Maandiko Matakatifu
Etheri 14


Mlango wa 14

Ubaya wa watu unaleta laana juu ya nchi—Koriantumuri anajihusisha kwa vita dhidi ya Gileadi, halafu Libu, na kisha Shizi—Damu na mauaji yanafunika nchi.

1 Na sasa kulianza kuwa na laana kuu juu ya nchi yote kwa sababu ya uovu wa watu, ambamo kwake, ikiwa mtu angeweka chombo chake au upanga wake juu ya rafu yake, au mahali ambapo angeiweka, tazama, kufikia kesho yake, hangeipata, kubwa hivyo ilikuwa laana juu ya nchi.

2 Kwa hivyo kila mtu alishikilia kile kilichokuwa chake, kwa mikono yake, na hangeomba wala kuazima; na kila mtu aliweka kipini cha upanga wake kwenye mkono wa kulia, katika kulinda mali yake na maisha yake, na ya mabibi zake na watoto wake.

3 Na sasa, baada ya muda wa miaka miwili, na baada ya kifo cha Sharedi, tazama, kulitokea kaka wa Sharedi na akafanya vita na Koriantumuri, ambamo Koriantumuri alimshinda na kumfukuza hadi kwenye jangwa la Akishi.

4 Na ikawa kwamba kaka wa Sharedi alifanya vita dhidi yake katika jangwa la Akishi; na vita vilikuwa vikubwa sana, na maelfu wengi walianguka kwa upanga.

5 Na ikawa kwamba Koriantumuri alizingira jangwa; na kaka wa Sharedi alitoka nje ya jangwa wakati wa usiku, na kuua sehemu ya jeshi la Koriantumuri, wakati walipokuwa wamelewa.

6 Na akaja mbele hadi kwenye nchi ya Moroni, na kujiweka kwenye kiti cha enzi cha Koriantumuri.

7 Na ikawa kwamba Koriantumuri aliishi na jeshi lake katika jangwa kwa muda wa miaka miwili, wakati ambapo alipata nguvu nyingi kwa jeshi lake.

8 Sasa kaka wa Sharedi, ambaye jina lake lilikuwa Gileadi, pia alipata nguvu nyingi kwa jeshi lake, kwa sababu ya vikundi vyake vya siri.

9 Na ikawa kwamba kuhani mkuu wake alimuua wakati alipokuwa amekalia kiti chake cha enzi.

10 Na ikawa kwamba mmoja wa wale wa kundi ovu la siri alimuua katika njia ya siri, na akajipatia ufalme; na jina lake lilikuwa Libu; na Libu alikuwa mtu mnene, kuliko mtu yeyote miongoni mwa watu wote.

11 Na ikawa kwamba katika mwaka wa kwanza wa Libu, Koriantumuri alikuja kwenye nchi ya Moroni, na kufanya vita na Libu.

12 Na ikawa kwamba alipigana na Libu, ambamo kwake Libu alimpiga mkono wake kwamba alimjeruhi; walakini, jeshi la Koriantumuri lilimshambulia Libu, kwamba alikimbia hadi kwenye mipaka juu ya ukingo wa bahari.

13 Na ikawa kwamba Koriantumuri alimfuata; na Libu akafanya vita na yeye juu ya ukingo wa bahari.

14 Na ikawa kwamba Libu alishinda jeshi la Koriantumuri, kwamba walikimbia tena hadi kwenye nyika ya Akishi.

15 Na ikawa kwamba Libu alimfuata mpaka akafikia nchi wazi ya Agoshi. Na Koriantumuri alikuwa amechukua watu wote na yeye wakati alikimbia mbele ya Libu katika ile sehemu ya nchi ambapo alikimbilia.

16 Na baada ya kuja kwenye tambarare za Agoshi alifanya vita na Libu, na kumpiga mpaka akafa; walakini, kaka wa Libu alimshambulia Koriantumuri badala yake, na vita vikawa vikali sana, ambapo Koriantumuri alikimbia mbele ya jeshi la kaka wa Libu.

17 Sasa jina la kaka wa Libu lilikuwa Shizi. Na ikawa kwamba Shizi alimfukuza Koriantumuri, na kuangamiza miji mingi, na aliua wote wanawake na watoto, na alichoma miji hiyo.

18 Na kukaenea woga juu ya Shizi katika nchi nzima; ndiyo, mlio ulienda kote nchini—Ni nani anaweza kushindana na jeshi la Shizi? Tazama, husafisha dunia mbele yake!

19 Na ikawa kwamba watu walianza kujikusanya pamoja kwa majeshi, kote kwenye uso wa nchi.

20 Na waligawanyika; na sehemu yao moja ilikimbilia jeshi la Shizi, na sehemu nyingine ikakimbilia jeshi la Koriantumuri.

21 Na vita vilikuwa vikubwa na vya kudumu, na kuonekana kwa damu kuliendelea kwa muda mrefu na mauaji, kwamba uso wa nchi ulifunikwa na miili ya waliokufa.

22 Na vita vilikuwa vya upesi sana na haraka kwamba hakukuwa na aliyebaki kuzika waliokufa, lakini walienda mbele kutoka kwa umwagaji wa damu hadi kwa umwagaji wa damu mwingine, wakiacha miili ya wote wanaume, wanawake, na watoto imetawanywa juu ya uso wa nchi, kuwa mawindo ya minyoo ya mwili.

23 Na uvundo kutoka hapo ulienea juu ya uso wa nchi, hata juu ya uso wote wa nchi; kwa hivyo watu walisumbuliwa mchana na usiku, kwa sababu ya uvundo wa wafu.

24 Walakini, Shizi hakuacha kumkimbiza Koriantumuri; kwani alikuwa ameapa kujilipiza kisasi juu ya Koriantumuri kwa damu ya kaka yake, ambaye alikuwa amemuua, na neno la Bwana ambalo lilimjia Etheri kwamba Koriantumuri hangeuawa kwa upanga.

25 Na hivyo tunaona kwamba Bwana aliwatembelea katika utimilifu wa ghadhabu yake, na uovu wao na machukizo yao yalitayarisha njia kwa maangamizo yao yasiyo na mwisho.

26 Na ikawa kwamba Shizi alimfuata Koriantumuri kwa upande wa mashariki, mpaka kufika kwenye mipaka kando ya ukingo wa bahari, na kule alifanya vita na Shizi kwa muda wa siku tatu.

27 Na uharibifu ulikuwa wa kutisha sana miongoni mwa majeshi ya Shizi kwamba watu walianza kuogopa, na kuanza kukimbia mbele ya majeshi ya Koriantumuri; na walikimbia hadi kwa nchi ya Korihori, na kuangamiza wakazi mbele yao, wale wote ambao hawakujiunga nao.

28 Na walipiga hema zao katika bonde la Korihori; na Koriantumuri akapiga hema zake katika bonde la Shuri. Sasa bonde la Shuri lilikuwa karibu na kilima Komnori; kwa hivyo, Koriantumuri alikusanya majeshi yake juu ya kilima Komnori, na akapiga tarumbeta kuelekea kwa majeshi ya Shizi kuwakaribisha kupigana.

29 Na ikawa kwamba walikuja mbele, lakini walikimbizwa tena; na wakaja tena safari ya pili, na wakakimbizwa tena safari ya pili. Na ikawa kwamba walikuja tena safari ya tatu, na vita vikawa vikali sana.

30 Na ikawa kwamba Shizi alimpiga Koriantumuri kwamba alimpatia majeraha mengi ya vidonda vikubwa; na Koriantumuri, kwa sababu ya kupoteza damu yake, alizirai, na alibebwa na kupelekwa mbali kama aliyekufa.

31 Sasa mauaji ya wanaume, wanawake na watoto pande zote mbili yalikuwa makubwa sana kwamba Shizi aliamuru watu wake wasiyafuatilie majeshi ya Koriantumuri; kwa hivyo, walirudi kwenye kambi yao.