Watetezi wa Tangazo la Familia
Na tusaidie kujenga ufalme wa Mungu kwa kusimama kwa ujasiri na kuwa watetezi wa ndoa, uzazi, na nyumba
Ni fursa na shangwe ilioje kuwa katika mkusanyiko huu mkuu wa wasichana na wanawake. Ni baraka jinsi gani sisi kama wanawake kuungana pamoja jioni ya leo kwa umoja na kwa upendo.
Hivi karibuni nilisoma hadithi ya Marie Madeleine Cardon, ambaye, pamoja na familia yake, walipokea injili ya urejesho ya Yesu Kristo kutoka kwa wamisionari wa kwanza walioitwa kuhudumu Italia mwaka wa 1850. Alikuwa msichana mdogo wa umri wa mwaka 17 ama 18 walipobatizwa. Jumapili, familia hio ikiwa na mkutano wa kuabudu katika nyumba yao kule juu kwenye Milima ya Alps kaskazini mwa Italia, genge la wanaume waliokasirika, ikiwa ni pamoja na watumishi kadhaa wa eneo hilo, walikusanyika wakiizingira nyumba na kuanza kupiga makelele, wakipaza sauti, na kutaka wamisionari watolewe nje. Sifikirii kwamba walikuwa na nia ya kufundishwa injili---walidhamiria kuwaumiza. Ilikuwa ni Marie mdogo ndiye aliyetoka nje ya nyumba ile ili kukabiliana na genge hilo.
Waliendelea na kupiga kelele kwa sauti na kutaka wamisionari watolewe nje. Marie aliinua Bibilia yake juu kwa mkono na kuwaamuru waondoke. Aliwaambia kwamba wamisionari walikuwa chini ya ulinzi wake na kwamba hawange hatarisha hata unywele mmoja katika vichwa vyao. Sikilizeni maneno yake mwenyewe: “Wote walisimama kwa mshangao. … Mungu alikuwa pamoja nami. Aliyaweka maneno hayo mdomoni mwangu, vinginevyo nisingeweza kuyanena. Mambo yakatulitulia, mara moja. Genge hilo katili lenye nguvu la wanaume lilisimama kwa unyonge mbele ya msichana mnyonge, aliyekuwa anatetemeka, lakini bado asiye na uoga.” Watumishi waliliomba genge liondoke, kitu ambacho walifanya kimya kimya wakiwa na aibu, hofu, na majuto. Mkusanyiko wa waaminio ulikamilisha mkutano wao kwa amani.1
Je huwezi kupiga picha akilini ya yule msichana, mdogo jasiri, umri sawa na wengi wenu, akikabiliana na lile genge na kutetea imani yake mpya aliyoipata kwa ujasiri na msimamo thabiti?
Kina dada, wachache wetu huenda watawahi kulazimika kukabiliana na genge lililo na hasira, lakini kuna vita vinavyoendelea katika dunia hii ambapo mafundisho yetu ya msingi na thamani yanavamiwa. Ninazungumzia hasa juu ya mafundisho juu ya familia. Utakatifu nyumbani na malengo ya msingi ya familia yanajaribiwa, yanakoselewa, na yanavamiwa kutoka kila upande.
Wakati Rais Gordon B. Hinckley akisoma kwa mara ya kwanza “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu” miaka 20 iliyopita mwaka huu, tulishukuru na kuthamini uwazi, urahisii, na ukweli wa waraka huu wa kiufunuo. Hatukutambua vyema wakati huo, jinsi ambavyo tungehitaji sana matangazo haya ya msingi katika ulimwengu wa sasa kama vigezo ambavyo tungetumia kupima kila fundisho jipya la kidunia linalotukabili kutoka kwa vyombo vya habari, intaneti, wasomi, televisheni na filamu, na hata wabunge. Tangazo juu ya familia limekuwa kiwango chetu cha kupimia filosofia za dunia, na ninashuhudia kwamba kanuni zilizomo katika kauli hii ni za kweli leo kama zilivyokuwa wakati zilipotolewa kwetu sisi na nabii wa Mungu takribani miaka 20 iliyopita.
Naomba nielezee jambo moja lililowazi? Ni nadra sana maisha kwenda sawa sawa kabisa kulingana na mpango kwa yeyote yule, na tuna ufahamu kabisa kwamba si kila mwanamke anapitia kile ambacho tangazo linaelezea. Ni muhimu bado kuelewa na kufundisha mpagilio wa Bwana na kutafuta utekelezaji wa mpango huo vyema tuwezavyo.
Kila mmoja wetu ana sehemu ya kutekeleza katika mpango huu, na kila mmoja wetu ana thamani sawa mbele za macho ya Bwana. Tunapaswa tukumbuke kwamba Baba wa Mbinguni mwenye upendo anafahamu nia zetu za haki na atatekeleza ahadi Zake kwamba hakuna kitakachozuiliwa kwa wale ambao anashika maagano yake kwa uaminifu. Baba wa mbinguni ana lengo na mpango kwa ajili ya kila mmoja wetu, lakini pia ana ratiba Wake mwenyewe. Moja ya changamoto ngumu kabisa katika maisha haya ni kuwa na imani katika wakati wa Bwana. Ni wazo zuri kuwa na mpango mbadala akilini, utakaotusaidia kuwa wenye kushika maagano, wenye hisani, na wanawake wema ambao wanajenga ufalme wa Mungu bila kujali jinsi maisha yetu yanavyokwenda. Tunahitaji kuwafundisha mabinti zetu kulenga kuwa na hali bora kabisa lakini pia kupanga kwa yasiyotarajiwa.
Wakati huu wa maadhimisho ya kumbu kumbu ya miaka ya tangazo juu ya familia, ningetaka kutoa changamoto kwetu sote sisi wanawake wa Kanisa kutetea “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu.” Kama vile Marie Madeleine Cardon alivyowatetea kwa ujasiri wamisionari na imani yake mpya, tunahitaji tutetee kwa ujasiri mafundisho yaliyofunuliwa na Bwana yanayoelezea ndoa, familia, majukumu matakatifu ya wanaume na wanawake, na umuhimu wa nyumba kama mahali patakatifu---hata wakati dunia inapiga kelele masikioni mwetu kwamba kanuni hizi ni za kale, zina mapungufu, au hazina maana tena. Kila mtu, bila kujali hali yao ya ndoa ama idadi ya watoto, anaweza kuwa mtetezi wa mpango wa Bwana ulioelezewa katika tangazo juu ya familia. Kwa vile ni mpango wa Bwana, unapaswa pia kuwa mpango wetu!
Kuna kanuni tatu zinazofundishwa katika tangazo juu ya familia ambazo ninafikiria zinahitaji sana watetezi imara. Ya kwanza ni ndoa kati ya mwanaume na mwanamke. Tunafundishwa katika maandiko, “Walakini si mwanamke pasipo mwanamume, wala mwanamume pasipo mwanamke, katika Bwana.”2Kwa yeyote kupokea ukamilifu wa baraka za ukuhani, lazima kuwe na mume na mke wakiwa wameunganishwa katika nyumba ya Bwana, wakifanya kazi pamoja kwa haki, na kubaki waaminifu katika maagano yao. Huu ni mpango wa Bwana kwa ajili ya watoto Wake, na hakuna kiwango cha majadiliano umma ama kukosoa kutabadili kile ambacho Bwana amesema. Tunapaswa tuendelee kuonyesha mfano wa ndoa za haki, kutafuta baraka hiyo katika maisha yetu, na kuwa na imani hata kama inakuja polepole. Tuweni watetezi wa ndoa kama vile Bwana ameitakasa tukiendelea kuonyesha upendo na hisani kwa wale walio na mtazamo tofauti.
Kanuni inayofuatia ambayo inahitaji sauti zetu za utetezi ni kuinua majukumu matakatifu ya kina mama na akina baba. Tunawafundisha kwa dhati watoto wetu kulenga juu katika maisha haya . Tunataka hasa kuhakikisha kwamba mabinti zetu wanajua kwamba wana uwezo wa kufaulu na kuwa chochote wanachoweza kufikiria. Tunatumainii watapenda kusoma, wataelimika, watakuwa wajuzi, na pengine hata kuwa Marie Curie ama Eliza R. Snow anayefuatia.
Je, tunawafundisha pia wana na mabinti zetu kwamba hakuna heshima ya juu zaidi, vyeo vya juu zaidi, na majukumu ya juu zaidi katika maisha haya kuliko yale ya mama na baba? Ningetumaini kwamba tunapowahimiza watoto wetu kufikia yale yaliyo bora zaidi katika maishani haya kwamba tuwafundishe pia kuheshimu na kuinua majukumu ambayo kina mama na kina baba wanatekeleza katika mpango wa Baba wa Mbinguni.
Binti yetu wa mwisho, Abby, aliona fursa ya kipekee kusimama kama mtetezi wa jukumu la mama. Siku moja alipata barua kutoka katika shule ya watoto wake kwamba walikuwa na Siku ya Maonyesho ya Kazi shuleni kwao. Wazazi walialikwa watume ombi ikiwa walitaka kuja shuleni kufundisha watoto kuhusu kazi zao, na Abby alihisi ushawishi wa kuja na kuzungumza kuhusu haki ya kuwa mama. Hakusikia lolote kutoka shuleni, na siku ya Maonyesho ya Kazi ilikuwa inakaribia, hatimaye alipiga simu shuleni, akifikiria huenda walikuwa wamepoteza ombi lake. Waandaji walijaribu juu chini na wakapata waalimu wawili waliokubali Abby kuja kuzungumza katika madarasa yao mwishoni mwa Siku ya Maonyesho ya Kazi.
Katika onyesho lake la kupendeza kwa watoto, Abby aliwafundisha, miongoni mwa mambo mengine, kwamba kama mama alihitajika kuwa kwa kiwango fulani mtaalamu katika uponyaji, saikolojia, dini, elimu, muziki, fasihi, sanaa, fedha, kupamba, urembeshaji nywele, kuendesha gari, michezo, sanaa ya upishi, na mengine mengi. Watoto walivutiwa. Alimalizia kwa kuwafanya kila mmoja wa watoto kuwakumbuka mama zao kwa kuandika kijibarua cha shukrani wakielezea shukrani kwa vitendo vingi vya huduma ya upendo wanayopata kila siku. Abby alihisi watoto waliwaona mama zao kwa mwanga tofauti sana na kwamba kuwa mama ama baba ilikuwa ni kitu cha thamani kubwa. Alituma ombi kushiriki tena mwaka huu Siku ya Kazi na alialikwa kutoa onyesho kwa madarasa darasa sita.
Abby alisema haya kwa sababu ya yale aliyoyapitia: “Naona ni kama ingekuwa rahisi katika ulimwengu huu kwa mtoto kupata ufahamu kwamba kuwa mzazi ni kazi ya ziada na hata wakati mwingine usumbufu muhimu. Nataka kila mtoto ajisikie kama wao ni kipaumbele muhimu zaidi kwa wazazi wao, na labda kuwaambia umuhimu wa kuwa mzazi kwangu kutawasaidia kutambua yote ambayo wazazi wao hufanya kwa ajili yao na kwa nini.”4
Nabii wetu mpendwa, Rais Thomas S. Monson, ni mfano mzuri wa kuheshimu wanawake na umama, hasa mamake mwenyewe. Kwa kurejea kina mama zetu wa duniani, amesema: “Na kila mmoja wetu authamini ukweli huu; mtu hawezi kumsahau mama na kumkumbuka Mungu. Mtu hawezi mkumbuka mama na kumsahau Mungu. Kwa nini? Kwa sababu watu hawa wawili watakatifu, Mungu na mama[wa duniani], washirikiana katika uumbaji, katika upendo, katika dhabihu, katika utumishi, ni kama kitu kimoja.”3
Kanuni ya mwisho tunayohitaji kusimama na kuitetea ni utakatifu wa nyumba. Tunahitaji kuchukua neno ambalo wakati mwingine huzungumziwa kwa kejeli na kuliinua. Ni neno wahifadhi boma. Sote, ---wanawake, wanaume, vijana, na watoto, waseja na wanandoa,--- tunaweza kujitahidi kuwa wahifadhi boma.Tunapaswa “tufanye nyumba zetu” kuwa mahali pa mpangilio, pa faraja, utukufu, na usalama. Nyumbani kwetu kunapaswa kuwa mahali ambapo Roho wa Bwana yupo kwa kiwango kikubwa na mahali maandiko na injili inasomwa, inafunzwa, na inatekelezwa. Italeta tofauti kiasi gani katika ulimwengu ikiwa watu wote wangejiona kama wajenzi wa maboma yenye wema. Tuteteeni nyumba kama mahali panaposhika nafasi ya pili kwa utakatifu kutoka hekalu.
Kina Dada, ninashukuru kuwa mwanamke katika siku hizi za mwisho. Tuna fursa na uwezo ambao hakuna kizazi kingine cha wanawake wamekuwa nao duniani. Na tusaidie kujenga ufalme wa Mungu kwa kusimama kwa ujasiri na kuwa watetezi wa ndoa, uzazi, na nyumba. Bwana anatuhitaji tuwe wapiganaji jasiri, wasioyumba, na wapiganaji wasioondoshwa ambao watatetea mpango Wake na kufundisha vizazi vijavyo ukweli Wake.
Ninatoa ushahidi kwamba Baba wa Mbinguni yu hai na anampenda kila mmoja wetu. Mwanawe, Yesu Kristo, ni Mwokozi na Mkombozi wetu. Ninawaachieni ushuhuda huu katika jina la Yesu Kristo, amina.