Tulieni, na Jueni Kuwa Mimi ni Mungu
Ibada ya MEK kwa Vijana Wazima • Mei 4, 2014 • San Diego, California
Wapendwa akina ndugu na dada zangu vijana, ninafurahi kuzungumza nanyi kutoka San Francisco, California. Ni furaha kuwa katika mkutano huu wa ibada wa MEK usiku wa leo. Tunawakaribisha ninyi nyote vijana wazima jioni hii, ikijumuisha ninyi wanafunzi muhimu wa shule ya upili mlio katika mwaka wa mwisho. Tuna furaha kuwa nanyi pamoja nasi. Tunawakaribisha wamisionari waliorejea nyumbani. Kanisa na Bwana wana shukrani kwenyu nyote kwa huduma yenu!
Pia, tunawakaribisha ninyi ambao ni wamisionari watarajiwa. Bwana anahitaji wasichana na wavulana wenye haki kumsaidia Yeye kukusanya Israeli na kutayarisha dunia kwa ajili ya Ujio Wake wa Pili.
Ninataka mjue kwamba Bwana anawapenda ninyi na kuwaamini ninyi. Urais wa Kwanza na Jamii ya Mitume Kumi na Wawili wanawaamini na kuwaombea kila mara. Ninyi ndiyo viongozi wa Kanisa wa siku za usoni, na Bwana ana baraka nyingi nzuri kwa ajili yenu kadri mnavyoishi maisha yenu.
Acheni nirudie na kusisitiza wazo hilo ---mtaongoza Kanisa miaka 20 na 30 ijayo kutoka sasa. Baadhi yenu mtahudumu kama maaskofu; marais wa vigingi; marais wa misheni; marais wa Msingi, Wasichana, na Muungano wa Usaidizi wa Akina Mama; na marais wa hekalu na walezi. Ndio, kuna wanaonisikiliza usiku wa leo ambao kwa uwezekano mkubwa huenda wakawa viongozi katika jamii na mataifa ya ulimwengu. Kutakuwa na wale ambao watakuwa washiriki wa urais mkuu wa wanawake ama hata Mkuu Mwenye Mamlaka wa Wale Sabini ama pengine mshiriki wa Jamiii ya Mitume Kumi na Wawili.
Leo hamjui yale makuu yaliyo katika siku zenu za usoni
Viongozi wa Kanisa
Nimesikia kwamba baadhi ya watu wanafikiria viongozi wa Kanisa huishi bila kujua yanayoendelea duniani. Yale wanayosahau ni kwamba sisi ni wanaume na wanawake waliopitia mengi, na tumeishi mahali pengi na kufanya kazi na watu wengi kutoka jamii tofauti. Majukumu yetu ya sasa hakika yanatufanya tusafiri duniani kote, ambapo tunakutana na viongozi wa kisiasa, dini, biashara, na wa fadhila wa dunia. Ingawa tumetembelea White House kule Washington D.C. na viongozi wa mataifa duniani kote, pia tumetembelea nyumba za waliomasikini duniani, ambapo tumekutana na kuwahudumia waliomasikini.
Unapozingatia kwa kina maisha yetu na hudumu, huenda ukakubali kwa kiwango kikubwa kwamba sisi huona na kukumbana na dunia katika njia ambayo wachache wengine hupitia. Utagundua kwamba sisi huona mengi yanayoendelea duniani kuliko watu wengi.
Wengine husema sisi ni wazee sana. Vyema, ni ukweli kwamba tisa kati yetu wana miaka zaidi ya 80 ! Mimi nina miaka 85.
Hata hivyo, kuna kitu kuhusu mtu binafsi na hekima ya akina Ndugu ambacho kinapaswa kuwapa kiwango cha faraja. Tumeyapitia yote, ikiwa ni pamoja na matokeo ya sheria na sera tofauti za umma, kukatishwa tamaa, majanga, na vifo katika familia zetu wenyewe. Tunaelewa kila kinachoendelea maishani mwenu.
Acheni pia niseme kwamba hakuna aliye na msimamo dhaifu miongoni mwa Wale Kumi na Wawili. Sote tuna utu wa Nguvu. Kwa hivyo wakati tumeungana katika uamuzi, mnaweza kuwa na uhakika kwamba tumeshauriana pamoja na kufikia uamuzi huo baada ya maombi mengi na mjadala wa kina.
Wajukuu wangu hata hufikiria kuwa mimi ni wakisasa. Nimesikia kwamba baadhi ya vijana wazima ambao bado hawajaoa husema kwamba nina ufahamu mwema wa mambo ya kisasa. Natumaini ni vyema kuwa wa kisasa!
Tuna ujana ndani ya roho zetu, na Bwana hutubariki kuisogeza kazi Yake mbele kwa njia za ajabu. Usiku wa leo nitajadili nanyi mada tatu muhimu: moja, tutazungumza kuhusu matumizi ya teknologia; pili, ningependa kuzungumza nanyi kuhusu kupambana na ponografia; na tatu, kuhusu fundisho la ndoa--- masuala matatu muhimu sana ambayo tunakabiliana nayo siku ya leo.
1. Matumizi ya Teknologia
Kwanza ni matumizi ya teknologia. Miaka ya 2007 na 2008, niliwazungumzia wanafunzi waliokuwa wanahitimu BYU-Hawaii na BYU-Idaho. Katika hafla hizo nilisema hatuwezi kubaki bila kutenda wakati wengine, ikiwa ni pamoja na wakosoaji wetu, wanaojaribu kufafanua kile Kanisa linafundisha.” 1 Wakati huo niliwahimiza wahitimu watumie maendeleo katika teknolojia kujihusisha katika mazungumzo duniani kote kuhusu Kanisa. Nilidhani nilikuwa ninafahamu mambo ya kisasa nilipopendekeza kuwa washiriki maoni yao kwenye blogi. Tangu wakati huo, nimetambulishwa kwa Facebook, Twitter, Pinterest, YouTube, Google+, Instagram, na kisha katibu wangu aliniambia punde nilipokuwa ninaondoka, kitu kuhusu Snapchat. Ee! Inaonekana kama ulimwengu wa teknolojia hauwezi kukoma kuendelea kwa muda wa dakika chache hata.
Simu yangu ya mkono inashangaza! Smartphone kwa kweli ni erevu! Zinatupa fursa nyingi mzuri, ikiwa ni pamoja na kupata habari, kupata maelekezo ya ramani, kubadilishana picha na ujumbe, na hata kwa kweli kuzungumza na mtu mara moja kwa muda.
Ulimwengu wa kisasa tunaoishi daima unabadilika, jambo ambalo kwa njia zingine ni nzuri na kwa njia zingine linaweza kuwa si zuri.
Tofauti kati ya Siku za Kale na Sasa
Kutoka siku za Adamu na Hawa hadi siku za Joseph na Emma Smith, dunia ilibadilika pole pole kutoka kizazi kimoja hadi kingine.
Watu katika siku za kale waliishi na mwanga halisi kutoka mbinguni na giza ya starehe, bila stima za njiani na taa za magari na uchafuzi wa mazingira wa nuru bandia inayopatikana katika miji yetu duniani kote. Katika miji ya sasa, ni vigumu kuona anga ya usiku kama vile Ibrahimu, Musa, Ruthu, Elizabeti, Yesu, na Watakatifu wa Siku za Mwisho wa hapo awali walivyoona.
Walifurahia pia utulivu halisi, na sauti ndogo zilizobuniwa na watu kukatiza mchana wao na hasa usiku wao. Makelele ya kisasa hutoka kwa magari, ndege, na makelele ambayo wengine wenu huchukulia kuwa muziki imeifanya kuwa vingumu kusikiliza sauti asili za dunia. (Lazima muelewe, kutoka kwa kizazi changu, kile mnadhani ni muziki na kile ninadhani ni muziki---tuko tofauti sana) Hauwezi kwenda katika mkahawa bila kusikia muziki ukichezwa ukingoni. Hata katika misitu iliyombali katika dunia, kimya mara nyingi huvunjwa na ndege ikipaa juu angani.
Mwishowe, watu wa nyakati za kale walipitia upweke katika njia hatuwezi kufikiria katika dunia yetu yenye msongamano na shughuli nyingi. Hata wakati tuko peke yetu siku hizi, tunaweza kuwasiliana na wengine kupitia vifaa vya mkono vya mawasiliano, kompyuta ndogo ya kupakata, na TV kutuburudisha na kutushughulisha.
Kama Mtume, nawauliza nyote swali sasa: Je! Mna wakati wa kibinafsi wa kimya? Nimewaza kama wale walioishi katika siku za kale kama walikuwa na fursa zaidi kutuliko sisi ya kuona, kuhisi na kupata uwepo wa Roho katika maisha yao.
Inaonekana, kadri dunia inavyokuwa na mwangaza zaidi, na makelele zaidi na shughuli zaidi, tuna changamoto kubwa zaidi kuhisi Roho katika maisha yetu. Kama maisha yako hayana muda wa kimya, ungeanza kutafuta muda wa kimya usiku wa leo?
Ushauri wa Kinabii
Ni muhimu kutulia na kusikiliza na kumfuata Roho. Tuna mambo mengi sana yanayoweza kutupotosha, kuliko wakati wowote mwingine katika historia ya dunia.
Kila mtu anahitaji muda wa kuwaza na kuwazua na kutafakari. Hata Mwokozi wa ulimwengu, wakati wa huduma Yake duniani, alipata wakati wa kufanya hivyo. “Naye alipokwisha kuwaaga makutano, alipanda mlimani faraghani, kwenda kuomba. Na kulipokuwa jioni, alikuwako huko peke yake.” 2
Sote tunahitaji muda wa kujiuliza maswali ama kuwa na mahojiano ya kibinafsi nasi wenyewe. Mara nyingi sisi huwa na shughuli nyingi na kuna makelele mengi ya kupotosha duniani hata kwamba ni vigumu kusikia maneno ya mbinguni “tulieni na jueni kuwa Mimi ni Mungu.” 3
Vifaa vya mikononi, kama vile smartphones, ni baraka, lakini vinaweza pia kutupotosha katika kuisikiliza “sauti ndogo, ya utulivu.” Vinapaswa viwe vitumishi vyetu, si wakuu wetu. Kwa mfano, ikiwa baadaye usiku huu utashiriki mawazo ya kuvutia kutoka mkutano huu wa ibada kwenye, smartphone yako ni mtumishi. Ukizurura bila lengo katika tovuti, smartphone yako ni mkuu wako.
Kumbuka kile Eliya alijifunza: “Bwana hakuwemo katika upepo; … Bwana hakuwemo katika tetemeko la nchi… Bwana alizungumza katika “sauti ndogo, ya utulivu.” 4
Matumizi Yetu ya Teknologia
Swali lingine: Kusema kweli, unatumia muda kiasi gani kila siku kwenye simu yako ama tableti, bila kujumuisha kazi ya shule na Kanisa?
Matumizi yake ni sahihi, nayo ni baraka. Hata hivyo, wakati smartphones zinaanza kuingilia kati ya uhusiano wetu na marafiki, familia---na hata muhimu zaidi na Mungu---tunahitaji kufanya mabadiliko. Kwa baadhi yenu, marekebisho yatakuwa kidogo; kwa wengine, huenda yakawa makubwa.
Pia nina wasi wasi kwamba matumizi ya kupindukia ya kutuma jumbe fupi, kutumia Facebook, kutumia Twitter, na Instagram yanachukua mahali pa mazungumzo---kuzungumza moja kwa moja na kuzungumza katika maombi na Baba wa Mbinguni na kufikiria juu ya vitu ambavyo vina umuhimu zaidi maishani.
Mara nyingi vijana hujikuta katika chumba kimoja na familia ama marafiki lakini wanashughulika sana katika mawasiliano na mtu ambaye hayupo pale, hivyo basi kupoteza fursa ya kufurahia wale ambao wako karibu. Haya yakitendeka pengine unapaswa uondoke chumbani mle na kutuma ujumbe mfupi kwao ili uweze kupata usikivu wao!
Mengi ya yale nimejifunza maishani mwangu yametokana na kuwasikiliza wale walio na uzoefu mkubwa, wale ambao wameishi kwa muda mrefu na kujifunza mambo mengi muhimu ambayo nilihitaji kujua. Tafadhali chukueni fursa kuwatembelea na kuzungumza na wazazi wenu, shangazi na wajomba, na akina babu wakati bado wako hai.
Pia nina wasiwasi kwamba baadhi yenu huangalia barua pepe zenu, ama akaunti za Facebook, Twitter, ama Instagram ama hutuma ujumbe mfupi wakati wa mkutano muhimu wa yote katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho la urejeo---mkutano wetu mtukufu wa sakramenti. Katika mkutano huu muhimu tunapaswa tuwe tunamlenga Bwana kupitia maombi, kuimba nyimbo, na kuchukua ishara ya mwili na damu Yake badala ya kutumia vifaa vya mikono vya kuwasiliana. Hauwezi kuwasiliana na Roho wakati wa wasilisho la sakramenti wakati unatazama ujumbe mfupi ama kuutuma kwenye smartphone yako ama tableti yako. Uwasiliano huu unahitaji Nuru ya Kristo, inayoshawishi mawazo yenu na hisia zenu za kina, ikitoa ndani yenu upendo mkuu na uchaji.
Ninajua kwamba wengi wenu mna maandiko na vyombo vingine vya Kanisa kwenye simu zenu na tableti. Na hata nimesikia kwamba baadhi ya wazazi na viongozi wa Kanisa wana wasiwasi kuhusu maendeleo haya ya kisasa, lakini mimi sina wasiwasi.
Kanisa daima limechukua maendeleo katika teknologia ili kusaidia kusongeza kazi ya Bwana mbele. Tulianza kuwatuma wamisionari wetu kwenye meli za matanga katika miaka ya 1830, lakini tulichukua maendeleo yaliyoletwa na meli za ingini ya mvuke katika miaka ya 1860. Na kisha tukakubali matumizi ya ndege kama njia bora ya kuwapeleka wamisionari wetu walikotumwa duniani kote katika miaka ya 1960.
Historia hujirudia kwa njia ya kufurahisha sana. Katika siku za kale, Israeli ilitunza maneno ya Mitume kwenye hati ya kukunja. Katika muda fulani, Wakristo wa awali walitumia kodeksi, toleo la kwanza la kitabu cha kisasa.
Hapa tuko miaka 2,000 baadaye, na ninyi vijana mnasoma maandiko yenu kwenye smartphones ama tableti---mkiyasoma kama vile Yesu alivyoyasoma alipopewa hati ya kukunja ya Isaya kusoma kule Nazareti. Ninyi pia mnaweza kuskroli5---lakini tafadhali msiskroli wakati wa mawasilisho ya sakramenti. Hakika, wakati wa dakika hizo chache mnaweza kulenga juu ya Upatanisho wa Mwokozi mnapotafuta Roho wa Bwana kuwabariki katika wiki ifuatayo. Na zingatieni kuweka smartphone zenu na tablet zenu katika airplane mode kwa masaa yote matatu ya mikutano ya Jumaplili. Bado mtakuwa na maandiko yenu, hotuba za mkutano mkuu, kitabu cha nyimbo, na vitabu vya kiada lakini hamtapotoshwa na jumbe fupi zinazokuja ama habari za moja kwa moja.
Makimbilio kutoka kwa Tufani
Pamoja na kupata wakati wa kuwaza na kutafakari, pia tunahitaji kupata mahali, kama ilivyotajwa katika Mafundisho na Maagano, ambapo patakuwa “ngome, na… makimbilio wakati wa tufani.” 6
Tunahitaji mahali maalum pa makimbilio ambapo tunaweza kujitoa kutoka kwa upotoshi wa vifaa vyetu vya kielektroniki kwa kuvifunga ili kwamba tuweze kuwasiliana na Roho wa Mungu.
Mahali pema zaidi pa kuwasiliana na Roho ni katika hekalu---nyumba ya Bwana. Hakika, pia majumba yetu ya Kanisa yaliyowekwa wakfu vile vile, ikiwa ni pamoja na madarasa ya seminari na vyuo na vyumba vingine vya majengo. Tunaweza kupata mahali pa makimbilio katika nyumba zetu ama tunapochagua kufunga vitu nje na kutulia na kujua kuhusu vitu vya Mungu.
Ili kutusaidia kuelewa dunia pale Adamu na Hawa, Ibrahimu na Sara, na Yusufu na Mariamu walimpata Mungu, na ili kutusaidia kupata mahali pa kuhisi na kusikiliza sauti ya Bwana leo, ninawaalika mwende hekaluni. Nendeni mara nyingi muwezavyo, na mzime smartphone zenu na mziweke mbali kabla muingie kwenye bustani za hekalu.
Katika maagizo yote katika nyumba ya Bwana, mtasikia lugha nzuri, maneno na ahadi zilizotolewa na Bwana kwa watoto Wake. Ni mahali pekee ambapo mnaweza kusikia maneno hayo mazuri na ya kuvutia.
Kama haustahiki kupata sifu ya hekalu hivi sasa, tembelea bustani la hekalu. Wacheni nidokeze jambo muhimu sana kama hamjawahi kulisikia tena: Hakuna kinachokuzuia wewe ama yeyote kutembelea bustani la hekalu. Bwana anakutaka ujitayarishe mwenyewe kustahiki kupata sifu ya hekalu na kwenda hekaluni punde uwezapo. Kutembea kwenye bustani kutaweka moyoni mwako tamaa ya kupata sifu na kuhudhuria hekalu kila mara.
Shetani, kinyume, hataki uende hekaluni ama hata usimame katika kivuli cha hekalu. Anakutaka uepuke hata kukaribia hekalu kwa sababu hekalu ni nyumba ya Bwana.
Ninawahakikishia kila mmoja wenu kwamba mnapoenda hekaluni ama kutembelea bustani za hekalu, mtatembea kwenye ardhi tukufu, kama vile akina babu wa kale walivyotembea zama za kale. Walikuwa wamelenga safari yao ya milele na vitu vya umuhimu maishani. Kama wao, mnaweza pia kulenga kuhisi nguvu na uwepo wa mbinguni.
Mkichagua, mnaweza kusikia sauti tulivu, ndogo ya Roho hekaluni ama kwenye ardhi tukufu kwa njia kamwe hamtaweza kwenye maduka makubwa, katika mikahawa, na katika mahali pa umma. Kwa kweli, mtapata kwamba hekalu ni mahali pazuri kupokea majibu ya maombi yenu.
Hivi majuzi, Rais Thomas S. Monson aliweka wakfu Hekalu la Gilbert Arizona. Wakati wa ombi la kuliweka wakfu alimwomba Bwana, “Roho Yako Tukufu awe hapa, na ushawishi wake uhisiwe na wote wanaokuja humu.” Pia aliomba: “Nyumba hii, Yako, iwe mahali pa utulivu, pa makimbilio wakati wa tufani za maisha na makelele ya dunia. Iwe nyumba ya tafakari tulivu kuhusu asili ya milele ya maisha na mpango Wako tukufu kwa ajili yetu.” 7
Mahekalu yote yaliyowekwa wakfu kwa Bwana ni “mahali pa utulivu, makimbilio kutoka kwa tufani za maisha na makelele ya dunia … [na] nyumba ya tafakari tulivu.”
Upinzani
Dunia ambapo tunaishi hivi sasa inajitenga haraka na mafundisho ya Kristo katika sheria na tamaduni zake. Matokeo yake, Shetani anafanya kazi kwa bidii kuwakanganya wana na binti wa Mungu na kuwapotosha wateule kwa kuwazuia kutimiza majukumu yao na kupokea ujalivu wa baraka za Bwana.
Shetani anataka mkome kutenda wema mliojifunza nyumbani, katika seminari na chuo, na kwenye misheni yenu---kama vile kusoma maandiko kila siku, kuomba kila siku, kupokea sakramenti kwa ustahiki kila wiki, na kutoa huduma kwa moyo wa kweli na dhati. Anataka pia uepuke kushiriki katika mapigano ya kiroho muhimu na yanayofaa ya siku zetu.
Kumbukeni, wapendwa wangu vijana, tuko vitani---lakini si vita vya bunduki na risasi. Hata hivyo, vita ni vya kweli, vina majeruhi wengi. Vita ni hasa endeleo la vita vile vilivyoanza katika maisha kabla ya maisha duniani.
Paulo alitualika “Vaeni silaha zote za Mungu.” Alisema, “Kwa maana kushindana kwetu si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho” 8
Kama Mtume wa Bwana Yesu Kristo, ninawaalika nyote mnaonisikiliza, katika dunia kubwa tunamoishi sasa, “vaeni silaha zote za Mungu” na mjiunge vitani leo, kama askari wa Helamani walivyofanya miaka mingi iliyopita. Msingoje hadi muoe ama muanze ajira ama muwe wazee. Kanisa linahitaji vijana wetu sasa hivi. Bwana anawahitaji sasa hivi!
Mtakumbuka kuwa askari vijana 2,000 “waliingia katika agano kupigania uhuru wa Wanefi”9 Kanisa linahitaji vijana shupavu wa kisasa ambao wamefanya agano “kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote mlipo” 10
Kitabu cha Mormoni kinawaelezea askari hawa kama ifuatayo:
“Wote walikuwa vijana … , na walikuwa mashujaa kwa uhodari, na pia kwa nguvu na vitendo; lakini tazama, hii haikuwa yote---walikuwa ... watu wa ukweli wakati wote kwa kitu chochote ambacho walikabidhiwa.
“Ndio, walikuwa watu wa ukweli na wenye busara, kwani walikuwa wamefundishwa kutii amri za Mungu na kutembea wima mbele yake.” 11
Ninyi wasichana na wavulana ndiyo mabinti na wana wa Helamani wa kisasa. Isemwe kuwahusu kama ilivyosemwa kuwahusu: “walikuwa sasa katika wakati huu … usaidizi mkuu.” 12
2. Kupambana na Ponografia
Jambo la pili ninalotaka kuzungumza nanyi kuhusu ni kwamba lazima mjiunge nasi katika vita dhidi ya ponografia. Ni ugonjwa mbaya unaoenea duniani kote. Ninawaomba usiku wa leo mnisikilizeni ninapoeleza mfano wa hekima wa Bwana.
Zaidi ya miaka 180 iliyopita, Bwana alifunua sheria yake ya afya, ikiwemo onyo kuhusu matumizi ya tumbaku. 13 Mamilioni ya watu walimsikiliza Bwana, lakini wengi hawakumsikiliza. Hakuna aliyejua kwa wakati huo ama hata nilipokuwa na umri sawa nanyi madhara ya muda mrefu ya kuvuta sigara. Leo, baada ya miaka ya utafiti wa kisayansi, tunajua madhara ya kuvuta sigara kuwa ni saratani ya mapafu na magonjwa mengine hatari. Sheria ya Bwana ya Neno la Hekima ilikuwa baraka ya kulinda.
Kwa njia kama hiyo Bwana kwa siku zetu ametuonya kuhusu madhara ya ponografia. Mamilioni ya watu wanafuata kwa uaminifu ushauri wa Bwana, na wengine wengi hawajafuata. Si lazima tungoje, marafiki zangu wapendwa, miaka 180 ama hata miaka 10 kugundua madhara ya kuangamiza ya ponografia kwa sababu utafiti wa sasa wa kisayansi umefunua kwamba ponografia huwadhuru vijana kwa njia mbali mbali na huharibu nafasi yao ya kuwa na uhusiano ndoa wa upendo na wa kudumu siku moja.
Utafiti umeonyesha kwamba matumizi ya ponografia ya kila mara yanaweza kusababisha tabia ya utumwa na kubadilisha akili ya mtu kwa njia ambayo itamfunga mtu huyo katika gereza la uteja.
Utafiti umebainisha pia kwamba ponografia huchangia matakwa yasiyoweza kutekelezwa na hutoa habari ya uongo kuhusu uhusiano mzuri wa mapenzi wa binadamu.
Ya hatari kabisa, ponografia hukufanya kuwaona watu kama viumbe ambavyo unaweza kupuuza na kutoheshimu kihisia na kimwili.
Jambo lingine la ponografia ni kwamba kwa kawaida ni kitendo cha “siri.” Watu wanaotumia ponografia mara nyingi huficha ukweli kwamba wao huitumia, ama angalau huficha kiwango cha matumizi yao, kwa kila mtu, ikiwa ni pamoja na wenzi wa mapenzi na waliooa. Utafiti umepata kwamba watu wanapojihusisha na aina hii ya kujificha---wanapofanya vitu ambavyo vinawaaibisha na kuviweka vitu hivyo kuwa siri kutoka kwa wana familia wao na marafiki---huwa havidhuru tu uhusiano wao na kuwaacha wakihisi upweke lakini pia huwafanya kuwa katika hatari ya mafadhaiko, wasiwasi na kutojiamini. Kuweka siri huvunja imani.
Kwanza kabisa, lazima tuepuke ponografia sisi wenyewe kwa sababu inaangamiza. Huangamiza uhusiano wa kweli, na mzuri wa binadamu---ikivunja ndoa na familia. Huangamiza roho ya mtu anayeitumia kama vile sumu inavyoua mwili na akili.
Wapendwa akina ndugu na dada zangu vijana, msidanganywe. Msifikirie kwamba mara mnapoenda misheni yenu ama mara mnapooa mnaweza kukoma tabia hii inayofunga. Ikiwa umejihusisha nayo sasa, ikiwa umefungwa katika kitendo hiki, pata usaidizi wa kiroho sasa hivi. Unaweza kushinda ponografia kwa usaidizi wa Mwokozi. Usingoje! Ninakusihi uachane nayo! Kuna vifaa vingi vya usaidizi kwenye LDS.org vitakavyoshinda giza la picha za ponografia.
Hizi ni siku za changamoto---lakini si ngumu kuliko siku za Helamani na askari wake shupavu waliposimama kupigania familia zao na Kanisa. Huu ni wakati wenu kusimama na kujiunga na kikosi cha wavulana na wasichana wema na wenye kujitolea kupigana vita dhidi ya ponografia. Hivi ni vita vimoja ambavyo lazima tushinde, na lazima uvishinde katika maisha yenu wenyewe.
3. Fundisho la Ndoa
Sasa, nataka kuzungumza nanyi kuhusu mada ya tatu kwa haraka. Na ninataka muielewe kwa kina muwezavyo, msimamo wa Kanisa juu ya ndoa kama vile Baba yetu wa Mbinguni ametupa kupitia maandiko na “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu.” Nakala hio iliyovuviwa inasema: “Familia imetakaswa na Mungu. Ndoa kati ya mwanaume na mwanamke ni muhimu kwa mpango Wake wa milele. Watoto wanafaa kuzaliwa katika pingu za ndoa, na kulewa na baba na mama wanaoheshimu maagano ya ndoa na uaminifu kamili.” 14
Mitume wana jukumu la kuwa walinzi kwenye minara kutazama na kufundisha mafundisho ya Kristo. Ninyi wote mnajua kwamba maana ya kitamaduni ya ndoa inashambuliwa leo. Kuna wale wanaotoa mjadala juu ya maana ya ndoa kwa kuielezea kulingana na haki za kiraia. Urais wa Kwanza na Jamii ya Mitume Kumi na Wawili walieleza msimamo na fundisho la Kanisa la malengo na mpango wa Mungu kwa ajili ya watoto Wake wa kiroho kupitia maisha duniani, ambayo ni muhimu kwa maisha yetu ya milele na uzima wa milele.
Ninadhani wengi wenu huenda hamjasoma kauli iliyotolewa mapema mwaka huu. Ninanukuu kutoka kwa kauli hii na kuwaomba msikize kwa makini:
“Mabadiliko katika sheria za kiraia hayabadilishi, hakika hayawezi kubadilisha sheria ya kimaadili ambayo Mungu ameweka. Mungu anatutarajia tushike na kuweka amri Zake bila kujali maono tofauti ama miondoko katika jamii. Sheria Yake ya usafi wa kimwili iko wazi: mahusiano ya kujamiana yanafaa tu kati ya mwanaume na mwanamke ambao wameoana kisheria kama mume na mke. Tunawahimiza mrejelee na mfundishe washiriki wa Kanisa fundisho lililo katika “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu’
Kauli inaendelea:
“Kama tu vile wale wanaoendeleza ndoa kati ya jinsia moja wanafaa kutendewa kwa utu, ni kweli pia kwa wanaoipinga …
“Kama washiriki wa Kanisa, tuna jukumu la kufundisha injili ya Yesu Kristo na kuangaza baraka kuu zinazokuja kutokana na kufuata amri za Mungu na pia matokeo yasiyoepukika ya kuzipuuza. Tunawaalika muombe kwamba watu kila mahali watalainisha mioyo yao juu ya kweli za injili, na kwamba hekima itapewa wale ambao wana jukumu la kuamua masuala muhimu ya siku za usoni za jamii.” 15
Ninajua mnampenda na kumfuata Bwana na kuwaidhinisha manabii Wake, lakini ninajua pia kwamba baadhi yenu huenda mkawa mmekanganyika juu ya matokeo mengi ya uamuzi wa Kanisa kufuata mpango uliofunuliwa wa Mungu kwa ajili ya watoto Wake.
Ninajua pia kwamba baadhi ya vijana wetu wanashindwa na kuelewa jinsi ya kueleza fundisho linalohusu familia na ndoa na bado ubaki kuwa mwema, mpole na mwenye upendo kwa wale ambao hawakubaliani. Huenda ukawa na hofu kwamba utaonekana kuwa mlokole na asiye waelewa wengine.
Huenda unamjua mtu anayesumbuka na uvutio wa jinsia moja ama ameamua kuishi katika uhusiano wa jinsia moja. Upendo wako wa mtu huyo kama mwana ama binti wa Mungu unaweza kufanya kuwe na mashindano ya kindani unapojaribu kumpenda na kusimama naye na bado upiganie mpango wa Bwana wa furaha ya milele.
Ninasema wazi usiku wa leo, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linaamini kwamba “uzoefu wa uvutio wa jinsia moja ni ukweli usiorahisi kuelewa kwa watu wengi. Uvutio wenyewe si dhambi, lakini kutendea hisia hizo ndio dhambi. Hata kama watu binafsi huwa hawachagui kuwa na hisia hizo, huwa wanachagua kuzitendea. Kwa upendo na uelewa, Kanisa linafikia watoto wote wa Mungu, ikiwa ni pamoja na [wale walio na uvutio wa jinsia moja].” 16
Kanisa halifundishi ama kuhimiza kuwatenga watu ama kutenda kwa njia zingine ambazo si za Kikristo. Lazima tuwapende na tujaribu kuwasaidia wengine kuelewa kwamba hakuna anayepaswa kupuuza ama kudharau amri za Mungu.
Ushuhuda na Onyo
Mwisho, katika “Familia: Tangazo kwa Ulimwengu,” Urais wa Kwanza na Jamii ya Mitume Kumi na Wawili walisema: “Tunaonya kwamba watu binafsi wanaoenda kinyume na maagano ya usafi wa kimwili, wanaowadhulumu wenzi wao ama watoto, ama wanaoshindwa kutimiza majukumu ya familia watawajibika siku moja mbele ya Mungu. Mbali, tunaonya kwamba kuvunjika kwa familia kutaletea watu, jamii, na mataifa shida zilizotabiriwa na manabii wa kale na wa kisasa.”17
Mimi ni mmoja wa wale waliojiunga katika onyo hilo. Kama mmoja wa walinzi kwenye mnara, nina jukumu la “kupuliza tarumbeta, na kuwaonya watu.” 18Jioni ya leo nimekuwa na ujasiri wa kuwaonya. Ninafanya hivyo kwa sababu ninawapenda na ninataka muelewe lazima tusimame mbele ya Mungu na kuzishika amri Zake. Huo ndiyo wajibu wangu.
Habari Njema
Onyo la Bwana pia linakuja na mwaliko wa kumjia Yeye. Baba yetu wa Mbinguni alijua matokeo ya kuishi katika ulimwengu ulioanguka, na hivyo basi, akapatiana Mwokozi “Kondoo aliyeuliwa kutoka mwanzo wa dunia” kwa ajili ya watoto wake. 19 Katika waraka wa Yohana, tunajifunza, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”20
Tafadhali kumbukeni kwamba injili ndio “habari njema.” Ndio ujumbe wa tumanini. Kama uko matatani sasa hivi, pata usaidizi. Bwana yu mwenye huruma na kusamehe.
Nabii Paulo alifundisha:
“Ni nani atakayetutenga na upendo wa Kristo? Je, Ni dhiki au shida, au adha, au njaa, au uchi, au hatari, au upanga? …
“Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda.
“Kwa maana nimekwisha kujua hakika ya kwamba, wala mauti, wala uzima, wala malaika, wala wenye mamlaka, wala yaliyopo, wala yatakayokuwapo,
“Wala yaliyo juu, wala yaliyo chini, wala kiumbe kingine cho chote hakitaweza kututenga na upendo wa Mungu ulio katika Yesu Bwana wetu.” 21
Kwa sababu ya Yesu Kristo, amani inaweza kuchukua mahali pa majuto. Uhusiano mema unaweza kurejeshwa. Ufungwa unaweza kushindwa.
Tunahitaji kufahamisha familia yetu na marafiki zetu juu ya ukweli huu kwamba---Mungu ni upendo, “na anawakaribisha wote kuja kwake na kupokea wema wake; na hamkatazi yeyote anayemjia” 22
Tunawahitaji, wapendwa vijana wazima wa Kanisa, mjishughulishe katika kazi ya uokovu kabla na wakati wa na baada ya misheni yenu.
Kutumia Teknologia Kubariki Maisha
Bwana anawaalika mjishughulishe na kutumia aina yoyote ya mawasiliano ya kijamii kwenye mtandao unayopendelea kushiriki injili na kuwa mwana na binti wa Helamani wa kisasa katika vita vikuu vya siku za mwisho. Anawataka muwe askari vijana waliosimama imara na pamoja ili kupigania ukweli. Anawataka muwe na ushujaa na imara mnapomkabili adui. Tunajua kwamba mwishowe Bwana atashinda na Shetani atashindwa.
Kupitia njia mbali mbali za mawasiliano ya kijamii katika mtandao, mnaweza kuwa na mawasiliano na familia, marafiki, na, kwenu ninyi wamisionari mliorudi nyumbani, hata na wale wachunguzi hapo awali na washiriki wapya. Mnaweza kusimama kama mashahidi wa ukweli na kutetea ufalme.
Kutetea Ufalme
Ninajua baadhi yenu mna wasiwasi kuhusu kuhukumiwa vibaya, kukejeliwa, na hata kuvurugwa mkisimama imara kwa ajili ya Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo na Kanisa. Ninaelewa wasiwasi wenu.
Nilihudumu katika Misheni ya Uingereza baada ya Vita vya Dunia vya Pili kama mmisionari kijana. Wakati huo Wamormoni walikuwa “wa kuzomewa na kudhauruliwa” 23na wamisionari walichekwa na kukejeliwa. Watu hata walitutupia vitu na wengine wangetutemea mate. Hata hivyo, hatukurudi nyuma, lakini tuliendelea kutoa ushuhuda wetu na kushiriki injili. Kama Abinadi, hatukurudi nyuma, kama Paulo hatukurudi nyuma, na kama Mwokozi, hatukurudi nyuma. Kwa wakati huo hatungefikiria matokeo ya bidii yetu. Tulikuwa na wilaya 14 na hakukuwa na kikingi. Leo, vigingi 46 vya Sayuni vinapatikana katika British Isles.
Marafiki zangu vijana wapendwa, msijali kuhusu wale walio katika jumba kubwa. Nefi aliona kwamba wangewakejeli na “kuwaonyesha kwa vidole vyao wale ambao walikuwa wanakuja na kula matunda.” 24 Msiwe kama wale ambao “baada ya kuonja matunda waliaibika, kwa sababu ya wale waliokuwa wakiwadharau; na wakaingia katika njia zilizokataliwa na wakapotea.” 25
Ninyi ni kikazi kikuu na muhimu, na huu ni wakati mzuri wa kuishi! Siku za usoni zina tumanini. Jiambieni wenyewe usiku wa leo, “Ninamsaidia Bwana ninapojitolea kushiriki ushuhuda wangu na kufundisha kweli ambazo Mungu amefunua katika siku hizi za mwisho.”
Sasa, mna fursa ya kutumia mawasiliano haya yote ya kijamii kushiriki kile mlichojifunza na kuhisi pengine hata usiku wa leo. Kumbukeni kwamba kuna wakati na mahali panapofaa kwenu kutumia mitandao ya mawasiliano ya jamii, na kushiriki mawazo yenu na ushuhuda ya vitu mnavyojifunza na kuhisi ni moja ya nyakati hizo.
Ushuhuda na Ushahidi
Bwana awabariki na hekima kushinda miaka yenu, ili kwamba mtambue kwa hekima kwamba tuko katika vita hivi na lazima tusimame pamoja, vijana kwa wazee. Ninaomba Baba yetu wa Mbinguni atawalinda na kuwabariki. Tafadhali, tena, jueni jinsi tunavyowapenda. Na ninaomba Baba yetu wa Mbinguni ambariki kila mmoja wenu, popote mlipo duniani humu, mnaosikiliza mkutano huu wa ibada usiku wa leo, na amani ya Bwana mioyoni mwenu, na ushahidi na uhakika kwamba Yesu Kristo yu hai, kwamba Yeye ni Mwana wa Mungu, kwamba hili ni Kanisa Lake. Amani hiyo na nguvu iwe nanyi. Baba yetu wa Mbinguni awalindeni. Msiwahi kusahau, katika safari hii mlipo, mna thamani, kila mmoja wenu, kwa siku za usoni za kuandaa dunia kwa siku Yesu Kristo atasema “imetosha” na atarudi na kuongoza na kutawala kama Mwokozi, Bwana wa mabwana, Mfalme wa wafalme, Mkombozi wa dunia, ninayeshuhudia yu hai. Tumekuwa tunazungumzia mambo yale ambayo ni muhimu Kwake usiku wa leo. Tuondokeni mkutano huu tukiwa tumejawa na upendo kwa Bwana na hamu ya kumtumikia Yeye ni ombi langu la unyenyekevu, katika jina takatifu na jina pendwa la Bwana Yesu Kristo, amina.
© 2014 na Intellectual Reserve, Inc. All rights reserved. Kiingereza kimeidhinishwa: 3/14. Tafsiri imeidhinishwa: 3/14. Tafsiri ya Be Still, and Know That I Am God. Swahili. PD50053655 743