Kuhifadhi Haki ya Kujiamulia, Kulinda Uhuru wa Kidini
Matumizi mema ya haki yetu ya kujiamulia yanategemea uwepo wa uhuru wetu wa dini.
Hii ni Jumapili ya Pasaka: siku ya shukrani na ukumbusho wa kuheshimu Upatanisho wa Mwokozi wetu Yesu Kristo na Ufufuo kwa wanadamu wote. Tunamwabudu Yeye, tunashukuru kwa uhuru wetu wa dini, uhuru wa kukusanyika, uhuru wa kusema, na haki yetu ya kujiamulia tuliyopewa na Mungu.
Jinsi manabii walivyotabiri kuhusu siku hizi za mwisho tunazoishi, kuna wengi waliochanganyikiwa kuhusu uhalisi wetu na kile tunachoamini. Wengine ni “wasingiziaji... [na] wasiopenda mema.”1 Wengine “wanasema kwamba uovu ni wema, na kwamba wema ni uovu; [na] wanatia giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza.”2
Wakati wale walio karibu nasi wanapofanya maamuzi juu ya namna ya kukabiliana na imani yetu, lazima tusisahau kwamba haki ya kujiamulia kimaadili ni sehemu muhimu ya mpango wa Mungu kwa watoto wake wote. Mpango huo wa milele, uliowasilishwa kwetu katika Baraza la Mbinguni, ulijumulisha hiki kipawa cha haki ya kujiamulia.3
Katika baraza hilo kuu, Lusiferi, anayejulikana kama Shetani, alitumia haki yake ya kujiamulia kupinga mpango wa Mungu. Mungu alisema, “Kwa sababu … Shetani aliasi dhidi yangu, na akatafuta kuangamiza haki ya mtu ya kujiamulia, ambayo Mimi, Bwana Mungu, nimempa, … nikamfanya atupwe chini.”4
“Na pia theluthi moja ya majeshi ya mbinguni aliyafanya yanigeuke kwa sababu ya haki yao ya kujiamulia.”5
Matokeo yake, watoto wa kiroho wa Baba wa Mbinguni ambao walichagua kukataa mpango Wake na kumfuata Lusiferi walipoteza hatima yao takatifu.
Yesu Kristo, akitumia haki Yake ya kujiamulia, alisema:
“Niko hapa, nitume mimi.”6
“Utakalo lifanyike, na utukufu uwe wako milele.”7
Yesu ambaye alitekeleza haki Yake ya kujiamulia kwa kukubali mpango wa Baba wa Mbinguni alitambuliwa na kuteuliwa na Baba kama Mwokozi wetu, aliyeteuliwa tangu mwanzo kulipia dhabihu ya upatanisho kwa wote. Vile vile kutekeleza haki yetu ya kujiamulia kutii amri kunatuwezesha kuelewa uhalisi wetu na kupokea baraka zote ambazo Baba yetu wa Mbinguni anazo---ikijumuisha nafasi ya kuwa na mwili, kupata furaha, kupata familia, na kurithi uzima wa milele.
Ili kutii amri, tunahitaji kujua mafundisho rasmi ya Kanisa hivyo ili tusitoke katika uongozi wa Kristo kwa kuvutiwa na vinavyobadilika kila mara vya watu binafsi.
Baraka tunazofurahia sasa ni kwa sababu tulichangua kumfuata Mwokozi kabla ya maisha haya. Kwa kila mtu anayesikia au kusoma maneno haya, uwe nani na chochote ulichofanya na maisha yako ya awali, kumbuka hili: haujachelewa sana kufanya uchaguzi ule ule tena na kumfuata Yeye.
Kupitia imani yetu katika Yesu Kristo, kuamini katika Upatanisho Wake, kutubu dhambi zetu, na kubatizwa, kisha tunaweza kupokea kipawa kitakatifu cha Roho Mtakatifu. Kipawa hiki hutoa ujuzi na ufahamu, ushauri na nguvu ya kujifunza na kupata ushahuda, nguvu, na utakaso wa kushinda dhambi, na faraja na himizo la kuwa waaminifu katika dhiki. Baraka hizi zisizo na kifani za Roho huongeza uhuru wetu na uwezo wa kufanya kilicho cha haki, kwa sababu “alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru.”8
Tunapotembea njia ya uhuru wa kiroho katika siku hizi za mwisho, ni lazima tuelewe kwamba matumizi mema ya haki yetu ya kujiamulia yanategemea uwepo wa uhuru wetu wa dini. Tayari tunajua kwamba Shetani hataki uhuru huu kuwa wetu. Alijaribu kuharibu uhuru wetu wa kimaadili huko mbinguni, na sasa duniani anadhoofisha vikali, kupinga, na kueneza mkanganyiko kuhusu uhuru wa dini---ni nini, na kwa nini, ni muhimu kwa maisha yetu ya kiroho na wokovu wetu.
.Kuna nguzo nne za msingi ya uhuru wa dini ambao sisi kama Watakatifu wa Siku za Mwisho lazima tuzitegemee na kuzilinda.
Yaa kwanza ni uhuru wa kuamini. Hakuna anayepaswa kushtumiwa, kuteswa, au kushambuliwa na watu binafsi au serikali kwa kile anachoamini kuhusu Mungu. Ni wa kibinafsi na muhimu sana. Tamko la zamani la imani yetu kuhusu uhuru wa dini linasema:
“Hakuna serikali inayoweza kudumu katika amani, isipokuwa sheria hizo zimetungwa na kutunzwa bila kuvunjwa endapo zitamhakikishia kila mtu uhuru wa kutoa mawazo. …
“… kwamba mahakimu wa serikali wanapaswa kuzuia makosa ya jinai, lakini kamwe hawapaswi kuthibiti uhuru wa mawazo [au] kukandamiza uhuru wa nafsi.”9
Uhuru huu wa msingi wa imani tayari umekubalika na Umoja wa Mataifa katika Azimio lake la Ulimwengu la Haki za Binadamu na katika nyaraka nyingine za haki za binadamu za kitaifa na kimataifa.10
Nguzo ya pili ya msingi wa uhuru wa kidini ni uhuru wa kushiriki imani yetu na watu wengine. Bwana anatuamuru, “Wafunzeni [injili] vijana vyenu … uketipo katika nyumba yako.”11 Pia alisema kwa wanafunzi Wake, “Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri injili kwa kila kiumbe.”12 Kama wazazi, wamisionari wa muda, na wamisionari waumini, tunategemea uhuru wa kidini ili kufundisha mafundisho ya Bwana katika familia zetu na duniani kote.
Nguzo ya tatu ya msingi wa uhuru wa kidini ni uhuru wa kuunda taasisi ya kidini na kuabudu kwa amani na watu wengine. Makala ya kumi na moja ya imani inasema, “Tunadai haki ya kumwabudu Mungu Mwenyezi kulingana na mwongozo wa dhamiri yetu sisi wenyewe, na tunawaruhusu watu wote haki hiyo, na waabudu namna, mahali, au chochote watakacho.” Nyaraka za Kimataifa za haki za binadamu na katiba nyingi za kitaifa zinaiunga mkono kanuni hii.
Nguzo ya nne ya msingi wa uhuru wa kidini ni uhuru wa kuishi imani yetu---Uhuru wa kutekeleza imani si tu nyumbani na kanisani lakini pia katika maeneo ya umma. Bwana anatuamrisha tusiombe tu kisiri13 bali pia tusonge mbele na “nuru [yetu] na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo [yetu] mema, wamtukuze Baba [yetu] aliye mbinguni.”14
Wengine huudhika tunapoleta dini yetu katika uwanja wa umma, ilihali watu wale wale ambao husisitiza kwamba maoni na matendo yao yavumiliwe katika jamii, mara nyingi huwa wazito sana katika kutoa uvumilivu huo huo kwa waumini wa dini nyingine ambao pia wanataka maoni na matendo yao yavumiliwe. Ukosefu mwingi wa heshima kwa maoni ya kidini unageuka kwa haraka kuwa chuki ya kijamii na kisiasa kwa watu wa kidini na taasisi.
Tunapopitia shinikizo nyingi za kunyenyekea kwa mahitaji ya kidunia, kuacha uhuru wetu wa kidini, na kuhujumu uwakala wetu, fikiria kile Kitabu cha Mormoni kinachofundisha kuhusu majukumu yetu. Katika kitabu cha Alma tunasoma kuhusu Amlisi, mtu “mjanja sana” na “mtu mwovu” ambaye alitaka kuwa mfalme wa watu na “angewanyang’anya haki na heshima zao, ... [ambayo] ilikuwa tisho kwa watu wa kanisa.”15 Walikuwa wamefundishwa na Mfalme Mosia kupaza sauti zao kwa kile kisichokuwa sahihi.16 Kwa hiyo “walikusanyika pamoja kote nchini, kila mtu kulingana na mawazo yake, kama ilikuwa wanamtaka au wanampinga Amlisi, katika vikundi tofauti, wakipingana sana na kuwa na mabishano ya kushangaza…wao kwa wao.”17
Katika majadiliano hayo, waumini wa Kanisa na wengine walikuwa na nafasi ya kukutana pamoja, kuona roho ya umoja, na kuongozwa na Roho Mtakatifu. “Na ikawa kwamba kura za watu zilikuwa kinyume cha Amlisi, kwamba hakufanywa mfalme wa watu.”18
Kama wafuasi wa Kristo tuna wajibu wa kufanya kazi pamoja na waumini wenye mawazo sawa, ili kupaza sauti zetu kwa kile kilichosahihi. Wakati ambapo waumini hawapaswi kudai au hata kuashiria kwamba wanazungumza kwa niaba ya Kanisa, sisi sote tumealikwa, katika viwango vyetu kama wananchi, kutoa ushuhuda wetu binafsi kwa uthabiti na upendo---“kila mtu kulingana na mawazo yake.”19
Alisema Nabii Joseph Smith:
“Nina ujasiri kutangaza mbele ya Mbingu kwamba mimi kama niko tayari kufa katika kutetea haki za mpresibiteri, Mbaptisti, au mtu mwema wa dhehebu nyingine yoyote [kama ilivyo kwa Mmormoni]; kwa kanuni hiyo hiyo ambayo itakiuka haki za Watakatifu wa Siku za Mwisho itakiuka haki za Wakatoliki, au ya dhehebu nyingine yoyote ambao si maarufu na wadhaifu mno kujitetea.
“Ni kupenda uhuru ambao unaivutia nafsi yangu—uhuru wa kiraia na kidini kwa jamii nzima ya wanadamu.”20
Kaka na dada zangu, tunawajibu wa kulinda uhuru huo mtakatifu, na haki kwetu wenyewe na vizazi vyetu. Mimi na wewe tunaweza kufanya nini?
Kwanza, tunahitajika kuwa uelewa. Ufahamu masuala katika jamii yako ambayo yanaweza kuwa na athari juu ya uhuru wa kidini.
Pili, katika uwezo wako binafsi, jiunge na wengine wanaoshiriki ahadi yetu ya uhuru wa kidini. Fanya kazi bega kwa bega ili kulinda uhuru wa kidini.
Tatu, ishi maisha yako ili uwe mfano mzuri wa kile unachoamini---katika neno na matendo. Jinsi tunavyoishi dini yetu ni muhimu zaidi kuliko yale tunayoweza kusema kuhusu dini yetu.
Ujio wa pili wa Mwokozi wetu unakaribia. Hebu tusichelewe katika kazi hii kubwa. Kumbukeni Kapteni Moroni ambaye aliinua bendera ya uhuru ikiwa na maneno: “kwa ukumbusho wa Mungu wetu, dini yetu, na uhuru, na amani yetu, wake zetu, na watoto wetu.”21 Acha tukumbuke majibu ya watu: wakitumia uwakala wao, “walikuja wakikimbia pamoja” na makubaliano ya kutenda.22
Wapendwa kaka na dada zangu, msitembee! Kimbieni! Kimbieni ili mpokee baraka za haki ya kujiamulia kwa kumfuata Roho Mtakatifu na kutumia uhuru ambao Mungu ametupa sote ili kufanya mapenzi Yake.
Natoa ushuhuda wangu maalum kwamba Yesu Kristo alitumia haki Yake ya kujiamulia kwa kufanya mapenzi ya Baba yetu wa Mbinguni.
Kuhusu Mwokozi wetu, tunaimba, “Damu yake ya thamani yeye aliimwaga kwa hiari; Uzima Wake aliutoa kwa hiari.”23 Na kwa sababu alifanya hivyo, tuna fursa yenye thamani ya “kuchagua uhuru na uzima wa milele” kupitia katika nguvu na baraka za Upatanisho.24 Acha tuchague uhuru kumfuata Yeye leo na siku zote, naomba katika jina Lake takatifu, hata Yesu Kristo, amina.