ya kwako pia.
Wakati Isaya alipoielezea Sabato kama “siku ya furaha,” pia alitufundisha jinsi ya kuifanya iwe ya furaha sana. Alisema:
“Kama ukigeuza … usifanye anasa yako siku ya utakatifu wangu; ukiita sabato siku ya furaha, … ukiitukuza [Bwana], kwa kutokuzifanya njia zako mwenyewe, wala kuyatafuta yakupendezayo, wala kusema maneno yako mwenyewe;
Ndipo utakapojifurahisha katika Bwana.”21
Kutofanya “anasa zako” mwenyewe kwenye Sabato kunahitaji nidhamu ya binafsi. Utatakiwa kujikana mwenyewe kwa mambo unayoyapenda. Kama utachagua kujifurahisha mwenyewe katika Bwana,, hautajiruhusu mwenyewe kuichukulia kama siku nyingine. Mambo ya kawaida na burudani yanaweza kufanywa wakati mwingine.
Fikiria hili: Katika kulipa zaka, tunarudisha moja ya kumi ya kipato chetu kwa Bwana. Kuifanya Sabato kuwa takatifu, tunaweka siku moja kati ya saba kuwa Yake. Hiyo ni fursa yetu ya kuweka wakfu yote fedha na muda Kwake yeye atupaye sisi maisha kila siku.22
Imani kwa Mungu inatuongoza katika upendo wa Sabato; imani katika Sabato inasababisha upendo kwa Mungu. Sabato takatifu kweli ni siku ya furaha.
Sasa, mkutano huu ukifikia mwisho, tunajua kwamba popote tuishipo tunatakiwa kuwa mfano kwa waaminio miongoni mwa familia, majirani, na marafiki.23 Waaminio wa kweli huifanya siku ya Sabato takatifu.
Ninamalizia kwa maneno ya buriani ya dhati ya Moroni, wakati akifunga Kitabu cha Mormoni. Aliandika, “Mje kwa Kristo na mkamilishwe ndani yake, na mjinyime ubaya wote; na ikiwa mtajinyima ubaya wote, na kumpenda Mungu na mioyo yenu, akili na nguvu zenu zote, basi … mmetakaswa katika Kristo.”24
Kwa upendo moyoni mwangu, ninawaachieni haya kama sala, ushuhuda, na baraka zangu katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.