Nyenzo za Ziada kwa ajili ya Kuwafundishia Watoto
Kiambatisho A: Kwa ajili ya Wazazi—Kuwaandaa Watoto Wako kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu


“Kiambatisho A: Kwa ajili ya Wazazi—Kuwaandaa Watoto Wako kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024 (2023)

“Kiambatisho A,” Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Nyumbani na Kanisani: Kitabu cha Mormoni 2024

Kiambatisho A

Kwa ajili ya Wazazi—Kuwaandaa Watoto Wako kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu

Kwa sababu Yeye anakupenda, anakuamini na anajua uwezo wako, Baba wa Mbinguni amekupatia wewe fursa ya kuwasaidia watoto wako waingie na wasonge kwenye njia Yake ya agano, njia ya kuelekea uzima wa milele (ona Mafundisho na Maagano 68:25–28). Hii inajumuisha kuwasaidia wajiandae kufanya na kuyashika maagano matakatifu, kama vile agano la ubatizo na maagano yanayofanyika hekeluni. Kupitia maagano haya, watoto wako watakuwa wamejiunganisha wao wenyewe kwa Mwokozi, Yesu Kristo.

Kuna njia nyingi za kuwaandaa watoto wako kwa ajili ya safari hii kwenye njia ya agano, na Baba wa Mbinguni atakusaidia ugundue njia iliyo bora zaidi ya kuwasaidia. Unapotafuta mwongozo wa kiungu, weka akilini kwamba siyo kujifunza kote kunafanyika wakati wa masomo yaliyopangiliwa. Ukweli ni kwamba, sehemu ya kitu kinachofanya kujifunza nyumbani kuwe na nguvu sana ni fursa ya kujifunza kwa mfano na kupitia nyakati ndogo ndogo na za kawaida kabisa—nyakati ambazo hujitokeza katika njia ya asili katika mtiririko wa maisha ya kila siku. Kama vile kufuata njia ya agano kulivyo mchakato endelevu, wa maisha yote, ndivyo ilivyo kujifunza kuhusu njia ya agano. (Ona “Nyumba na Familia,” Kufundisha katika Njia ya Mwokozi [2022], 30–31.)

mama akiwa na mtoto

Kuna njia nyingi za kuwaanda watoto wako kwa ajili ya safari yao kwenye njia ya agano ya Mungu.

Hapa chini kuna baadhi ya mawazo ambayo yanaweza kuongoza kwenye mwongozo zaidi wa kiungu. Unaweza kupata mawazo ya ziada kwa ajili ya kuwafundisha watoto wa umri wa Msingi katika “Kiambatisho B Kwa Ajili ya Msingi—Kuwaandaa Watoto kwa Maisha Yote kwenye Njia ya Agano ya Mungu.

Ubatizo na Uthibitisho

Nefi alifundisha kwamba “lango ambalo [sisi] tutaingilia kwenye” njia ya agano “ni toba na ubatizo wa maji” (2 Nefi 31:17). Jitihada zako za kuwasaidia watoto wako wajiandae kwa ajili ya ubatizo na uthibitisho zinaweza kuweka miguu yao kuwa thabiti kwenye njia ya agano. Jitihada hizi zinaanza kwa kufundisha kuhusu imani katika Yesu Kristo na toba. Pia zinajumuisha kufundisha jinsi gani tunafanya upya maagano yetu ya ubatizo kwa kupokea sakramenti kila wiki.

Hapa kuna baadhi ya nyenzo ambazo zinaweza kukusaidia: 2 Nefi 31; toleo maalumu la gazeti la Rafiki kuhusu ubatizo; Mada za Injili, “Ubatizo,” Maktaba ya Injili.

  • Wakati wowote unapokuwa na tukio ambalo linaimarisha imani yako katika Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, lishiriki na mtoto wako. Msaidie aelewe kwamba imani ni kitu ambacho kinaweza kuendelea kukua na kuwa imara zaidi na zaidi katika maisha yote. Ni yapi baadhi ya mambo ambayo mtoto wako anaweza kufanya ili kukuza imani imara katika Yesu Kristo kabla hajabatizwa?

  • Mtoto wako anapofanya uchaguzi usio sahihi, zungumza kwa furaha kuhusu zawadi ya toba. Na wakati wewe unapofanya uchaguzi usio sahihi, shiriki furaha ambayo inakuja wakati unapotubu. Shuhudia kwamba kwa sababu Yesu Kristo aliteseka na kufa kwa ajili ya dhambi zetu, alitupatia uwezo wa kubadilika. Wakati mtoto wako anapoomba msamaha, msamehe bila sharti na kwa furaha.

  • Mwambie mtoto wako kuhusu ubatizo wako. Onesha picha na shiriki kumbukumbu zako. Zungumza kuhusu jinsi ulivyohisi, jinsi maagano yako ya ubatizo yalivyokusaidia umjue Yesu Kristo vyema zaidi na jinsi yanavyoendelea kubariki maisha yako. Mhimize mtoto wako aulize maswali.

  • Panapokuwa na ubatizo katika familia yako au kata yako, nenda na mtoto wako ili aone. Zungumzeni pamoja kuhusu kile ambacho wewe na mtoto wako mlikiona na mlivyohisi. Kama inawezekana, zungumza na mtu anayebatizwa na muulize maswali kama yafuatayo: “Je, ni kwa jinsi gani ulifanya uamuzi huu? Ulijiandaa vipi?”

  • Wakati wowote unapogundua mtoto wako anafanya kitu alichoahidi kukifanya, mpe pongezi za dhati. Onesha kwamba kutimiza ahadi kunatusaidia tujiandae kushika maagano tunayofanya wakati tunapobatizwa. Ni ahadi ipi tunafanya na Mungu wakati tunapobatizwa? Ni kipi Yeye anatuahidi sisi? (ona Mosia 18:18–10, 13).

  • Wakati wewe na mtoto wako mnapopata tukio takatifu mkiwa pamoja (kama vile kanisani, wakati mkisoma maandiko, au wakati mkimhudumia mtu), mwambie kuhusu hisia au msukumo huo wa kiroho ulionao. Mwalike mtoto wako ashiriki jinsi anavyohisi. Tambua njia tofauti Roho anavyoweza kuzungumza na watu, ikijumuisha njia ambazo Yeye anazungumza na wewe binafsi. Msaidie mtoto wako atambue nyakati ambapo yaweza kuwa anapata uzoefu wa ushawishi wa Roho Mtakatifu.

  • Angalieni pamoja video kadhaa katika mkusanyiko wa video za Maktaba ya Injili zenye kichwa cha habari “Hear Him!” Zungumzeni pamoja kuhusu njia tofauti ambazo watumishi wa Bwana wanaisikia sauti Yake. Mwalike mtoto wako achore picha au atengeneze video kuhusu jinsi yeye anavyoisikia sauti ya Mwokozi.

  • Zungumzeni kuhusu jinsi kuwa muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kulivyokubariki wewe. Ni kwa jinsi gani umekuwa karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo unapowahudumia wengine na wengine wanapokuhudumia wewe? Msaidie mtoto wako afikirie njia za kuwahudumia na kuwaimarisha wengine akiwa kama muumini wa Kanisa.

  • Fanya sakramenti iwe ni tukio takatifu na la furaha kwa familia. Msaidie mtoto wako apange njia za kufokasi juu ya Yesu Kristo wakati wa sakramenti. Je, ni kwa jinsi gani tunaonesha kwamba sakramenti ni takatifu kwetu?

  • Matoleo mengi ya gazeti la Rafiki yanajumuisha makala, hadithi, na shughuli ili kuwasaidia watoto wajiandae kwa ajili ya ubatizo na uthibitisho. Mruhusu mtoto wako achague baadhi ili asome na afurahie pamoja nawe. (Ona pia mkusanyiko wa “Preparing for Baptism” katika sehemu ya watoto ya Maktaba ya Injili.)

    mvulana akibatizwa

    Nefi alifundisha kwamba “lango ambalo [sisi] tutaingilia kwenye” njia ya agano “ni toba na ubatizo wa maji” (2 Nefi 31:17).

Uwezo, Mamlaka na Funguo za Ukuhani

Ukuhani ni mamlaka na nguvu za Mungu ambazo kwazo Yeye hubariki watoto Wake. Ukuhani wa Mungu uko duniani leo katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Waumini wote wa Kanisa ambao wanashika maagano yao—ikijumuisha watoto—wanabarikiwa kwa nguvu ya ukuhani wa Mungu katika nyumba zao ili kujiimarisha wao wenyewe na familia zao (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla: Kuhudumu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, 3.5, Nguvu hii itawasaidia waumini katika kufanya kazi ya Mungu ya wokovu na kuinuliwa katika maisha yao binafsi na ya familia (ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla2.2).

Tunapokea ibada kwa mamlaka ya ukuhani. Wakati wanaume na wanawake wanapohudumu katika miito ya Kanisa, wanafanya hivyo kwa mamlaka ya ukuhani, chini ya maelekezo ya wale walio na funguo za ukuhani. Watoto wote wa Baba wa Mbinguni—wana na mabinti Zake—watabarikiwa pale wanapokuja kuuelewa vyema ukuhani.

Ili kujifunza zaidi kuhusu ukuhani, ona Russell M. Nelson, “Hazina za Kiroho,” Liahona, Nov. 2019, 76–79; Russell M. Nelson, “Thamani ya Nguvu ya Ukuhani,” Liahona, Mei 2016, 66–69; “Kanuni za Ukuhani,” sura ya 3 katika Kitabu cha Maelezo ya Jumla.

  • Zifanye ibada za ukuhani ziwe sehemu endelevu ya maisha ya familia yako. Kwa mfano, msaidie mtoto wako ajiandae kiroho kwa ajili ya sakramenti kila wiki. Mhimize mtoto wako atafute baraka za ukuhani wakati anapokuwa mgonjwa au anapohitaji faraja au mwongozo. Ifanye iwe tabia kubainisha njia ambazo Bwana anaibariki familia yako kupitia nguvu za ukuhani.

  • Mnaposoma maandiko pamoja, tafuta fursa za kujadili jinsi Mungu anavyowabariki watu kupitia nguvu Yake. Shiriki uzoefu wako mwenyewe wa wakati ambapo Mungu alikubariki wewe kupitia ukuhani Wake. Kwa mifano ya baraka tunazopokea kutoka kwa Mungu kwa njia ya Ukuhani, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 3.23.5.

  • Jifunze safu ya mamlaka ya ukuhani ya mtu aliye katika familia yenu. (Wenye Ukuhani wa Melkizedeki wanaweza kupokea nakala ya safu yao ya mamlaka kwa kutuma barua pepe kwa LineofAuthority@ChurchofJesusChrist.org; ona pia “Request a Priesthood Line of Authority” katika Kituo cha Msaada kwenye ChurchofJesusChrist.org.) Zungumzeni kuhusu kwa nini ni muhimu kujua kwamba mamlaka ya ukuhani yanatoka kwa Yesu Kristo Mwenyewe. Je, ni kwa nini Yeye huyashiriki pamoja nasi?

  • Mfundishe mtoto wako kwamba baada ya ubatizo, yeye anaweza kupokea nguvu za ukuhani kwa kushika agano la ubatizo. Rejeleeni pamoja ujumbe wa Rais Russell M. Nelson “Hazina za Kiroho” (Liahona, Nov. 2019, 76–79). Mwambie mtoto wako jinsi ambavyo ibada za ukuhani zimeleta nguvu ya Mungu katika maisha yako. Kwa orodha ya baadhi ya njia ambazo kwa hizo sisi tunabarikiwa kwa nguvu za ukuhani, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla3.5.

  • Jadilianeni swali hili “Je, Mtumishi wa Bwana yukoje? Someni pamoja Mafundisho na Maagano 121:36–42, na tafuteni majibu. Wakati wowote unapogundua mtoto wako (au mtu mwingine yeyote) akitumia mojawapo ya kanuni au sifa zilizoko katika mistari hii, ibainishe.

  • Wakati wewe au mtoto wako mnapotumia funguo kufungua mlango au kuwasha gari, chukua muda huo kulinganisha funguo hizo na funguo zinazoshikiliwa na viongozi wenye ukuhani. (Kwa ajili ya maana ya funguo za ukuhani, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 3.4.1). Je, funguo za ukuhani “zinafungua” au “kuwasha” nini kwa ajili yetu sisi? Ona pia Gary E. Stevenson, “Je, Ziko Wapi Funguo na Mamlaka ya Ukuhani?,” Liahona, Mei 2016, 29–32; “Where Are the Keys?” (video) Maktaba ya Injili,

  • Unapokuwa unasimikwa kwa ajili ya wito, mwalike mtoto wako awepo, kama inawezekana. Mruhusu mtoto wako akuone ukitekeleza wito wako. Unaweza hata kutafuta njia sahihi ambazo yeye anaweza kukusaidia. Eleza jinsi unavyoihisi nguvu ya Bwana katika wito wako.

Kwenda hekaluni—Ubatizo na Uthibitisho kwa niaba ya Wafu

Mahekalu ni sehemu ya mpango wa Baba wa Mbinguni kwa watoto Wake. Ndani ya mahekalu, tunafanya maagano matakatifu na Baba wa Mbinguni wakati tunaposhiriki katika ibada takatifu, ambazo zote zinatuelekeza kwa Yesu Kristo. Baba wa Mbinguni ametoa njia kwa watoto Wake wote kufanya maagano na kushiriki katika ibada, ikiwajumuisha wale ambao hawakupokea ibada na maagano hayo katika maisha haya. Mwanzoni mwa mwaka atakaokuwa anatimiza miaka 12, mtoto wako atakuwa amefikisha umri wa kutosha kubatizwa na kuthibitishwa hekaluni kwa niaba ya mababu waliokufa.

  • Hudhurieni hekaluni mara nyingi kadiri hali yenu inavyoruhusu. Zungumza na mtoto wako kuhusu kwa nini unakwenda na jinsi gani hekalu linakusaidia wewe uhisi uko karibu zaidi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo.

  • Pitieni upya na mjadili maswali ya kibali cha hekaluni pamoja. Zungumza na mtoto wako kuhusu kile kinachotokea katika mahojiano ya kibali cha hekaluni. Shiriki kwa nini kuwa na kibali cha hekaluni ni muhimu kwako.

  • Someni pamoja Malaki 4:6. Zungumza kuhusu jinsi mioyo yenu inavyoweza kuwageukia babu zenu. Jifunzeni zaidi kuhusu mababu zenu kwa kutafiti historia ya familia pamoja kwenye FamilySearch.org. Watafuteni mababu ambao wanahitaji kubatizwa na kuthibitishwa. Mshauri wa kazi ya hekaluni na historia ya familia wa eneo lenu anaweza kuwasaidia.

  • Pitieni upya pamoja baadhi ya nyenzo katika mkusanyiko wenye kichwa cha habari “Hekalu” katika kipengele cha watoto cha Maktaba ya Injili. (Ona pia “Preparing Your Child for Temple Baptisms and Confirmations” kwenye ChurchofJesusChrist.org.)

Kupokea Baraka ya Patriaki

Baraka ya patriaki inaweza kuwa chanzo cha mwongozo, faraja na ushawishi wa kiungu. Baraka hiyo ina ushauri binafsi kutoka kwa Baba wa Mbinguni kuja kwetu sisi na hutusaidia tuelewe utambulisho wetu na lengo letu la milele. Msaidie mtoto wako ajiandae kupokea baraka ya patriaki kwa kumfundisha juu ya umuhimu na asili takatifu ya baraka ya patriaki.

(Ili kujifunza zaidi, ona Mada za Injili, “Patriarchal Blessings,” Maktaba ya Injili.

  • Shiriki na mtoto wako uzoefu wako wa kupokea baraka ya patriaki. Ungeweza kushiriki mambo kama vile jinsi ulivyojiandaa kuipokea, imekusaidiaje kuja karibu zaidi na Mungu na jinsi unavyoitumia baraka hiyo katika maisha yako. Pia ungeweza kumwalika mtoto wako azungumze na washiriki wengine wa familia ambao wamekwisha kupokea baraka zao za patriaki.

  • Pangeni muda wa kurejelea pamoja baadhi ya nyenzo katika Mada za Injili, “Baraka za Patriaki.” Kujua kuhusu mchakato wa kupokea baraka ya patriaki, ona Kitabu cha Maelezo ya Jumla18.17.

  • Kama unao mababu waliopokea baraka za patriaki, ingeweza kuwa ya kuhamasisha kuzisoma baadhi pamoja na mtoto wako. Ili kuomba baraka za mababu waliofariki, ingia katika ChurchofJesusChrist.org, bofya ikoni ya akaunti juu kwenye kona ya kulia ya skirini na chagua “Baraka ya Patriaki.”

  • Baada ya mtoto wako kuwa amepokea baraka ya patriaki, waalike wanafamilia waliokuwepo waandike hisia zao na wazishiriki hisia hizo kwa mtoto wako.

Kwenda Hekaluni—Endaumenti

Mungu anataka kuwapa, au kuwabariki, watoto Wake wote kwa “uwezo utokao juu” (Mafundisho na Maagano 95:8). Tunaenda hekaluni ili kupokea endaumenti yetu binafsi mara moja tu, lakini maagano tunayofanya na Mungu na nguvu za kiroho anazotupatia kama sehemu ya endaumenti hiyo vinaweza kutubariki kila siku ya maisha yetu.

  • Weka picha ya hekalu katika nyumba yako. Mwambie mtoto wako kuhusu hisia unazopata ndani ya hekalu. Zungumza mara kwa mara kuhusu upendo wako kwa Bwana na nyumba Yake na maagano ambayo umefanya humo.

  • Fanyeni utafiti pamoja kwenye temples.ChurchofJesusChrist.org. Someni kwa pamoja makala kama vile “About the Temple Endowment” na “Prepare for the House of the Lord.” Mwombe mtoto wako aulize maswali yoyote aliyonayo kuhusu hekalu. Kwa mwongozo kuhusu kile unachoweza kuzungumza nje ya hekalu, ona ujumbe wa Mzee David A. Bednar “Kujiandaa Kupata Kila Kitu Kinachohitajika” (Ensign au Liahona, Mei 2019, 101–4; ona hususani sehemu yenye kichwa cha habari “Mafunzo na Maandalizi ya Hekaluni Yanayolenga Nyumbani na Kusaidiwa na Kanisa”).

  • Wewe na mtoto wako mnaposhiriki katika ibada au kuwa mashahidi wa ibada zingine (kama vile sakramenti au baraka ya uponyaji), tengeni muda wa kujadili ishara zilizohusika katika ibada hiyo. Je, ishara hizo zinawakilisha nini? Je, ni kwa jinsi gani zinashuhudia juu ya Yesu Kristo? Hii inaweza kumsaidia mtoto wako ajiandae kutafakari maana ya kiishara ya ibada za hekaluni, ambazo pia zinashuhudia juu ya Yesu Kristo.

  • Msaidie mtoto wako atambue jinsi anavyoshika agano la ubatizo lililoelezwa katika Mosia 18:8–10, 13. Pia msaidie mtoto wako atambue jinsi Bwana anavyombariki. Jenga kujiamini kwa mtoto wako katika uwezo wake wa kushika maagano.

  • Zungumza kwa uwazi na mara kwa mara kuhusu jinsi maagano yako ya hekaluni yanavyoongoza chaguzi zako na kukusaidia uwe karibu zaidi na Yesu Kristo. Ungeweza kutumia Kitabu cha Maelezo ya Jumla, 27.2, ili kurejelea maagano tunayofanya hekaluni.

Kutumikia Misheni

Mzee David A. Bednar alifundisha: “Kitu kimoja kilicho muhimu sana unachoweza kufanya ili kujiandaa kwa ajili ya wito wa kuhudumu ni kuwa mmisionari mapema kabla hujaenda misheni. … Kitu muhimu hapa sio kwenda misheni; badala yake cha muhimu hapa ni wewe kuwa mmisionari na kutumikia katika maisha yetu yote kwa moyo wetu, nguvu, akili, na uwezo wetu wote. … Unajiandaa kwa ajili ya kazi ya umisionari kwa maisha yote” (“Kuwa Mmisionari,” Liahona, Nov. 2005, 45–46). Uzoefu mtoto wako alionao wa kuwa mmisionari utambariki milele, siyo tu kwa kipindi cha muda fulani atakachohudumu kama mmisionari.

Ili kujifunza zaidi, ona Russell M. Nelson, “Kuhubiri Injili ya Amani,” Liahona, Mei 2022, 6–7; M. Russell Ballard, “Huduma ya Umisionari Imebariki Maisha Yangu Milele,” Liahona, Mei 2022, 8–10; Matayarisho ya Umisionari: Kuzoea Maisha ya Umisionari, Maktaba ya Injili.

  • Fanyia mazoezi jinsi ya kushiriki injili katika njia za kawaida. Daima kuwa macho kuona fursa za kushiriki na wengine hisia zako kuhusu Baba wa Mbinguni na Mwokozi na baraka unazopokea kama muumini wa Kanisa Lake. Waalike wengine waungane na familia yako katika shughuli za Kanisa na za kifamilia.

  • Tafuta fursa za familia yako kukutana na wamisionari. Waalike wawafundishe rafiki zako au wape nafasi ya kuwafundisha watu nyumbani mwako. Waulize wamisionari kuhusu uzoefu wanaoupata na jinsi gani huduma ya umisionari inavyowasaidia wao kujongea karibu zaidi na Yesu Kristo. Pia waulize kile walichofanya (au wanachotamani kuwa wangefanya) ili kujiandaa kuwa wamisionari?

  • Ikiwa ulitumikia misheni, zungumza kwa uwazi na mara kwa mara kuhusu uzoefu wako. Au waalike marafiki au wanafamilia ambao walitumikia misheni wazungumzie uzoefu wao. Ungeweza pia kuzungumza kuhusu njia ambazo umeshiriki injili na wengine maisha yako yote. Msaidie mtoto wako afikirie njia anazoweza kushiriki injili.

  • Mpe mtoto wako fursa za kuifundisha familia yako kanuni za injili. Mtoto wako pia anaweza kufanya mazoezi ya kushiriki imani yake kwa wengine. Kwa mfano, mngeweza kujadili maswali kama “Ni kwa jinsi gani tungeweza kutambulisha Kitabu cha Mormoni kwa mtu ambaye hajapata kukisikia?” au “Ni kwa jinsi gani tungeweza kuelezea uhitaji wetu wa Mwokozi kwa mtu asiye Mkristo?”

  • Msaidie mtoto wako ahisi faraja kuzungumza na watu. Je, ni zipi baadhi ya njia nzuri za kuanzisha mazungumzo? Mhimize mtoto wako ajifunze jinsi ya kusikiliza kile wengine wanachosema, kuelewa kile kilicho katika mioyo yao na kushiriki kweli za injili ambazo zingeweza kubariki maisha yao.

  • Tafuta fursa kwa ajili ya mtoto wako kujifunza kuhusu tamaduni na imani zingine. Msaidie atambue na aheshimu kanuni nzuri na za kweli katika imani za wengine.

Kwenda Hekaluni—Kuunganishwa

Ndani ya hekalu, mume na mke wanaweza kufunga ndoa ya milele. Hili linatokea katika ibada inayoitwa kuunganishwa. Hata kama ibada hii inaweza kuwa baada ya miaka mingi ijayo kwa mwanao au binti yako, mambo madogo madogo, rahisi na endelevu mnayofanya pamoja wakati wa miaka hiyo yanaweza kumsaidia ajiandae kwa ajili ya baraka hii ya kupendeza.

  • Someni pamoja “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” katika Maktaba ya Injili. Tangazo hili linafundisha nini kuhusu furaha katika maisha ya familia na kuhusu ndoa zenye mafanikio? Pamoja na mtoto wako chagueni moja ya kanuni zilizoorodheshwa katika tangazo ili mjifunze. Mnaweza kutafuta maandiko yanayohusiana na kanuni hiyo kutoka katika Mwongozo wa Maandiko. Mnaweza pia kuweka malengo ya kutumia kanuni hiyo kwa ukamilifu zaidi katika familia yenu. Mnapofanyia kazi malengo yenu, jadilini pamoja matokeo ambayo kanuni hiyo huleta katika maisha ya familia.

  • Pamoja na mtoto wako, someni ujumbe wa Rais Dieter F. Uchtdorf “Katika Kuwasifu Wale Wanaookoa” (Ensign au Liahona, Mei 2016, 77–80). Mnapofika kwenye sehemu yenye kichwa cha habari “Jumuiya ya Vitu vya Kutumia Mara Moja na Kutupa,” mnaweza kutafuta vitu ndani ya nyumba yenu ambavyo vinatumika mara moja na kutupwa na vitu vingine ambavyo si vya kutupwa. Zungumzeni jinsi mnavyotumia vitu kwa njia ya utofauti ikiwa mnataka vidumu kwa muda mrefu. Je, hii inapendekeza nini kuhusu jinsi tunavyopaswa kuchukulia uhusiano wa ndoa na familia? Tunajifunza nini kingine kutoka kwenye ujumbe wa Rais Uchtdorf kuhusu jinsi Mwokozi anavyoweza kutusaidia tujenge ndoa na familia imara?

  • Kama umeoa au kuolewa, kuwa muwazi kwa mtoto wako kuhusu mambo mnayohisi mnafanya vyema kama wanandoa, mambo mnayojifunza na jinsi ambavyo mnajaribu kuboresha. Kama wewe na mwenza wako mmekwisha unganishwa hekaluni, mwoneshe mtoto wako kwa mfano jinsi mnavyojitahidi kushika maagano baina yenu wana ndoa pamoja na Bwana. Mwambie mtoto wako jinsi mnavyojitahidi kuwafanya Baba wa Mbinguni na Mwokozi wawe kiini cha uhusiano wenu na jinsi Wao wanavyowasaidia.

  • Wakati maamuzi ya kifamilia yanapohitaji kufanyika, itisha baraza la familia na majadiliano. Hakikisha kwamba maoni ya washiriki wote wa familia yanasikilizwa na kuthaminiwa. Tumia mijadala hii kama fursa ya kuweka mfano wa mawasiliano yenye afya na ukarimu katika mahusiano ya familia, hata wakati ambapo si kila mmoja anaona mambo kwa njia sawa.

  • Kunapokuwa na kutokukubaliana au mfarakano katika familia, onesha uvumilivu na huruma. Msaidie mtoto wako aone jinsi ya kutatua mfarakano katika njia kama za Kristo kunavyoweza kumsaidia yeye ajiandae kwa ajili ya familia yenye furaha. Someni pamoja Mafundisho na Maagano 121:41–42, na zungumzeni kuhusu jinsi kanuni katika mistari hii zinavyoweza kutumika katika ndoa.