Njoo, Unifuate
Septemba 30–Oktoba13. Waefeso: ‘Kwa Kusudi la Kuwakamilisha Watakatifu’


Septemba 30–Oktoba 13 Waefeso: ‘Kwa Kusudi la Kuwakamilisha Watakatifu’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Agano Jipya 2019 (2019)

Septemba 30–Oktoba 13 Waefeso,” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: 2019

familia ikitazama picha

Septemba 30–Oktoba 13

Waefeso

“Kwa Kusudi la Kuwakamilisha Watakatifu”

Fikira na mawazo kuhusu jinsi na namna ya kufundisha vitakuja wakati kwa sala ukijifunza Waefeso, hotuba za mkutano mkuu wa hivi karibuni, muhtasari huu na Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Watu Binafsi na Familia.

Andika Misukumo Yako

ikoni ya kushiriki

Alika Kushiriki

Fikiria kuwaalika washiriki wa darasa kuandika sentensi moja kwa ufupi juu ya kitu walichojifunza katika kusoma kwao wiki hii na kisha ambatisha ufupisho wao kwenye ubao. Pasipo mpangilio chagua ufupisho mchache, na waalike washiriki wa darasa waliouandika kuelezea mawazo yao.

ikoni ya kufundisha

Fundisha Mafundisho

Waefeso 2:19–22; 4:4–8, 11–16

Manabii na mitume—na sisi sote—tunaliimarisha na kuliunganisha kanisa.

  • Je, wewe na washiriki wa darasa lako mngeweza kujenga kitu kwa pamoja ili kuonyesha jinsi gani Kanisa “linajengwa juu ya msingi wa mitume na manabii” na jinsi gani Mwokozi ni “jiwe kuu la pembeni”? (Waefeso 2:20). Labda washiriki wa darasa wangeweka alama kwenye matofali au vikombe vya karatasi na kuvipanga kama mnara au piramidi, na Yesu Kristo na mitume na manabii wakiwa msingi. Kisha ungeweza kuonyesha nini kingetokea kama Kristo na mitume na manabii wangeondolewa. Kwa nini jiwe kuu la pembeni ni mfano mzuri wa Yesu Kristo na kazi Yake katika Kanisa? (Kwa maelezo juu ya jiwe kuu la pembeni, ona “Nyenzo za Ziada.”) Washiriki wa darasa wangeweza kuchunguza Waefeso 2:19–22; 4:11–16 kwa ajili ya baraka ambazo tunapokea kwa sababu ya mitume, manabii na viongozi wengine wa Kanisa. Tunaweza kufanya nini ili kujenga maisha yetu kwenye mafundisho yao?

    jiwe la pembeni la hekalu

    Yesu Kristo ni jiwe la pembeni la Kanisa.

  • Ili kuonyesha jinsi gani mafundisho yanaweza kutoeleweka pasipokuwepo na maelekezo endelevu kutoka kwa manabii na mitume, ungeweza kucheza mchezo ambapo unamsimulia hadithi fupi mshiriki mmoja wa darasa bila kuruhusu mtu mwingine yeyote kusikia. Kisha mwalike mshiriki huyo wa darasa kurudia hadithi hiyo kwa mshiriki mwingine na kuendelea mpaka hadithi iwe imesimuliwa kwa washiriki kadhaa. Kisha muulize mtu wa mwisho ambaye amesikia hadithi kuliambia darasa kile alichosikia. Je, kuna kitu chochote kimebadilika kwenye hadithi? Nini kingetokea kama mwalimu angesahihisha makosa kabla? Ni nini shughuli hii inatufundisha kuhusu kwa nini kanisa la Kristo lazima “lijengwe juu ya msingi wa mitume na manabii”?

  • Kama washiriki wa darasa lako walisikiliza mkutano mkuu tangu mlipokutana kwa mara ya mwisho, waalike kuelezea ni kwa jinsi mambo yaliyofundishwa wakati wa mkutano yaliwasaidia kutimiza kusudi lililosemwa katika Waefeso 4:11–16.

  • Labda ungeweza kuwapa muda washiriki wa darasa kuorodhesha baadhi ya shughuli au majukumu ambayo wameombwa kuyatimiza kanisani (ona Waefeso 4:1)—kwa mfano, kaka au dada mhudumu, mzazi, mfuasi wa Kristo na kadhalika. Kisha wangeweza kubadilishana orodha na mshiriki mwingine wa darasa, kusoma Waefeso 4:4–8, 11–16, na kuelezea ni kwa namna gani miito na majukumu katika orodha zao husaidia kujenga mwili wa Kristo. Tunawezaje kufanya kazi pamoja ili kuwa na umoja chini ya “Bwana mmoja, imani moja na ubatizo mmoja”?

Waefeso 5:22–6:4

Kufuata mfano wa Kristo kunaweza kuimarisha mahusiano ya kifamilia.

  • Ingawaje Waefeso waliishi kwenye utamaduni ambao wake walikuwa hawachukuliwi kuwa sawa na waume zao, waraka huu bado unabeba baadhi ya ushauri wa thamani kwa wanandoa leo. Ungeweza kuandika maswali kama yafuatayo kwenye ubao na kuwaalika washiriki wa darasa kuyajadili wakati wakisoma Waefeso 5:22–33 katika makundi: Ni kwa namna gani Kristo alionyesha upendo kwa Kanisa? Tunaweza kufanya nini kufuata mfano Wake katika namna ya kuwachukulia wenzi wetu? Ungeweza kuwaalika washiriki wa darasa kutoa mifano waliyoiona ya wenzi wakitendeana katika njia kama za Kristo. Tuanawezaje kutumia kanuni hizi katika mahusiano mengine ya kifamilia?

  • Wakati ushauri wa Paulo “waheshimu baba yako na mama yako” (Waefeso 6:12) ulikuwa ukielekezwa kwa watoto, unaweza kutumika kwetu sote, bila kujali umri wetu au hali ya kifamilia. Waalike washiriki wa darasa kufikiria kuhusu ni kwa namna gani wanaweza kutumia ushauri wa Paulo katika Waefeso 6:1–3 katika hali zao wenyewe. Kwa mfano, ni kwa namna gani tunaweza kuwaheshimu wazazi wetu hata kama chaguzi zao haziendani na mafundisho ya Yesu Kristo? Ungeweza kuwapa washiriki wa darasa dakika chache kuandika kile wanachoweza kufanya ili kuwaheshimu vizuri zaidi wazazi wao.

  • Kama wao ni wazazi—au wazazi watarajiwa—wa watoto wadogo katika darasa lako, wangeweza kunufaika kwa kujadiliana Waefeso 6:4. Inamaanisha nini kuwalea watoto katika “makuzi na maonyo ya Bwana”? Labda washiriki wa darasa wenye watoto wakubwa wangeweza kuelezea hii humaanisha nini kwao na kwa namna gani wamejaribu kutumia ushauri huu katika familia zao.

Waefeso 6:10–18

Silaha za Mungu zitatusaidia kutulinda dhidi ya uovu.

  • Ni kipi kingeweza kuwasaidia washiriki wa darasa kujitahidi kuvaa silaha za Mungu kila siku? Ungeweza kuandaa shughuli ambayo washiriki wa darasa wangehusisha vipande vya silaha na kanuni au maadili vinavyowakilisha katika Waefeso 6:14–17. Ni kwa namna gani kila kipande cha silaha kinasaidia kutulinda kutokana na uovu? (Kwa msaada, ona “Nyenzo za Ziada.”) Ni kwa namna gani washiriki wa darasa wamevaa silaha hizi? Kama sehemu ya mjadala huu, ungeweza kushiriki ufafunuzi wa Rais N. Eldon Tanner katika “Nyenzo za Ziada.” Tunaweza kufanya nini ili kutambua na kuimarisha udhaifu wowote katika silaha zetu?

ikoni ya kujifunza

Himiza Kujifunza Nyumbani

Ili kuwahamasisha washiriki wa darasa kusoma Wafilipi na Wakolosai, ungeweza kuwaambia kwamba moja ya Makala ya Imani msingi wake uko kwenye mstari unaopatikana katika moja ya nyaraka hizi. Je, wanaweza kuupata katika kujifunza kwao wiki hii?

ikoni ya nyenzo

Nyenzo za Ziada

Waefeso

Je, jiwe kuu la pembeni ni nini?

Jiwe kuu la pembeni ni jiwe la kwanza linalowekwa kwenye kona ya msingi. Linatumika kama rejeo katika upimaji na upangaji wa mawe mengine, ambapo ni lazima yalingane na jiwe kuu la pembeni. Kwa sababu linabeba uzito wa jengo zima, jiwe kuu la pembeni lazima liwe imara, bila kutikisika na ni la kutegemewa (ona “Jiwe la pembeni,” Ensign Jan. 2016, 74–75).

Silaha za Mungu

Kiuno kimefungwa na mshipi wa ukweli:Kipande hiki cha silaha ni kama mkanda unaofungwa kuzunguka kiuno. Neno funga pia linaweza kumaanisha kujikinga na, kuimarisha au kuweka mkazo.

Dirii:Dirii huulinda moyo na viungo vingine muhimu vya mwili.

Vazi la kulinda miguu:Hii humaanisha kifuniko cha ulinzi kwa miguu ya mwanajeshi .

Ngao:Ngao inaweza kulinda karibia kila sehemu ya mwili kutokana na mashambulizi mbalimbali.

Kofia ya chuma:Kofia ya chuma hulinda kichwa

Upanga:Upanga unaturuhusu kuchukua hatua dhidi ya adui.

“Chunguza silaha zako”

Rais N. Eldon Tanner, ambaye alitumikia kama mshauri katika Urais wa Kwanza, aliwaalika waumini wa Kanisa kutathmini uwezo wa silaha zao binafsi kwa kutafakari jitihada zao za kuishi injili. Kisha alifafanua:

“Kama … silaha zetu ni dhaifu, kuna sehemu ya mwili wetu inayoweza kupatikana kuwa haina ulinzi, eneo lililo wazi kwa mashambulizi, na tutaathirika kwa kujeruhiwa au kuharibiwa na Shetani, ambaye atatafuta mpaka apate udhaifu wetu, kama tunao.

“Chunguza silaha zako. Je, kuna sehemu ambayo iko wazi na haina ulinzi? Chagua sasa kuongeza kipande chochote ambacho kinakosekana. Bila kujali ni kwa namna gani silaha zako ni kuukuu au zinakosa baadhi ya vipande, daima kumbuka kwamba iko ndani ya uwezo wako kufanya maboresho muhimu kukamilisha silaha zako.

“Kupitia kanuni kuu ya toba unaweza kugeuza maisha yako na kuanza sasa kuvaa silaha za Mungu kupitia kujifunza, sala, na azimio la kumtumikia Mungu na kutii amri zake” (“Put on the Whole Armor of God,” Ensign, Mei 1979, 46).

Kuboresha Ufundishaji Wetu

Jitahidi kupata upendo kama wa Kristo. Mwingiliano wako na wale unaowafundisha lazima uhamasishwe na upendo. Wewe pamoja na wale unaowafunza mtabarikiwa pale mnapoomba kukuza upendo kama wa Kristo na kutafuta njia za kuuonyesha (ona Kufundisha katika Njia ya Mwokozi, 6; Moroni 7:48).