Maandiko Matakatifu
Etheri 15


Mlango wa 15

Mamilioni ya Wayaredi wanauawa katika vita—Shizi na Koriantumuri wanawakusanya watu wote kwenye vita vya kufa—Roho wa Bwana inakoma kushughulika nao—Taifa la Wayaredi linaangamizwa kabisa—Koriantumuri pekee anabaki.

1 Na ikawa baada ya Koriantumuri kupona kutokana na majeraha yake, alianza kukumbuka maneno ambayo Etheri alikuwa amemzungumzia.

2 Aliona kwamba walikuwa wameuawa kwa upanga kitambo karibu milioni mbili ya watu wake, na alianza kuhuzunika moyoni mwake; ndiyo, walikuwa wameuawa milion mbili ya watu wakuu, na pia wake zao na watoto wao.

3 Alianza kutubu kwa uovu ambao alikuwa amefanya; alianza kukumbuka maneno ambayo yalizungumzwa kwa midomo ya manabii wote, na aliona kwamba yametimizwa hadi sasa, kila chembe; na nafsi yake iliomboleza na kukataa kutulizwa.

4 Na ikawa kwamba aliandika barua kwa Shizi, akimwuliza awasamehe watu, na angeacha ufalme kwa ajili ya maisha ya watu.

5 Na ikawa kwamba baada ya Shizi kupokea barua yake aliandika barua kwa Koriantumuri, kwamba kama angejisalimisha, ili amuue kwa upanga wake mwenyewe, kwamba angeacha maisha ya watu.

6 Na ikawa kwamba watu hawakutubu kutoka kwa maovu yao; na watu wa Koriantumuri walichochewa kuwa na hasira dhidi ya watu wa Shizi; na watu wa Shizi walichochewa kuwa na hasira dhidi ya watu wa Koriantumuri; kwa hivyo, watu wa Shizi walifanya vita na watu wa Koriantumuri.

7 Na wakati Koriantumuri alipoona kwamba alikuwa karibu kushindwa alikimbia tena mbele ya watu wa Shizi.

8 Na ikawa kwamba alifikia maji ya Ripliankumu, ambayo, kwa tafsiri, ni kubwa, au kushinda yote; kwa hivyo, walipofikia maji haya walipiga hema zao; na Shizi pia akapiga hema zake karibu na wao; na kwa hivyo kesho yake walipigana.

9 Na ikawa kwamba walipigana vita vikali sana, ambamo kwake Koriantumuri alijeruhiwa tena, na akazirai kwa kupoteza damu.

10 Na ikawa kwamba majeshi ya Koriantumuri yalizidi kushambulia majeshi ya Shizi kwamba waliwashinda, kwamba waliwasababisha kukimbia kutoka mbele yao; na walikimbilia upande wa kusini, na kupiga hema zao mahali palipoitwa Ogathi.

11 Na ikawa kwamba jeshi la Koriantumuri lilipiga hema zao kando ya kilima Rama; na kilikuwa kile kile kilima ambapo baba yangu Mormoni alificha maandishi kwa ulinzi wa Bwana, ambayo yalikuwa matakatifu.

12 Na ikawa kwamba waliwakusanya watu wote pamoja juu ya uso wa nchi, wale ambao walikuwa hawajauawa, isipokuwa Etheri.

13 Na ikawa kwamba Etheri aliona matendo yote ya watu; na aliona kwamba watu ambao walikuwa wafuasi wa Koriantumuri walikusanywa pamoja kuwa jeshi la Koriantumuri; na watu waliokuwa wafuasi wa Shizi walikusanyika pamoja kwenye jeshi la Shizi.

14 Basi, walikusanya watu pamoja kwa muda wa miaka minne, kwamba wangepata wale wote ambao walikuwa juu ya uso wa nchi, na ili wapate nguvu yote ambayo iliwezekana kupata.

15 Na ikawa kwamba baada ya wote kukusanyika pamoja, kila mtu kwenye jeshi ambalo alitaka, na wake zao na watoto wao—wote wanaume, wanawake na watoto wakijihami na silaha za vita, wakiwa na ngao, na dirii, na vyapeo, na wakiwa wamevalia kwa njia ya vita—walisonga mbele mmoja dhidi ya mwingine kupigana; na walipigana ile siku yote, na hakuna aliyeshinda.

16 Na ikawa kwamba wakati ilipokuwa usiku walikuwa wamechoka, na wakarudi kwenye vituo vyao; na baada ya kurudi kwenye vituo vyao walianza kulia na kuomboleza kwa sababu ya watu wao ambao walikuwa wameuawa; na vilio vyao vilikuwa vikuu sana, pamoja na maombolezo yao na makelele, kwamba vilipenya anga kwa wingi.

17 Na ikawa kwamba kesho yake walienda tena kupigana, na siku hiyo ilikuwa kubwa na ya kutisha; walakini, hawakushinda, na wakati usiku ulipowadia tena walipenya anga na vilio vyao, na kulia kwao, na maombolezo yao, kwa vifo vya watu wao.

18 Na ikawa kwamba Koriantumuri aliandika tena barua kwa Shizi, akitaka kwamba asije tena kwa vita, lakini akubali ufalme, na kuhurumia maisha ya watu.

19 Lakini tazama, Roho wa Bwana ilikuwa imekoma kuwaongoza, na Shetani alikuwa na uwezo kamili juu ya mioyo ya watu; kwani walikuwa wamejisalimisha kwa ugumu wa mioyo yao, na upofu wa akili zao kwamba waharibiwe; kwa hivyo walienda tena vitani.

20 Na ikawa kwamba walipigana ile siku yote, na usiku ulipowadia walilalia panga zao.

21 Na kesho yake walipigana mpaka hata usiku ukafika.

22 Na usiku ulipofika walikuwa na hasira, kama vile mtu aleweshwavyo na divai; na walilalia tena panga zao.

23 Na kesho yake walipigana tena; na usiku ulipofika wote walikuwa wameuawa isipokuwa watu wa Koriantumuri hamsini na wawili, na watu wa Shizi sitini na tisa.

24 Na ikawa kwamba walilalia panga zao usiku huo, na kesho yake wakapigana tena, na walipigana kwa nguvu zao zote kwa panga na ngao zao, siku hiyo yote.

25 Na wakati usiku ulipofika kulikuwa na watu wa Shizi thelathini na wawili, na watu wa Koriantumuri ishirini na saba.

26 Na ikawa kwamba walikula na kulala, na kujitayarishia kifo kesho yake. Na walikuwa wanene na wenye nguvu wakilinganishwa na watu wa kawaida.

27 Na ikawa kwamba walipigana kwa muda wa masaa matatu, na walizirai kwa kupoteza damu.

28 Na ikawa kwamba baada ya watu wa Koriantumuri kupata nguvu ya kutosha tena kwamba wangeweza kutembea, walikuwa karibu kukimbia kwa maisha yao; lakini tazama, Shizi aliamka, na pia watu wake, na akaapa kwa ghadhabu yake kwamba angemuua Koriantumuri au sivyo angeuawa kwa upanga.

29 Kwa hivyo, aliwafuata, na kesho yake akawapata; na wakapigana tena kwa upanga. Na ikawa kwamba wote walipokuwa wamekufa, isipokuwa Koriantumuri na Shizi, tazama Shizi alikuwa amezirai kwa kupoteza damu.

30 Na ikawa kwamba wakati Koriantumuri alikuwa amelalia upanga wake, ili apumzike kidogo, alikata kichwa cha Shizi.

31 Na ikawa kwamba baada ya kukata kichwa cha Shizi, kwamba Shizi alijiinua kwa mikono yake na kisha akaanguka; na baada ya kujitahidi kuvuta pumzi, akafa.

32 Na ikawa kwamba Koriantumuri alianguka ardhini, na kuwa kama hana uhai.

33 Na Bwana akamzungumzia Etheri, na kumwambia: Nenda mbele. Na akaenda mbele, na aliona kwamba maneno ya Bwana yalikuwa yote yametimizwa; na akamaliza maandishi yake; (na ile sehemu moja kwa mia sijaandika) na akayaficha kwa njia ambayo watu wa Limhi waliyapata.

34 Sasa maneno ya mwisho ambayo yameandikwa na Etheri ni haya: Kama Bwana anataka kunichukua nikiwa hai, au kama nitavumilia mapenzi ya Bwana kimwili, haijalishi, ikiwa nitaokolewa katika ufalme wa Mungu. Amina.