Sehemu ya 117
Ufunuo uliotolewa kupitia Joseph Smith Nabii, huko Far West, Missouri, 8 Julai 1838, juu ya wajibu wa haraka wa William Marks, Newel K. Whitney, na Oliver Granger.
1–9, Watumishi wa Bwana hawapaswi kutamani mambo ya kimwili, kwani “mali ni nini kwa Bwana?”; 10–16, Wao waache udhaifu wa nafsi, na dhabihu zao zitakuwa takatifu kwa Bwana.
1 Amini hivyo ndivyo asemavyo Bwana kwa mtumishi wangu William Marks, na pia kwa mtumishi wangu Newel K. Whitney, na wapange vizuri biashara zao haraka na wasafiri kutoka nchi ya Kirtland, kabla Mimi, Bwana, sijaipeleka tena theluji juu ya dunia.
2 Na waamke, na kuinuka, na watoke, na wasikae, kwani Mimi, Bwana, ninaamuru.
3 Kwa hiyo, kama watakaa haitakuwa vyema kwao.
4 Na watubu dhambi zao zote, na tamaa zao mbaya zote, mbele zangu, asema Bwana; kwani mali ni nini kwangu? asema Bwana.
5 Acha mali za Kirtland zitolewe kwa ajili ya madeni, asema Bwana. Acha ziende, asema Bwana, na chochote kitakachobakia, acha kibaki mikononi mwenu, asema Bwana.
6 Kwani sina ndege wa angani, na pia samaki baharini, na wanyama milimani? Sijaumba dunia? Je, Mimi sishikilii hatima ya majeshi yote ya mataifa ya dunia?
7 Kwa hiyo, je, sitafanya mahali pa jangwa kuota chipukizi na kuchanua, na kuzaa kwa wingi? Asema Bwana.
8 Je, hakuna nafasi ya kutosha juu ya milima ya Adamu-ondi-Amani, na juu ya mbuga za Olaha Shineha, au nchi ambayo Adamu aliishi, hata ninyi mkatamani kile ambacho ni tone, na kudharau mambo mazito zaidi?
9 Kwa hiyo, njooni huku juu katika nchi ya watu wangu, hata Sayuni.
10 Na mtumishi wangu William Marks awe mwaminifu katika mambo machache, naye atakuwa mtawala juu ya mengi. Na aongoze katikati ya watu wangu katika mji wa Far West, na abarikiwe kwa baraka za watu wangu.
11 Na mtumishi wangu Newel K. Whitney aone aibu kwa kundi la Wanikolai na siri zao zote za machukizo, na udhaifu wote wa nafsi yake mbele zangu, asema Bwana, na aje huku katika nchi ya Adamu-ondi-Amani, na kuwa askofu kwa watu wangu, asema Bwana, siyo kwa maneno bali kwa matendo, asema Bwana.
12 Na tena, ninawaambia, ninamkumbuka mtumishi wangu Oliver Granger; tazama, amini ninamwambia yeye kwamba jina lake litakumbukwa kuwa takatifu kutoka kizazi hadi kizazi, milele na milele, asema Bwana.
13 Kwa hiyo, na apambane kwa dhati kwa ajili ya ukombozi wa Urais wa Kwanza wa Kanisa langu, asema Bwana; na ikiwa ataanguka atainuka tena, kwani dhabihu yake itakuwa takatifu zaidi kwangu Mimi kuliko mafanikio yake, asema Bwana.
14 Kwa hiyo, na aje huku haraka, katika nchi ya Sayuni; na katika wakati ufaao atafanywa kuwa mfanya biashara kwa jina langu, asema Bwana, kwa faida ya watu wangu.
15 Kwa hiyo na mtu yeyote asimdharau mtumishi wangu Oliver Granger, bali na baraka za watu wangu ziwe juu yake milele na milele.
16 Na tena, amini ninawaambia, acha watumishi wangu wote katika nchi ya Kirtland wamkumbuke Bwana Mungu wao, na nyumba yangu pia, kuitunza na kuilinda iwe takatifu, na kuwafukuza wabadili fedha katika wakati wangu Mimi mwenyewe, asema Bwana. Hivyo ndivyo. Amina.