“Juni 6–12. Ruthu; 1 Samweli 1–3; ‘Moyo Wangu Wamshangilia Bwana’” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: Agano la Kale 2022 (2021)
“Juni 6–12. Ruthu; 1 Samweli 1–3” Njoo, Unifuate—Kwa Ajili ya Shule ya Jumapili: 2022
Juni 6–12
Ruthu; 1 Samweli 1–3
“Moyo Wangu Wamshangilia Bwana”
Ni muhimu kuwa tayari kufundisha, lakini hakikisha kwamba mipango yako ni pamoja na kuwapa washiriki wa darasa fursa ya kushiriki kile walichojifunza.
Andika Misukumo Yako
Alika Kushiriki
Ili kuwahimiza washiriki wa darasa kushiriki kile walichojifunza wiki hii, unaweza kuwaalika waandike ubaoni neno au kifungu kutoka Ruthu 1–4 au 1 Samweli 1–3 ambacho kiliwahamasisha wakati wa masomo yao ya binafsi au ya familia. Soma machache kwa sauti, ukiuliza washiriki wa darasa washiriki jinsi maneno na vifungu hivyo vimewahamasisha.
Fundisha Mafundisho
Kristo anaweza kugeuza msiba kuwa ushindi.
-
Ingawa washiriki wa darasa lako wanaweza kuwa na majaribu yao binafsi ambayo ni tofauti na yale ya Ruthu na Hana, wanaweza kujifunza kutokana na njia ambazo wanawake hawa waaminifu walitumia kwenye upotevu na maumivu ya moyo. Ili kuwasaidia kufanya hivyo, unaweza kugawanya darasa katika vikundi vidogo na alika kila kikundi kusoma sura kutoka Ruthu 1–4 au 1 Samweli 1. Kwenye ubao, unaweza kuandika maswali kama haya: Ruthu au Hana walikuwa wanakabiliwa na majaribu gani? Walionyeshaje imani yao katika Bwana wakati wa majaribu yao? Vikundi vingeweza kutafuta majibu kwa moja au zaidi ya maswali na kuelezea kile wanachopata. Tunajifunza nini kutoka katika hadithi hizi kuhusu jinsi Bwana anavyoweza kutusaidia katika majaribu yetu?
-
Sio kila mtu anayeomba mtoto hupokea mmoja, na sio kila mtu ambaye mwenzi wake hufa anaolewa au anaoa tena. Lakini changamoto zetu binafsi, bila kujali ni nini, zinaweza kuwa fursa za kurejea kwa Mwokozi na kuimarisha imani yetu Kwake. Unaweza kuwaomba washiriki wa darasa kusoma Ruthu 2:11–12 na 1 Samweli 1:9–11 na kuongelea jinsi majaribu ya Ruthu na Hana yalivyoimarisha uhusiano wao na Bwana. Washiriki wa darasa pia wanaweza kushiriki jinsi imani yao wenyewe ilivyoimarishwa kwa sababu walimgeukia Yesu Kristo wakati wa jaribu.
Ili kuunga mkono mjadala huu, unaweza kualika mshiriki mmoja au zaidi wa darasa kuja akiwa amejiandaa tayari kushiriki mawazo kutoka katika moja ya ujumbe ufuatao: Ujumbe wa Dada Reyna I. Aburto “Iwe Mawingu au Jua, Bwana, Kaa pamoja Nami!” (Liahona, Nov. 2019, 57–60); sehemu yenye kichwa cha habari “Furaha ya Kushinda kupitia Kristo” kutoka kwenye ujumbe wa Mzee D. Todd Christofferson “Furaha ya Watakatifu” (Liahona, Nov. 2019, 16–17); au maneno ya Rais Elaine S. Dalton katika “Nyenzo za Ziada.” Waombe washiriki wa darasa kushiriki kile walichojifunza kuhusu jinsi majaribu yetu yanavyoweza kuwa fursa kwa ajili ya imani kubwa katika Yesu Kristo.
Tunapaswa kusikiliza na kutii sauti ya Bwana.
-
Kunaweza kuwa na watu katika darasa lako ambao, kama Samweli, wamesikia sauti ya Bwana lakini hawakugundua kama ni ya Kwake. Unwaeza kuwaalika washiriki wa darasa kupitia upya 1 Samweli 3, wakiangalia kile ambacho Samweli alifanya ambacho kinaweza kutusaidia katika juhudi zetu za kusikia na kutii sauti ya Bwana. Unaweza pia kuwaomba washiriki wawili wa darasa kuigiza tena maongezi kati ya Samweli na Eli.
-
Wakati mwingine tunajikuta katika hali kama ya Eli—tunakuwa na fursa ya kumsaidia mtu kutambua sauti ya Bwana. Labda washiriki wa darasa wangeweza kushiriki jinsi walivyofanya hivi kwa marafiki, washiriki wa familia zao, au wengine. Ni maandiko au uzoefu gani ambao tumeshiriki kuwasaidia wengine kuelewa ni jinsi gani Bwana anawasiliana na sisi? (ona, kwa mfano, Mafundisho na Maagano 6:22–23; 8:2–3; 9:7–9).
Nyenzo za Ziada
Hatuko peke yetu kamwe.
Rais Elaine S. Dalton alifundisha:
“Safari ya maisha wakati mwingine hutupeleka kwenye njia zisizotarajiwa. Kuna milima na kona katika barabara ambayo hakuna yeyote kati yetu anayeweza kutarajia. Lakini kwa kila moja ya milima na kona hizi pia kuna fursa—fursa ya kuchagua majibu yetu na mpango wetu wa utekelezaji. Ugumu katika maisha unaweza kuwa fursa za kutusaidia kuwa karibu zaidi na Mwokozi na kumtumaini Yeye kikamilifu. Katika mchakato wa kuishi karibu na Yeye kila siku, tunakuza sifa na tabia kama za Kristo. …
“Kama Ruthu na Hana, sisi sote tutapata shida. Yawezekana tusiweze daima kuelewa usanifu wa Bwana wa maisha yetu, lakini ni ushuhuda wangu kwamba hatuko peke yetu kamwe. Yupo nasi daima, na anatuahidi, ‘Hamuwezi kuona kwa macho yenu ya asili, kwa wakati huu, mipango ya Mungu wenu juu ya mambo yale ambayo yatakuja hapo baadaye, na utukufu utakaofuata baada ya taabu kubwa’ [Mafundisho na Maagano 58:3]” (“Masomo kutoka kwa Ruthu na Hana,” Ensign, Apr. 2006, 35, 37).
Ona pia Yohana 14:18; Alma 38:5.