Njoo, Unifuate
Septemba 14–20. 3 Nefi 8–11: “Inukeni na Mje Kwangu”


“Septemba 14–20. 3 Nefi 8–11: ‘Inukeni na Mje Kwangu,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Septemba 14–20. 3 Nefi 8–11” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2020

Yesu anawatokea Wanefi

Mimi ni Nuru ya Ulimwengu, na James Fullmer

Septemba 14–20

3 Nefi 8–11

“Inukeni na Mje Kwangu”

Soma 3 Nefi 8–11 ukiwa na watoto unaowafundisha akilini. Mawazo yaliyoko katika muhtasari huu yanaweza kusaidia kuongoza maandalizi yako.

Andika Misukumo Yako

ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Onyesha picha ya Yesu Kristo akitokea katika Amerika, kama ile iliyoko kwenye muhtasari wa wiki hii katika Njoo Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia. Waalike watoto kuonyesha maelezo katika picha na kushiriki jambo wanalojua kuhusu hadithi iliyofafanuliwa.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo

3 Nefi 8–11

Yesu Kristo ananialika nije Kwake.

Unaweza kushindwa kushiriki na watoto maelezo yote ya kutokea kwa Mwokozi kwa watu wa Nefi, lakini unaweza kuwasaidia kuhisi upendo Alioonyesha kwa watu katika 3 Nefi 8–11.

Shughuli za Yakini

  • Wasimulie watoto kuhusu dhoruba na giza vilivyoelezewa katika 3 Nefi 8, ukichukua tahadhari kwa kutowatisha au kuwavuruga. Ungeweza kutumia “Mlango wa 42: Ishara za Kusulubiwa kwa Kristo” (Hadithi za Kitabu cha Mormoni, 117–19, au video inayohusiana kwenye ChurchofJesusChrist.org). Waulize watoto ni kwa jinsi gani wangeweza kuhisi kama wangekuwepo kwenye dhoruba na giza hilo. Elezea kwamba dhoruba na giza vilikuwa ishara kwamba Yesu alikuwa amekufa, na onyesha picha ya Kusulubiwa (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na. 57). Kisha soma 3 Nefi 9:13. Ni nini Yesu alisema angefanya kwa wale waliotubu? Wasaidie watoto kuelewa kwamba neno “ponya” katika mstari huu humaanisha kwamba Yesu angewasamehe.

  • Onyesha picha kwenye Muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia wakati ukielezea kwa maneno yako mwenyewe Mwokozi aliyefufuka akiwatokea Wanefi na Walamani. Soma vifungu vifupi vya maneno kutoka 3 Nefi 11 ambavyo vitawasaidia kuhisi utakatifu wa tukio hili. Waalike kufumba macho yao na kufikiria jinsi ambavyo wangehisi kama wangepata kumwona Yesu. Au onyesha dakika ya kwanza ya video “My Joy Is Full” (ChurchofJesusChrist.org). Waambie watoto kuhusu jinsi unavyohisi wakati unaposoma na kutafakari matukio haya. Shuhudia kwamba Yesu anatutaka sote kuja Kwake na kuhisi upendo Wake. Kamilisha ukurasa wa shughuli pamoja na watoto.

3 Nefi 10:4–6

Yesu huwalinda watu Wake kama kuku anavyowalinda vifaranga wake.

Taswira ya kuku kukusanya vifaranga vyake inaweza kuwafundisha watoto kuhusu faraja na ulinzi Mwokozi anaotoa kama tutakuja Kwake.

Shughuli za Yakini

  • Onyesha picha ya kuku akiwatunza vifaranga wake. Soma 3 Nefi 10:6, na wasimulie watoto kuhusu jinsi kuku anavyowaita vifaranga wake na kuwalinda chini ya mbawa zake kunapotokea hatari. Jadili ni kwa jinsi gani Yesu ni kama kuku na sisi ni kama vifaranga. Ni kwa jinsi gani tunaweza kuja Kwake ili kupata usalama?

  • Weka picha ya Yesu ukutani. Waalike watoto kutembea kuzunguka darasa wakati ukisoma 3 Nefi 10:4 kwa sauti. Waambie watembee kuelekea picha ya Yesu wakati wanaposikia maneno “aliwakusanya” au “kusanya.” Rudia shughuli hii unaposoma mstari wa 5 na 6. Shiriki pamoja na watoto jinsi ulivyokuja kwa Mwokozi kwa ajili ya usalama, na shuhudia kwamba Yeye atatulinda kutokana na hatari za kiroho wakati tunapotii amri zake.

3 Nefi 11:21–26

Yesu Kristo anataka mimi nibatizwe.

Watoto unaowafundisha wanajitayarisha kwa ubatizo. Mafundisho ya Kristo katika vifungu hivi vya maneno yanaweza kuwasaidia kujua kwa nini ubatizo ni muhimu.

Shughuli za Yakini

  • Soma 3 Nefi 11:21–26, na waalike watoto kusimama kila mara wanaposikia neno “batiza.” Eleza kwamba Yesu alitufundisha njia sahihi ya kubatiza. Onyesha picha ya mtoto akibatizwa (ona Kitabu cha Sanaa ya Injili, na.104). Ikiwa watoto wamewahi kuona ubatizo kabla, waalike kuelezea kile walichoona. Nani alifanya ubatizo, na aliufanya kwa namna ipi?

  • Mapema kabla, mwalike baba wa mmoja wa watoto kuhudhuria darasa lako na kushiriki pamoja na watoto kwa nini ni muhimu tubatizwe kwa kuzamishwa na mtu aliye na ukuhani. Angeweza pia kuwaelezea watoto nini kitatokea wakati watakapobatizwa na baraka watakazopokea. Muhimize kutumia 3 Nefi 11:23–26 katika maelezo yake.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa

3 Nefi 8–11

Wakati ninapokuwa gizani, Yesu Kristo anaweza kuwa nuru yangu.

Ujumbe mmoja wenye nguvu kwenye milango hii ni kwamba Yesu Kristo ni nuru ya ulimwengu, na Anaweza kuwa nuru ya maisha yetu.

Shughuli za Yakini

  • Someni pamoja 3 Nefi 8:5–7, 11–23, na 10:9–13 (ikiwezekana, fanya chumba kiwe na giza wakati unaposoma). Pumzika kusoma mara kadhaa na waulize watoto ingekuwaje kupitia matukio haya. Soma pamoja na watoto baadhi ya maneno aliyoongea Yesu Kristo kwa watu wakati walipokuwa kwenye giza (ona 3 Nefi 9:13–14, 18). Kwa nini Yesu Kristo Anajiita Nuru ya Ulimwengu? Ni nini Yesu aliwaalika watu, pamoja nasi, kufanya ili Yeye aweze kuwa nuru yetu? (ona 3 Nefi 9:20–22).

  • Waonyeshe watoto ramani ya ulimwengu, na wasaidie kutafuta Yerusalemu na Amerika. Eleza kwamba maangamizo yaliyoelezewa katika 3 Nefi 8 ilikuwa ni ishara kwa watu wa Amerika kwamba Yesu Kristo alikuwa amesulubiwa Yerusalemu. Someni pamoja 3 Nefi 11:1–15, na waombe watoto wakuambie wakati wanapopata jambo katika mistari hii ambalo linawasaidia kuhisi upendo wa Mungu. Shiriki mstari wa 37, na shuhudia kwamba Mwokozi anawapenda watoto wote. Toa ushuhuda wako kuhusu ukweli wa kile unachosoma.

Yesu akiwaonyesha Wanefi alama katika mikono Yake

Mmoja baada ya Mwingine, na Walter Rane

3 Nefi 11:1–8

Ninaweza kujifunza kutambua sauti ya Mungu katika maisha yangu.

Mwanzoni watu hawakuielewa sauti waliyosikia kutoka mbinguni. Ni nini watoto wanaweza kujifunza kutoka kwenye maelezo haya kuhusu kupokea ufunuo?

Shughuli za Yakini

  • Soma 3 Nefi 11:1–4 pamoja na watoto, ukipumzika kuuliza maswali kama “Kwa nini unadhani watu hawakuielewa sauti?” Kisha waalike wasome mstari wa 5–7 kupata kile watu walichofanya ambacho kiliwasaidia kuielewa sauti katika mioyo yao. Ni kwa jinsi gani tunaweza kujaribu kumsikiliza Mungu wakati Anapozungumza kwenye mioyo yetu kupitia Roho Mtakatifu?

  • Weka wimbo wa Kanisa au wimbo wa watoto kwa sauti ya chini ili kwamba iwe vigumu kusikia. Waulize watoto kama wanaweza kuelewa maneno ya wimbo. Kisha wasaidie watoto kutafuta 3 Nefi 11:3 kwa ajili ya maelezo ya sauti kutoka mbinguni. Kwa nini Mungu hazungumzi nasi kwa sauti ya “juu” au ya “ukali”? Je, tunaweza kufanya nini ili Kumsikia vizuri zaidi?

ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Waalike watoto kumsimulia mtu kuhusu matembezi ya Yesu huko Amerika—kama itawezekana, mtu ambaye hajui kuhusu matembezi hayo.

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Kabiliana na usumbufu kwa upendo. “Mara nyingine mtoto hutenda katika njia ambazo huvuruga kujifunza kwa wengine darasani. Wakati haya yanapotendeka, kuwa mvumilivu, mwenye upendo, na mwenye kuelewa kuhusu changamoto ambazo mtoto anaweza kuwa anakabiliana nazo. … Ikiwa mtoto anayesababisha vurugu ana mahitaji maalum, zungumza na mtaalamu wa watu wenye ulemavu katika kata au kigingi au tembelea disabilities.ChurchofJesusChrist.org ili kujua jinsi unavyoweza kukidhi mahitaji hayo kwa njia bora” (Kufundisha katika njia ya Mwokozi,26).