Ukuhani---Zawadi Tukufu
Kila mmoja wetu amethaminiwa na mojawapo wa vipawa vya thamani vinavyotunukiwa binadamu.
Moja ya kumbukumbu yangu iliyowazi kabisa akilini ni kuhudhuria mkutano wa ukuhani kama shemasi mpya aliyesimikwa na kuimba wimbo wa kufungua, “Njooni, wana wote wa Mungu waliopokea ukuhani.”1 Usiku wa leo, kwa wote waliokusanyika hapa katika Kituo cha Mikutano na, hasa, duniani kote, ninapiga mwangwi roho ya wimbo huo ya kipekee na kuwaambieni, Njooni, wana wote wa Mungu waliopokea ukuhani, tuzingatieni wito wetu; turejeleeni majukumu yetu; tuamueni juhudi yetu; na tumfuateni Yesu Kristo, Bwana wetu. Ingawa tunaweza kunatofautiana kwa umri, tamaduni, ama utaifa, tunaungana kama kitu kimoja katika majukumu yetu ya ukuhani.
Kwa kila mmoja wetu, urejesho wa Ukuhani wa Haruni kwake Oliver Cowdery na Joseph Smith kupitia kwa Yohana Mbatizaji, ni muhimu sana. Vile vile, urejesho wa Ukuhani wa Melkizediki kwake Joseph na Oliver kupitia Petro, Yakobo, na Yohana, ni tukio la thamani.
Tuchukueni kwa makini zaidi wito, majukumu, na juhudi zinazokuja na ukuhani tulionao.
Nilihisi jukumu mkubwa nilipoitwa kuwa karani wa akidi yangu ya mashemasi. Nilitayarisha kwa makini kabisa kumbukumbu nilizoweka, kwani nilitaka kufanya vyema niwezavyo kutimiza wito huo. Nilifurahia sana kazi yangu. Kufanya yote niwezavyo, kwa uwezo wangu wote, kumekuwa lengo langu katika jukumu lolote nililokuwa nalo.
Ninatumaini kila mvulana aliyetawazwa kwa Ukuhani ya Haruni anapewa ufahamu wa kiroho wa utukufu wa jukumu lake aliyopewa, pamoja na fursa za kutekeleza majukumu hayo. Nilipokea fursa hiyo kama shemasi wakati uaskofu ulipouliza kwamba nipeleke sakramenti kwa mtu asiyeondoka kwake aliyeishi takribani maili moja kutoka kwa kanisa. Asubuhi hiyo ya kipekee ya Jumapili, nilipobisha kwenye mlango wa Ndugu Wright na kusikia sauti yake hafifu, “Njoo ndani,” Niliingia si tu nyumba yake lakini pia chumba kilichojawa na Roho wa Bwana. Nilikaribia kitandani mwa Ndugu Wright na kwa makini nikaweka kipande cha mkate kwa mdomo wake. Kisha nilishikilia kijikombe cha maji, ili kwamba aweze kunywa. Nilipoondoka, niliona machozi machoni pake aliposema, “Mungu akubariki, kijana wangu.” Na Mungu alinibariki---na shukrani kwa nembo tukufu za sakramenti na kwa ukuhani niliokuwa nao.
Hakuna shemasi, mwalimu, ama kuhani kutoka kwa kata yetu atawahi kusahau matembezi ya kukumbuka tuliyofanya kule Clarkson, Utah, kwenye kaburi la Martin Harris, mmoja wa mashahidi watatu wa Kitabu cha Mormoni. Tulipozingira itale refu iliyoalamisha kaburi yake, na mmoja wa viongozi wetu wa akidi alipotusomea maneno hayo ya kugusa moyo kutoka kwa “Ushuhuda wa Mashahidi Watatu,” unaopatikana mwanzoni mwa Kitabu cha Mormoni, tulipata upendo wa kumbukumbu hiyo tukufu na kweli zinazopatikana ndani yake.
Wakati wa miaka hio lengo letu lilikuwa kuwa kama wana wa Mosia. Kuwahusu ilisemwa:
“Walikuwa wameongezwa nguvu kwa ufahamu wa ukweli; kwani walikuwa watu ambao wana ufahamu mwema na walikuwa wameyapekua maandiko kwa bidii, ili wajue neno la Mungu.
“Lakini haya siyo yote; kwani walikuwa wamejitoa kwa sala, na kufunga; kwa hivyo walikuwa na moyo wa unabii, na roho ya ufunuo, na walipofunza, walifunza kwa uwezo na mamlaka ya Mungu.”2
Siwezi kufikiria kuhusu lengo linalostahili zaidi kuliko hili kwa mvulana kuwa nalo kuliko kuelezewa kama vile wana wajasiri na wema wa Mosia.
Nilipokaribia siku yangu ya kuzaliwa ya 18 na kujiandaa kuingia katika huduma ya jeshi iliyokuwa ni lazima kwa wavulana wakati wa Vita Vya Dunia II, nilipendekezwa kupokea Ukuhani wa Melkizediki, lakini kwani nilihitaji kumpigia simu rais wangu wa kigingi, Paul C. Child, kwa ajili ya mahojiano. Alikuwa mmoja aliyependa na kuelewa maandiko matakatifu, na ilikuwa ni nia yake kwamba wengine wote walipaswa wayapende na kuyaelewa vile vile. Nikiwa nimesikia kutoka kwa baadhi ya marafiki wenzangu juu ya mahojiano yake ya kina na uchunguzi, nilitamani ufunuo wa kiasi kidogo sana wa ufahamu wangu wa maandiko; hivyo basi, nilipompigia simu nilipendekeza tukutane Jumapili iliyofuata wakati nilijua ilikuwa tu saa moja kabla ya wakati wake wa mkutano wa sakramenti.
Jibu lake: “Ee, Ndugu Monson, hiyo haitatupa muda wa kutosha kupekua maandiko.” Kisha alipendekeza wakati uliokuwa masaa matatu kabla ya mkutano wake wa sakramenti, na alinieleza niende na maandiko yangu ya binafsi yaliyoalamishwa na kuwekwa marejeleo.
Nilipofika nyumbani kwake Jumapili, nilisalimiwa kwa upendo, na kisha mahojiano yakaanza. Rais Child alisema, “Ndugu Monson, unao Ukuhani wa Haruni. Je, umewahi tumikiwa na malaika?” Nilijibu kwamba sikuwahi. Alipouliza kama nilijua nilikuwa na haki ya kupokea utumishi huo, nilijibu tena kwamba sikuwa ninajua.
Alishauri,”Ndugu Monson, kariri kutoka akilini sehemu ya 13 ya Mafundisho na Maagano.”
Nilianza, ‘“Juu yenu ninyi watumishi wangu, katika jina la Masiya ninawatunukia Ukuhani wa Haruni, ambao hushikilia funguo za huduma za malaika---”’
“Tua,” Rais Child alielekeza. Kisha kwa sauti tulivu, ya ukarimu, alishauri, “Ndugu Monson, usiwahi kusahau kwamba kama mwenye Ukuhani wa Haruni una haki ya kupokea utumishi wa malaika.”
Ilikuwa ni kama malaika alikuwa chumbani siku hiyo. Sijawahi kusahau mahojiano hayo. Bado ninahisi roho ya siku hiyo tukufu tuliposoma kwa pamoja majukumu, wajibu na baraka za Ukuhani wa Haruni na Ukuhani wa Melkizediki---baraka ambayo haziji tu kwetu bali pia kwa familia zetu na wengine tulio na fursa ya kuwahudumia.
Niliteuliwa kuwa mzee, na siku ya kuondoka kwangu kujiunga na jeshi la majini, mshiriki wa uaskofu wangu wa kata alijiunga na familia yangu na marafiki katika kituo cha gari la moshi kuniaga kwaheri. Kabla tu ya wakati wa gari la moshi kuondoka, aliweka mkononi mwangu kitabu kidogo kilicho na kichwa Missionary Handbook.Nilicheka na kusema kwamba sikuwa ninaenda misheni.
Alijibu, “Kichukuwe tu ingawaje. Huenda kikakusaidia.”
Kilinisaidia. Nilihitaji chombo kigumu, cha mstatili kuweka chini ya begi langu ili nguo zangu zingebaki kuwa imara na hivyo basi haigekuwa na mikunjo mingi. Missionary Handbook ilikuwa tu kile nilichohitaji, na ilitumika vyema katika begi langu kwa wiki 12.
Usiku kabla ya mapumziko yetu ya Krismasi, mawazo yetu yalikuwa juu ya nyumbani. Kambini kulikuwa na kimya, lakini kisha kimya kilivunjwa na rafiki yangu katika kitanda kilichokaribu---kijana Mmormoni, Leland Merrill---aliyeanza kulia kwa maumivu. Niliuliza ni kwa nini alikuwa analia, na alisema alihisi mgonjwa sana. Hakutaka kwenda katika zahanati ya kambi, kwani alijua kwamba kufanya hivyo kungezuia kwenda kwake nyumbani siku iliyofuata.
Alionekana kuathirika zaidi muda ilivyopita. Hatimaye, akijua kwamba nilikuwa mzee, aliniuliza nimpe baraka ya ukuhani.
Sikuwa nimewahi kuombea mtu hapo awali, sikuwa nimewahi kuombewa, na sikuwahi kushuhudia mtu akiombewa. Niliomba usaidizi kimoyomoyo, nilikumbuka Missionary Handbook chini ya begi langu. Nilitoa kila kitu ndani ya begi kwa haraka na kuchukua kitabu kile karibu na mwangaza. Hapo nilisoma jinsi ya kuwaombea wagonjwa. Na wanajeshi wengi wa baharini wakiwa wanatazama, niliendelea na maombi. Kabla nirudishe kila kitu ndani ya begi langu, Leland Merrill alikuwa analala kama mtoto. Aliamka siku iliyofuata akiwa anajisikia vizuri. Shukrani sote tulihisi kwa ajili ya nguvu ya ukuhani ilikuwa ya haina kifani.
Miaka imeniletea fursa nyingi zaidi ya kuwaombea wale walio na mahitaji zaidi ya kiwango ninachoweza kuhesabu. Kila fursa imenipata nikiwa na shukrani nyingi sana kwamba Mungu amenikabidhi zawadi yake tukufu. Ninauheshimu ukuhani. Nimeshuhudia nguvu yake mara nyingi. Nimeuona uwezo wake. Nimeshangazwa na miujiza imetenda.
Kina Ndugu, kila mmoja wetu amekabidhiwa moja ya zawadi yenye thamani zaidi kuwahi kabithiwa wanadamu. Tunapoheshimu ukuhani wetu na kuishi maisha yetu ili kwamba wakati wote tunastahili, baraka za ukuhani zitatiririka kutupitia. Ninapenda maneno yanayopatikana katika Mafundisho na Maagano sehemu ya 121, mstari wa 45, yanayotuambia kile ambacho lazima tufanye ili kuwa wenye kustahili: “Na moyo wako pia uwe umejaa hisani kwa wanadamu wote, na kwa jamaa ya waaminio, na wema uyapambe mawazo yako bila kukoma; ndipo kujiamini kwako kutakuwa imara katika uwepo wa Mungu; na mafundisho ya ukuhani yatatonatona juu ya roho yako kama umande utokao mbinguni.”
Kama walio na ukuhani wa Mungu, tunashughulika katika kazi ya Bwana Yesu Kristo. Tumeitikia wito Wake; tuko katika kazi Yake. Tujifunzeni kumhusu Yeye. Tufuateni nyayo Zake. Tuishini kulingana na maelekezo Yake. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tayari kwa huduma yoyote atakayo tuita tufanye. Hii ni kazi Yake. Hili ni Kanisa Lake. Hakika, Yeye ni nahodha wetu, Mfalme wa Utukufu, hata Mwana wa Mungu. Ninashuhudia kwamba Yu hai na ninatoa ushahidi huu katika jina Lake takatifu, amina.