2010–2019
Watakatifu wa Siku za Mwisho Endeleeni Kujaribu
Aprili 2015


10:29

Watakatifu wa Siku za Mwisho Endeleeni Kujaribu

Tunapojaribu, kustahimili, na kuwasaidia wengine kufanya vivyo hivyo, sisi tunakuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho wakweli.

Ndugu na dada zangu wapendwa, mnamo Desemba 2013 ulimwengu uliomboleza kifo cha Nelson Mandela. Baada ya miaka 27 ya kufungwa jela kwa ajili ya nafasi yake katika jitihada za kupinga ubaguzi wa rangi, Mandela alikuwa rais wa kwanza wa Afika ya Kusini aliyechaguliwa kidemokrasia. Msamaha wake kwa wale waliomfunga ulikuwa wa kustaajabisha. Alipokea heshima kote ulimwenguni na kutukuzwa. 1 Kila mara Mandela alikataa kutukuzwa huko kwa kusema, “mimi siyo mtakatifu—kwamba, isipokuwa kama mnafikiria kuwa mtakatifu ni mtu mwenye dhambi anayeendelea kujaribu kila mara.”2

Kauli hii – “mtakatifu ni mwenye dhambi anayeendelea kujaribu kila mara”---inapawa ilete hakikisho tena na kuwatia moyo waumini wa Kanisa. Ingawa tunatambulika kama “Watakatifu wa Siku za Mwisho,” mara nyingine huwa tunakosa ujasiri katika kielelezo hiki. Neno Watakatifu linatumika kwa kawaida kuwalenga wale ambao washapata hali ya kuinuliwa ya utukufu au hata ukamilifu. Tunajua vyema kwamba sisi si wakamilifu.

Teolojia yetu inatufundisha, ingawa, kwamba tunaweza kutakaswa kwa kurudia na mwendelezo wa “kutegemea kabisa kwenye” mafundisho ya Kristo: kuifanyia kazi imani yetu katika Yeye, kutubu, kupokea sakramenti katika kufanya upya maagano na baraka za ubatizo, na kumtegemea Roto Mtakatifu kama mwenza wa kila wakati. Tunavyofanya hivyo, tukakuwa kama Kristo na kuvumilia hadi mwisho, na yote yanayoambatana nayo.3 Katika maelezo ya kawaida, Mungu anajali sana kuhusu sisi ni nani na tunaelekea kuwa nani, kuliko juu ya sisi wakati fulani tulikuwa nani. 4 Anajali kwamba tunaendelea kujaribu.

Tamthilia ya kuchekesha As You Like It, imeandikwa na mwandishi Muingereza wa michezo William Shakespeare, inaonyesha mabadiliko ya ghafla katika maisha ya mhusika. Kaka mkubwa anajaribu kufanya kaka yake mdogo auwawe. Hata kwa kujua hili, mdogo wake wa kiume anamuokoa kaka yake muovu asiuawe. Wakati kaka yake mkubwa anapojua kuhusu huruma huu usiyostahili, anabadilika kabisa na kile kinachoitwa “uongofu,” Baadaye wanawake kadhaa walimkaribia kaka yao mkubwa na kumuuliza, “Siyo wewe ambaye mara kadhaa ulijaribu kumuua [kaka yako]?

Kaka mkubwa akajibu, “Mwanzoni nalikuwa; lakini sasa siyo: Sioni aibu kukwambia nani nilikuwa, kwa kuwa mazungumzo yangu yana ladha tamu, kuwa kile nilicho.” 5

Kwetu sisi, kwa sababu ya Rehema ya Mungu na upatanisho wa Yesu Kristo, badiliko kama hilo siyo tu hadithi ya kufikiria. Kupitia Ezekieli, Bwana anatangaza:

“Na kwa habari ya uovu wake mtu mwovu, hataanguka kwa ajili ya uovu huo, siku ile atakapoghairi na kuuacha uovu wake. …

“… Kama atageua na kuiacha dhambi yake, na kutenda yaliyo halali na haki;

“… Akirudisha rehani, na kumrudishia mtu mali yake aliyomnyang’anya, akizifuata sheria za uzima, asitende uovu wo wote; hakika ataishi, hatakufa. …

“Katika dhambi zake zote alizozitenda, hata mojawapo haitakumbukwa juu yake; ametenda yaliyo halali na haki.”6

Katika rehema zake, Mungu anaahidi msamaha tunapotubu na kuyakimbia maovu—zaidi ya kwamba dhambi zetu hazitatajwa kamwe kwetu. Kwetu sisi, kwa sababu ya Upatanisho wa Kristo na toba yetu, tunaangalia katika matendo yetu yaliyopita na kusema, “Huyo alikuwa mimi lakini sivyo nilivyo sasa.” Bila kujali uovu, tunaweza kusema, “Huyo ndio nilivyokuwa. Lakini huyo muovu niliyekuwa si tena nilivyo.”7

Rais Thomas S. Monson amefundisha, “Moja ya zawadi kubwa ya Mungu kwetu ni furaha ya kujaribu tena, kwani hakuna kushindwa tena kunakopaswa kuwa kwa mwisho.”8 Hata kama tumekuwa watenda dhambi wa makusudi na wakujitambua au kwa kurudia rudia tumekumbana na kushindwa na kukatishwa tamaa, kipindi tunapoamua kujaribu tena, Upatanisho wa Kristo unaweza kutusaidia. Na tunatakiwa kukumbuka kwamba siyo Roho Mtakatifu ambaye anatuambia tumeshapotea sana kwamba tunapaswa kukata tamaa.

Matamanio ya Mungu kwamba Watakatifu wa Siku za Mwisho waendelee kujaribu yanapitiliza zaidi ya kuishinda dhambi. Iwe tunapata taabu kwa sababu ya uhusiano uliyovunjika, changamoto za kiuchumi, au magonjwa, au kama matokeo ya dhambi za mtu mwingine, Upatanisho wa Milele wa Mwokozi unaweza kuponya—hasa hasa—wale ambao wamepata taabu bila hatia. Anaelewa vyema jinsi ilivyo kutaabika bila hatia kama matokeo ya dhambi za mtu mwingine. Kama ilivyotabiriwa, Mwokozi “atawaganga waliovunjika moyo, … …kuwapa … taji la maua badala ya majivu, mafuta ya furaha badala ya maombolezo, vazi la sifa badala ya roho nzito.”9 Bila kujali ni nini, kwa msaada wake, Mungu anatutegemea Watakatifu wa Siku za Mwisho kuendelea kujaribu.

Jinsi vile Mungu hufurahia tunapovumilia,Yeye anakatishwa tamaa kama hatutambui kwamba wengine wanajaribu pia. Rafiki yetu mpendwa Thoba alitusimulia jinsi gani alijifunza somo hili kutoka kwa mama yake, Julia. Julia na Thoba walikuwa miongoni mwa waongofu wa kwanza weusi Afrika ya Kusini. Baada ya utawala wa ubaguzi kuisha, waumini weusi na weupe waliruhusiwa kuhudhuria kanisani pamoja. Kwa wengi, usawa wa mawasiliano kati ya matabaka ulikuwa mpya na wenye changamoto. Siku moja wakati Julia na Thoba wanahudhuria kanisani, walihisi kuwa hawatendewi vyema na baadhi ya waumini weupe. Walipokuwa wanaondoka, Thoba alilalamika kwa uchungu kwa mama yake. Julia alimsikiliza kwa umakini mpaka Thoba alipotoa hasira zake. Baadaye Julia akasema: “Ee, Thoba, Kanisa ni kama hospitali kubwa, na sisi wote tunaumwa kwa namna moja au nyingine. Tunakuja kanisani ili kupata msaada.”

Dokezo la Julia lilionyesha umaizi wa thamani. Siyo tu tuvumilie wakati wengine wakiyafanyia kazi maumivu yao, lazima pia tuwe wenye upendo, wavumilivu, wenye kutoa msaada, na waelewa. Jinsi vile Mungu anatupa hamasa ya kuendelea kujaribu, anatutegemea pia kuwaruhusu wengine nafasi ya kufanya vivyo hivyo, kwa wakati wao. Upatanisho utakuja katika maisha yetu hata katika kipimo kikubwa. Hivyo tutagundua kwamba bila kujali tofauti zinazodhaniwa, kila mmoja wetu anahitaji kiasi fulani cha Upatanisho wa milele.

Miaka kadhaa iliyopita, kijana mmoja mahiri aliyejulikana kama Curtis alipata mwito kutumikia kama mmisionari. Alikuwa ni aina ya mmisionari ambaye kila rais wa misheni aliomba kuwa naye. Alikuwa na mtazamo na alifanya kazi kwa bidii. Kuna wakati, alipewa jukumu la kuwa mwenza wa mmisionari asiyekuwa na ujuzi, hakuwa na uzoefu wa kuongea na watu, na hakuwa na msisimuko na hamasa ya kufanya kazi.

Siku Moja wakati wanaendesha baiskeli zao, Curtis aliangalia nyuma na kuona kwamba mwenza wake alikuwa ameshuka kwenye baiskeli kwa ghafla na alikuwa anatembea. Kimya kimya, Curtis alielezea masikitiko yake kwa Mungu; Ni kazi iliyoje kuwekwa pamoja na mwenza ambaye alilazimika kumburuta kila sehemu ili awe naye karibu. Baadaye kitambo, Curtis alikuwa na hisia ya ajabu kama vile Mungu alikuwa anamwambia, “Unajua, Curtis, kulinganisha na mimi, wawili wenu hamna tofauti.” Curtis alijifunza kwamba alihitaji kuwa na subira na mwenza wake asiye mkamilifu ambayo mbali na hayo alikuwa anajaribu kwa njia yake.

Mualiko wangu kwetu sisi ni kujifanyia tathmini katika maisha yetu, kutubu, na kuendelea kujaribu. Kama hatujaribu, ni watenda dhambi wa siku za mwisho; Kama hatutavumilia, tutakuwa wakata tamaa wa siku za mwisho; na kama hatutawaruhusu wengine kujaribu, tutakuwa wanafiki wa siku za mwisho.10 Tunavyojaribu, kuvumilia, na kuwasaidia wengine kufanya hivyo, tunakuwa watakatifu wa siku za mwisho wakweli. Tunavyobadilika, tutaona kwamba Mungu kweli anajali zaidi juu ya sisi ni nani na juu ya sisi tunakuwa nani, kuliko juu ya sisi tulikuwa nani wakati fulani.11

Ninashukuru sana kwa Mwokozi, kwa upatanisho Wake wa milele, na kwa manabii wa siku za mwisho ambao hututia moyo kuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho, tukiendelea kujaribu. 12 Nashuhudia juu ya uhalisi wa maisha ya Mwokozi katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Ona Nelson Rolihlahla Mandela, Long Walk to Freedom (1994); “Biography of Nelson Mandela,” nelsonmandela.org/content/page/biography; and President Barack Obama’s Dec. 10, 2013, eulogy for Nelson Mandela, at whitehouse.gov/the-press-office/2013/12/10/remarks-president-obama-memorial-service-former-south-african-president-. The diversity of the awards is indicated by Mandela receiving the Nobel Peace Prize, the United States Presidential Medal of Freedom, and the Soviet Order of Lenin.

  2. Ona kwa mfano, hotuba ya Nelson Mandela katika Taasisi ya Baker ya Chuo Kikuu cha Rice mnamo Oktoba 26, 1999. Inawezekana alikuwa ananukulu kauli inayojulikana sana inayohusishwa Robert Louis Stevenson: “Watakatifu ni watenda dhambi wanaondelea kujaribu.” Kwa miaka mingi wengi wameelezea kauli hizo hizo. Kwa mfano, Confucius alipewa sifa kwa kusema, “Utukufu wetu mkuu haupo katika sianguki kamwe….lakini katika kuamka kila mara tuangukapo.”

  3. Ona kwa mfano, 2 Nefi 31:2–21; 3 Nefi 11:23–31; 27:13–21; Moroni 6:6; Mafundisho na Maagano 20:77, 79; 59:8–9; Handbook 2: Administering the Church (2010), 2.1.2.

  4. Kusema kwamba “Mungu anajali milele yote kuhusu sisi ni nani na ni nani tunakuwa, Zaidi ya kuhusu ni nani tulikuwa” haimaanishi kwamba Mwokozi hajali matokeo ya dhambi binafsi kwa wengine. Kiukweli, Mwokozi anajali milele yote kuhusu wale wanaopata maumivu, kuumizwa, na kuvunjika moyo kwa sababu ya dhambi zao. Mwokozi “atajichukulia unyonge [wa watu Wake], ili moyo wake ujae rehema, … kulingana na mwili jinsi ya kuwasaidia watu wake kulingana na unyonge wao” (Alma 7:12).

  5. William Shakespeare, As You Like It, act 4, scene 3, lines 134–37.

  6. Ezekieli 33:12, 14–16.

  7. Matumizi ya njeo ya wakati wa sasa katika vitenzi yanaonekana sana katika maandiko mengi yanayohusiana na Hukumu ya Mwisho. Ona, kwa mfano, 2 Nefi 9:16; Mormoni 9:14; Mafundisho na Maagano 58:42–43.

  8. Thomas S. Monson, “The Will Within,” Ensign, May 1987, 68.

  9. Isaya 61:1–3; ona pia Luka 4:16–21.

  10. Mnafiki kama linavyotumika katika Agano Jipya linaweza kutafsiriwa kutoka Kigriki kama “mwenye kujifanya; neno la Kigriki humaanisha “mcheza sanaa,” au “mtu anayejifanya, anayeonyesha kitamthiliya, au kutia chumvi” ((Mathayo 6:2, tanbihi a). Kama tusipowapatia wengine nafasi ya kubadilika kwa mwendo wao wenyewe, basi sisi tunajifanya kuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho.

  11. Ona muhtasari wa 4, hapo juu.

  12. Idadi ya mara ujumbe huu hutokea katika mahubiri ya Urais wa Kwanza na Akidi ya Mitume Kumi na Wawili huonyesha umuhimu, Rais Dieter F. Uchtdorf alisisita hivi aliposema, Juu ya kanuni zote zilifunzwa na manabii katika karne zote, moja ambayo imesisitiziwa tena na tena ni ujumbe wa matumaini na kutia moyo kwamba binadamu wanaweze kutubu, kubadilisha mwenendo, na kurudi katika njia ya kweli ya uanafunzi” (“You Can Do It Now!” Ensign au Liahona, Nov. 2013, 56).