Je! Ni Nini Mpango Makini wa Kanisa la Kristo ?
Mkutano wa Ibada ya MEK kwa Vijana • Januari 12, 2014 • Chuo Kikuu cha Brigham Young-
Ni furaha jioni hii kuwa pamoja na wale viongozi na wazazi watarajiwa wa Kanisa hili. Kwa sababu hiyo, naamini takdiri ya Kanisa hili iko salama na inag’aa. Ipasavyo, ningependa kuzungumza kuhusu Kanisa ambalo mtasimamia siku moja.
Katika sehemu ya kwanza ya Mafundisho na Maagano, Bwana anatoa kauli hii kali na muhimu: “[ Hili ni ] kanisa pekee la kweli na lililo hai usoni mwa dunia yote” ( M & M 1:30). Hii ina maana gani ? Hainamaanishi kwamba makanisa mengine hayana ukweli fulani, kwa kuwa yanao. Hainamaanishi kwamba makanisa mengine hayatendi mema, kwa hakika yanatenda mengi mema. Kinachomaanisha ni kwamba hili ni kanisa la pekee ambalo lina ukweli wote ambao umefunuliwa katika kipindi hiki - kanisa pekee ambalo lina maagizo yanayohitajika kwa ajili ya uokovu, na kanisa pekee ambalo lina ukuhani wa Mungu wa kutenda maagizo hayo na thibitisho la kiungu. Ni ushahidi tulionao wa madai haya?
Miaka michache iliyopita mke wangu nami tulihitaji nyumba kubwa zaidi kwa ajili ya familia yetu iliyokuwa inakuwa kubwa, hivyo basitulipata shamba lakujenga. Tuliweka muda kuutengeneza mpango makini ambao ungefaa kabisa kwa mahitaji ya familia yetu. Mke wangu alisanifu mlango wa kujikunja kati ya chumba chetu cha familia na sebule ambao ungefunguka kwa ajili ya shughuli kubwa za familia na vijana. Tukiwa na nafasi ya ziada juu ya karakana, tulisanifu chumba ambacho watoto wetu wangeweza kushiriki katika shughuli zenye kuleta siha. Chumba kidogo kilijengwa nyuma ya karakana kwa ajili ya kuruhusu hifadhi ya chakula na hifadhi nyingine. Haya na mambo mengine ya usanifu yalishirikishwa katika mpango makini. Nyumba kisha ilijengwa kufuatia ramani hizi.
Nyumba ilipokuwa inajengwa, mara kwa mara tuliwasilisha kwa mjenzi maagizo ya mabadiliko ambayo yalibadilisha mpango makini upya. Wakati nyumba hatimaye ilipokamilika, ilikuwa ni kwa kuzingatia mpango makini wetu halisi kama ulivyofanywa upya mara kwa mara. Kama ungechukua mpango makini wetu na kuulinganisha na kila nyumba duniani, ni nyumba ngapi ambazo zingefanana nayo kikamilifu? Moja tu---nyumba yetu. Ah, huenda kuna mifanano kwa nadra kwa hapa na pale- chumba kilicho na ukubwa sawa, madirisha yanayofanana---lakini msingi kwa msingi, chumba kwa chumba, paa kwa paa, kutakuwa na nyumba moja tu ambayo mpango makini wake ambao unafanana kikamilifu---nyumba yetu.
Katika njia inayofanana Kristo alijenga nyumba iliyofaa kabisa na mahitaji ya kiroho ya watoto wake. Iliitwa Kanisa Lake. Mpango makini wa kiroho wa Kanisa hili unaweza kupatikana katika Agano Jipya. Mara kwa mara Mwokozi alifanya “maagizo ya mabadiliko” kwa mpango makini. Maagizo ya mabadiliko kama hayo yalikuja kwa njia ya ufunuo. Kwa mfano, Mwokozi awali aliamuru Mitume wake wahubiri injili kwa nyumba ya Israeli lakini si kwa Mataifa (ona Mathayo 10:5–6). Baada ya Kupaa kwa Mwokozi, hata hivyo, alimpa Petro maagizo ya mabadiliko ya kiroho--- ufunuo kwa njia ya ono---kwamba injili ilipaswa sasa kufundishwa pia kwa Mataifa (ona Matendo ya Mitume 10). Uzoefu huu wa Petro ulifundisha kanuni angalau mbili muhimu ya uongozi katika Kanisa la Kristo : moja, mpango makiniuliweza kubadilishwa, lakini tu kwa ufunuo kutoka kwa Kristo, na pili, ufunuo kama ule ungekuja kwake Mtume ambaye alikuwa msemaji wa Mungu duniani. Kwa kusema vingine, Kanisa la Mungu lingetawaliwa na ufunuo wa Mungu na kwa utaratibu.
Ikiwa mtu angetaka kugundua Kanisa la Kristo leo, angependa kulinganisha mpango makini wa kiroho unaopatikana katika Agano Jipya na kila kanisa la Kikristo katika dunia mpaka agundue kanisa ambalo limeendana na mpango makini - shirika kwa shirika, fundisho kwa fundisho, agano kwa agano, tunda kwa tunda, na ufunuo kwa ufunuo. Kwa kufanya hivyo hueanda akapata baadhi ya makanisa ambayo yanafanana---fundisho moja au mawili ambayo yanapishana, agano ambalo ni sawa, baadhi ya ofisi ambazo zina majina sawa---lakini atapata tu kanisa moja, Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, ambalo linaendana na mpango makini katika kila hali halisi. Sasa, ningependa kuweka dai hilo kwenye jaribio.
Hebu turejelee kwenye ukurasa wa kwanza wa mpango makini na kugundua ni ulikuwa vipi mpangilio wa Kanisa la Kristo kama ilivyofunuliwa hapo ndani.
Kwanza, Kanisa la Kristo lilijengwa juu ya mitume na manabii. Wakati Paulo alipokuwa anawaandikia washiriki wachache wapya wa Kanisa, alisema kuwa walikuwa sasa “wako juu ya msingi... wa mitume na manabii,, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la pembeni" (Waefeso 2:20; mlazo umeongezewa).
Mitume walielewa haja muhimu ya kuweka Jamii ya Mitume Kumi na Wawili kamili. Wakati Mtume mmoja, kama vile Yuda, alikufa na sehemu ya msingi ilikuwa "imechipuliwa mbali," Mitume wale wengine 11 walikusanyika na kuchagua mrithi ili kwamba msingi ungekuwa mzima tena (ona Matendo ya Mitume 1:22–25).
Utaratibu huu ni ushahidi muhimu wa kudumisha Jamii ya Mitume Kumi na Wawili. Wakiwa muhimu sana hawa Mitume kwa ustawi wa Kanisa hadi Paulo akatangaza ni kwa muda gani tuliwahitaji: “Hadi sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani" (Waefeso 4:13). Na kisha akaeleza ni kwa nini: Ili kwamba, nukuu “tusibebwe na kila upepo wa mafundisho” (Waefeso 4:14). Ipasavyo, Mitume walikuwa muhimu kwa kuweka mafundisho kuwa safi.
Tuseme kwa muda ningekuwa namsimulia mtu hadithi mwishoni mwa safu mbele yangu, na kisha angeshiriki na mtu karibu naye, na kadhalika mpaka ingetiririka kwenye safu hadi mwisho wa sehemu. Nini kingetokea katika hadithi hiyo? Ingebadilika. Daima hubadilika; hiyo ni asili ya binadamu. Hivyo ndivyo ilikuwa na mafundisho yaliyofundishwa na Mitume walipokwenda katika miji mbalimbali na vijiji. Mafundisho yalivyoenda kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine, yalianza kubadilika. Imradi tu Mitume walikuwa wanapatikana, wangesahihisha mafundisho kwa njia ya nyaraka au mahubiri ya kibinafsi. Lakini wakati Mitume walipokuwa wametoweka,---kulikuwa hakuna tena mfumo wa kupima na kusahihisha, hakukuwa tena na mfumo wa kukagua naa kurekebisha, na hivyo basi mafundisho yakawa yameharibiwa au kupotea.
Kwa sababu hii na nyingine, mwongozo unaonyesha kwamba mitume na manabii waliunda msingi wa Kanisa la Kristo. Je, unajua kuhusu amri yoyote ya mabadiliko katika Agano Jipya, kuna ufunuo wowote ambao ulifanya upya mpango makini na kusema kwamba Mitume hawahitajiki tena? Mimi sijui. Ikiwa hivyo ndivyo ilivyo, basi Kanisa la kweli la Kristo leo linapaswa liwe na mitume na manabii kama msingi wake.
Ili kusaidia Mwokozi na Mitume wake katika kuhubiri injili kwa ulimwengu, Mwokozi aliwachagua watu wengine, walioitwa Sabini, ili kuandaa njia. Tunasoma kuhusu hawa Sabini katika Luka, Luka, sura ya 10. Je, unajua kuhusu kanisa hivi leo ambalo linalingana na mpango makini huu---ambalo lina ofisi ya Wale Sabini?
Mpango makini wa Agano Jipya hufunua juu ya maafisa wengine wanaounda sehemu ya mpangilio wa Kanisa la Kristo: Maaskofu (ona 1 Timotheo 3; Tito 1:7); wazee (ona Matendo ya Mitume 14:23; Tito 1:5); shemasi (ona Wafilipi 1:1); wainjilisti (ona Waefeso 4:11), kumaanisha, baba wakuu1; na wachungaji (ona Waefeso 4:11), kumaamisha watu kama vile maaskofu na maraisi wa vigingi ambao wanasimamia zizi.2
Makala ya sita ya imani ya Kanisa inarejelea mpango makini huu: “Tunaamini katika mpangilio ule ule uliokuwepo katika Kanisa la Kwanza, yaani, mitume, manabii, wachungaji, walimu, wainjilisti, na kadhalika" (Makala ya Imani 1: 6; mlazo umeongezwa). Kwa maneno mengine, tunaamini Kanisa la sasa la Yesu Kristo linapaswa liwe na mpangilio ule ule uliokuwepo kwa Kanisa la Kristo la asili, kubadilika tu kwa mabadiliko ya kinabii. Kwa hiyo, kila moja ya ofisi hizi inapatikana katika Kanisa letu leo.
Je! Ni kwa njia gani Mitume wa Kristo na maafisa wengine walichaguliwa? Je, Mwokozi alikwenda kwenye shule bora zaidi za kiteolojia za nyakati hizo na kuchagua wanafunzi wale waliofuzu zaidi? Hakufanya hivyo. Badala yake, mwongozo unatuambia kwamba Alimchagua Petro, mvuvi, na Mathayo, mtoza ushuru, na baadaye Paulo, mjenga hema. Kila mmoja alichaguliwa kutoka cheo na hali---katika kiini ni huduma ya kujitolea. Leo Kanisa lina jamii ya Mitume kumi na wawili ambao vile vile wamechaguliwa kutoka katika cheo na hali ya Kanisa. Mmoja huenda akawa ni mwalimu, mwingine mhandisi, mwingine wakili, na kadhalika.
Je, Mitume wa Kristo na maafisa wengine waliwasilisha maombi kwa ajili ya huduma? Hawakufanya hivyo. Mpango makini unatuambia jinsi Kristo alivyowachagua maafisa Wake: “, na kuwatuma ninyi” (Yohana 15:16; mlazo umeongezwa). Wakati Kristo alipowateua Mitume Wake, Yeye aliwapa nini? Mathayo na Luka wanameandika jibu : “aliwapa uwezo” (Mathayo 10:1; ona pia Luka 9:1)—uwezo wa ukuhani ili kutenda katika jina Lake na kufanya kazi Yake. Hiyo ndiposa mpango makini unatuambia “Mwana wa Mtu … aliwapa mamlaka watumishi Wake” (Marko 13:34). Kwa nini? Ili waweze kutenda katika jina Lake na dhibitisho Lake. Kila mtu ambaye ana ukuhani wa Mungu katika kanisa hili leo anaweza kufuatilisha ukuhani wake hadi kwake Yesu Kristo, chanzo cha mamlaka na nguvu, basi kwamba yeye, vivyo hivyo, ana haki ya dhibitisho ya Kristo---muhuri Wake wa idhini---kama ilivyotakiwa na mpango makini.
Jina la kanisa liliyoanzishwa na Kristo lilikuwa ni gani? Ikiwa tunabatizwa katika jina la Kristo, ikiwa tunaomba katika jina la Kristo, ikiwa tunaokolewa katika jina la Kristo, na ikiwa Yeye ndiye mwanzilishi na msingi mkuu wa Kanisa Lake, ungetarajia jina la Kanisa Lake liwe nini?--Kanisa la Yesu Kristo. Mwokozi, alipokuwa anazungumza na watu katika wakati wa Kitabu cha Mormoni, alifundisha wazo la msingi kwa nini Kanisa lilihitaji kuwa na jina Lake: “Na jinsi ya kuwa ni kanisa langu ila liitwe kwa jina langu ? Kwa maana kama kanisa limeitwa katika jina la Musa basi ni kanisa la Musa, au kama ni limeitwa kwa jina la mwanadamu basi ni kanisa la mwanadamu, ila kama litaitwa kwa jina langu basi ni kanisa langu, kama iwe kwamba wamejengwa juu ya injili yangu (3 Nefi 27:8; mlazo umeongezwa) .
Ni kwa sababu hii kwamba Paulo aliwakemea baadhi ya washiriki wa mapema wa Kanisa ---kwa sababu walijiita majina ya wanafunzi fulani, badala ya jina la Kristo. Ipasavyo, Paulo aliandika:
"Sasa mimi ninasema hivi, kwamba kila mmoja wenu asema, Mimi ni wa Paulo; na Mimi ni wa Apolo na mimi ni wa Kefa, na Mimi ni wa Kristo.
"Je, Kristo amegawanyika? Paulo ndiye aliyesulubiwa kwa ajili yenu? Au je, mlibatizwa kwa jina la Paulo? "(1 Wakorintho 1:12–13).
Kwa maneno mengine, hatuchukui juu yetu jina lolote lingine ila la Yesu Kristo
Ipasavyo, mpango makini unatufundisha kwamba Kanisa la Kristo lazima liwe na jina Lake. Daima imeonekana kwangu kuwa miujiza kwamba Matengenezo yalikuwepo kwa zaidi ya miaka 300 kabla ya wakati wa Joseph Smith na hakuna aliyefikiria kuita kanisa lake jina la Yesu Kristo. Bila shaka, tangu wakati wa Joseph Smith, wengine wamefuata nyayo, lakini katika njia ya ajabu Bwana alihifadhi matumizi ya jina Lake mpaka wakati wa Joseph Smith na Rejesho la Kanisa la Kristo.
Sasa, hebu twende kwenye ukurasa wa pili wa mpango makini. Ni yapi yaliyokuwa mafundisho ya Kanisa laKristo ? Hebu tuchunguzie machache:
Je, Mungu ni roho tu ama Yeye anao mwili wa nyama na mifupa pia? Mpango makiniunafundisha nini?
Baada ya Ufufuo wa Kristo, aliwajia wanafunzi Wake ambao kwa makosa walidhani kwamba alikuwa ni roho ( ona Luka 24:37). Ili kurekebisha kosa hili, Alisema, “Tazameni mikono yangu na miguu yangu, ya kwamba ni mimi mwenyewe: nishikeni, na muone; maana roho haina mwili na mifupa kama mnionavyo” (Luka 24:39; mlazo umeongezwa ).
Ili kuondoa shaka yoyote juu ya asili ya kimwili ya mwili Wake uliofufuka, aliwauliza wanafunzi Wake, "Je, mnayo hapa nyama yoyote ? " (Luka 24:41). Kisha maandiko yameandikwa:
"Wakampa kipande cha samaki wa kuokwa, na asali."
"Na alikichukua, na akala mbele yao" (Luka 24:42–43).
Akiwa na mwili huo mtukufu wa nyama na mifupa, uliofufuka, Kristo alipaa mbinguni (ona Matendo ya Mitume 1:9),3 ambapo ameketi katika mkono wa kulia wa Mungu Baba na yuko katika “sura ya mtu wake " (Waebrania 1:3). Huu ni ukweli halisi uliofundishwa na Joseph Smith kama sehemu ya Urejesho wa Kanisa la Kristo : "Baba ana mwili wa nyama na mifupa kama unaoonekana kama wa mtu, Mwana pia " (M&M 130:22).
Je, Mungu na Yesu ni Kiumbe kimoja, kama inavyofundishwa na sehemu kubwa ya ulimwengu wa Kikristo, au Viumbe viwili tofauti ? Mpango makini unasema nini?
Idadi ya marejeo katika Biblia ya utambulisho tofauti na majukumu ya Baba na Mwana ni kubwa kushangaza. Katika Bustani ya Gethsemane, akitambua maumivu makali ambayo yalikuwa bado kuwa Yake, Mwokozi alitangaza, " i mapenzi yangu, bali yako yatimizwe,” (Luka 22:42). Hiki ni kitendo kikuu cha kujiwasilisha ambacho duniani imewahi kujua. Lakini ni kuwasilisha kupi kungekuwepo kama hakungekuwa na Kiumbe kingine ambapo kwake Angeweza kujiwasilisha---ikiwa Yeye na Baba walikuwa kiumbe kimoja? Kwa nini Mwokozi anaomba kwake Baba ama kulia kwa sauti, "Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha ?" (Marko 15:34). Je, angewezaje kuachwa ikiwa hakungekuwa na Kiumbe kingine tofauti wa kumuacha Yeye? Je, Stefano alimuonaje Yesu akiwa amesimama upande wa kulia wa Mungu kama Wao si watu wawili (ona Matendo ya Mitume 7:55–56)?
Wakati Joseph Smith alipoibuka kutoka kwa kichaka cha miti, alikuwa amejifunza kwa ajili yake mwenyewe ukweli huu. Alikuwa amemuona Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo, wakiwa wamesimama upande kwa upande ; alikuwa amesikia Baba akimrejelea yule mwingine kama “Mwanawe Mpendwa” (Joseph Smith—Historia 1:17). Katika siku hiyo tukufu mbinguni ilivunja hadithi za kibinadamu za zamani kuhusu asili ya Mungu na ikafunua na kuthibitisha ukweli rahisi kama ulivyofundishwa awali katika mpango makini---kwamba Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo, wana umoja wa malengo na mapenzi lakini ni tofauti wa utambulisho.
Mpango makini unasema nini kuwahusu wale ambao kamwe hawakupata nafasi sawa kusikia injili ya Yesu Kristo walipokuwa duniani? Je, wamehukumiwa? Je, hatuna maarifa yaliyofunuliwa kuhusu hali yao ya kiroho?
Hili ni swali kubwa linaloathiri mabilioni ya maisha. Hakika Mungu amezungumzia jambo hili. Na katika kweli, Amelizungumzia. Mpango makini unalo jibu.
Petro aliandika: "Kwa sababu hiyo, ilikuwa habari njema pia kwa wale walio wafu, ili kwamba waweze kuhukumiwa kulingana na wanaume katika mwili, lakini kuishi kulingana na Mungu katika roho" (1 Petro 4:6). Mafundisho haya yalipotea katika Uasi kufuatia kifo cha mitume wa Kristo, lakini yalirejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith.
Je! kuna mbinguni tatu au mbinguni moja? Kwa miaka ulimwengu wa Kikristo umefundisha kuna mbinguni moja na jehanamu moja, lakini mpango makini asili unafundisha nini?
Paulo alifundisha,: "Kuna fahari moja ya jua, na fahari nyingine ya mwezi, na fahari nyingine ya nyota " (1 Wakorintho 15:41). Paul hatimaye alithibitisha ukweli wa jambo hili la mbinguni ya sura tatu wakati alieleza maono ya mtu "aliyechukuliwa juu mbinguni ya tatu" (2 Wakorintho 12:2). Je! kungeweza kuwa na mbingu wa tatu kama hakungekuwa na mbingu wa pili ama wa kwanza? Tena, mafundisho haya yaliyorejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith yalikuwa katika usawa halisi na mpango makiniasili.
Je, ndoa huendelea kwa milele au huishia katika kifo? Mpango makini unatoa unasema nini?
Kwa mujibu wa nguvu iliyopewa Mitume kwamba kila wanachopaswa kufunga duniani, lazima kifungwe mbinguni (ona Mathayo 18:18), Paulo alitangaza, "Wala mwanamume pasipo mwanamke, wala mwanamke pasipo mwanamume, katika Bwana "(1 Wakorintho 11:11), kumaanisha kuwa ubora ni kwa mwanamume na mwanamke kufungwa pamoja milele katika uwepo wa Mungu. Petro alidhibitisha ukweli huu. Akizungumzia waume na wake, alisema kwamba wanapaswa kuwa "warithi pamoja wa neema ya uzima " (1 Petro 3:7), si wakiwa wametengana, si kwa kibinafsi, lakini pamoja wakitembea njia kama warithi wa uzima wa milele. Hayo ni mafundisho yaliyofundishwa katika mpango makini; hayo ni mafundisho yanayofundishwa katika Kanisa la Kristo leo.
Ukurasa wa tatu wa mpango makini unasoma, "Maagizo katika Kanisa la Kristo." Mpango makini ni mahususi sana katika suala hili. Kwa mfano, je, tunabariki ama kubatiza watoto wachanga na watoto wadogo? Mpango makini unafundisha nini?
Mwokozi alitoa mfano wa wazi kwetu. Akizungumzia watoto wadogo, maandiko yanasoma, "Akawakumbatia, akaweka mikono yake juu yao, akawabarikia. ” (Marko 10:16; mlazo umeongezwa). Mathayo alithibitisha kwamba, kwa watoto wadogo, Mwokozi "akaweka mikono yake juu yao" (Mathayo 19:15). Mpango makini unafundisha kwamba watoto wachanga na watoto wadogo hupewa baraka, si kubatizwa. Kwa kweli, hakuna tukio hata moja ya ubatizo wa mtoto mchanga popote katika Agano Jipya lote. Kwa nini? Kwa sababu halikuwa agizo katika Kanisa la Kristo. Mtu anayetafuta Kanisa la Kristo leo angetafuta kanisa ambalo huwapa baraka watoto wachanga si kuwabatiza.
Je! Ubatizo ni muhimu kwa ajili ya wokovu? Mpango makini unafundisha nini?
Baada ya Kristo kuweka mfano kwa kubatizwa, alitangaza bayana, " Mtu asipozaliwa kwa maji na Roho , hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu" (Yohana 3:5; mlazo umeongezwa) . Petro alifundisha vivyo hivyo: "Tubuni, mkabatizwe kila mmoja wenu kwa jina la Yesu Kristo kwa ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu" (Matendo ya Mitume 2:38; mlazo umeongezwa). Kile kinachofundishwa katika mpango makini hasa ni kile kinachofundishwa katika Kanisa la Kristo leo.
Ubatizo hufanywa kwa kunyunyuziwa, umiminaji, au kuzamishwa ? Mpango makini unatoa ushahidi angalau mara nne kwamba ubatizo unapaswa ufanywe kwa kuzamisha:
Kwanza, Mwokozi, Mfano wetu mkuu, alikuja juu " Mara nje ya maji " (Mathayo 3:16), kuonyesha lazima iwe kwanza alikwenda chini ndani ya maji.
Pili, Yohana Mbatizaji “alikuwa akibatiza huko Ainoni, karibu na Salimu, kwa sababu huko kulikuwa na maji tele" (Yohana 3:23; mlazo umeongezwa). Kwa nini angesafiri hadi mahali pa "maji tele" kama kunyunyiza au kumiminiwa zilikuwa njia zilizokubaliwa za ubatizo?
Tatu, Paulo anatuambia kwamba ubatizo ni ishara ya kifo, kuzikwa, na ufufuo wa Yesu Kristo (ona Warumi 6:3–5). Mshiriki mpya anaposimama katika maji ya ubatizo, huwakilisha mtu yule wa kitambo ambaye yu karibu kufa. Anapozamishwa majini, dhambi zake “huzikwa”na kusamehewa na ishara ya nguvu ya utakaso ya maji. Kisha, anapotoka majini, yeye husimama kama mwakilishi wa mtu mpya ama aliyefufuka katika Yesu Kristo. Ishara hiyo yote ambayo ni msingi wa ubatizo inaenda sambamba na ubatizo kwa kuzamisha, lakini---inapotea kabisa---na unyunyuzi na umiminizaji.
Na nne, neno la Kiyunani ambalo kwalo ubatizo umetafsiriwa linamaanisha kuzamisha ama kutia majini.
Will Durrant, mwanahistoria maarufu duniani, alijua kile ambacho mpango makini ulifunua na hivyo alisema "Kwa karne ya tisa njia ubatizo ya awali ya Kikristo kwa uzamisaji kamili ilikuwa imebadilishwa na ... unyunyuzi kama njia isiyo na hatari sana kwa afya katika jamii za kaskazini.”4
Haipaswi kuwa mshangao kwamba Joseph Smith alipokea ufunuo juu ya namna ambayo ubatizo unapaswa ufanywe ambayo ni sambamba kikamilifu na mpango makini wa Kristo (ona M&M 20:73–74).
Je, ubatizo kwa ajili ya wafu ulikuwa agizo katika Kanisa la Kristo la awali? Ulikuwepo.
Washiriki wa Kanisa kule Korintho walikuwa wanashiriki katika agizo sahihi lililojulikana kama ubatizo wa wafu. Watu hawa, hata hivyo, walishuku ukweli wa ufufuo. Wakiwa wamehisi uholela wa kile walichokuwa wanafanya kikilinganishwa na kile walichoamini, Paulo alitumia ushiriki wao katika agizo sahihi la ubatizo kwa ajili ya wafu ili kuthibitisha mafundisho sahihi ya Ufufuo. “Au je! Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu watafanyaje? Kama wafu hawafufuliwi kamwe, kwa nini kubatizwa kwa ajili yao?" (1 Wakorintho 15:29).
Mara tu mtu akisha vuka daraja ya kimafundisho na akatambua kwamba ubatizo ni muhimu kwa wokovu (ambao ndiyo), kisha kimantiki huongozwa kuamini katika ubatizo wa wafu--- hakuna kuukimbia. Vinginevyo, ni jinsi gani mtu hujibu swali gumu “Je wale waliokufa bila nafasi ya kubatizwa?" Wale wanakabiliwa na swali hili wana chaguo nne wanazoweza kuchagua kutoka kwazo:
Kwanza, wanaume na wanawake ambao hawajabatizwa watahukumiwa kwenda jehanamu. Jibu kama hilo, hata hivyo, ni kinyume na ukweli wa maandiko kwamba "Mungu hana upendeleo kwa watu" (Matendo ya Mitume 10:34) na kwamba Mungu anataka "watu wote kuokolewa " (1 Timotheo 2:4).
Pili, pengine Mungu hakumaanisha kwa kweli kile alichosema--labda ubatizo si muhimu kwa kweli kwa ajili ya wokovu. Lakini hii si kweli kwa sababu Mungu daima humaanisha kile asemacho: "Ni mimi, Bwana, nimenena, nimesema, na mimi si udhuru kwangu" (M&M 1:38; ona pia Mosia 2:24).
Tatu, wengine huamini kwamba hali mpya iitwayo " ubatizo kwa hamu" inaweza kubadilishwa kwa ajili ya ubatizo wa maji . Kwa maneno mengine, kama mtu anataka kumfuata Yesu lakini hakuwa na nafasi ya kubatizwa duniani, basi hamu yake ya kustahili inakuwa mbadala wa kukubalika badala ya ubatizo wa maji. Tatizo la chaguo hili ni kwamba haina uhimili wa kimaandiko. Maandiko hayasemi, " Mtu asipozaliwa kwa hamu, " lakini badala yake, " Mtu asipozaliwa kwa maji na Roho, hawezi kamwe kuingia katika ufalme wa Mungu” (Yohana 3:5; mlazo umeongezwa).
Chaguo la nne ni kwamba Mungu kwa kweli alimaanisha kile alichosema alipoamurisha kila mtu abatizwe, na kwa sababu ya haya alitoa kwa huruma njia kwa kila mtu kubatizwa hata kama nafasi haikupatikana maishani duniani. Hiyo ni ubatizo kwa ajili ya wafu. Hiyo ndiyo chaguo lililosambamba na mpango makini.
Mpango makini unasema nini kuhusu namna ambayo karama---si tu uwepo wa muda, lakini karama ya kudumu---ya Roho Mtakatifu hutolewa baada ya mtu kubatizwa? Je, huwa inashuka moja kwa moja juu ya mtu kufuatia ubatizo wake? Je, huja kama upepo unaopuliza, ama kunalo agizo tukufu, utaratibu tukufu ambao lazima ufuatwe ili kupokea karama hii? Mpango makini unatoa jibu.
Baada Philip kubatiza washiriki wachache wapya katika Samaria, Petro na Yohana waliwasili. Maandiko kisha yanafunua namna agizo linapaswa lifanywe. :“Kisha [ Petro na Yohana ] wakawawekea mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu” ” (Matendo ya Mitume 8:17; mlazo umeongezwa).
Utaratibu huo huo ulifuatiliwa baada ya Paulo kuwabatiza washiriki wapya kule Efeso
"Baada ya kusikia hayo, walibatizwa kwa jina la Bwana Yesu.
“Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao " (Matendo ya Mitume 19:5–6; mlazo umeongezwa).
Kwa mara nyingine tena mpango makini na Kanisa la Kristo lililorejeshwa upo katika ulinganisho kamilifu.
Ukurasa ufuatayo wa mpango makini huenda ukasoma: “Matunda ya Kanisa la Kristo.” Mwokozi alitoa jaribio hili la ukweli "Kwa matunda yao mtawatambua " (Mathayo 7:20). Ni nini matunda ya Kanisa la Kristo kama ulivyoshuhudiwa katika mpango makini?
Moja, wale Watakatifu wa awali walijitahidi kuwa watu wenye afya. Paulo alifundisha kuwa miili yetu ni "hekalu" ambazo zinaweka roho zetu na kwa hiyo, zinapaswa kuchukuliwa kama takatifu: "Je, hamjui kwamba ninyi ni hekalu la Mungu, na kwamba Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? (1 Wakorintho 3:16; ona pia 1 Wakorintho 6:19). Kwa sababu ya haya washiriki wa Kanisa la Kristo walikuwa na baadhi ya sheria ya afya, kama vile baadhi ya vikwazo juu ya kunywa mvinyo vinavyopatikana katika Waefeso 5 na 1 Timotheo 3. Kwa mujibu wa sheria hii ya kiungu ya kuchukulia miili yetu kama mahekalu, Joseph Smith alipokea sheria ya afya kutoka kwa Bwana kwa ajili ya washiriki wa Kanisa la Kristo lililorejeshwa, inayojulikana kama Neno la Hekima. Kama matokeo ya kuishi sheria hii ya afya, utafiti ya mara kwa mara umethibitisha kwamba washiriki wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ni miongoni mwa watu wenye afya bora zaidi duniani. Hili ni mmoja wa matunda ya kuishi sheria ya afya ya Kristo.
Tunda la pili la Kanisa la Kristo lilikuwa miujiza yake na karama za Roho. Zimeandikwa kwenye ukurasa baada ya ukurasa katika Agano Jipya. Ni ushahidi kwamba nguvu ya Mungu ipo katika Kanisa la Kristo (ona Waebrania 2:4). Lakini kwa bahati mbaya, kwa ujio wa uasi, miujiza ilikoma---wanahistoria wanaukubali kwa urahisi, na warekebishaji wanaikiri. Paul Johnson, mhistoria maarufu alisema, " Imekubalika angalau tangu nyakati za kifalme [ kumaanisha wakati wa Konstantine ] kwamba ni “umri wa miujiza’ ulikuwa umekamilika, kwa dhana kwamba viongozi wa Kikristo hawangeweza tena kueneza Injili, kama mitume, na msaada wa nguvu isiyo ya kawaida.”5
Kwa nini wakati ulimefika ambapo hakukuwa na miujiza tena na karama za Roho?-Kwa sababu mti uliozaa matunda, yaani Kanisa la Kristo, haukuwa tena duniani na imani ya watu ilididimia. John Wesley alibainisha ukosefu huu wa karama za Roho kutoka Kanisa katika siku zake: “Haikuonekana kwamba karama hizi za ajabu za Roho Mtakatifu zilikuwa za kawaida katika Kanisa kwa zaidi ya karne mbili au tatu.”6
Inatosha kusema, ninaweza kushuhudia, kama wengi wenu, kwamba hii ni siku ya miujiza na karama za Roho katika Kanisa la Urejesho la Kristo, kama vile ilivyokuwa katika Kanisa Lake la asili.
Kunalo tunda la tatu---mpango makini wa Kanisa la Kristo umeandikwa matukio mengi ya malaika na maono. Baadhi ya watu huangalia na shaka leo Kanisa linalodai malaika na maono, lakini kwa kutenda hivyo wanasahau kwamba malaika na maono yalikuwa sehemu muhimu ya Kanisa la asili la Kristo: malaika akimtangazia Mariamu kuzaliwa kwa Kristo; malaika wakiwajia Petro, Yakobo na Yohana kwenye Mlima wa Mabadiliko; malaika akimtoa Petro na Yohana kutoka gerezani; malaika akizungumza na Konekio; malaika akimuonya Paulo juu ya ajali ya wa meli iliyokuwa karibu kutendeka; malaika aliyemujia Yohana Mfunuzi; ono la Stefano la Baba na Mwana; ono la Yohana la siku za mwisho; na mengine mengi. Swali halipaswi kuwa “Ni vipi Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linaweza kuwa Kanisa la kweli na madai yake ya malaika na maono?” Badala yake, swali linapaswa liwe “ Kanisa lolote leo linawezaje kudai kuwa Kanisa la kweli la Kristo isipokuwa liwe na malaika na maono---kama tu vile ilivyokuwa katika Kanisa la Kristo la asili, kama tu vile ilivyofunuliwa katika mpango makini Wake?
Kuna matunda mengine mengi ambayo yako sambamba na Kanisa la asili la Kristo:
Lilikuwa kanisa la umisionari---Mitume wakiamuriwa “nendeni kwa hiyo, na kuwafundisha mataifa yote" (Mathayo 28:19). Leo tuna wamisionari zaidi ya 80,000 wakitimiza amri hiyo na kuzaa matunda ya kufanya hivyo.
Lilikuwa kanisa la maadili---mpango makini unatufundisha kwamba Watakatifu wa asili katika Kanisa la Kristo waliamuriwa wavalie mavazi ya kujisitiri na kujiepusha na mahusiano kabla ya ndoa. Ni makanisa mangapi hayafundishi tu viwango hivyo vya kimaadili bali pia kuviishi?
Kanisa la Kristo la asili likikuwa Kanisa lililo na msingi wa familia. Waume waliamuriwa wawapende na kuwa waaminifu kwa wake zao (ona Waefeso 5:23–25), watoto waliamuriwa kuwatii wazazi wao (ona Waefeso 6:1), na Maaskofu waliamriwa watawale vizuri nyumba zao (ona 1 Timotheo 3:4–5). Leo Kanisa letu, kama Kanisa la Kristo la asili, linatambuliwa kama Kanisa la kifamilia. Matunda ya Kanisa la Kristo yameandikwa kwa makini katika Biblia na yanalingana na Kanisa la Urejesho la Kristo leo.
Kristo alianzisha Kanisa Lake duniani, lakini ukurasa wa mwisho wa mpango makini unaonyesha lilikuwa na uhusiano na mbinguni---yaani, ufunuo wa kiungu. Bila uhusiano huu Kanisa lingekuwa si zaidi ya shirika linaloendeshwa na binadamu likitawaliwa na nguvu za dhana. Nabii Amos alitangaza, “Hakika Bwana Mungu hatafanya neno lo lote, bila kuwafunulia watumishi wake manabii siri yake.” (Amosi 3:7). Paulo alithibitisha kuwa ufunuo ulikuwa ni sehemu muhimu ya Kanisa na ulitarajiwa kuwa endelevu, kwani alitangaza: “Nitakuja kwa maono na mafunuo ya Bwana" (2 Wakorintho 12:1; ona pia Matendo ya Mitume 1:2).
Sambamba na mafundisho ya hayo ya msingi, Kanisa la Kristo leo linahusishwa na mbinguni kwa ufunuo unaoendelea. Tamko la Kanisa la imani katika suala hili, linalojulikana kama makala ya tisa ya imani, inasema ifuatavyo: “Tunaamini yale yote Mungu ameyafunua, na ambayo sasa anafunua, na tunaamini kwamba bado Yeye atayafunua mambo mengi makuu na muhimu yahusuyo Ufalme wa Mungu.”
Kama mtu angelinganisha mpango wa Kanisa la Kristo la asili dhidi ya kila kanisa duniani leo, angepata kwamba hatua kwa hatua, mpangilio kwa mpangilio, fundisho kwa fundisho, agizo kwa agizo, matunda kwa matunda, na ufunuo kwa ufunuo, litalinganishana tu na moja--Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Ikiwa mtu atakana Kanisa hili baada ya kusoma mpango makini, basi huenda itamuharibia kwa ajili ya kanisa lolote lingine kwa sababu anajua zaidi. Atakuwa kama Petro, ambaye aliulizwa na Mwokozi, “Je, Ninyi nanyi mwataka kuondoka? " (Yohana 6:67). Petro alijibu kwa jibu ambalo linapaswa lichapishwe katika kila moyo na litambulike katika kila nyumba: “Tuende kwa nani? Wewe unayo maneno ya uzima wa milele” (Yohana 6:68).
Mtu akigeuka kutoka Kanisa, ataenda wapi ili kujifunza kuhusu kweli zilizorejeshwa kuhusu asili ya Mungu kama ilivyofunuliwa katika Sacred Groove, ukamilifu zaidi wa Upatanisho kama ilivyofunzwa katika Kitabu cha Mormoni, mahubiri ya Injili kwa wafu, viwango vya utukufu, na familia ya milele? Ataenda wapi ili kupata maagizo ambayo yanaweza kumwokoa na kumwinua? Ataenda wapi ili kuunganishwa na mke wake na watoto wake milele? Ataenda wapi atakapotaka baraka ya ukuhani ya faraja ama uponyaji kwa ajili wa mwana familia? Ataenda wapi ili kupata nabii wa Mungu? Atatafuta bila kupata mafundisho hayo na maagizo hayo na nguvu hizo na manabii hao, kwa kuwa ni ya kipeeke tu katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Mtu hawezi kuwa na mafundisho na maagizo kama yalivyorejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith bila ya kumkubali Joseph Smith na historia ya msingi ambayo ni msingi wa hayo. Hayawezi kutenganishwa. Yanaandamana. Huwezi kuyaita matunda mema na kisha kuuita mti mbaya. Mwokozi aliufundisha ukweli huo kitambo: “mti mwema hauwezi kuzaa matunda mabaya, wala mti mbaya hauwezi kuzaa matunda mazuri " (Mathayo 7:18). Ipasavyo, kama tunda la kimafundisho tuliyojadili usiku wa leo ni jema, basi mti ambao kwake yametoka---Joseph Smith na historia ya msingi inayoandama kweli hizo zilizofunuliwa---vile vile ni mwema. Huwezi kuwa na moja bila nyingine.
Katika hotuba ya mkutano mkuu, miaka michache iliyopita, Mzee B. H. Roberts alizungumzia mafanikio ya Joseph Smith, na kisha, na kama alikuwa akiwazungumzia wakosoaji wa Joseph, alisema: “Yafikieni! Yafikieni! Nasema, ama na mkono mmoja kwenye midomo bakini mmenyamaza jina lake linapotajwa.”7
Wasiwasi ya kihistoria au kijamii ambayo wengine huenda wakawa nayo, madai ya migogoro ya kisayansi---haya ni matukio ya kando; kituo cha kati ni mafundisho, maagano, nguvu ya ukuhani, na matunda mengine ya Kanisa letu, mengi ambayo yamejadiliwa usiku wa leo. Lakini wengine wanaweza kujibu, “Naamini haya yote, lakini nawezaje kukabiliana na wakosoaji na maswali yao mahususi?”
Wakili anajua kwamba baada ya mwendesha mashtaka kuwasilisha shahidi wake muhimu, kesi dhidi ya mshtakiwa imetupwa katika mwanga wake mbaya kabisa. Mtu aliye na haraka kutoa hukumu katika hatua hiyo huenda akaamua mshtakiwa ana hatia, lakini kisha jambo la kuvutia hutokea katika chumba cha mahakama. Mshtakiwa huanza hoja kwake shahidi yule yule, na yafuatayo hutendeka mara nyingi: majibu halisi wa shahidi huanza kudidimia chini ya shinikizo la kuhojiwa. Shahidi aliyeonekana kutoweza kushindwa sasa ana baadhi ya mambo yasiyosawa na pengine hata mashimowazi katika kukumbuka matukio. Hadithi iliyoonekana kuwa dhabiti ya shahidi huanza kuvunjikana na kubomoka kwa kila swali jipya aulizwalo. Shahidi alikuwa na uwezo wa kuhimili maswali rahisi ya mwendesha mashtaka wake lakini wakati maswali magumu ya upinzani yalipokuja, hangehimili kiwango chao au asili ya uchunguzi. Wakati mahojiano yanapokamilika shahidi haaminiwi kwa kiwango kikubwa. Mtazamaji ambaye awali alikuwa tayari “kuhukumu” mshtakiwa sasa anaona kwa macho tofauti kutokuwa na hatia yoyote ya mtu yule.
Vile vile, baadhi ya wakosoaji hutupa maswali ya upande mmoja kwa Kanisa ambayo yananuiwa kuweka Kanisa katika mwanga wake mbaya iwezekanavyo. Lakini huegemea upande zote.8 Mashahidi wakuu wa mwendesha mashitaka hawana kinga dhidi ya mahojiano, na wala si wakosoaji wakali kabisa wa Kanisa. Sijawahi kupata mpinzani yeyote ambaye angeweza kunipa majibu ya kuridhisha kwenye “mahojiano” kwa maswali yafuatayo:
Kwanza, Joseph Smith alijuaje kurejesha mafundisho na maagizo kutoka kwa Bibilia, kama vile mafundisho ya uwepo kabla ya maisha duniani, asili ya kweli ya Mungu, injili kuhubiriwa kwa wafu, ubatizo kwa wafu, na mengine mengi yaliyojadiliwa usiku wa leo, wakati mafundisho na maagizo kama hayo hayakuwa yanafundishwa na makanisa mengine ya kisasa ya wakati wake? Kwa nini Joseph Smith alikuwa aliyeyagundua na kuyarejesha pekee yake? Hata ikiwa anazingatiwa kuwa mashuhuri kiteolojia, hakukuwa na watu wengine shuhuri kama yeye katika miaka 1800 kufuatia ushiriki ya Mwokozi ambao wangeweza kufanya vile vile?
Pili, ikiwa Kanisa hili si Kanisa la Kristo, basi kwa nini Kanisa hili lina matunda yale yale kama ya Kanisa la Kristo la asili, yaani, miujiza na karama za Roho, ufunuo wa kisasa kutoka kwa mitume na manabii, malaika na maono, watu wenye afya mzuri, watu wenye maadili, watu wenye nia ya umisionari, na watu ambao wanatilia mkazo kwa kila familia? Mwokozi hakutangaza “kwa matunda yao mtawatambua” (Mathayo 7:20).
Hakika, maswali mengi zaidi katika mahojiano yanaweza kuulizwa. Kuna baadhi ya maswali, hata hivyo, ambayo yanashinda na kuvuka mengine yote---kikweli yanaunda msingi wa swala. Yatosha kusema, maswali mengine yana umuhimu tu zaidi ya mengine katika kugundua ukweli. Ukija kujua kwamba Joseph Smith alirejesha mafunzo na maagizo ya bibilia yaliyorejelewa hapo awali, ukija kujua kwamba Kanisa la Yesu Kristo la Watakatiu wa Siku za Mwisho lina matunda yale yale kama Kanisa la Kristo asili, ama ukija kujua kwamba Kitabu cha Mormoni ni cha asili ya kiungu, basi unajua kwamba Joseph Smith ni nabii. Na ikiwa Joseph Smith ni nabii, basi hili ndilo Kanisa la pekee lililo la kweli na hai duniani mzima---maswali mengine yote ni dhaifu kwa kulinganishwa. Ni kama hukumu ya Mahakama Kuu juu ya swala. Kufikia hapo, maamuzi yote ya mahakama ya chini yaliyo kinyume, maswali yote ya wakosoaji, yawe magumu aje ama kukanganya ama kufurahisha, si sababu kuu tena katika swali la ukweli. Kwa nini? Kwa sababu tayari umejibu maswali ya muhimu---maswali yale muhimu-ambayo ni nguzo ya msingi ya kujua ukweli.
Yatosha kusema, ninaweza kuuishi na mapungufu michache ya kibinadamu, hata miongoni mwa manabii wa Mungu---hilo ni jambo la kutarajiwa katika viumbe vya duniani. Ninaweza kuishi na madai machache ya matokeo kisayansi kinyume na Kitabu cha Mormoni; muda utabadilisha hayo. Na ninaweza kuishi na kasoro chache za kihistoria; ni ndogo katika mazingira ya jumla ya ukweli. Lakini siwezi kuishi bila kweli za mafundisho na maagizo zilizorejeshwa na Joseph Smith, Siwezi kuishi bila ukuhani wa Mungu kubariki familia yangu, na siwezi kuishi bila kujua mke wangu na watoto wameunganishwa nami milele. Hii ndio chaguo tunayokumbana nalo---maswali machache yasiyojibiwa kwa upande mmoja na wingi wa mafundisho dhabiti na nguvu ya Mungu kwa upande mwingine. Na kwangu mimi, na natumahi kwenu ninyi, chaguo ni rahisi na sawa kimantiki.
Nashuhudia kwamba Kanisa ambalo siku moja mtasimamia lina jina la Kristo kwa sababu hakika lina Mpangilio wake ulioidhinishwa, mafunzo Yake, maagizo Yake, nguvu Zake, matunda Yake, na ufunuo Wake endelezi, yote ambayo yanarejelewa katika mpango makini wake mtukufu. Tuwe na macho ya kiroho ili kuona ukaribiano kati ya mpango makini na Kanisa la urejesho la Kristo leo, kwani ni mmoja wa ushahidi wa kuvutia wa Mungu kwetu. Kwa haya ninashuhudia na kuomba katika jina la Yesu Kristo, amina.
© 2014 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Kiingereza kiliidhinishwa: 9/13. Tafsiri iliidhinishwa: 9/13. Tafsiri ya What Is the Blueprint of Christ’s Church? Lugha. PD50051805 743