“Septemba 7–13. 3 Nefi 1–7: ‘Inua Kichwa Chako na Uchangamke,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)
“Septemba 7–13. 3 Nefi 1–7,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2020
Septemba 7–13
3 Nefi 1–7
“Inua Kichwa Chako na Uchangamke”
Kama utahitaji mawazo ya ziada unapojiandaa kufundisha, ona “Nyenzo za Ziada kwa ajili ya Kufundisha Watoto” na “Kukidhi Mahitaji ya Watoto Wadogo” mwanzoni mwa muhtasari huu.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Waalike watoto kushiriki kile wanachokumbuka kujifunza wiki iliyopita kuhusu ishara Samweli Mlamani alizosema zingewasaidia watu kujua kwamba Yesu alikuwa amezaliwa. Waambie watoto kwamba leo watazungumza kuhusu watu walioona ishara hizo zikitokea.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Nyota mpya ilitokea wakati Yesu Kristo alipozaliwa.
Maelezo ya Agano Jipya ya kuzaliwa kwa Mwokozi yanajulikana vizuri, hata kwa watoto. Wiki hii ni fursa kubwa ya kuwafundisha watoto darasani kwako kuhusu miujiza waliyoshuhudia Wanefi wakati Yesu alipozaliwa.
Shughuli za Yakini
-
Kabla ya darasa, weka nyota ukutani. Waalike watoto kutafuta ukutani kitu ambacho kwa kawaida hakipo pale. Waambie watoto kwamba Wanefi waliona nyota mpya angani wakati Yesu alipozaliwa. Fanyia ufupisho maelezo katika 3 Nefi 1:4–15, na 19–21. Ungeweza pia kutumia “Mlango wa 41: Ishara za Kuzaliwa kwa Kristo” (Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 114–16, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org).
-
Waonyeshe watoto picha ya kuzaliwa kwa Mwokozi (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, ) na. 30), na waimbe wimbo wa Krismasi wanaoupenda, kama vile “The Nativity Song” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 52–53). Wasaidie watoto kuelewa kwamba Wanefi walikuwa mbali sana kutoka mahali Yesu alipozaliwa, lakini walijua alikuwa amezaliwa kwa sababu ya ishara walizoona. Shuhudia kwamba japokuwa hatukuona kuzaliwa kwa Mwokozi, Roho Mtakatifu anaweza kutusaidia kujua kwamba hadithi kuhusu kuzaliwa kwake zilizoko kwenye maandiko ni za kweli.
Maneno ya nabii daima yanatimia.
Bwana alimwambia Nefi, “[nitaionyesha]” dunia kwamba nitatimiza yote ambayo nimesababisha kuzungumzwa kwa midomo ya manabii wangu watakatifu” (3 Nefi 1:13).
Shughuli za Yakini
-
Onyesha picha zinazofafanua jinsi ambavyo Mungu amezungumza kupitia manabii, kama vile Nuhu (Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 7–8; ona Mwanzo 6–7) na Samweli Mlamani (Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 81; ona Helamani 14:1–7). Waalike watoto kushiriki kile wanachojua kuhusiana na hadithi hizi.
-
Wasomee watoto 3 Nefi 1:20, na shiriki ushuhuda wako kwamba maneno ya manabii daima yanatimia. Waalike watoto kuwasikiliza manabii kwenye mkutano mkuu ujao.
Ninaweza kumfuata Yesu Kristo.
Mormoni alitangaza, “Mimi ni mwanafunzi wa Yesu Kristo.” Unawezaje kuwasaidia watoto kujiona wao pia kama wanafunzi?
Shughuli za Yakini
-
Soma 3 Nefi 5:13, na waalike watoto kurudia kifungu cha maneno “Mimi ni mwanafunzi wa Yesu Kristo.” Wafundishe kwamba mwanafunzi wa Yesu Kristo hujaribu kumfuata Yeye. Shiriki mambo machache Mormoni aliyofanya ili kuwa kama Yesu, kama vile kufundisha neno la Mungu na kutii amri za Mungu (ona 3 Nefi 5:13–18). Wasaidie watoto kufikiria jinsi wanavyoweza kuwa wanafunzi.
-
Kwenye kipande cha karatasi, wasaidie watoto kuchora mkono wao, kuukata na kuuondoa mchoro. Andika “Mimi ni mwanafunzi wa Yesu Kristo” kwenye upande mmoja, na waalike wachore kitu wanachoweza kufanya ili kuwa mwanafunzi kwenye upande wa pili (ungeweza kuhitaji kuwasaidia kufikiria mawazo). Imbeni pamoja wimbo kuhusu kumfuata Mwokozi, kama vile “I’m Trying to Be like Jesus” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 78–79).
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Ahadi za Mungu, zinazotolewa kupitia manabii Wake, daima zinatimia.
Maelezo katika 3 Nefi 1:4–21 yanaweza kusaidia kujenga imani ya watoto kwamba Mungu daima hutimiza ahadi Zake.
Shughuli za Yakini
-
Waalike watoto kulinganisha unabii wa Samweli Mlamani katika Helamani 14:1–7 na utimiaji wake katika 3 Nefi 1:19–21. Shuhudia kwamba ahadi za Mungu zilizozungumzwa kupitia manabii Wake daima zinatimia.
-
Soma pamoja na watoto maelezo yanayopatikana katika 3 Nefi 1:4–10. Waulize watoto ni jinsi gani wangeweza kuhisi kama wangekuwa mmoja wa waaminio walioishi wakati huo. Waalike watoto kusoma maelezo yaliyobakia katika mistari 11–15 na kupendekeza njia za kumalizia sentensi hii: “funzo la hadithi hii ni …” ni kwa jinsi gani tunaweza kuonyesha uaminifu wetu kwa Mungu wakati tunapokuwa na hofu au kukata tamaa?
-
Shiriki jambo ambalo nabii wetu aliye hai ametuahidi. Je, tunaweza kufanya nini ili kuonyesha imani yetu kwamba maneno ya manabii yametoka kwa Mungu?
3 Nefi 2:11–12; 3:13–14, 24–26
Tunakuwa imara zaidi pale tunapokusanyika pamoja.
Wanefi ilibidi wakusanyike pamoja kwa ajili ya usalama wao. Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto kuona kwamba kukusanyika pamoja na marafiki waadilifu kunaweza pia kuwapa nguvu ya kiroho?
Shughuli za Yakini
-
Soma pamoja na watoto mistari ifuatayo, na waalike kutafuta sababu kwa nini Wanefi walikusanyika pamoja na baraka zilizokuja juu yao: 3 Nefi 2:11–12 na 3:13–14, 24–26. Kwa nini ni muhimu kwetu “kukusanyika” pamoja leo katika familia zetu na kanisani? Ni kwa jinsi gani kukusanyika hutufanya imara kiroho?
-
Tumia somo la vitendo kufundisha kwamba tunakuwa imara pamoja kuliko tunapotengana. Kwa mfano, waalike watoto wajaribu kuvunja kijiti kimoja na kisha vijiti vingi vilivyowekwa pamoja au kuchana karatasi moja na kisha karatasi nyingi zilizowekwa pamoja. Ni kwa namna gani sisi ni kama vijiti au karatasi? Ni kwa jinsi gani tunaweza kuimarishana pale tunapokusanyika pamoja katika familia zetu au kanisani?
-
Eleza kwamba Yesu anawakusanya watu Wake Kanisani leo kupitia kazi ya umisionari (ona 3 Nefi 5:24–26). Mwalike mmisionari wa muda wote au mmisionari wa kata kushiriki uzoefu unaoonyesha jinsi watu walivyoimarishwa kwa kukusanyika Kanisani.
3 Nefi 4:30–33; 5:12–26; 6:14; 7:15–26
Mimi ni mwanafunzi wa Yesu Kristo.
Ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto kujiona kama wanafunzi wa Yesu Kristo, kama Mormoni alivyojiona? (ona 3 Nefi 5:13).
Shughuli za Yakini
-
Onyesha picha ya Mormoni (kama vile Kitabu cha Sanaa ya Injili, na.73). Mwalike kila mtoto kufanya zamu na kurudia kile Mormoni alichosema katika 3 Nefi 5:13: “Mimi ni mwanafunzi wa Yesu Kristo.” Inamaanisha nini kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo? (ona M&M 41:5).
-
Ligawe darasa katika makundi madogo, na lipangie kila kundi kusoma kuhusu moja ya mifano ifuatayo ya wanafunzi: Walamani walioongoka (ona 3 Nefi 4:30–33; 6:14), Mormoni (ona 3 Nefi 5:12–26), na Nefi (ona 3 Nefi 7:15–26). Ni kwa jinsi gani watu hawa walikuwa wanafunzi wa Yesu Kristo? Ni nini tunaweza kufanya kufuata mifano yao?
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto kufikiria jambo watakalofanya wiki hii ili kuwa wafuasi wa Kristo. Wahimizi kuliandika na kulishiriki na familia zao.