Mikutano ya Ibada ya Ulimwenguni Kote
Msingi Dhabiti Jinsi Gani


Msingi Dhabiti Jinsi Gani

Mkutano wa Ibada ya MEK kwa Vijana Wazima • Novemba 2, 2014 • Ogden Tabernacle, Ogden, Utah

Ni furaha tele kwa Dada Hallstrom nami kuwa nanyi jioni ya leo. Tunapotazama katika nyuso za wale ambao tunaweza kuwaona usiku wa leo, tunataswiri vijana wazima duniani kote, wote waseja na walioana, wanaoshiriki katika tangazo hili. Tuna fursa kubwa ya kusafiri sehemu nyingi sana Kanisani kote. Tumekutana na wengi wenu na wengi kama ninyi. Tumekutana na vijana wazima ambao wameongoka na wale wanaotia bidii kuongoka zaidi. Tumekutana na vijana wazima ambao wamepotea na wale ambao wamepatikana---ama, kwa usahihi, waliojipata wenyewe. Tumekutana na wale ambao si wa imani yetu, wale ambao wamebatizwa hivi karibuni, na wale ambao wametoka kwa familia ambazo vizazi vingi vimekuwa Kanisani. Tunashuhudia kwamba wote ni watoto wa Mungu na wana fursa kamili ya kupata kila baraka ya uzima wa milele.

Kwa niaba ya uongozi wa Kanisa, ninaweza kusema kwa shauku, “Tunawapenda!” Kuwatazama kwa karibu manabii na mitume na kuwajua kama ninavyowajua, ninaweza kusema bila shaka kwamba wanawajali vijana wazima wa Kanisa sana. Ninyi ni sehemu muhimu ya yale yanayotendeka sasa na yale yatakayotendeka katika siku za usoni. Tunawahitaji!

Mkutano huu unatoka Ogden Tabernacle, jumba nzuri lililokarabatiwa mkabala na Hekalu maridadi la Ogden Utah. Hekalu hilo na tabenakulo hili liliwekwa wakfu upya na Rais Thomas  S. Monson wiki sita tu zilizopita. Hekalu hii ni mojawapo ya mahekalu 143 yanayotumika hivi sasa katika Kanisa na yaliyosambaa duniani kote. Kama ishara ya jinsi umri wangu ulivyo, ama pengine kwa kusema kwa njia bayana zaidi, jinsi Bwana anavyoharakisha kazi Yake, nilipozaliwa kulikuwa na takribani mahekalu manane tu.

Kwa kutumia hekalu kama mfano, usiku wa leo nitazungumza kuhusu misingi. Kwa usanifu na ujenzi wa kila hekalu, kazi ya maana hufanyika kwa kile ambacho hakiwezi kuonekana kwa urahisi wakati mradi umemalizika - msingi. Kwa mfano, huu ni mchoro wa msanii unaoonyesha Hekalu la Philadelphia Pennsylvania, ambalo kwa sasa lipo kwenye ujenzi. Litakapokamilika, jumba hili la ajabu litakuwa na urefu wa futi 82  hadi kwenye paa lake na kurefuka futi 195 hadi juu ya malaika Moroni. Kama mnavyoweza kuona, litakuwa la ajabu! Hata hivyo, jengo hili la ajabu na la kuvutia litakavyokuwa, bado litaweza kuathiriwa na upepo mharibifu na maji ya ardhini yanayoenea. Hali hizi kali, zikiachwa bila kushughulikiwa, zinaweza kuharibu vibaya na hata kubomoa jumba hili nzuri.

Kwa kujua nguvu hizi zitaweza bila huruma kushambulia hekalu, wahandisi walisanifu na wajenzi walichimba shimo la futi 32 kwenda chini ya eneo nzima la jengo. Shimo lilichimbwa ndani ya mawe halisi ya mitale ya Pe nnsylvania ili kutoa msingi usiohamishika ambao juu yake kutajengwa. Zege imara na misingi ilifunguliwa kwenye msingi wa mwamba wa mitale kwa nanga za mawe ili kuhimili hata upepo wenye nguvu nyingi na maji ya chini ya ardhi yanye nguvu. Nanga zilichibiwa futi 50 hadi 175 ndani ya mawe ya mitale na kukazwa kwa paundi 250,000 kwa kila inchi ya mraba. Nanga zilitengwa futi 15 katika pande zote.

Ninatoa maelezo kwa utondoti kama hayo ili kufundisha jambo hili: Tofauti na kujenga jengo (ambalo kwa maelezo yoyote kila hali ni la muda), katika kujenga maisha yetu ya milele (na hatimaye, ya uzima wa milele), sisi wakati mwingine hutilia maanani kwa kiwango kidogo sana kwenye uhandisi na ujenzi wa misingi yetu. Kwa hiyo, sisi huachwa tumehatarishwa sana na kuharibiwa na nguvu hatari.

Tunaishi katika dunia ambayo inaweza kutuchanganya---ikiruhusiwa, inaweza kutusababishia kusahau asili yetu ya kweli. Rais Thomas  S. Monson alisema:

“Maisha duniani ni wakati wa majaribio, wakati wakujithibitisha wenyewe kustahili kurudi kwa uwepo wa Baba yetu wa Mbinguni. Ili tuweze kujaribiwa, lazima tupitie changamoto na shida. Mambo haya yanaweza kutuvunja, na sura za nafsi zetu zinaweza kuvunjika na kutawanyika---yaani, ikiwa msingi wetu wa imani, ushuhuda wetu wa kweli haukuwekwa ndani yetu kwa kina.

“Tunaweza kutegemea imani na ushuhuda wa wengine kwa muda tu. Hatimaye lazima tuwe na msingi wetu wenyewe wenye nguvu na dhabiti, ama tutashindwa kustahimili dhoruba ya maisha, ambayo itakuja.”1

Yesu Kristo aliielezea hivi, akizungumzia juu ya mtu anayemsikia na kumfuata:

“Mfano wake ni kama mtu ajengaye nyumba, na alichimba chini sana, na kuweka msingi juu ya mwamba; na mafuriko yalipokuja, mkondo ulipiga nyumba ile kwa nguvu, na haukuweza kuitikisa; kwa kuwa ilikuwa imejengwa juu ya mwamba.

“Lakini yule anayesikia na hatendi, ni kama mtu aliyejenga nyumba juu ya ardhi pasipokuwa na msingi, mkondo ukaishukia kwa nguvu, na ikaanguka mara moja; na maangamizi ya nyumba ile yalikuwa makubwa” (Luka 6:48–49).

Yesu Kristo ndiye mwamba ambapo lazima tujenge msingi wetu. Bwana alijirejelea mwenyewe kama “jiwe la Israeli” na akasema kwa kuhimiza, “Yule ajengaye juu ya mwamba huu hataanguka kamwe (M&M 50:44).

“Mpeni ukuu Mungu wetu.” alisema Musa. “Yeye ni Mwamba, kazi yake ni kamilifu” (Kumbukumbu la Torati 32:3--4). Daudi alisema, “Bwana ndiye jabali langu, na ngome yangu, … ngao yangu … mnara wangu,” (2 Samweli 22:2–3). Bwana alimwambia Henoko, “Mimi ndiye Masiya, Mfalme wa Sayuni, Mwamba wa Mbingu” (Musa 7:53). Nephi alimtukuza Bwana kama “mwamba wa wokovu wangu” na “Mwamba wa haki yangu” (2 Nefi 4:30, 35). Isaya alimwita Bwana “jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulioimara” ” (Isaya 28:16). Paulo aliwazungumzia mitume na manabii kama msingi wa Kanisa, na “Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni” (Waefeso 2:20).2

Hili sio fundisho jipya. Kwa njia moja ama nyingine, sote tunalielewa. Tumefundishwa na wazazi, katika Msingi, katika madarasa yetu ya Wasichana na jamii za Ukuhani wa Haruni, katika seminari, katika chuo, na wamisionari wa muda, na marafiki, na viongozi wa Kanisa wa eneo letu, na kwa maandiko, na manabii walio hai na mitume. Basi, kwa nini ni vigumu sana kwa wengi wetu kuliishi?

Kwa kunena kwa njia rahisi, linahitaji kutoka kwenye akili zetu hadi kwenye mioyo yetu na nafsi zetu. Linahitaji kuwa zaidi ya kile ambacho wakati mwingine sisi hufikiria ama hata kile ambacho sisi wakati mwingine huhisi---lazima liwe asili yetu. Uhusiano wetu na Mungu, Baba yetu, na mpango Wake wa milele, na pamoja na Yesu Kristo, Mwanawe na Mwamba wetu, linahitaji liwe limewekwa dhabiti ili kwamba kwa kweli liwe jiwe la pembeni la msingi wetu. Kitambulisho chetu kisha kinakuwa kwanza kile cha kiumbe cha milele---mwana ama binti wa Mungu---na ya mpokea wa shukrani wa baraka za Upatanisho wa Yesu Kristo. Vitambulisho vyetu vingine vya haki ndipo vinaweza kujengwa kwa usalama juu ya mwingi huo kwa sababu tutajua vile ambavyo ni vya milele na vile ambavyo ni vya muda ni jinsi ya kuvipa kipau mbele. Na vitambulisho vingine na vitendo vinavyoambatana navyo (vingine vinavyothaminiwa sana na ulimwengu) tunaweza hata kuchagua kuvitupa.

Ninaupenda wimbo uliothaminiwa “How Firm a Foundation.” Ufafanuzi ninaoupenda sana (haishangazi) umefanywa na Kwaya ya Mormon Tabernacle. Nikiketi mbele ya kwaya wakati wa mkutano mkuu na kusikiliza na kuhisi nguvu ya kinanda na sauti na muziki na maneno ya muziki yananifanya nitake kusimama na kuungana nao. Nikiwa najua kwamba ningesidikizwa nje ya Kituo cha Mkutano, mimi hujizuia. Sikilizeni wimbo huu unaopendwa ulioimbwa wiki nne tu zilizopita katika kikao cha Jumapili asubuhi cha mkutano mkuu. Furahia maneno; hasa sikilizeni yale ya mstari wa mwisho. Ni mstari wa saba hasa lakini uliimbwa kama mstari wa nne.

Hivi majuzi, nilikuwa katika mkutano katika Hekalu la Salt Lake na washiriki wa Urais wa Kwanza, Jamii ya Mitume Kumi na Wawili, na Wakuu Wenye Mamlaka wengine wote wanaofanya kazi katika makao makuu ya Kanisa. Tuliimba beti tatu za kawaida za wimbo huu mzuri, tukimalizia ubeti wa tatu kama tunavyofanya kila mara katika mikutano ya sakramenti na mikutano mingine. Lakini wakati huu Rais Monson alisema “Tuimbeni ubeti wa saba.” Na Wakuu hawa wote Wenye Mamlaka, ikiwa pamoja na manabii na mitume walio hai, tuliimba:

Nafsi ambayo inamwemea Yesu kwa msimamo

Mimi sitaweza, siwezi, kutoroka kwenda maadui zake;

Hiyo nafsi, ingawa jehanamu yote itazingatia kutikisa,

Mimi Kamwe, hapana kamwe, Mimi kamwe, hapana kamwe,

Mimi kamwe, hapana kamwe, hapana kamwe sitamwacha!3

Je, hii inaelezea wewe ni nani? Je, inaelezea angalau yule unayejitahidi kufanya uwe? Juhudi za kujenga na kudumisha msingi wa kiroho sio rahisi. Mchakato wa ujenzi ni kazi kubwa, na utunzaji ni jitihada za maisha.

Kwenu ninyi ambao kwa kweli mnajaribu sana, tunawapa hongera kwa kweli na tunataka kujua nini mnachokifanya. Tafadhali tumieni vyombo vya habari vya kijamii kushiriki kile mnachofanya kwa kutumia #cesdevo, na kukamilisha kauli “Ninajenga msingi wangu wa kiroho kwa …” Majibu yatatofautiana kama hali za kibinafsi zinavyotofautiana, na hiyo ni sawa. Tena, swali la kukamilishwa ni “Ninajenga msingi wangu wa kiroho kwa  …” Tutashukuru kusikilia kutoka kwenu na kufundishwa nanyi kuhusu nini kinachotokea katika maisha yenu.

Kama hamjawahi kuwa na msingi tunaozungumzia, ama kwa kupuuza umeuacha ukavunjika ama kutawanyika, hatujachelewa sana kufanya kazi kwa uangalifu na usalama ili kufanya vyema ziadi. Nyenzo zote unazohitaji zinapatikana kwa ajili yako. Hizi ni nyenzo zile zile za kukuza msingi uliojengwa. Mnajua ni zipi. Zinajumuisha sala dhabiti ya kila siku na ya hali ya juu; mafunzo ya kila siku ya injili kupitia maandiko; kushiriki kikamilifu katika mikutano ya Kanisa, hasa kwa kushiriki sakramenti na moyo wa kweli; huduma ya kujitolea; na kuweka maagano kwa dhati.

Nyenzo nyingine ya maana ni ushauri wa manabii walio hai. Kuna wanaume kumi na watano duniani ambao wanakubaliwa kama manabii, waonaji, na wafunuaji. Wanashikilia funguo za Ukuhani wa Mungu. Sisi hufundishwa nao kilamara. Sisi huinua mikono yetu ili kuwaidhinisha mara kadhaa kwa mwaka. Sisi huwaombea kila siku. Hata hivyo, baraka ya kipekee ya kukubali ujumbe wao inaweza kuelekeza kwa ukosefu wa kuelewa umuhimu wake.

Rais Henry  B. Eyring alionya: “Kutafuta njia ya usalama katika ushauri wa manabii kuna maana kwa wale walio na imani ya nguvu. Wakati Nabii anapozungumza, wale walio na imani ndogo wanaweza kufikiria kwamba wanasikia mtu mwenye hekima tu akitoa ushauri mzuri. Kisha kama ushauri wake ukionekana kufurahisha na kueleweka, sawa na kile wanachotaka kufanya, wanauchukua. Ikiwa haukubaliki, wao hufikiria wenye makosa ama wao huona hali zao kama zinakubali wao kuwa waliokubaliwa kuwa kinyume na ushauri huo.”

Rais Eyring aliendelea: “Uongo mwingine ni kuamini kwamba uchaguzi wa kukubali ama kutokubali ushauri wa manabii si zaidi ya kuamua kama kukubali ushauri mzuri na kupata manufaa yake ama kubaki tulipo. Lakini chaguo la kutokubali ushauri wa kinabii hubadilisha upande ule ambapo tumesimama. Inakuwa hatari zaidi.”4

Kujenga na kutunza msingi, kumbuka kanuni tatu: mtazamo, msimamo, na nidhamu. Mtazamo ni uwezo wa kuona. Katika maandhari ya injili, wakati mwingine sisi huliita hili “mtazamio wa milele” Kama Yakobo alivyoelezea, ni kuona “vile vitu vilivyo, na  … vile vitu vitakavyokuwa” (Yakobo 4:13).

Kujitolea ni utayari wa kuweka ahadi. Mara nyingi sisi huita haya “maagano.” Kwa njia rasmi, sisi huweka maagano na Mungu kupitia maagizo ya ukuhani. Kumbuka “katika ibada hizo, nguvu za uchamungu hujidhihirisha” (M&M 84:20). Ukiongezea Mungu, tunapaswa tuwe tayari kufanya masharti kwetu wenyewe, kwa wenzi (ama kuwa mwenzi), kwa marafiki, na kwa wale tunaowahudumia.

Nidhamu ya kibinafsi inaweza kufafanuliwa kama uwezo wa kuishi kulingana na mtazamio tulionao na pamoja na maagano tuliyoweka. Kukuza nidhamu ya binafsi ni muhimu kwa kuendelea kwa sababu huunganisha bila hitilafu kujifunza na kutenda. Hatimaye, nguvu ya msingi wetu wa kiroho inaonyeshwa na jinsi tunavyoishi maisha yetu, hususani katika nyakati za kukata tamaa na changamoto.

Miaka mingi iliyopita Rais Gordon  B. Hinckley alisimulia hadithi ya Caroline Hemenway, aliyezaliwa Januari  2, 1873, katika Jiji la Salt Lake, mtoto wa pili katika watoto 11:

“Akiwa na umri wa miaka ishirini na mbili Caroline aliolewa na George Harman. Walijaliwa watoto saba, mmoja ambaye alikufa akiwa bado mchanga. Kisha, akiwa na umri wa miaka thelathini na tisa, mumewe alifariki dunia na aliachwa mjane.

“Dada yake Grace, alikuwa ameolewa na kaka wa mumewe, David. Mnamo 1919, wakati wa mlipuko wa homa ya mafua, David alishambuliwa sana, na kisha mkewe, Grace akawa mgonjwa. Caroline aliwahudumia na watoto wao pamoja na wake wenyewe. Katikati ya shida hizi, Grace alijifungua mtoto wa kiume, na kisha yeye akafariki ndani ya masaa machache. Caroline alimchukua mtoto yule mchanga nyumbani kwake na kule akamlea na kuokoa maisha ya mtoto. Wiki tatu baadaye binti yake mwenyewe, Annie, alifariki dunia.

“Wakati huu Caroline alikuwa amepoteza watoto wake wawili, mumewe, na dada yake. Mzigo ulikuwa mzito sana. Alizimia. Alizinduka kutoka na ugonjwa mkali wa sukari. Lakini hakupunguza kasi. Aliendelea kumlea mtoto wa dadake; na shemeji yake, baba wa mtoto, alikuja kila siku kumuona mvulana. David Harman na Caroline walioana baadaye, na kulikuwa sasa na watoto kumi na tatu katika nyumba yao.

“Kisha miaka mitano baadaye David alikumbana na janga lililotoa jaribio kubwa kwa wale walioomboleza naye. Siku moja alitumia dawa ya kusafisha iliyo kali sana katika kutayarisha mbegu kwa ajili ya kupanda. Hii ilimwagikia mwilini mwake, na matokeo yalikuwa mabaya sana. Ngozi na nyama vilianguka kutoka kwenye mifupa yake. Ulimi na meno yake yalianguka. Dawa ile kwa hakika ilimla hai.

“Caroline alimhudumia katika ugonjwa huu mbaya, na alipokufa aliachwa na watoto watano wake mwenyewe na wanane wa dadake, na shamba ya ekari 280 ambalo yeye na watoto walilima, walipanda, walimwagilia maji, na walivuna ili kupata vya kutosha kukidhi mahitaji yao. Wakati huu alikuwa pia rais wa Muungano wa Usaidizi wa Kina Mama, nafasi aliyoshikilia kwa miaka kumi na minane.

“Wakati akihudumia familia yake kubwa na akitoa mkono wa msaada kwa wengine, alioka mikate minane kila siku na kufua bunda arubaini za nguo kila wiki. Aliweka matunda na mboga kwenye mikebe kwa tani, na alifuga kuku elfu moja wa mayai ili kupata pesa kidogo. Kujitegemea kulikuwa kiwango chake. Uzembe alichukulia kuwa dhambi. Aliwahudumia walio wake wenyewe na kusaidia wengine katika roho ya ukarimu ambao usingeruhusu yeyote ambaye angemfahanu kuwa na njaa, kukosa nguo, ama kuwa na baridi.

“Baadaye aliolewa na Eugene Robison, ambaye, si muda mrefu baadaye, aliugua kiarusi. Kwa miaka mitano hadi kifo chake alimuuguza na kumhudumia katika mahitaji yake yote.

“Hatimaye, akiwa amechoka, mwili wake ukiwa umeteseka kwa madhara ya ugonjwa wa kisukari, alifariki akiwa na umri wa miaka sitini na saba. Tabia za uchapaji kazi na bidii alizoweka katika watoto wake ziliwazawadia jitihada zao kwa miaka. Mtoto mdogo wa dada yake, aliyemlea kutoka saa ya kuzaliwa kwake, pamoja na kaka zake na dada, wote wakitenda kutoka hisia ya upendo na shukrani, [walikipa Chuo Kikuu cha Brigham Young] kiasi kikubwa cha pesa iliyoahidiwa ili kuwezesha kujengwa kwa jumba zuri lililo [na jina lake].”5

Kuwa na msingi dhabiti ni ulinzi wa mwisho kutoka kwa makonde ya ulimwengu. Tunapaswa tutafute kwa dhati kile Walamani ambao walifundishwa na Amoni na ndugu zake walipata wakati ilisemwa kuwahusu kwamba walikuwa “wamemgeukia Bwana, [na] hawakuanguka kamwe kutoka kanisani.” (Alma 23:6).

Mary Ann Pratt aliolewa na Parley  P. Pratt mnamo 1837. Baada ya kuhamia Missouri, pamoja na watakatifu wale wengine, walivumilia mateso ya kuhofisha. Wakati Parley alichukuliwa, pamoja na Nabii Joseph, na genge kule Far West, Missouri, na kufungwa jela, Mary Ann alikuwa kitandani, akiwa anaugua vibaya sana, akiwalea watoto wawili wadogo.

Baadaye, Mary Ann alimtembelea mumewe kwenye Jela na kukaa naye kwa muda. Aliandika, “Nilikaa naye gerezani, ambapo palikuwa mahali penye maji, giza, pachafu, bila uingizaji wa hewa, pakiwa tu na wavu ndogo upande mmoja. Tulilazimika kulala mahali hapa.

Baada ya Parley kuachiliwa kutoka jela, Mary Ann na mumewe walihudumu katika misheni kule New York na Uingereza na walikuwa miongoni mwa wale ambao “walifanya safari ya kuchosha kukusanyika kwa mara ya mwisho kule Utah,” alivyoielezea. Parley hatimaye alikufa kifo cha mfiadini akihudumu misheni ingine.

Licha ya maisha haya ya shida, Mary Ann Pratt alibaki mkweli. Alisema kwa ushupavu, “Nilibatizwa katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.... nikiwa nimesawishiwa juu ya ukweli wa mafundisho yake na mahubiri ya kwanza niliyosikia; na nikasema moyoni mwangu, ikiwa kuna watatu pekee yake wanaoshikilia imani kwa dhabiti, nitakuwa mmoja wa idadi hiyo; na kupitia udhalimu wote nimelazimika kupitia daima nimehisi vile vile; moyo wangu haujawai kugeuka kutoka uamuzi huo.”6

Mada tunayojadili usiku wa leo ni ya kibinafsi sana. Tunaweza kufundishwa na wengine. Tunaweza kuwatazama wengine. Tunaweza kujifunza kutoka kwa makosa na mafanikio ya wengine. Lakini hakuna anayeweza kutufanyia haya. Hakuna anayeweza kutujengea msingi wetu wa kiroho. Katika jambo hili sisi ni wajenzi wetu wenyewe.

Kama Helamani alifunza kwa nguvu sana, “Na sasa, wana wangu, kumbukeni, kumbukeni kwamba ni juu ya mwamba wa Mkombozi wetu, ambaye in Kristo, Mwana wa Mungu, kwamba lazima mjenge msingi wenu; kwamba ibilisi atakapotuma mbele pepo zake kali, ndio, mishale yake kumbungani, wakati mvua yake ya mawe na dhoruba kali itapiga juu yenu, hautakuwa na uwezo juu yenu kuwavuta chini kwenye shimo la taabu na msiba usioisha, kwa sababu ya mwamba ambako kwake mmjengwa, ambao in msingi imara, msingi ambako watu wote wakijenga hawataanguka” (Helamani 5:12).

Mmoja wa uzoefu wa ushawishi mkubwa katika ujenzi wa msingi katika maisha yangu ulitokea zaidi ya miaka 36 iliyopita. Baada ya kukamilisha masomo yetu ya chuo kikuu, Diane nami tulihamia Honolulu (ambako ndiko nilikozaliwa na kulelewa) kuanza msimu uliofuata wa maisha yetu. Ilitokea kuwa msimu mrefu---miaka 27. Ni Simu tu kutoka kwa nabii ilitufanya tuondoke Hawaii.

Hekalu la Hawaii, sasa linajulikana kama Hekalu la Laie Hawaii kwa sababu kuna mahekalu mawili Hawaii, liliwekwa wakfu kwa mara ya kwanza na Rais Heber  J. Grant siku ya (sawa kabisa) Thanksgiving, Novemba  27, 1919. Lilikuwa hekalu la kwanza kujengwa nje ya eneo la Utah, isipokuwa huko Kirtland na Nauvoo. Kwa takriban miongo sita liliwahudumia Washiriki kule Hawaii na, kwa wingi wa muda huo, wale waliokuwa kote Pasifiki na Asia. Nusu wa miaka ya 1970, kulikuwa na haja ya hekalu kufungwa, kupanuliwa, na kujengwa upya. Hivyo basi, hekalu lilihitaji kuwekwa wakfu upya, jambo lililotendeka mnamo Juni  13, 1978.

Aliyekuwa anasimia mkutano wa kuweka wakfu upya alikuwa Rais wa Kanisa Spencer  W. Kimball. Pamoja naye walikuwa washauri wake wa kwanza na wapili, N. Eldon Tanner na Marion G. Romney. Pia waliohudhuria walikuwa Ezra Taft Benson, Rais wa jamii ya Mitume Kumi na Wawili, na wengine wa Wale Kumi na Wawili na Wale Sabini. Si jambo unaloweza kuona katika Kanisa kubwa la leo, kuwa na ndugu wakuu wengi namna hiyo pamoja kwa ajili ya tukio mbali na makao makuu ya Kanisa. Lakini hiyo ilikuwa baraka yetu mwaka wa 1978.

Nilikuwa kiongozi mdogo wa ukuhani wakati huo na niliombwa na kamati ya kusimamia uwekaji wakfu upya wa hekalu kusimamia usalama wa eneo hilo na maandalizi ya usafiri ya Rais Kimball na washirika wake. Sitaki kuelezea majukumu yangu kana kwamba yalikuwa makubwa sana; yalikuwa tu ya kusaidia na nyuma ya shughuli zenyewe. Hata hivyo, lile jukumu langu liliruhusu kuwa karibu na Rais Kimball. Kwa muda wa wiki mzima uliojumuisha siku tatu za vikao vya uwekaji wakfu upya hekalu, mkusanyiko wa watakatifu, na mkutano mkuu mkubwa wa eneo, nilimtazama Rais wa Kanisa kwa karibu. Nilimwona akifundisha, akishuhudia, na akutoa utabiri kwa mamlaka na nguvu. Niliona jitihada yake ya kutochoka ya kutumikia “yule mmoja,” akiomba akutane kwa faragha na watu binafsi aliowapata katika mikutano ama njiani. Nilimshuhudia akitumika masaa yote kama “chombo mikononi mwa Mungu” (Alma 17:9). Nilivutiwa kabisa!

Katika mwisho wa wiki, tulikuwa kwenye uwanja wa ndege kwa ajili ya kuondoka kwa Rais Kimball na washiriki wake. Tena, nikihimiza jukumu langu pungufu na la kusaidia, ninashiriki yafuatayo: Rais Kimball alinijia kunishukuru kwa ajili ya jitihada zangu ndogo. Hakuwa mrefu sana kimwili, nami ni mtu mkubwa. Alinishika kwa kola za koti langu na kunivuta chini kwa nguvu kufikia urefu wake. Kisha akanibusu kwenye shavu na kunishukuru. Baada ya kutembea hatua chache, Rais Kimball alirudi. Alinishika vile vile na kunivuta chini tena. Wakati huu alinibusu kwenye shavu lingine na kuniambia alinipenda. Kisha akaondoka.

Mwaka kabla ya hapo, wasifu wa Spencer  W. Kimball ulikuwa umechapishwa, ulioandikwa na mtoto wake na mjukuu wake. Wakati huo niliupata na kuusoma, nikagundua kwamba ni wa kuvutia. Hata hivyo, baada ya tukio hili la kibinafsi sana na Spencer Woolley Kimball, nilienda nyumbani kutoka kwa uwanja wa ndege na kuchukua toleo lile kubwa kutoka kwa rafu ya maktaba, nikihisi hamu kubwa ya kulisoma tena. Kwa siku chache zilizofuata, kila saa la kazi ambalo sikuwa na wajibu mwingine, nilikuwa ninasoma na kutafakari. Unaona, sasa nilikuwa ninasoma kumhusu mtu ambaye nilimpenda kwa dhati. Sasa nilikuwa nasoma kumhusu mtu ambaye nilijua alinipenda. Sasa nilikuwa nasoma kumhusu mtu ambaye ningemfanyia chochote kwa sababu nilijua chochote ambacho angeuliza kingekuwa kwa manufaa yangu.

Kupitia furaha ya kina ya tukio hilo, nilipata tukio lingine. Hili ni la kibinafsi sana kushiriki, lakini kulipitia nilihisi aibu sana. Nilielewa kwamba sikuwa na upendo ule ule na heshima kwa wale walio wa muhimu kabisa, washiriki wa Uungu, na hasa kwa Yesu aliye Kristo, Mwokozi na Mkombozi. Hii ilinitia motisha kujifunza “wasifu” Wake na kupitia sala na kufunga na kutafakari kujua kwamba sasa nilikuwa ninasoma kumhusu mtu ambaye nilimpenda sana. Sasa nilikuwa ninasoma kuhusu mtu niliyejua alinipenda. Sasa nilikuwa ninasoma kuhusu mtu ambaye ningemfanyia chochote kwa sababu nilijua chochote kile ambacho angeuliza kingekuwa kwa manufaa yangu.

Wapendwa marafiki zangu vijana, ninashuhudia kwamba ufahamu huu umeleta tofauti kubwa sana katika maisha yangu na katika familia yangu. Ninaharakisha kuongeza kwamba haujatufanya kwa njia ya kimiujiza kuwa bila dosari na haijafanya maisha kuwa rahisi hasa. Hiyo ingekuwa kinyume na mpango wa Mungu. Lakini kile kilichotoa ni msingi wa tumaini---“mng’aro mkamilifu wa tumaini” (2 Nefi 31:20). Hakujawahi kuwa na fikra ya kukata tamaa, kuacha ama kurudi nyuma. Ninawaombeeni tukio kama hilo pia.

Hata kwa ukubwa wenu, miongoni mwa mkusanyiko wa kiasi hiki, kuna shangwe kubwa na uchungu mwingi. Kibinafsi, mnaweza kuhisi kwa kina uzito wa mizigo mizito ya maisha. Pengine mambo katika familia yako hayako vile upendavyo. Pengine unapambana na imani yako. Kuna uwezekano unakumbana na jambo kutoka kwa siku zako za kale---huenda jambo ambalo umefanya ama jambo ulilotendewa bila haki. Baadhi yenu mna changamoto za kimwili ama kiakili ama kihisia zinazoonekana kuwa nyingi sana kuvumilia. Bila kujali hali yako, kuwa na msingi dhabiti kutarahisisha mzigo wako. Na ujumbe wa wimbo unaoimbwa mara nyingi “Mimi ni Mtoto wa Mungu”7 moyoni mwako na katika nafsi yako na si tu kwenye mdomo wako, na pamoja na kutegemea kila wakati kwenye Upatanisho wa Mwokozi, Yesu Kristo, kunaweza kuwa na amani na faraja hata katika nyakati ngumu sana.

Leo inaweza kuwa siku muhimu, hata ya kihistoria katika maisha yetu. Inaweza kuwa siku ya kufanya uamuzi na kuchukua jitihada ya nidhamu kujenga ama kuimarisha msingi wetu. Kwa wengine wetu, huenda ikawa ni siku ya kuacha uraibu ama vitendo vya kuudhi ambavyo vinamuudhi Mungu. Kwa wengine, huenda ikawa ni siku ya kupanga upya vipaumbele vya maisha yetu na kufanya upendo wetu kwa Mungu kuwa mkuu. Inastahili gharama yoyote. Hakika, ni msingi wa kazi ya maisha yetu.

Kwa nafsi na kibinafsi iwezekanavyo kwa mkusanyiko mkubwa sana, ninatangaza ushahidi wangu wa Yesu Kristo, jiwe la katikati la Kanisa na mwamba wa maisha yetu. Ninashuhudia kuwa jina Lake ni tukufu. Ninashuhudia kwamba mamlaka Yake na misheni Yake na, muhimu kabisa, Upatanisho Wake, unaomwezesha kila mmoja wetu, bila kujali hali yetu ya zamani ama ya sasa, kuja Kwake (ona Moroni 10:32), katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Thomas S. Monson, “How Firm a Foundation,” Ensign or Liahona, Nov. 2006, 62.

  2. Maandiko yametoholewa kutoka kwa Robert J. Matthews, “I Have a Question,” Ensign, Jan. 1984, 52.

  3. “How Firm a Foundation,” Hymns, no. 85.

  4. Henry B. Eyring, “Finding Safety in Counsel,” Ensign, May 1997, 25.

  5. Gordon B. Hinckley, “Five Million Members—a Milestone and Not a Summit,” Ensign, May 1982, 45–46.

  6. Hadithi ya Mary Ann Pratt imetoka kwa Sheri Dew, Women and the Priesthood: What One Mormon Woman Believes (2013), 94–95; ona pia Edward W. Tullidge, The Women of Mormondom (1877), 406–7.

  7. “I Am a Child of God,” Hymns, no. 301.

Chapisha