Kama Mtaweza Kuwajibika
Acha tusonge mbele kwa kujifunza wajibu wetu, kufanya maamuzi sahihi, kutenda kulingana yale maamuzi, na kukubali mapenzi ya Baba yetu.
Nilikuwa na umri wa miaka 12 tu wakati wamisionari walipowasili kwa mara ya kwanza kuhubiri katika mji ambapo nilizaliwa kaskazini mwa Chile. Jumapili moja, baada ya kuhudhuria tawi dogo kwa miezi sita, mmisionari alinipatia mkate alipokuwa anapitisha sakramenti. Nilimtazama na kwa upole nikasema, “Siwezi.”
“Kwa nini?” yeye akajibu.
Nikamwambia, “Kwa sababu mimi si muumini wa Kanisa.”1
Mmisionari huyu hakuweza kuamini. Macho yake yalikuwa angavu. Mimi nikadhani alifikiria, “Lakini huyu kijana yupo katika kila mkutano! Inawezekanaje yeye si muumini wa Kanisa?”
Siku iliyofuata, wamisionari walifika nyumbani kwetu haraka, na wakafanya kila kitu ambacho wangeweza kufanya kuifundisha familia yangu yote. Kwa vile familia yangu haikuwa na hamu, ilikuwa tu mahudhurio yangu ya kila wiki kwa zaidi ya miezi sita ambayo yaliwafanya wamisionari wahisi kujiamini sana kuendelea. Mwishowe, siku kubwa niliokuwa ninaingojea ikaja wakati waliponialika kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo. Wamisionari walinielezea kwamba kwa sababu mimi nilikuwa mtoto, ningehitaji ruhusa ya wazazi wangu. Nilienda kumwona baba yangu, nikifikiria kwamba jibu lake la upendo lingekuwa “Mwanangu, wakati utakapofika umri wa kuwajibika, utaweza kufanya maamuzi yako mwenyewe.”
Wakati wamisionari walipokuwa wakizungumza naye, mimi niliomba kwa dhati ili moyo wake uguswe ili anipe ruhusa niliyotaka. Jibu lake kwa wamisionari likuwa kama ifuatavyo: “Wazee, kwa zaidi ya miezi sita, nimemwona mwanangu Jorge akiamka mapema kila asubuhi ya Jumapili, na kuvalia nguo zake nzuri, na kutembea hadi kanisani. Nimeona tu ushawishi bora kutoka kwa Kanisa katika maisha yake.” Kisha, akisema nami, alinishangaza kwa kusema, “Mwanangu, kama wewe utaweza kuwajibika kwa maamuzi haya, basi una ruhusa yangu kubatizwa.” Mimi nilimkumbatia baba yangu, nikampiga busu, na nikamshukuru kwa kile alichokifanya. Siku iliyofuata nilibatizwa. Wiki iliyopita ilikuwa ni siku ya makumbusho ya mwaka wa 47 ya ile siku muhimu katika maisha yangu.
Je! Sisi tuna jukumu gani kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo? Rais Joseph Fielding Smith alieleza kama ifuatavyo: “Sisi tuna majukumu mawili muhimu. … Kwanza, kutafuta wokovu wetu wenyewe; na, pili, wajibu wetu kwa binadamu wenzetu.”2
Haya, basi, ndiyo majukumu muhimu ambayo Baba yetu ametupatia sisi: kutafuta wokovu wetu wenyewe na ule wa wengine, kwa uelewa huu kwamba katika kauli hiiwokovu humaanisha kufikia kiwango cha juu sana cha utukufu ambacho Baba yetu hutoa kwa watoto Wake watiifu.3 Majukumu haya ambayo yamekabithiwa kwetu---na ambayo tuliyakubali kwa hiari---sharti yaelezee vipaumbele vyetu, hamu zetu, maamuzi yetu, na mwenendo wetu wa kila siku.
Kwa mtu ambaye amepata kuelewa kwamba, kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, kuinuliwa kwa hakika kunawezekana, kushindwa kukupata huleta maangamizo. Basi, kinyume cha wokovu ni maangamizo, kama vile kinyume cha ufanisi ni kudorora. Rais Thomas S. Monson ametufundisha kwamba “watu kwa kweli hawawezi kutosheka na uhafifu mara wanapoona ubora upo karibu nao.”4 Ni kwa vipi, basi, tuweze kutosheka kwa chochote kilicho chini kuliko kuinuliwa ikiwa tunajua kwamba kuinuliwa kunawezekana?
Nikubalieni nishiriki kanuni nne muhimu ambazo zitatusaidia kutimiza hamu zetu za kuwajibika kwa Baba yetu wa Mbinguni, pamoja na kujibu matarajio Yake kwamba tutakuwa kama Yeye alivyo.
1. Kujifunza Wajibu Wetu
Kama tutafanya mapenzi ya Mungu, kama tutawajibika Kwake, ni sharti tuanze kwa kujifundisha, kuelewa, kukubali, na kuishi kulingana na mapenzi Yake kwetu. Bwana amesema, “Kwa sababu hiyo, sasa acha kila mtu na ajifunze wajibu wake, na kutenda kazi katika ofisi ambayo ameteuliwa, kwa bidii yote.”5 Kuwa na hamu kufanya kile kilicho sahihi haitoshi kama hatuakikishi kuelewa kile Baba yetu anatarajia kutoka kwetu na anatutaka tufanye.
Katika hadithi ya Alice in Wonderland, Alice hajui njia gani ya kwenda, kwa hiyo anamuuliza Chesire Cat, “Je! Unaweza kuniambia, tafadhali, ni njia gani ninapaswa kwenda kutoka hapa?”
Yule paka anajibu, “Hiyo inategemea kwa kiwango kikubwa pale unapotaka kufika”
Alice anasema, “Mimi sijali sana ni wapi.”
“Basi haijalishi ni njia gani utaenda,” akasema yule paka.6
Hata hivyo, sisi tunajua njia ambayo inaelekea kwenye “mti, ambao matunda yake yalitamanika kumfurahisha mwanadamu”7---“njia, imesonga iendayo uzimani”---ni nyembamba, inahitaji juhudi kusafiri katika njia hiyo, na “nao waionao ni wachache.”8
Nefi anatufundisha kwamba “maneno ya Kristo yatawaelezea vitu vyote mnavyostahili kutenda.”9 Kisha anaongezea “Roho Mtakatifu, atawaonyesha vitu vyote ambavyo mnastahili kutenda.”10 Basi, viini ambavyo vinaturuhusu kujifunza wajibu wetu ni maneno ya Kristo ambayo tunapokea kupitia manabii wa kale na wa sasa na ufunuo wa kibinafsi ambao tunapokea kupitia kwa Roho Mtakatifu.
2. Kufanya Uamuzi
Iwe tumejifunza kuhusu Urejesho wa injili, amri fulani, wajibu unaohusiana na kutumika katika wito, au maagano tunayofanya katika hekalu, chaguo ni letu kama tutatenda kulingana na ile elimu mpya au la. Kila mtu hujichagulia mwenyewe kwa hiari kuingia katika agano takatifu kama vile ubatizo, au ibada za hekaluni. Kwa sababu kuapa viapo ilikuwa kitu cha kawaida katika maisha ya kidini ya watu hapo kale, sheria ya kale ilisema “msiape uongo kwa jina langu.”11 Hata hivyo, katika wakati wa meridiani, Mwokozi alifunza njia ya juu sana ya kuweka masharti yetu wakati Yeye alisema kwamba ndio ilimaanisha ndio na la ilimaanisha la. 12 Neno la mtu linapaswa kuwa linatosha kuonyesha ukweli wake na sharti lake kwa mtu mwingine na hata zaidi wakati yule mtu mwingine ni Baba yetu aliye Mbinguni. Kuheshimu sharti huwa onyesho la ukweli na uaminifu wa neno letu.
3. Kutenda Vilivyo
Baada ya kujifunza wajibu wetu na kufanya maauzi ambayo yanahusiana na kujifunza na uelewa ule, sharti sisi tutende vilivyo.
Mfano wa nguvu sana wa azimio thabiti la kutimiza sharti Lake na Baba Yake hutoka kwa uzoefu wa Mwokozi wa mtu aliyekuwa mgonjwa wa kupooza alipoletwa Kwake kuponywa. “Naye Yesu, alipoiona imani yao, akamwambia yule mwenye kupooza, Mwanangu, umesamehewa dhambi zako.”13 Sisi tunajua kwamba Upatanisho wa Yesu Kristo ni muhimu katika kupokea msamaha wa dhambi zetu, lakini wakati wa tukio la uponyaji wa mtu mwenye kupooza, hilo tukio kuu lilikuwa bado halijafanyika; Gethsemane ilikuwa bado haijafanyika. Hata, hivyo Yesu hakubariki tu mtu huyu mwenye kupooza na uwezo wa kusimama na kutembea, bali pia Yeye alimpatia msamaha wa dhambi zake, kwa hivyo akatoa ishara isiyokanika kwamba Yeye hangeshindwa, kwamba Yeye angetimiza lile sharti Yeye alikuwa amefanya na Baba Yake, na kwamba katika Gethsemane na kwenye msalaba Yeye angefanya kile alichokuwa ameahidi kufanya.
Njia ambayo tumechagua kutembea ni nyembamba. Katika njia hiyo kuna changamoto ambazo zinahitaji imani yetu katika Yesu Kristo na juhudi zetu bora za kukaa katika njia hiyo na kusonga mbele. Tunahitaji kutubu na kuwa watiifu na wenye subira, hata kama hatuelewi hali zote ambazo zinatuzingira. Ni sharti tuwasamehe wengine na kuishi kulingana na kile ambacho tumejifunza na kwa chaguo tulizofanya.
4. Kwa Hiari Kukubali Mapenzi ya Baba
Ufuasi huhitaji sisi siyo tu kujifunza wajibu, kufanya maamuzi sahihi, na kutenda kulingana nayo, bali pia muhimu ni ukuzaji wetu wa upendeleo na uwezo wa kukubali mapenzi ya Mungu, hata kama hayawiani na hamu zetu takatifu au matakwa yetu.
Napendezwa na heshimu mtazamo wa mwenye ukoma ambaye alikuja kwa Bwana, “akamsihi na kumpigia magoti, na kumwambia, Ukitaka, waweza kunitakasa.”14 Mwenye ukoma hakudai chochote, hata ingawa hamu yake inaweza kuwa ilikuwa njema; alikuwa tu tayari kukubali mapenzi ya Bwana.
Miaka kadhaa iliyopita, wenzi wapendwa, waaminifu ambao walikuwa marafiki zangu walibarikiwa na kuwasili kwa mwana aliyetamaniwa sana, ambaye walikuwa wamemuombea sana. Nyumba hiyo ilikuwa imejawa na furaha hali marafiki zetu na binti yao, ambaye ndiye aliyekuwa mtoto wake peke yake wakati huo, walifurahia uwepo wa mvulana mchanga aliyewasili. Siku moja, hata hivyo, kitu kisichotarajiwa kilitokea: yule mvulana mchanga, ambaye alikuwa na umri wa miaka mitatu tu, ghafula akazimia kwa muda mrefu. Punde nilipojua hali hiyo, nilimpigia simu rafiki yangu kuonyesha ufadhili wetu katika wakati huo mgumu. Lakini jibu lake likawa somo kwangu. Alisema, “Ikiwa ni mapenzi ya Baba kumchukua Kwake, basi mambo yote ni sawa kwetu.” Maneno ya rafiki yangu hayakuwa na kiwango chochote cha malalamishi, uasi, au kutoridhika. Kinyume kabisa, yote ningeweza kuhisi katika maneno yake ilikuwa ni shukrani kwa Mungu kwa kuwaruhusu kuwa na mwana huyu mchanga kwa huo muda mfupi, pamoja na hiari yake kukubali mapenzi ya Baba kwa ajili yao. Siku chache baadaye, yule mdogo alichukuliwa kwenda kwenye nyumba yake ya selestia.
Na tusonge mbele kwa kujifunza wajibu wetu, tukifanya maamuzi sahihi, tukitenda kulingana na hayo maamuzi, na kukubali mapenzi ya Baba yetu.
Nina shukrani na furaha jinsi gani kwa maamuzi ambayo baba yangu alifanya miaka 47 iliyopita. Kwa muda mrefu, nimekuja kuelewa kwamba sharti alililonipa---kuwajibika kwa yale maamuzi---kulimaanisha kuwajibika kwa Baba yangu wa Mbinguni na kutafuta wokovu wangu mwenyewe na ule wa binadamu wenzangu, kwa hiyo kuwa zaidi kama vile Baba yangu anavyotarajia na anavyotaka niwe. Katika jina la Yesu Kristo, amina.