2010–2019
Ni Wazuri na Hawana Hila
Aprili 2015


10:26

Ni Wazuri na Hawana Hila

Habari njema za injili ya Yesu Kristo ni kwamba tamaa za mioyo yetu zinaweza kubadilishwa na nia zetu zinaweza kuelimishwa na kusafishwa.

Kwa bahati mbaya, kulikuwa na wakati katika maisha yangu nilipovutiwa na vyeo na mamlaka. Nilianza bila ya kujitambua. Nilipokuwa najiandaa kutumikia kama mmisionari, kaka yangu mkubwa aliteuliwa kuwa kiongozi katika misheni yake. Nilisikia mambo mengi mazuri yakisemwa juu yake hivyo nikashindwa kujizuia na kutaka mambo hayo yasemwe juu yangu. Nilitarajia na huenda niliomba juu ya nafasi kama hiyo.

Ninashukuru, nikiwa natumikia misheni yangu, nilijifunza somo zuri. Mkutano uliopita, nilikumbushwa somo lile.

Mwezi Octoba, Rais Dieter F. Uchtdorf alisema: “Katika maisha yangu, nilipata nafasi ya kujuana na baadhi ya wanaume na wanawake wenye uwezo na wenye akili ambao wapo katika ulimwengu huu. Nilipokuwa mdogo, nilivutiwa na wale waliokuwa na elimu, waliotimiza, waliofanikiwa, na kupongezwa na ulimwengu. Lakini kwa miaka kadhaa, nimekuja kugundua kwamba nimekuwa nikivutiwa na watu wazuri na walio barikiwa ambao kwa kweli ni wazuri na hawana hila.”1

Shujaa wangu kwenye Kitabu cha Mormoni ni mfano mzuri wa mtu mwema na aliyebarikiwa ambaye hakika alikuwa mzuri na hana hila. Shibloni alikuwa mmoja wa wana wa Alma Mdogo. Tunawaelewa zaidi kaka zake, Helamani, ambaye angemfuata baba yake kama mtunza kumbukumbu na nabii wa Mungu, na Koriantoni, ambaye alijulikana kama mmisionari ambaye alihitaji ushauri kutoka kwa baba yake. Kwa Helamani, Alma aliandika mistari 77 (ona Alma 36–37). Kwa Koriantoni, Alma alitumia mistari 91 (ona Alma 39–42). Kwa Shibloni, kijana wake wa kati, Alma aliandika mistari 15 tu (ona Alma 38). Hata hivyo maneno yake katika mistari hiyo 15 ni yenye nguvu na yenye kufundisha.

“Na sasa, mwana wangu, ninaamini kwamba nitakuwa na shangwe kuu juu yako, kwa sababu ya uthabiti wako na imani yako kwa Mungu; kwani kwa njia hiyo umeanza katika ujana wako kumtegemea Bwana Mungu wako, hata hivyo natarajia kwamba utaendelea kutii amri zake; kwani heri yule atakaye vumilia hadi mwisho.

“Ninakuambia wewe, mwana wangu, kwamba tayari nimekuwa na shangwe kubwa kwako, kwa sababu ya uaminifu wako na bidii yako, na subira yako, na uvumilivu wako miongoni mwa watu” (Alma 38:2–3).

Kwa nyongeza ya kuongea na Shiblon, Alma pia aliongea kumhusu yeye kwa Kariantoni. Alma alisema: “Hujachunguza unyofu wa kaka yako, uaminifu wake na bidii yake kwa kutii amri za Mungu? Tazama, si yeye amekuwekea mfano mzuri?” (Alma 39:1).2

Inaonekana kwamba Shibloni alikuwa ni mwana aliyetaka kumridhisha baba yake na kwenda kutenda yaliyo mema kwa sababu ilikuwa vyema badala ya kufanya kwa kutukuzwa, nafasi, madaraka, cheo, au mamlaka. Helamani lazima alijua na kuheshimu hili kuhusu kaka yake, kwani alimpa Shibloni usimamizi wa kumbukumbu tukufu alizopokea kutoka kwa baba yake. Hakika Helamani alimwamini Shibloni kwa sababu “alikuwa mtu mwenye haki, na alitembea wima mbele ya Mungu; na alitazamia kutenda mema siku zote, kutii amri za Bwana Mungu wake” (Alma 63:2). Ikaonekana kuwa tabia halisi ya Shibloni, mengi hayakuandikwa juu yake toka alipochukua kumbukumbu takatifu hadi pale alipompa mwana wa Helamani aitwaye Helamani (ona Alma 63:11).

Shibloni hakika alikuwa mwema na asiye na hila. Alikuwa mtu aliyejitolea muda wake, vipaji na nguvu zake kuwasaidia na kuwainua wengine kwa sababu ya upendo kwa Mungu na wanadamu wenzake (ona Alma 48:17–19; 49:30). Anaelezewa vyema kabisa kwa maneno ya Rais Spencer W. Kimball: “Wanaume na wanawake wema mara nyingi wana hamu ya kutumikia kuliko kutawala.”3

Katika ulimwengu ambao kutukuzwa, cheo, madaraka, sifa, na mamlaka vinatafutwa kila mahali, ninawaheshimu watu wema na waliobarikiwa ambao ni wazuri na hawana hila, wale ambao wanatiwa hamasa na upendo wa Mungu na majirani zao, wale wanawake na wanaume ambao wanahamasika kutumikia kuliko kutawala.”

Leo kuna wengine ambao wangependa sisi tuamini kutafuta kwetu uhusiano kunaweza kutoshelezwa tu kwa kupata cheo na madaraka. Hata hivyo, tunashukuru, kuna wengi ambao hawashawishiki kwa jambo hili. Wanapata uhusiano katika kutaka kuwa wema na bila hila. Nimewaona watu wa aina hii katika maisha yangu na katika tamaduni zenye imani. Na nimewaona wengi miongoni mwa wafuasi wa Kristo walioongoka.4

Ninawaheshimu wale wanaotumikia kila wiki katiki kata na matawi duniani kote kwa kwenda mbele zaidi katika kutimiza wito wao. Lakini wito unakuja na kwenda. Cha kuvutia zaidi kwangu ni kwa wengi wasio na wito maalumu wanapotafuta njia ya kutumikia na kuwainua wengine. Kaka mmoja anakuja kanisani mapema kwa ajili ya kupanga viti na hubaki kwa ajili ya kusafisha kanisa. Dada mmoja kwa makusudi huchagua kiti karibu na dada kipofu katika kata yake siyo tu aweze kumsalimia lakini pia aweze kuimba kwa sauti ili dada kipofu aweze kusikia maneno naye aimbe. Ukiangalia kwa karibu katika kata au tawi lako, utapata mifano kama hii. Mara zote kuna waumini wanaoonekana kujua nani anahitaji msaada na wakati gani wa kuutoa.

Huenda somo langu la kwanza kuhusu Watakatifu wema wasio na hila nilijifunza nilipokuwa mmisionari kijana. Nilihamia kwenye eneo pamoja na mwenza wangu ambaye sikumfahamu. Niliwasikia wamisionari wengine wakisema jinsi ambavyo alikuwa hajawahi pata majukumu ya kiuongozi na jinsi alivyosumbuka na lugha ya Kikorea japokuwa alikuwa pale nchini kwa muda mrefu. Lakini nilipokuja kumjua huyu mmisionari, niligundua kuwa alikuwa ni mmisionari mtiifu na mwema zaidi ya niliowajua. Alijifunza wakati muafaka wa kujifunza, na alifanyakazi muda wa kufanyakazi. Aliondoka nyumbani na kurudi kwa muda muafaka. Alikuwa na bidii ya kujifunza Kikorea japokuwa lugha hiyo ilikuwa ngumu kwake.

Nilipogundua maneno niliyoyasikia yalikuwa siyo ya kweli, nilihisi mmisionari huyu alikuwa akihukumiwa kwa kutofanikiwa kwake. Nilitaka kuiambia misheni yote kile nilichokigundua kuhusu mmisionari huyu. Nilishiriki na rais wangu wa misheni kusudi langu la kusahihisha jambo hili. Jibu lake lilikuwa, “Baba wa Mbinguni anamjua kijana huyu kuwa ni mmisionari mwenye mafanikio, nami najua hivyo.” Aliongeza, “Nawe sasa unajua, hivyo nani mwingine anahusika?” Rais huyu wa mishei mwenye busara alinifundisha mimi kile kilichokuwa muhimu katika kutumikia, na haikuwa sifa, cheo, uwezo, heshima, au mamlaka. Hili lilikuwa somo zuri kwa mmisionari kijana aliyekuwa akilenga kwenye vyeo.

Nikiwa na somo hili akilini, nikaanza kuangalia nyuma katika maisha yangu na kuona ni mara ngapi nilikuwa nimevutiwa na wanaume na wanawake ambao kwa nyakati hizo hawakuwa na vyeo vikubwa. Mmoja wa mfano wa Shibloni alikuwa mwalimu wangu wa seminari wakati nikiwa shule ya sekondari. Mtu huyu mwema alifundisha seminari kwa miaka miwili au mitatu, lakini aliufungua moyo wangu kwa njia ambayo alinisaidia kupata ushuhuda. Hakuwa mwalimu maarufu shuleni, lakini mara zote alikuwa amejiandaa na ushawishi wake kwangu ulikuwa ni mkubwa na wa milele. Moja ya mara chache nilizomwona mtu huyu katika miaka 40 toka aliponifundisha ilikuwa ni pale alipokuja kuniona kwenye msiba wa baba yangu. Hakika, hilo halikuwa jambo la kuvutiwa na cheo au madaraka.

Ninamheshimu mwalimu yule aliyejitolea na wengine walio kama yeye ambao ni wazuri na wasio na hila. Ninamheshimu mwalimu wa Shule ya Jumapili ambaye hawafundishi tu wanafunzi wake wakati wa darasa Jumapili bali pia anawafundisha na kuwashawishi wanafunzi hawa kwa kuwaalika nyumbani kupata kifungua kinywa. Ninawaheshimu viongozi vijana wanaohudhuria michezo na kazi za kitamaduni za wasichana na wavulana katika kata zao. Ninamheshimu mtu anayeandika muhtasari wa kushawishi majirani na wanawake ambao sio tu wanatuma kadi za Krismasi bali huzigawa kwa wanafamilia na marafiki wanaohitaji kutembelewa. Ninampongeza kaka ambaye huwachukua majirani kutembea wakati ule wa siku za kiza cha Alzheimer---akiwapa wote yeye na mkewe mabadiliko ya mwendo.

Vitu hivi havifanywi kwa ajili ya kusifiwa au kuhimidiwa. Wanaume na wanawake hawa hawasukumwi na uwezekano wa kupata cheo au madaraka. Ni wafuasi wa Kristo, wakienda kutenda mema daima, na kama Shibloni, wanajaribu kumtii Baba yao wa Mbinguni.

Inanihuzunisha pale ninaposikia baadhi wameacha kutumikia au hata kuacha kuja kanisani eti kwa sababu wamepumzishwa toka kwenye wito wao au wanahisi kama wamenyang’anywa cheo. Ninatumaini siku moja watakuja kujifunza kile nilichojifunza nikiwa mmisionari kijana---kwamba huduma nzuri zaidi mara nyingi inajulikana na Mungu. Katika kutafuta changu na chetu, tumemsahau Yeye na Yake.

Wengine wanaweza kusema, “Lakini mimi nina safari ndefu ya kuwa kama wale uwasemao.” Habari njema za injili ya Yesu Kristo ni kwamba matamanio ya mioyo yetu yanaweza kubadilishwa na malengo yetu yanaweza kuelimishwa na kutakaswa. Tunapobatizwa katika kundi la kweli la Mungu, tunaanza juhudi za kuwa viumbe wapya (ona 2 Wakorintho 5:17; Mosia 27:26). Kila wakati tunapofanya upya maagano ya ubatizo kwa kupokea sakramenti, tunasonga mbele hatua moja kufikia lengo kuu. 5 Tunapovumilia katika maagano yale, tunapata nafasi ya kuomboleza na wale waombolezao na kuwafariji wale wanaohitaji faraja (ona Mosia 18:9). Katika maagano yale, tunapata neema inayotuwezesha sisi kumtumikia Mungu na kuzitii amri Zake, ikiwemo kumpenda Mungu kwa moyo wetu wote na kuwapenda jirani zetu kama tunavyojipenda wenyewe.6 Katika agano hilo, Mungu na Kristo wanatusaidia ili tuweze kuwasaidia wale wenye kuhitaji msaada wetu (ona Mosia 4:16; ona pia mistari ya 11–15).

Hakika ninachokihitaji katika maisha ni kuwafurahisha baba zangu---wote wa duniani na wa mbinguni---na kuwa kama Shibloni.7

Ninamshukuru Baba yangu wa Mbinguni kwa watu wa aina ya Shibloni ambao mifano yao inanipa mimi---na sisi sote---tumaini. Katika maisha yao, tunaona ushahidi wa upendo wa Baba wa Mbinguni na Mwokozi mwenye kujali na mwenye huruma. Ninaongeza ushuhuda wangu juu ya ushuhuda wao pamoja na ahadi kwamba tujitahidi kuwa zaidi kama wao, katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Dieter F. Uchtdorf, “Lord, Is It I?” Ensign au Liahona, Nov. 2014, 58; mkazo umeongezewa.

  2. Helamani hakwenda kuwafundisha Wazorami, hivyo tunajua kwamba Alma anaongelea juu ya Shibloni pale anaposema, “kaka yako” (ona Alma 31:7; 39:2).

  3. Spencer W. Kimball, “The Role of Righteous Women,” Ensign, Nov. 1979, 104.

  4. “Bwana alitufundisha kwamba tunapoongoka kwa dhati katika injili Yake, mioyo yetu itageuzwa toka kwenye kujali ubinafsi na kugeukia katika kuwainua wengine wanaposonga mbele kwenye uzima wa milele. Ili kupata uongofu huo, tunaweza kuomba na kutenda katika imani ili kuwa kiumbe kipya kilichowezeshwa na Upatanisho wa Yesu Kristo. Tunaweza kuanza kwa kuomba kwa ajili ya imani ya kutubu ubinafsi na kwa ajili ya kipawa cha kuwajali zaidi wengine kuliko sisi wenyewe. Tunawaweza kuomba kwa ajili ya uwezo wa kuacha kiburi na wivu” (Henry B. Eyring, “Testimony and Conversion,” Ensign or Liahona, Feb. 2015, 4–5).

  5. “ [Mungu] ni asiyekufa na ni mkamilifu. Sisi ni wenye kufa na si wakamilifu. Hata hivyo tunatafuta njia kata katika umauti ambapo tunaweza kuungana na Yeye kiroho. Kwa kufanya hivyo tunapata yote neema na uweza wa nguvu Zake. Zile nafasi maalumu ikijumuisha … ubatizo na kuthibitishwa … [na] kupokea nembo za Chakulacha Bwana” (Jeffrey R. Holland, To My Friends [2014], 80).

  6. “Watakatifu wa Siku za Mwisho ambao wanajiona katika yote wanayofanya kama watoto wa Mungu wanachukulia kwa uhalisi kufanya na kuweka masharti. Mpango wa wokovu umechongwa na maagano. Tunaahidi kutii amri. Naye Mungu anaahidi Baraka katika maisha haya na milele. Yeye ni thabiti katika kile anachohitaji, yeye kamili katika kuweka ahadi yake. Kwa sababu anatupenda na kwa sababu kusudi la mpango huu ni kuwa kama yeye, anahitaji uthabiti kutoka kwetu. Na ahadi anazofanya kwetu daima zinajumuisha nguvu za kukua katika uwezo wetu wa kuweka maagano. Yeye utuwezesha kujua sheria zake. Tunapojaribu kwa mioyo yetu yote kufikia viwango vyake, yeye hutupatia uwenzi wa Roho Mtakatifu. Kwani hiyo yote huongeza uwezo wetu wa kuweka masharti na kubainisha kile kilicho chema na kweli. Na hiyo ndiyo nguvu ya kujifunza, yote katika mafunzo yetu ya duniani na kujifunza kile tunahitaji kwa milele” (Henry B. Eyring, “A Child of God” [Brigham Young University devotional, Oct. 21, 1997], 4–5; speeches.byu.edu). Ona pia David A. Bednar, “Bear Up Their Burdens with Ease,” Ensign or Liahona, May 2014, 87–90.

  7. Kutoka kwa kumbukumbu zangu za mapema, nilitaka kumfurahisha baba yangu. Nilipokuwa ninakua na kupata ushuhuda, pia nilipata hamu ya kumfurahisha Baba wa Mbinguni. Baadaye katika maisha yangu, nilijifunza kuhusu Shibloni na kuongezea kwenye malengo ya maisha yangu kuwa kama yeye.