“Januari 11–17. Mafundisho na Maagano 2; Historia ya—Joseph Smith 1:27–65: ‘Mioyo ya Watoto itawageukia Mababu Zao,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Januari 11–17. Mafundisho na Maagano 2; Historia ya—Joseph Smith 1:27–65,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Mafundisho na Maagano 2021
Januari 11–17
Mafundisho na Maagano 2; Historia ya—Joseph Smith 1:27–65.
“Mioyo ya Watoto Itawageukia Mababu Zao”
Kabla hujasoma mawazo katika muhtasari huu, jifunze Mafundisho na Maagano 2 na Historia ya—Joseph Smith 1:27–65, na unandike misukumo yako ya kiroho.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Ili kuwahimiza washiriki wa darasa kushiriki umaizi na uzoefu ambao walipata walipokuwa wakijifunza maandiko haya, unaweza ukawaomba washiriki mstari ambao uliwasababisha kutafakari kwa kina zaidi kuliko kawaida. Ni nini kiliwavutia katika mstari huo?
Fundisha Mafundisho
Historia ya—Joseph Smith 1:27–65
Joseph Smith aliitwa na Mungu kufanya kazi Yake.
-
Darasa lako linaweza likafaidika kutokana na kufanya mapitio ya hadithi hiyo katika Historia ya—Joseph Smith 1:27–65? Ungeweza kumwalika mshiriki wa darasa kuifupisha, au washiriki wa darasa wangeweza kusimuliana hadithi hiyo wakiwa wawili wawili au katika makundi. Wahimize kujumuisha maelezo mengi kadri wanavyoweza kukumbuka. Ni kwa jinsi gani hadithi hii inaimarisha ushuhuda wetu wa wito mtakatifu wa Joseph Smith? Ni masomo gani tunajifunza kutoka kwenye hadithi hii kuhusu Mungu Anavyofanya Kazi Yake?
-
Fikiria kuonyesha vitu au picha zinazohusiana na kazi ambayo Joseph Smith aliitwa kuifanya, kama vile Kitabu cha Mormoni au picha ya Hekalu. Washiriki wa darasa wangeweza kupata mistari katika Historia ya—Joseph Smith 1:33–42 ambayo inafundisha vipengele hivi vya huduma ya Nabii. Je, ni kwa jinsi gani kazi ya Mungu kwake Joseph Smith inahusuana na kazi ambayo Mungu yu nayo kwetu? Ni nini manabii wetu wanaoishi hutufundisha kuhusu kazi hii?
Eliya alikuja kugeuza mioyo yetu kuwaelekea mababu zetu.
-
Je, washiriki wa darasa lako wangenufaika kutokana na majadiliano kuhusu Eliya alikuwa nani na kuhusu nguvu za kufunganisha alizorejesha? Washiriki wa darasa wanaweza kusoma kuhusu Eliya katika Kamusi ya Biblia au Mwongozo wa Maandiko au kufanya mapitio ya hadithi kutoka katika maisha yake (ona 1 Wafalme 17–18). Je, ni nini habari hii huongezea katika uelewa wetu wa Mafundisho na Maagano 2? Ungeweza pia kuzungumzia kuhusu kufunga kitu humaanisha nini. Pengine baadhi ya vitu vingeweza kusaidia, kama vile mkebe wa chakula, mfuko wa kuhifadhi wa plastiki wenye zipu, au muhuri unaoidhinisha hati. Ni kwa jinsi gani vitu hivi vinatusaidia kuelewa inamaanisha nini kufunganisha familia pamoja? Je, uwezo huu unasaidiaje kutimiza lengo la uumbaji wa dunia? (ona Mafundisho na Maagano 138:47–48 na maneno ya Rais Russell M. Nelson katika “Nyenzo za Ziada”). Ili kuwasaida washiriki wa darasa kuona jinsi unabii katika Mafundisho na Maagano 2 ulitimizwa, unaweza kujadili Mafundisho na Maagano 110:13–16.
-
Labda kujifunza kuhusu “ahadi zilizofanywa kwa baba” (Mafundisho na Maagano 2:2) kunaweza kuwasaidia wale unaowafundisha kuelewa vyema nguvu za ukuhani ambazo Eliya alitumwa kurejesha. “Mababu” ni kina nani? (ona Mafundisho na Maagano 27:9–10). Ni ahadi gani Bwana alimpa Ibrahamu, Isaka, na Yakobo? (ona Mwanzo 17:1–8; 22:16–18; 26:1–5, 24; 28:11–15; Ibrahimu 2:8–11). Inamaanisha nini “kupanda” ahadi hizi katika mioyo yetu? Ni kwa jinsi gani kufanya hivi kutatusaidia kuigeuza mioyo yetu kwa mababu zetu?
-
Ili kuwatia moyo washiriki wa darasa kuigeuza mioyo yao kwa mababu zao, unaweza kuwaalika washiriki wachache waongoze mjadala kuhusu mada hiyo. Zingatia kumjumuisha mshauri wa kazi ya hekalu na kazi ya historia ya familia. Unaweza kuanza kwa kusoma Mafundisho na Maagano 2:2–3 na kualika viongozi wa mjadala washiriki uzoefu ambapo mioyo yao iligeuzwa kwa mababu zao. Ni nini kimetendeka maishani mwao ambacho kiliwasaidia wao kutaka kujifunza kuhusu historia ya familia yao? Ni mapendekezo yapi wanaweza kutoa ili kuwasaidia washiriki wengine wa darasa waweze kujihusisha na kazi ya historia ya familia na huduma ya hekalu? Kauli ya Rais Dallin H. Oaks katika “Nyenzo za Ziada” na video “The Promised Blessings of Family History” na “If We Put God First” (ChurchofJesusChrist.org) vinaweza kusaidia kuwatia moyo washiriki wa darasa. Pia ungeweza kuwaelekeza washiriki kwenye FamilySearch.org kwa ajili ya mawazo.
Nyenzo za Ziada
Lengo la Uumbaji.
Rais Russell M. Nelson alifundisha:
“Maisha ya milele, yaliyowezeshwa na Upatanisho, ni lengo kuu la Uumbaji. Kusema sentensi hiyo katika hali yake hasi, kama familia hazingefungwa katika mahekalu matakatifu, dunia nzima ingeangamia.
“Malengo ya Uumbaji, Anguko, na Upatanisho vyote hukutana katika kazi takatifu inayofanyika katika mahekalu ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho” (“Upatanisho,” Ensign, Nov. 1996, 35). Ona pia Musa 1:39.
Kila mmoja anaweza kufanya kitu fulani.
Rais Dallin H. Oaks alifundisha: “Katika kazi ya kuwakomboa wafu kuna majukumu mengi yanayopaswa kutekelezwa. … Juhudi zetu siyo kulazimisha kila mtu afanye kila kitu, bali kumtia moyo kila mtu kufanya kitu fulani” (“Historia ya Familia: ‘Kwa Busara na Mpangilio,’” Ensign, Juni 1989, 6).