“Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano Jipya 2023 (2023)
“Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2023
Kutumia Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi
Kujiandaa Kufundisha katika Msingi
Kujifunza binafsi na kifamilia nyumbani kunapaswa kuwa kitovu cha kujifunza injili. Hii ni kweli kwako na kwa watoto unaowafundisha. Unapojiandaa kufundisha, anza kwa kuwa na uzoefu wako mwenyewe katika maandiko. Maandalizi yako muhimu zaidi yatatokea wakati wewe unapoishi injili, unapopekua maandiko, na kutafuta mwongozo wa kiungu wa Roho Mtakatifu.
Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia ni sehemu muhimu kwa vyote kujifunza kwako binafsi na kwa maandalizi yako ya kufundisha. Itakusaidia kupata uelewa wa kina wa kanuni za mafundisho zinazopatikana katika maandiko. Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi itakupa shughuli kwa ajili ya maandiko mengi na hadithi wanazoalikwa kujifunza nyumbani katikati ya wiki.
Wakati wa maandalizi yako, mawazo na misukumo itakujia kuhusu watoto unaowafundisha. Utapokea umaizi juu ya jinsi kanuni katika maandiko zitakavyobariki maisha yao. Utaongozwa ili uwahamasishe kuzigundua kanuni hizo wakati wanapojifunza kutoka katika maandiko wao wenyewe na pamoja na familia zao.
Mawazo ya Kufundisha
Unapojiandaa kufundisha, ungeweza kupata mwongozo wa ziada kwa kuchunguza mihtasari katika nyenzo hii. Usifikirie mawazo haya kama maelekezo ya hatua kwa hatua lakini badala yake ni kama mapendekezo ya kuchochea kupata mwongozo wako mwenyewe. Unawajua watoto hawa, na utapata kuwajua hata vizuri zaidi pale unapochangamana nao darasani. Bwana anawajua pia, na Atakuongoza kwa njia bora za kuwafundisha na kuwabariki watoto.
Nyenzo zingine nyingi zinapatikana kwa ajili yako ili kuweza kutumia wakati unapojiandaa, ikiwa ni pamoja na mawazo katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia na magazeti ya Kanisa. Kwa maelezo zaidi kuhusu nyenzo hizi na zingine, ona “Nyenzo za Ziada za Kufundishia Watoto” katika nyenzo hii.
Baadhi ya Mambo ya Kukumbuka
-
Kila mara unapokutana na watoto, fikiria jinsi unavyoweza kuwasaidia wahisi upendo wa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo na kutambua ushawishi wa Roho Mtakatifu.
-
Wazazi wana jukumu muhimu la kuwafundisha watoto wao. Kama mwalimu, una jukumu muhimu la kusaidia, kuhimiza, na kujenga juu ya kujifunza injili nyumbani. Kuwa mwangalifu kwa watoto ambao wazazi wao hawafundishi injili nyumbani mwao. Jumuisha watoto wote katika majadiliano ya injili, bila kujali mazingira yao ya nyumbani.
-
Kurudia rudia ni vyema. Watoto hujifunza ukweli wa injili kwa ufanisi zaidi wakati ukweli huo unapofundishwa kwa kurudiwa rudiwa kupitia shughuli mbalimbali. Ikiwa unaona kuwa shughuli fulani ya kujifunza inafaa kwa watoto, fikiria kuirudia, hasa ikiwa unafundisha watoto wadogo zaidi. Unaweza pia kurejelea tena shughuli kutoka kwenye somo lililopita.
-
Baba wa Mbinguni anataka wewe ufanikiwe kama mwalimu. Ametoa nyenzo nyingi ili kukusaidia, ikijumuisha mikutano ya baraza la walimu. Katika mikutano hii unaweza kushauriana na walimu wengine kuhusu changamoto zinazokukabili. Unaweza pia kujadili na kufanyia mazoezi kanuni za kufundisha kama Kristo.
-
Kama unafundisha watoto wadogo na unahitaji msaada wa ziada, ona “Kukidhi Mahitaji ya Watoto Wadogo” katika nyenzo hii.
Nyenzo hii inajumuisha mihutasari ya kufundishia kwa kila wiki ya mwaka. Katika Jumapili ambazo darasa la Msingi halifanyiki kwa sababu ya mkutano mkuu, mkutano wa kigingi au sababu nyingine yoyote, familia zinahimizwa kuendelea kusoma Agano Jipya nyumbani kulingana na ratiba iliyoainishwa katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia. Usihofu kuhusu masomo uliyokosa; fundisha muhtasari uliopangwa kila wiki.