Mkutano Mkuu
Inua Moyo Wako na Ufurahi
Mkutano mkuu wa Aprili 2022


11:27

Inua Moyo Wako na Ufurahi

Tulizaliwa katika wakati huu kwa ajili ya kusudi takatifu, kukusanywa kwa Israeli.

Akizungumza na Thomas B. Marsh, mwongofu wa hivi karibuni, Bwana alisema kwa kutia moyo, “Inua moyo wako na ufurahi, kwani saa ya huduma yako imewadia” (Mafundisho na Maagano 31:3).

Naamini mwaliko huu unaweza kutumika kama mwongozo wa kiungu kwa waumini wote wa Kanisa. Hata hivyo, sisi kila mmoja wetu alipokea kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni misheni ya kukusanya Israeli kwenye pande zote mbili za pazia.

“Kukusanya huko,” Rais Russell M. Nelson alisema, “ndilo jambo muhimu sana linalofanyika duniani leo. Hakulinganishwi na chochote katika ukubwa, hakulinganishwi na chochote katika umuhimu, hakulinganishwi na chochote katika utukufu.”1

Hakika, kuna mambo mengi yanayostahili katika ulimwengu. Haiwezekani kuyataja yote. Kwani haungependa kushiriki katika jambo kubwa lililo karibu na wewe na pale mchango wako unapoweza kuleta tofauti? Kukusanya huko kunaleta tofauti ya milele kwa wote. Watu wa umri wote wanaweza kushiriki katika jambo hili bila kujali hali zao na pale wanapoishi. Hakuna jambo lingine katika ulimwengu ambalo linajumuisha zaidi.

Akisema mahususi kwa vijana, Rais Nelson alisema kwamba: “Baba Yetu wa Mbinguni amehifadhi wengi wa watoto wake wa kiroho walio wazuri—labda … timu Yake iliyo bora zaidi—kwa ajili ya awamu hii ya mwisho. Roho hao wazuri—wachezaji hao bora, hao mashujaa—ni ninyi!”2

Ndiyo, ninyi mmeandaliwa kabla ya maisha haya na kuzaliwa sasa ili kushiriki katika kazi hii kuu ya kukusanya Israeli kwenye pande zote za pazia katika hizi siku za mwisho (ona Mafundisho na Maagano 138:53–56).

Kwa nini jambo hili ni muhimu sana? Kwa sababu “thamani ya nafsi ni kubwa mbele za Mungu” (Mafundisho na Maagano 18:10). Na kwa sababu “yeyote aaminiye katika [Yesu Kristo] na kubatizwa, huyo ataokolewa; na … watarithi ufalme wa Mungu” (3 Nefi 11:33). Zaidi ya hayo, “yale yote Baba yangu aliyonayo watapewa” wale ambao watapokea ibada Zake na kuyashika maagano Yake (Mafundisho na Maagano 84:38). Kama nyongeza, “watenda kazi ni wachache” (Luka 10:2).

Ni katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho pekee ndipo tunapata nguvu, mamlaka, na njia ya kutoa baraka kama hizo kwa wengine, iwe kwa walio hai au wamekufa.

Kama Rais Nelson alivyosema: “Wakati wo wote unapofanya kitu cho chote kinachomsaidia mtu yeyote—upande wo wote wa pazia—unachukua hatua kuelekea kufanya maagano na Mungu na kupokea ibada zao muhimu za ubatizo na za hekaluni, unasaidia katika kukusanya Israeli. Ni rahisi tu hivi.”3

Wakati kukiwa na njia nyingi za kusaidia katika kukusanya, ningependa kuzungumza kipekee juu ya njia moja mahususi: kutumikia kama mmisionari. Kwa wengi wenu, hii itamaanisha kuwa mmisionari wa kufundisha. Kwa wengine wengi, itamaanisha kuwa mmisionari wa huduma. Lakini ulimwengu hujaribu kuvuruga mawazo ya vijana kutoka kwa hili jukumu takatifu sana kwa kutumia hofu na mashaka.

Baadhi ya vivuta mawazo vingeweza kuwa kupatwa na janga la ulimwengu, kuacha kazi nzuri, kusimama kimasomo, au kuwa hasa unavutiwa na mtu kimapenzi. Kila mmoja atakuwa na jozi ya changamoto zake mwenyewe. Vivuta mawazo kama hivyo vinaweza kutokea wakati ule ule wa kuanza huduma ya Bwana, na chaguzi ambazo zinaonekana kuwa wazi baadaye daima si rahisi wakati huo.

Najua kutokana na uzoefu wa akili iliyochanganyikiwa ya kijana kama huyo. Nilipokuwa ninajiandaa kwenda misheni yangu, baadhi ya nguvu za kushangaza zilijaribu kunivunja moyo. Mmoja alikuwa daktari wangu wa meno. Alipogundua miada yangu ilikuwa kwa minajili ya kuwa mmisionari, alijaribu kunishawishi nisitumikie. Sikuwa na wazo hata kidogo kuwa daktari wangu wa meno alikuwa anapinga Kanisa.

Kusimamisha kwangu masomo pia ilikuwa tatizo. Nilipoomba ruhusa ya miaka miwili kutohudhuria programu yangu ya chuoni, niliambiwa kwamba haitawezekana. Ningeipoteza nafasi yangu hapo chuoni kama singerudi baada ya mwaka mmoja. Katika Brazili, hili lilikuwa jambo zito sana kwa vile vigezo vya kukubaliwa katika programu ya chuo vilikuwa vigumu na mitihani migumu sana.

Baada ya kusisita mara nyingi, niliambiwa lakini kwa shingo upande kwamba baada ya kutohudhuria kwa mwaka mmoja, ningefanya maombi kwa sababu za kipekee. Yangeweza kukubaliwa au yasikubaliwe. Nilingia hofu kutokana na wazo la kufanya mtihani mgumu tena baada ya miaka miwili bila kusoma.

Pia nilikuwa hasa nilivutiwa na msichana fulani. Baadhi ya marafiki zangu kadhaa nao walikuwa wanavutiwa vile vile. Nikafikiria mwenyewe, “Kama nikienda misheni, nitapoteza bahati yangu.”

Lakini Bwana Yesu Kristo alikuwa mwongozo wangu mkubwa wa kutoogopa juu ya siku za usoni nilipojitahidi kumtumikia Yeye kwa moyo wangu wote.

Yeye pia alikuwa na misheni ya kutimiza. Kwa maneno Yake mwenyewe, Yeye alisema, “Kwa kuwa mimi sikushuka kutoka mbinguni ili niyafanye mapenzi yangu, bali mapenzi yake aliyenipeleka.” (Yohana 6:38). Na Je, misheni Yake ilikuwa rahisi? Hapana haikuwa rahisi. Mateso Yake, ambayo yalikuwa sehemu muhimu ya misheni Yake, yalimsababisha Yeye, “hata Mungu, mkuu kuliko wote, kutetemeka kwa sababu ya maumivu, na kutoka damu kwenye kila kinyweleo, na kuteseka mwili na roho—na kutamani [Yeye] hasinywe kikombe kichungu, na kusita—

“Hata hivyo, utukufu na uwe kwa Baba, na [Yeye] akachukua na kukamilisha maandalizi [Yake] kwa wanadamu” (Mafundisho na Maagano 19:18–19).

Kutumikia misheni inaweza kuonekana kuwa vigumu kwetu. Pengine huhitaji kwamba tuachane na vitu muhimu kwa muda. Bwana hakika anajua hili, na Yeye daima atakuwa upande wetu.

Kwa kweli, katika ujumbe wao kwa wamisionari katika Hubiri Injili Yangu, Urais wa Kwanza uliahidi, “Bwana atawazawadia na kuwabariki sana mnapomtumikia Yeye kwa unyenyekevu na kwa maombi.”4 Ni kweli kwamba watoto wote wa Mungu wanabarikiwa katika njia moja au nyingine, lakini kuna tofauti kati ya kubarikiwa na kubarikiwa sana katika huduma Yake.

Unakumbuka changamoto ambazo nilifikiri nilikabiliana nazo kabla ya misheni? Daktari wangu wa meno? Nilipata mwingine. Chuo changu? Waliondoa kikwazo kwa ajili yangu. Unamkumbuka yule msichana? Aliolewa na mmoja wa marafiki zangu wa dhati.

Lakini Mungu kwa kweli alinibariki sana. Na nilijifunza kwamba baraka za Bwana zinawezza kuja katika njia tofauti na jinsi tunavyotarajia. Hata hivyo, mawazo Yake sio mawazo yetu (ona Isaya 55:8–9).

Miongoni mwa baraka nyingi za utajiri Yeye alizonipa mimi kwa sababu ya kumtumikia Yeye kama mmisionari ni imani kubwa katika Yesu Kristo na Upatanisho Wake na elimu na ushuhuda imara juu ya mafundisho Yake, ili kwamba nisiyumbishwe kwa urahisi na “kila upepo wa elimu” (Waefeso 4:14). Nilipoteza hofu yangu ya kufundisha. Uwezo wangu wa kukabiliana na changamoto nikiwa na matumaini uliongezeka. Kwa kuwatazama watu binafsi na familia niliokutana au kuwafundisha kama mmisionari, nilijifunza kwamba mafundisho ya Mungu ni ya kweli wakati Yeye anaposema kwamba dhambi haituletei furaha ya kweli na kwa utiifu wa amri za Mungu hutusaidia kustawi vyote kiroho na kimwili (ona Mosia 2:41; Alma 41:10). Na nimejifunza mimi mwenyewe kwamba Mungu ni Mungu wa miujiza (ona Mormoni 9).

Mambo haya yote yalikuwa ya msingi katika maandalizi yangu kwa ajili ya maisha ya utu uzima, ikijumuisha uwezekano wa ndoa na hali ya kuwa mzazi, huduma ya Kanisa, na maisha ya kitaaluma na ya kijamii.

Baada ya misheni yangu, nilifaidika kutokana na ongezeko langu la ujasiri wa kujiwasilisha mwenyewe kama mfuasi mwaminifu wa Yesu Kristo na Kanisa Lake katika hali zote na kwa watu wote, hata kushiriki injili na mwanamke mrembo ambaye angekuja kuwa mwenzi wangu mwema mpendwa wa milele, mwenye hekima, mcheshi, na nuru ya maisha yangu.

Ndiyo, Mungu alinibariki sana, zaidi ya kile ambacho ningefikiria, kama jinsi Yeye atakavyofanya kwa wale wote “watakao mtumikia Yeye kwa unyenyekevu na maombi.” Milele ninayo shukrani kwa Mungu kwa ajili ya wema Wake.

Misheni yangu imeunda maisha yangu. Nilijifunza juhudi za kutumaini katika Mungu zinastahili, kutumaini katika hekima Yake na rehema na katika ahadi Zake. Hata hivyo, Yeye ni Baba yetu, na bila shaka yoyote, Yeye hutaka kilicho bora kwa ajili yetu.

Vijana wapendwa kote duniani, natoa mwaliko ule ule ambao nabii wetu, Rais Nelson, ametoa kwenu nyote “kujisajili katika batalioni ya vijana ya Bwana ili kukusanya Israeli.” Rais Nelson alisema:

“Hakuna chochote chenye matokeo makubwa. Hakuna kabisa.

“Kukusanya huku hakuna budi kumaanisha kila kitu kwenu. Hii ni kazi ambayo kwayo wewe ulitumwa duniani.”5

Tulizaliwa katika wakati huu kwa ajili ya kusudi takatifu, kukusanywa kwa Israeli. Tunapohudumu kama wamisionari, tutapatwa na changamoto nyakati fulani, lakini Bwana Mwenyewe ni mfano wetu mkuu na kiongozi katika hali kama hizo. Yeye anaelewa misheni ngumu ni nini. Kwa msaada Wake, tunaweza kufanya mambo magumu. Yeye atakuwa katika upande wetu (ona Mafundisho na Maagano 84:88), na Yeye atatubariki sana tunapomtumikia Yeye kwa unyenyekevu.

Kwa ajili ya sababu hizo zote, mimi sishangai kwamba Bwana alimwambia Thomas B. Marsh na sisi sote, “Inua moyo wako na ufurahi, kwani saa ya huduma yako imewadia.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli” (mkutano wa ibada wa vijana ulimwenguni kote, Juni 3, 2018), HopeofIsrael.ChurchofJesusChrist.org.

  2. Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli.”

  3. Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli.”

  4. Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Huduma ya Umisionari (2019), v.

  5. Russell M. Nelson, “Tumaini la Israeli.”