Agano Jipya 2023
Kukidhi Mahitaji ya Watoto Wadogo


“Kukidhi Mahitaji ya Watoto Wadogo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: Agano Jipya 2023 (2023)

“Kukidhi Mahitaji ya Watoto Wadogo,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Msingi: 2023

Watoto wa Msingi

Kukidhi Mahitaji ya Watoto Wadogo

Watoto wako tayari na wana nia ya kujifunza injili ikiwa itawasilishwa katika njia wanayoweza kuelewa. Hasusani kama unafundisha watoto wadogo, fikiria kutumia aina zifuatazo za shughuli ili kuwasaidia kujifunza.

  • Imba. Nyimbo za Kanisa na nyimbo kutoka Kitabu cha Nyimbo za Watoto zinafundisha mafundisho kwa nguvu zaidi. Tumia kielezo cha mada nyuma ya Kitabu cha Nyimbo za Watoto kutafuta nyimbo zinazohusiana na kanuni za injili unazofundisha. Wasaidie watoto kuhusisha jumbe za nyimbo na maisha yao. Kwa mfano, unaweza kuuliza maswali kuhusu maneno au virai katika mashairi ya wimbo. Mbali na kuimba, watoto wanaweza kufanya vitendo vinavyoendana na nyimbo au kusikiliza tu nyimbo wakati wakifanya shughuli zingine. Kwa ajili ya mawazo mengine, angalia sehemu za “Kutumia Muziki ili Kufundisha Mafundisho” na “Kuwasaidia Watoto Kujifunza na Kukumbuka Nyimbo za Msingi pamoja na Nyimbo za Kanisa” katika “kiambatisho cha kitabu hiki cha kiada.

  • Sikiliza au igiza hadithi. Watoto wadogo wanapenda hadithi—kutoka katika maandiko, kutoka katika maisha yako, kutoka katika historia ya familia yako, au kutoka kwenye magazeti ya Kanisa. Tafuta njia za kuwashirikisha kwenye usimuliaji wa hadithi. Wanaweza kushikilia picha au vitu, kuchora picha ya kile wanachokisikia, kuigiza hadithi, au hata kusaidia kusimulia hadithi. Wasaidie watoto kutambua ukweli wa injili katika hadithi unazowasimulia.

  • Soma andiko. Watoto wadogo wanaweza kushindwa kusoma vizuri, lakini bado unaweza kuwahusisha katika kujifunza kutoka kwenye maandiko. Unaweza kuhitaji kuzingatia mstari mmoja, kirai muhimu, au neno. Unaposoma maandiko kwa sauti, unaweza kuwaalika watoto wasimame au wainue mikono yao wakati wanaposikia neno fulani au kirai unachotaka kukizingatia. Wanaweza hata kukariri virai vifupi kutoka katika maandiko ikiwa watavirudia mara kadhaa. Kadiri wanavyosikia neno la Mungu, watamsikia Roho.

  • Changamka. Kwa sababu watoto wadogo mara nyingi wana nguvu, panga njia za kuwawezesha kuzunguka zunguka—kuandamana, kurukaruka, kuinama, kutembea, na vitendo vingine vinavyohusiana na kanuni au hadithi unayofundisha. Matendo haya yanaweza pia kuwa ya ufanisi wakati mnaimba pamoja.

  • Tazama picha au angalia video. Unapowaonesha watoto picha au video zinazohusiana na kanuni ya injili au hadithi, waulize maswali ambayo yanawasaidia kujifunza kutoka kwenye kile wanachokiona. Kwa mfano, ungeweza kuuliza, “Je, ni nini kinatokea katika picha au video hii? Kinakufanya ujisikie vipi?” Programu ya Maktaba ya Injili, ChurchofJesusChrist.org, na children.ChurchofJesusChrist.org ni mahali pazuri pa kutafuta picha na video.

  • Wasaidie na kuwahimiza watoto kushiriki uzoefu. Watoto wadogo wanaweza wasiwe na mengi ya kushiriki kama watoto wakubwa wanavyofanya, lakini ikiwa utawapa mwongozo maalum, wanaweza kushiriki hisia zao na uzoefu wao juu ya kile wanachojifunza.

  • Buni. Watoto wanaweza kujenga, kuchora, au kupaka rangi kitu kinachohusiana na hadithi au kanuni wanayojifunza. Wahimize kupeleka ubunifu wao nyumbani na kuwaelezea wanafamilia ili kuwasaidia watoto kukumbuka yale waliyojifunza.

  • Shiriki katika masomo ya vyombo. Somo rahisi la kitendo linaweza kuwasaidia watoto kuelewa kanuni ya injili ambayo ni ngumu kwao kuielewa. Wakati unapotumia masomo ya vyombo, tafuta njia za kuwafanya watoto kushiriki. Watajifunza zaidi kutokana na uzoefu wa kuchangamana kuliko kuangalia tu onyesho.

  • Igiza Nafasi. Watoto wanapoigiza-nafasi ya aina fulani watakayokutana nayo katika maisha halisi, wanaelewa vizuri zaidi jinsi kanuni ya injili inavyohusika kwenye maisha yao.

  • Rudia shughuli. Watoto wadogo wanaweza kuhitaji kusikia mawazo mara nyingi zaidi ili kuyaelewa. Usiogope kurudia hadithi au shughuli mara nyingi, hata wakati wa somo hilo hilo. Kwa mfano, unaweza kusimulia hadithi ya maandiko mara kadhaa kwa njia tofauti wakati wa somo—kwa kusoma kutoka kwenye maandiko, kufupisha kwa maneno yako mwenyewe, kuonesha video, kuwaruhusu watoto wakusaidie kusimulia hadithi hiyo, kuwaalika kuigiza hadithi hiyo, na kadhalika. Ikiwa shughuli iliyotumiwa katika darasa inarudiwa pia nyumbani, marudio yatawasaidia watoto kujifunza na kukumbuka.

  • Changamana na wengine. Watoto wanajenga stadi za kijamii na mara nyingi wanafurahia kujifunza na kucheza na rika lao. Watengenezee fursa za kushiriki, kupeana zamu, na kushirikiana wakati wanapojifunza.

  • Shiriki katika shughuli tofauti tofauti. Watoto wadogo kwa kawaida huwa na usikivu wa muda mfupi, na wana mitindo tofauti ya kujifunza. Tumia shughuli tofauti tofauti, na uwe makini na ishara zinazoonesha kuwa watoto wanahitaji mabadiliko ya mwendo. Kwa mfano, huenda ukahitaji kubadilisha mara kwa mara kati ya shughuli za ukimya na za kuchangamka.

mwalimu na mtoto katika darasa la Msingi

Sehemu ya jukumu lako kama mwalimu wa watoto wadogo—katika nyongeza ya kufundisha kanuni za injili—ni kuwasaidia watoto kujifunza jinsi ya kushiriki kwa namna inayofaa katika darasa la Kanisa. Kwa mfano, wanaweza kuhitaji kujifunza kuhusu kupeana zamu, kushiriki jambo, kuwaheshimu wengine, na kadhalika. Walimu wengine hutengeneza chati zenye majukumu kwa kila mtoto kushiriki katika darasa kwa namna fulani (kama vile kusema sala, kushikilia picha, au kupitisha karatasi). Majukumu yanaweza kubadilika kila wiki. Hii huwasaidia watoto kupeana zamu na kuzingatia tabia sahihi ya darasa.

Watoto—hasa watoto wadogo—mara nyingi hufaidika na utaratibu wa kawaida, unaoweza kutabirika. Kwa sababu watoto wadogo wana vipindi vifupi vya utulivu na wakati mwingine hupata shida kufokasi kwa kipindi kizima cha darasa, ni vizuri zaidi ikiwa utaratibu huu unahusisha mabadiliko ya mara kwa mara kutoka kwenye aina moja ya shughuli hadi nyingine. Kwa mfano, utaratibu wako wa kudumu wa darasa unaweza kujumuisha mapumziko ya mara kwa mara ili kupaka rangi picha, kuimba wimbo, na kadhalika.