“Oktoba 16–22. 1 na 2 Wathesalonike: ‘Kamilisheni Kile Kilichopungua Katika Imani Yenu’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano Jipya 2019 (2019)
“Oktoba 16–22. 1 na 2 Wathesalonike,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2023
Oktoba 16–22
1 na 2 Wathesalonike
“Kamilisheni Kile Kilichopungua Katika Imani Yenu”
Unaposoma kwa maombi 1na 2 Wathesalonike watoto wakiwa akilini mwako, utapata kanuni ambazo wao wanahitaji kuelewa.
Alika Kushiriki
Katika somo la wiki iliyopita, uliwaalika watoto kutumia kile walichojifunza kwa namna fulani? Waache watoto watumie dakika chache za mwanzo za darasa la wiki hii kushiriki uzoefu wao.
Fundisha Mafundisho: Watoto Wadogo
Ninapofuata amri za Mungu, nitakuwa niko tayari kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo.
Hatujui lini Mwokozi atarudi duniani. Lakini tunaweza kumtazamia Yeye na kujiandaa kwa ajili ya ujio Wake
Shughuli Yamkini
-
Mwalike mama mmoja kushiriki kwa kifupi kuhusu ilikuwaje kwake yeye kusubiri kuzaliwa kwa mtoto wake. Soma 1 Wathesalonike 5:2–3, na waeleze watoto kwamba Yesu Kristo atakuja duniani tena, lakini hakuna ajuaye kwa uhakika ni lini—kama vile mama asivyojua kwa uhakika lini mtoto atazaliwa.
-
Waombe watoto kuzungumza kuhusu muda walipojiandaa kwa ajili ya safari au tukio. Walifanya nini ili kujiandaa? Lete sanduku la nguo au begi, na waache watoto wajifanye wanalipakia katika maandalizi ya safari. Kwa kila kitu wanachojifanya kukiweka sandukuni, wasaidie watoto kufikiria juu ya njia moja tunayoweza kujiandaa kwa ajili ya Yesu kuja tena.
-
Wasomee watoto 1 Wathesalonike 5:6 na ueleza kwamba kama hatujiandai kwa ajili ya Yesu kuja tena, ni kama tumelala usingizi na hatutakuwa tayari kwa ajili yake. Waalike watoto kujifanya wamelala. Eleza kwamba kama tunajiandaa, ni kama tumeamka na tunamsubiri Yeye. Waalike kuamka.
-
Imbeni pamoja wimbo kuhusu Ujio wa Pili, kama vile “When He Comes Again” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 82–83).
Paulo alifundisha kwamba ukengeufu ungetokea kabla ya Yesu Kristo hajaja tena.
Kanisa ambalo Yesu Kristo alilianzisha hatimaye liliangukia kwenye ukengeufu, inamaanisha kwamba mamlaka ya ukuhani na ukweli wa injili viliondolewa kutoka duniani. Paulo alitabiri kwamba ukengeufu huu, au “kupotoka,” kungetokea kabla ya Ujio wa Pili wa Mwokozi.
Shughuli Yamkini
-
Baada ya kusoma 2 Wathesalonike 2:3 pamoja na watoto, acha wakusaidie kujenga mnara kutokana na vikombe vya plastiki au matofali. Waambie watoto kwamba vikombe au matofali vinawakilisha sehemu muhimu za Kanisa la kweli, kama vile ukweli wa injili, ukuhani, kuunganishwa hekaluni, na manabii. Baada ya Paulo na Mitume wengine kufariki, mambo haya yalipotea, na Kanisa la kweli halikuwepo duniani kwa miaka mingi. Mwalike mtoto kugonga mnara na kuangusha, na eleza kwamba hii iliitwa Ukengeufu au “kupotoka.” Wakati Yesu Kristo aliporudisha Kanisa lake, iliitwa Urejesho.
-
Onyesha Kitabu cha Mormoni na picha za nabii na hekalu. Waombe watoto waseme “ukengeufu” wakati unaficha vitu hivyo katika mfuko na “ Urejesho” wakati unapovitoa vitu hivyo nje.
-
Imbeni nyimbo ambazo zinafundisha ukweli ambao uliondolewa wakati wa Ukengeufu na kurejeshwa katika siku yetu, kama vile “The Church of Jesus Christ,” “The Priesthood Is Restored,” na “I Love to See the Temple” (Kitabu cha Nyimbo za Watoto, 77, 89, 95).
Fundisha Mafundisho: Watoto Wakubwa
Ninapofuata amri za Mungu, nitakuwa niko tayari kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo.
Ushauri wa Paulo unaweza kutusaidia kuwa tayari na kuitazamia siku ile kuu wakati Mwokozi anapokuja duniani tena.
Shughuli Yamkini
-
Mwalike mtoto asome 1 Wathesalonike 5:1–6 wakati watoto wengine wakifuatilia. Baada ya kila mstari, muombe mtoto kufanya muhtasari wa kile yeye anafikiri mstari huo unasema. Unaweza kutaka kueleza kwamba “siku ya Bwana” maana yake ni Ujio wa Pili wa Yesu Kristo. Je, ni kwa nini Ujio wa Pili unafananishwa na mwizi wa usiku au mwanamke karibu ya kujifungua?
-
Waambie watoto wafikirie kwamba Mwokozi atatembelea darasa lenu wakati fulani leo. Tunawezaje kujiandaa kwa ajili ya ziara Yake? Wasaidie watoto kufikiria juu ya mambo tunayoweza kufanya ili kujiandaa kwa ajili ya siku ambayo Yesu Kristo anarudi. Kwa mfano, tunaweza kutubu, kusamehe, kuboresha uhusiano wetu na familia zetu, kumfuata nabii, kutafuta kuwa na ushawishi wa Roho Mtakatifu na kushika maagano yetu. Watie moyo watoto kuchagua kitu kimoja watakachofanya ili kujiandaa wenyewe kumpokea Mwokozi wakati wa Ujio Wake.
Paulo alifundisha kwamba ukengeufu ungetokea kabla Yesu Kristo hajaja tena.
Kama watoto wanaelewa kwamba Kanisa la Yesu Kristo na injili Yake viliondolewa kutoka duniani wakati wa Ukengeufu Mkuu, umuhimu wa Urejesho utakuwa wazi zaidi kwao.
Shughuli Yamkini
-
Mwalike mmoja wa watoto asome 2 Wathesalonike 2:1–3. Kulingana na mstari hii, nini kingetokea kabla ya “siku ya Kristo” ambayo ina maana ya Ujio wa Pili? Kirai “kupotoka” kinamaanisha nini? Hakikisha kwamba watoto wanaelewa inamaanisha Ukengeufu Mkuu, ambao ulitokea baada ya vifo vya Mitume wa Mwokozi. Ungetaka kushiriki taarifa kutoka “Ukengeufu” katika Mwongozo wa Maandiko (scriptures.ChurchofJesusChrist.org).
-
Wasaidie watoto kuorodhesha ubaoni baadhi za kweli na baraka tunazofaidi kwa sababu ya injili. Futa vitu hivi kimoja kimoja, na waulize watoto jinsi gani maisha yao yangekuwa tofauti bila vitu hivi. Elezea kwamba kweli hizi zilipotea wakati wa Ukengeufu Mkuu. Kwa nini ilikuwa muhimu kwamba Kanisa la Yesu Kristo lirejeshwe duniani katika siku za mwisho? Waalike watoto “kurejesha” au kuandika upya ukweli na baraka ubaoni.
Baba wa Mbinguni ananitaka nifanye kazi.
Je, ni kwa jinsi gani unaweza kuwasaidia watoto kuona kazi kama baraka, sio kitu cha kukwepa?
Shughuli Yamkini
-
Waalike watoto kuchukua zamu kusoma mistari kutoka 2 Wathesalonike 3:7–13 na kutafuta matatizo ambayo Watakatifu walikuwa wanakabiliana nayo. Je, ni kwa nini Baba wa Mbinguni anataka tufanye kazi? Je, nini kingetokea kama katu hatungejifunza kufanya kazi kwa bidii? Waache watoto wachukue zamu kuigiza kazi za kawaida za kila siku wakati watoto wengine wanakisia wenzao wanafanya nini.
-
Waalike watoto wazungumze kuhusu wakati ambapo walifanya bidii kwenye kazi, mradi au lengo. Je, ni kwa jinsi gani walijisikia kuhusu wao wenyewe walipokuwa wamemaliza? Inamaanisha nini kuwa “msichoke katika kufanya mema”? (2 Wathesalonike 3:13). Je, ni kitu gani kinatusaidia kuendelea wakati kazi inapoonekana kuwa ngumu?
Himiza Kujifunza Nyumbani
Waalike watoto kumwambia mwanafamilia au rafiki sababu moja ya wao kushukuru kuwa tuna injili duniani leo (ukurasa wa shughuli ya wiki hii unaweza kuwapatia mawazo).