Mlango wa 14
Sayuni na mabinti zake watakombolewa na kutakaswa katika siku ya milenia—Linganisha Isaya 4. Karibia mwaka 559–545 K.K.
1 Na katika siku ile, wanawake saba watamshika mwanaume mmoja, wakisema: Tutakula mkate wetu wenyewe, na kuvaa mavazi yetu wenyewe; turuhusu tu tuitwe kwa jina lako ili tuondolewe aibu yetu.
2 Katika siku ile tawi la Bwana litakuwa la urembo na tukufu; matunda ya udongo yatakuwa mema na ya kupendeza kwa wale waliokimbia kutoka Israeli.
3 Na itakuwa kwamba, wale waliobaki Sayuni na kubaki Yerusalemu wataitwa watakatifu, kila mmoja aliyeandikwa miongoni mwa wale walio hai Yerusalemu—
4 Wakati Bwana atakapokuwa ameuosha uchafu wa mabinti za Sayuni, na kuisafisha damu ya Yerusalemu kutoka kati yake kwa roho ya hukumu na kwa roho ya kuchoma.
5 Na Bwana ataumba juu ya kila makao ya mlima wa Sayuni, na juu ya kila mkusanyiko wake, wingu na moshi mchana na mngʼaro wa miale ya moto usiku; kwani juu ya utukufu wote wa Sayuni kutakuwa na ulinzi.
6 Na kutakuwa na hema kwa kivuli mchana kwa sababu ya joto, na mahali pakukimbilia, na kujificha nyakati za dhoruba na mvua.