Kwa nini Ndoa na Familia ni Muhimu – Kote Ulimwenguni
Familia ni kitovu cha maisha na ni ufunguo wa furaha ya milele.
Novemba iliyopita nilikuwa na fursa ya kualikwa---pamoja na Rais Henry B. Eyring na Askofu Gérald Caussé---kuhudhuria kongamano juu ya ndoa na familia kule Vatican Roma, Italia. Katika mahudhurio walikuwepo wawakilishi wa kidini kutoka madhehebu 14 tofauti na kutoka katika mabara sita kati ya mabara saba yaliyoko, wote walikuwa wamealikwa ili kuelezea imani yao kuhusu kile kinachotendeka kwa familia katika ulimwengu wa sasa.
Papa Francis alifungua kikao cha kwanza cha mkutano kwa kauli hii: “Sasa tunaishi katika utamaduni wa vitu vya muda, ambapo watu zaidi na zaidi wanakata tamaa kirahisi juu ya ndoa kama sharti la kijamii. Mapinduzi haya katika tabia na maadili mara nyingi yamepeperushaa bendera ya uhuru, lakini kwa kweli yameleta uharibifu wa kiroho na kimwili kwa binadamu wengi sana, hasa walio maskini zaidi na walio katika mazingira hatarishi. ... Daima ndio wao wanoteseka zaidi katika mgogoro huu.”1
Akirejea kwa wale wa kizazi chipukizi, yeye alisema ni muhimu kwamba “wasikubali [dhana] ya uongo ya mambo ya muda, lakini badala yake wawe wana mageuzi kwa ujasiri wa kutafuta ukweli na upendo wa kudumu, wakienda kinyume na utaratibu wa kawaida”; hii ni sharti ifanyike.2
Hii ilifuatiliwa na siku tatu za maonyesho na mahojiano ambapo viongozi wa kidini walizungumzia mada ya ndoa kati ya mwanaume na mwanamke. Nilipokuwa ninasikiliza kutoka kwa viongozi hawa wengi na wakubwa wa kidini wa ulimwengu, niliwasikia wakikubaliana kabisa kwa pamoja na kuelezea kukubaliana na imani ya kila mmoja juu ya utakatifu wa asasi ya ndoa na umuhimu wa familia kama kitengo cha msingi katika jamii. Nilipata hisia ya nguvu juu ya usawa na umoja kati yetu na viongozi hawa.
Kulikuwa na wengi walioona na kuelezea umoja huu, na walifanya hivyo kwa njia nyingi. Moja ya yaliyonipendeza kabisa ilikuwa wakati msomi wa Kiislamu kutoka Iran alinukuu aya mbili neno kwa neno kutoka katika tangazo letu wenyewe juu ya familia.
Wakati wa kongamano, niliona kwamba wakati imani na madhehebu na dini tofauti zinapoungana juu ya ndoa na familia, wanaungana pia kwenye maadili na uaminifu na kujitolea ambayo kwa kawaida huhusishwa na familia. Ilikuwa ajabu kwangu kuona jinsi ndoa na vipaumbele vinavyolenga familia vinapita na kuvuka tofuauti zozote za kisiasa, kiuchumi, au kidini. Wakati tunapokuja katika upendo kwa mke au mme na matumaini, wasiwasi, na ndoto kwa watoto, sote tuko sawa.
Ilikuwa vizuri sana kuwa katika mikutano na wahadhiri kutoka duniani kote wakizungumzia kilimwengu hisia zao juu ya umuhimu wa ndoa kati ya mwanaume na mwanamke. Kila moja ya hotuba zao zilifuatiwa na ushuhuda kutoka kwa viongozi wengine wa dini. Rais Henry B. Eyring alitoa ushuhuda wa mwisho katika kongamano. Alitoa ushuhuda wenye nguvu juu ya uzuri wa ndoa ambapo mume na mke wanajitolea nafsi zao na katika imani yetu katika baraka zilizoahidiwa za familia milele.
Ushuhuda wa Rais Eyring ulikuwa hitimisho la kufaa kwa siku hizo tatu za kipekee.
Sasa, huenda unauliza, “Kama wengi walihisi kufanana huko kwa vipaumbele vya familia na imani, kama imani na dini hizo zote kimsingi zilikubaliana juu ya kile ndoa inapaswa iwe, na kama zote zilikubali juu ya thamani inayopaswa iwekwe kwenye nyumba na mahusiano ya familia, basi, ni kwa namna gani sisi tuko tofauti ? Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linajibainisha na kujitofautisha vipi kutoka kwa wengine duniani? ”
Hili hapa jibu: wakati ilikuwa vizuri kuona na kuhisi kwamba tuna mengi yanayofanana na wengine duniani kuhusiana na familia zetu, ni sisi tu tulio na mtazamo wa milele wa injili ya urejesho.
Kile injili iliyorejeshwa huleta kwa majadiliano juu ya ndoa na familia ni kikubwa na kina umuhimu mkubwa kiasi kwamba hakiwezi kusisitizwa vya kutosha: Tunaifanya mada kuwa ya milele! Tunachukua ahadi na utukufu wa ndoa kwa kiwango cha juu zaidi kwa sababu ya imani yetu na uelewa kuwa familia zina chanzo kabla ya dunia hii iwe na kwamba zinaweza kusonga mbele hadi milele.
Fundisho hili limefunzwa kwa urahisi sana, kwa nguvu, na kwa uzuri na maandishi ya Ruth Gardner ya wimbo wa Msingi, “Families Can Be Together Forever”. Tua kwa dakika na ufikirie kuhusu watoto wa Msingi kote duniani wakiimba maneno haya katika lugha yao ya mama, kwa nguvu zao zote, kwa shauku ambayo tu familia inaweza kuleta.
“Familia zinaweza kuwa pamoja milele
Kupitia Mpango wa Baba wa Mbinguni,
Daima nataka kuwa pamoja na familia yangu.
Na Bwana amenionyesha jinsi ya kufanya hivyo.”3
Teolojia mzima ya injili yetu ya urejesho ina msingi katika familia na agano jipya na la milele la ndoa. Katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunaamini katika maisha kabla ya kuja duniani ambapo sote tuliishi kama watoto halisi wa kiroho wa Mungu Baba yetu wa Mbinguni. Tunaamini kwamba sisi tulikuwa, na bado sisi ni, wanafamilia wa familia Yake.
Tunaamini kwamba ndoa na uhusiano wa familia unaweza kuendelea kupita kaburi---kwamba ndoa iliyofanywa na wale walio na mamlaka sahihi katika mahekalu Yake itaendelea kuwa halali katika ulimwengu ujao. Sherehe zetu za ndoa huondoa maneno ”hadi kifo kitutenganishe” na badala yake kusema ”kwa muda na milele.”
Pia tunaamini kwamba familia za kitamaduni zenye nguvu siyo tu asasi muhimu ya jamii imara, uchumi imara, na utamaduni imara wa maadili bali pia kwamba ni asasi muhimu za milele na za ufalme, na serikali ya Mungu.
Tunaamini kwamba shirika na serikali ya Mbinguni itajengwa kwa misingi ya familia na jamaa.
Ni kwa sababu ya imani yetu kuwa ndoa na familia ni ya milele ili kwamba sisi, kama kanisa, tunataka kuwa kiongozi na mshiriki katika harakati duniani kote ya kuziimarisha. Tunajua kwamba si wale tu wananaojishughulisha katika dini ambao wana maadili sawa na vipaumbele vya ndoa za kudumu na uhusiano imara wa familia. Idadi kubwa ya watu wa kilimwengu wameamua kwamba ndoa ya dhati na maisha ya staili ya kifamilia ni maisha ya busara zaidi, ya gharama nafuu, na njia yenye furaha zaidi ya kuishi.
Hakuna mtu ambaye amewahi kubuni njia ya ufanisi zaidi ya kukuza kizazi kijacho kuliko kaya ya wazazi walioona pamoja na watoto.
Kwa nini ndoa na familia iwe jambo la umuhimu---kila mahali? Kura za maoni ya umma zinaonyesha kwamba ndoa bado ni hali bora na ya tumaini miongoni mwa wengi katika kila kikundi cha umri---hata miongoni mwa kizazi cha milenia, ambapo tunasikia kwa mengi kuhusu watu wanaochagua kutooa au kuolewa, uhuru binafsi, na kuishi pamoja badala ya kufunga ndoa. Ukweli ni kwamba walio wengi duniani kote bado wanataka kuwa na watoto na kujenga familia zenye nguvu.
Mara tunapokuwa tumeoa au kuolewa na mara tunapokuwa na watoto, usawa wa kweli miongoni mwa wanadamu wote unakuwa dhahiri zaidi. Kama ”watu wanaopenda familia”---bila kujali tunapoishi ama imani yetu ya dini---tunashiriki mengi ya mapambano sawa, marekebisho ya kifamilia sawa, na matumaini sawa, wasiwasi, na matarajio kwa ajili ya watoto wetu.
Kama vile mwandishi wa New York Times David Brooks alivyosema: “Watu hawana maisha bora zaidi wanapokuwa wamepewa uhuru binafsi mwini wa kufanya kile wanachotaka. Wanaishi vyema zaidi wakati wanapokuwa wamefungwa katika ahadi zinazoshinda uchaguzi binafsi---kujitolea kwa familia, Mungu, fani na nchi.”4
Tatizo moja ni kwamba vyombo vya habari na burudani vingi ambavyo dunia inavyo havionyeshi vipaumbele na maadili ya wengi. Kwa sababu fulani, wingi wa televisheni zetu, sinema, muziki na Intaneti huonyesha vizuri hali za wachache wanaojisingizia kama walio wengi. Uasherati na kutokuwa na maadili, kuanzia vurugu dhahiri hadi ngono ya burudani, inaonyeshwa kama jambo la kawaida na inaweza kusababisha wale walio na maadili kuhisi kama sisi tumepitw na wakati ama tunatoka kipindi cha kale. Katika dunia inayoshawishiwa na vyombo vya habari na intaneti, haijawahi kuwa vigumu zaidi kulea watoto wanaowajibika na kuweka ndoa na familia pamoja kama wakati huu.
Licha ya kile vyombo vya habari na burudani huenda vikapendekeza, hata hivyo, na licha ya kushuka katika mwelekeo wa ndoa na familia kwa wengine, wengi wa wanadamu bado wanaamini kuwa ndoa inapaswa iwe kati ya mwanamume mmoja na mwanamke mmoja. Wanaamini katika uaminifu ndani ya ndoa, Na wanaamini katika nadhiri za ndoa za ”katika magonjwa na afya” na ”hadi kifo kitutenganishe.”
Tunahitaji kujikumbusha mara kwa mara, kama nilivyokumbushwa Roma, juu ya ukweli wa ajabu wa kutuliza na kufariji kwamba ndoa na familia bado ni matarajio na maadili ya watu wengi na kwamba hatuko peke yetu katika imani hizi. Haijawahi kuwa changamoto zaidi kupata uwiano wa kweli kati ya kazi, familia na mahitaji binafsi kuliko ilivyo katika siku zetu. Kama kanisa, tunataka kusaidia katika yote tunayoweza ili kujenga na kusaidia ndoa na familia imara.
Hiyo ndiyo sababu Kanisa hushiriki kikamilifu na kutoa uongozi kwa miungano mbalimbali na jitihada za mitaguso mbali mbali ili kuimarisha familia. Ndiyo sababu sisi huelezea maadili yetu yanayozingatia familia katika vyombo vya habari na vile vya kijamii. Ndiyo sababu sisi hutoa kumbu kumbu zetu za nasaba na familia zetu kwa mataifa yote.
Tunataka sauti yetu isikike dhidi ya njia zote za staili za maisha bandia na mbadala zinazojaribu kuchukua nafasi ya asasi ya familia ambayo Mungu Mwenyewe alianzisha. Tunataka pia sauti zetu zisikike katika kuunga mkono furaha na ukamilifu ambao familia asilia huleta. Lazima tuendelee kupaza sauti hiyo duniani kote katika kutangaza kwa nini ndoa na familia ni muhimu sana, kwa nini ndoa na familia hakika ni za maana, na kwa nini daima zitakuwa hivyo.
Kaka zangu na dada zangu, injili ya urejesho inalenga katika ndoa na familia. Pia ni juu ya ndoa na familia ambapo tunaweza kuungana sana na dini zingine. Ni kuhusu ndoa na familia ambapo tunaweza kupata usawa wetu mkuu na dunia yote. Ni kuhusu ndoa na familia ambapo Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho lina fursa kubwa ya kuwa nuru juu ya kilima.
Acha nimalizie kwa kutoa ushahidi (na miongo yangu tisa katika dunia inaniruhusu kusema haya) kwamba ninapozidi kuzeeka, ndivyo zaidi ninavyotambua kwamba familia ni kitovu cha maisha na ufunguo wa furaha ya milele.
Natoa shukrani kwa ajili ya mke wangu, watoto wangu, wajukuu wangu na vitukuu vyangu, na kwa binamu na kwa wakwe zangu wote na kwa familia kwa ujumla ambao hufanya maisha yangu kuwa na furaha tele na, ndio, hata ya milele. Kuhusu ukweli huu wa milele natoa ushuhuda wangu mtakatifu wa nguvu katika jina la Yesu Kristo, amina.