Njoo, Unifuate
Januari 13–19. 1 Nefi 8–10: “Njoo na Ule Tunda”


“Januari 13–19. 1 Nefi 8–10: ‘Njoo na Ule Tunda,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Kitabu cha Mormoni 2020 (2020)

“Januari 13–19. 1 Nefi 8–10,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: 2020

 Ono la Lehi la mti wa uzima

Ndoto ya Lehi, na Steven Lloyd Neal

Januari 13–19

1 Nefi 8–10

“Njoo na Ule Tunda”

Kabla ya kusoma mawazo katika muhtasari huu, soma 1 Nefi 8–10 na fikiria kuhusu changamoto na fursa zinazowakabili watu unaowafundisha. Andika misukumo yako kuhusu kanuni zipi kutoka katika sura hizi unapaswa kuzilenga katika darasa.

Andika Misukumo Yako

ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Ono la Lehi lina matumizi mengi kwa ajili ya siku zetu. Mwanzoni mwa darasa, ungeweza kutaka kuwaalika washiriki wa darasa kushiriki utambuzi wao pale wanaposoma kuhusu ono hili. Watie moyo kushiriki mistari maalumu na maana wanayopata kwa ajili ya maisha yao.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho

1 Nefi 8:10–16

Tunapopata uzoefu wa upendo wa Mungu, tunatamani kuwasaidia wengine wapate uzoefu huo.

  • Ni kawaida kushiriki vitu tunavyovipenda na watu tunaowapenda, lakini wakati mwingine tunaona ni vigumu kushiriki injili. Majadiliano kuhusu ono la Lehi yanaweza kuwasaidia washiriki wa darasa kupata fursa za kushiriki injili. Ungeweza kumpa mshiriki wa darasa kipande cha tunda na muombe ashawishi darasa lote kula tunda hili mara kwa mara. Ni kwa jinsi gani somo hili la vitendo linafanana na uzoefu wa Lehi katika 1 Nefi 8:10–16? Tunajifunza nini kutokana na uzoefu wa Lehi ambacho kitatusaidia tunaposhiriki injili? Kama sehemu ya majadiliano haya, unaweza kutaka kushiriki video “Mambo Mazuri ya Kushiriki” (ChurchofJesusChrist.org).

  • Mzee David A. Bednar alifundisha, “Tunda juu ya mti ni ishara ya baraka za Upatanisho” (Ndoto ya Lehi: Kushikilia Daima Fimbo ya Chuma,” Ensign au Liahona, Okt. 2011, 34). Fikiria kuwasiliana na washiriki wachache wa darasa mapema na waombe kutafakari juu ya 1 Nefi 8:11–16 na kufikiria kuhusu maswali kama haya: Ni kwa jinsi gani ninaweza kuelezea utamu ambao Upatanisho wa Yesu Kristo umeleta katika maisha yangu? Ni kwa jinsi gani nimewapungia mkono wengine waje kuonja utamu wake? (ona mstari wa 15). Ni kwa jinsi gani wengine wamenialika kutafuta baraka za Upatanisho wa mwokozi? Ninavutiwa kufanya nini ninaposoma 1 Nefi 8:11–16? Waalike washiriki hawa kushiriki majibu yao wakati wa darasa, na waalike washiriki wote wa darasa kutoa utambuzi wao wakati wa majadiliano.

Ono la Lehi la mti wa uzima

Minerva K. Teichert (1888–1976), Nyumba ya Ulimwengu, 1954, mafuta juu ya ubao , 36 x 48 inchi. Makumbusho ya Sanaa ya Chuo Kikuu cha Brigham Young

1 Nefi 8:19–38

Neno la Mungu linatuongoza kwa Mwokozi na linatusaidia kuhisi upendo wake.

  • Njia mojawapo ya kuanza majadiliano kuhusu ono la Lehi ni kuwaalika washiriki wachache wa darasa kuchora taswira ya ono ubaoni, wakitumia 1 Nefi 8:19–38 kama mwongozo. Au ungeweza kuonyesha picha ya ono la Lehi kutoka kwenye muhtasari wa wiki hii katika Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia. Kisha ungeweza kumwalika kila mshiriki wa darasa kutafuta mistari ambayo inatoa tafsiri ya moja ya alama katika mchoro au picha—tafsiri hizi zinaweza kupatikana katika 1 Nefi 11:4–25, 35–36; 12:16–18; na 15:21–33, 36. Wakati washiriki wa darasa wanashiriki kile walichopata, waalike kujadili kile ambacho alama hizi zinatufundisha. Kwa mfano, ni kitu gani jengo kubwa na pana linatufundisha kuhusu majivuno? Ni kitu gani fimbo ya chuma inatufundisha kuhusu neno la Mungu? Wanaweza pia kuzungumza kuhusu jinsi ono la Lehi lilivyowasaidia kuja kwa Kristo. Ni kwa jinsi gani tumejiona sisi wenyewe katika ono hili?

  • Ujumbe mmoja maarufu katika ono la Lehi ni umuhimu wa neno la Mungu, uliooneshwa na fimbo ya chuma. Kusaidia kusisitiza ujumbe huo, ungeweza kuligawa darasa katika makundi manne na wapangie kila kundi kujifunza kuhusu makundi manne ya watu ambao Lehi aliwaona, kama ilivyoelezwa katika “Nyenzo za Ziada” na katika 1 Nefi 8:21–23, 24–28, 30, na 31–33. Kisha waruhusu washiriki wa darasa kushiriki wao kwa wao kile walichojifunza. Ungeweza pia kutoa dakika chache kwa washiriki wa darasa kutafakari kile wanachohisi kuvutiwa kufanya kuhakikisha kwamba “wanashikilia kwa nguvu ile fimbo ya chuma” (1 Nefi 8:30).

1 Nephi 10:17–19

Mungu atafunua ukweli kwetu kama tutautafuta kwa bidii.

  • Ukungu wa giza ambao unaficha njia yetu na sauti za dhihaka kutoka jengo kubwa na pana vinaweza kufanya iwe vigumu kwetu sisi kupata ukweli. Kusoma pamoja kuhusu mfano wa Nefi kama mtafutaji wa ukweli kungeweza kusaidia. Ungeweza kuanza majadiliano kwa kuwauliza washiriki wa darasa kutambua baadhi ya jumbe zinazokanganya ulimwengu unazotuma. Kwa mfano, ni mawazo gani ya kidunia ambayo manabii na mitume wametuonya kuyahusu katika mkutano mkuu wa hivi karibuni? Fikiria kutengeneza orodha ubaoni ya hatua ambazo Nefi alichukua ili kupata ushahidi wake mwenyewe wa ukweli wa ono la baba yake (ona 1 Nefi 10:17–19; 11:1). Je, tunawezaje kufuata mfano wake tunapotafuta ukweli?

ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Kuwatia moyo washiriki wa darasa kusoma 1 Nefi 11–15, waalike kutafuta ni namna gani taswira zifuatazo zinahusika na ndoto ya Lehi: mtoto mchanga Yesu, msalaba, mama wa makahaba, umati uliokusanyika pamoja kwa vita, na vitabu.

ikoni ya nyenzo

Nyenzo za Ziada

Video za Kitabu cha Mormoni.

Fikiria kuonesha video ambayo inaonesha kwa picha matukio kutoka katika sura hizi (ona mkusanyiko wa video za Kitabu cha Mormoni kwenye ChurchofJesusChrist.org au Gospel Library app).

Makundi manne ya watu katika ndoto ya Lehi.

Kundi la 1.“Katika 1 Nefi 8:21–23 tunajifunza kuhusu kundi la kwanza la watu waliosonga mbele na walianza katika njia ambayo ilielekea kwenye mti wa uzima. Hata hivyo, wakati watu walipokabiliwa na ukungu wa giza, ambao unawakilisha ‘majaribu ya shetani’ (1 Nefi 12:17, walipoteza njia yao, walizurura mbali na walipotea. Fahamu kwamba hakuna palipotajwa katika mistari hii fimbo ya chuma. Wale ambao hawajali au kuchukulia kiwepesi neno la Mungu huwa hawana fursa kwenye ile dira takatifu ambayo inaonesha njia ya kwenda kwa Mwokozi.”

Kundi la 2.“Katika 1 Nefi 8:24–28 tunasoma kuhusu kundi la pili la watu ambao waliipata njia nyembamba iliyosonga ambayo iliongoza kwenye mti wa uzima. Kundi hili ‘lilisonga mbele na kupenya ukungu wa giza, wakishikilia fimbo ya chuma, hadi wakafika na kula matunda ya mti’ (mstari wa 24). Hata hivyo, wakati wakazi waliovalia kifahari wa lile jengo kubwa na pana walipowadhihaki kundi hili la pili la watu, ‘Waliaibika‘ na ‘wakaingia katika njia zilizokataliwa na wakapotea’ (mstari wa 28). … Hata pamoja na imani, msimamo, na neno la Mungu, kundi hili hatimaye lilipotea—labda kwa sababu kwa muda fulani tu walisoma au walijifunza au walipekua maandiko.”

Kundi la 3.“Katika mstari wa 30 tunasoma kuhusu kundi la tatu la watu waliosonga mbele ‘daima wameshikilia ile fimbo ya chuma, hadi wakafika na kuinama na kula matunda ya ule mti.’ Kishazi muhimu katika msitari huu ni daima kushikilia kwa nguvu kwenye fimbo ya chuma. Kundi la tatu pia lilisonga mbele kwa imani na kusadiki sana; hata hivyo, hakuna ishara kwamba walizurura mbali, waliingia katika njia zilizokataliwa, au walipotea. Labda kundi hili la tatu la watu kwa uaminifu walisoma na walijifunza na walipekua maandiko. … Hili ni kundi ambalo wewe na mimi tunatakiwa kujitahidi kujiunga nalo.”

Kundi la 4.“Kundi la nne halikutafuta mti, wakitamani badala yake jengo kubwa na pana kama hatma ya mwisho wa safari yao (ona 1 Nefi 8:31–33).”

(David A. Bednar, “Ndoto ya Lehi: Kushikilia Daima Fimbo ya Chuma,” Ensign au Liahona, Okt. 2011, 34–36.)

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Onyesha kujiamini kupitia matarajio makubwa. Wanafunzi wengine hawajiamini katika uwezo wao wa kujifunza injili wao wenyewe. Waahidi washiriki wa darasa kwamba wanapojitahidi kujifunza wao wenyewe, Roho Mtakatifu atawafundisha. Ungeweza kupendekeza njia za kuwasaidia kuanza. (Ona Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 29–30.)