“Juni 28–Julai 4. Mafundisho na Maagano 71–75: ‘Hakuna Silaha Iliyotengenezwa dhidi Yenu Itakayofanikiwa,’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Mafundisho na Maagano 2021 (2020)
“Juni 28–Julai 4. Mafundisho na Maagano 71–75,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: 2021
Juni 28–Julai 4
Mafundisho na Maagano 71–75
“Hakuna Silaha Iliyotengenezwa dhidi Yenu Itakayofanikiwa”
Unaposoma Mafundisho na Maagano 71–75, fikiria kuhusu watu unaowafundisha. Unajua nini kuhusu wao? Ni kipi wanachohitaji?
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Waalike washiriki wa darasa kushiriki baadhi ya kweli walizozipata wakati wakijifunza Mafundisho na Maagano 71–75. Ni uzoefu gani wameupata kwa kweli hizi?
Fundisha Mafundisho
Tunaweza kufuata mwongozo wa Roho Mtakatifu tunapotetea imani yetu.
-
Je, tumewahi kuhisi hofu au wasiwasi kuhusu kutetea imani yetu? Labda ungeweza kuwaalika washiriki wa darasa kuandika kwenye ubao maneno au virai wanavyopata katika Mafundisho na Maagano 71 ambavyo vinaelezea jinsi Bwana alivyomueleza Joseph na Sidney kujibu ukosoaji wa Ezra Booth na wengine. Kisha washiriki wa darasa wangeweza kujadili katika vikundi vidogo kile maelekezo haya yanachomaanisha kwetu leo. Kwa nini ni muhimu kwamba tufanye “kulingana na sehemu ya Roho” Bwana anayotupatia? (mstari wa 1).
Inaweza kuwa yenye kusaidia kutazama video “Everyday Example: When Beliefs Are Questioned” (ChurchofJesusChrist.org). Washiriki wa darasa wanaweza kutafuta njia ambazo kweli katika sehemu ya 71 zinadhihirishwa katika video hiyo. Labda wangeweza pia kushiriki mifano ya namna Mwokozi alivyowajibu wakosoaji Wake (kwa mfano, ona Mathayo 22:15–22; 26:59–64; Yohana 10:37–38).
Maaskofu ni wasimamizi juu ya maslahi ya kiroho na ya kimwili ya ufalme wa Bwana.
-
Ni jinsi gani maagizo ya Bwana kwa Newel K. Whitney, wakati alipoitwa kuwa askofu kule Kirtland, yanaweza kusaidia wale unaowafundisha kuwa na shukrani kwa ajili ya maaskofu ambao wameitwa kuwatumikia? Ungeweza kuwaomba washiriki wa darasa lako kuchunguza Mafundisho na Maagano 72:8–16, wakitafuta baadhi ya majukumu ya Askofu Whitney na kisha kuyalinganisha na majukumu ya maaskofu leo (ona maelezo ya Rais Gordon B. Hinckley kuhusu majukumu ya askofu katika “Nyenzo za Ziada” au video husika, “The Office of Bishop” [ChurchofJesusChrist.org]). Labda washiriki wa darasa wangeweza kushiriki jinsi walivyobarikiwa kupitia huduma ya askofu. Tunaweza kufanya nini ili kumuidhinisha askofu wetu kikamilifu?
Tunaweza tafuta nafasi za kushiriki injili.
-
Bwana alimwambia Joseph Smith na Sidney Rigdon wahubiri injili “ilimradi yawezekana” (Mafundisho na Maagano 73:4) wakati pia walipokuwa wakishughulika na kutafsiri Biblia. Labda washiriki wa darasa wanaweza kushiriki baadhi ya njia ambazo wamegundua “zinawezekana”—au ni halisi—kushiriki injili miongoni mwa majukumu yao mengine. Wanaweza kupata ushauri wenye kusaidia kutoka kwenye ujumbe wa Mzee Dieter F. Uchtdorf “Kazi ya Umisionari: Kushiriki Kilicho Moyoni Mwako” (Ensign au Liahona, Mei 2019, 15–18).
Mungu anatutaka “tufanye kazi kwa nguvu [zetu].”
-
Maagizo ya Bwana kwa wazee kadhaa kuhusu jinsi ya kushiriki injili yangeweza kuwachochea washiriki wa darasa kushiriki injili kwa bidii. Ungeweza kuandika kwenye ubao Fanya kazi kwa bidii na kuwaomba washiriki wa darasa waorodheshe maneno na virai ambavyo vinawajia akilini wakati wanapofikiria kuhusu mtu anayefanya kazi kwa bidii katika kushiriki injili. Pia wangeweza kujadili maana ya “kungojea ” au “kuwa mzembe” katika kushiriki injili. Ni nini Mafundisho na Maagano 75:2–16 inatufundisha jinsi Mwokozi anavyowasaidia wale wanaomhudumia Yeye kwa uaminifu?
Nyenzo za Ziada
Majukumu ya askofu.
Rais Gordon B. Hinckley alifundisha:
“Ninabeba moyoni mwangu shukrani kubwa kwa ajili ya maaskofu wetu. Nina shukrani kubwa mno kwa ajili ya ufunuo wa Mwenyezi ambao kupitia kwao ofisi hii ilibuniwa na kufanya kazi. …
“… Tunakutarajia usimame kama kuhani mkuu msimamizi wa kata, mshauri wa watu, mlinzi na msaidizi wa wale walio katika shida, mfariji wa wale walio na huzuni, na mgawaji kwa wenye mahitaji. Tunatarajia usimame kama mwagalizi na mlinzi wa mafundisho ambayo yanafundishwa katika kata yako, wa ubora wa mafundisho, wa kujaza ofisi nyingi ambazo ni muhimu. …
“… Unahitajika kuhakikisha kuwa hakuna anayekosa chakula au mavazi au makazi. Ni sharti ujue hali za wote unaowasimamia.
“Ni sharti uwe mfariji na kiongozi wa watu wako. Mlango wako daima uwe wazi kwa vilio vyovyote vya dhiki. Lazima uwe na nguvu za kuwasaidia kubeba mizigo yao. Ni lazima ufikie kwa upendo hata kwa yule ambaye ni mtenda mabaya” (“Wachungaji wa Kundi la Mifugo,” Ensign, Mei 1999, 52–53).