Kuokoa Misha Yako
Mkutano wa Ibada wa MEK kwa Vijana Wazima • Septemba 14, 2014 • Chuo Kikuu cha Brigham Young
Wakati Yesu na Mitume wake walikuwa pamoja katika Kaisarea Filipi, aliwauliza swali hili, “Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?” 1 Petro, na ufasaha wa uchaji na nguvu, alijibu, “Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.” 2 Inanifurahisha kusoma maneno hayo; inanifurahisha kuyasema. Muda mfupi baada ya wakati huu mtakatifu, hata hivyo, Yesu alizungumza na Mitume juu ya kifo chake kilichokuwa njiani na ufufuo, na Petro akakinzana Naye. Hii ilimzalia Petro makemeo makali kwamba hakuwa na uwiano na, ama hakuwa “anayawaza” mambo ya Mungu “bali mambo ya wanadamu.” 3 Kisha Yesu, “akionyesha baadaye ongezeko la upendo kwa yule [Alikuwa] amekemea,” 4 kwa upole alimuelekeza Petro na Ndugu zake juu ya kuchukua msalaba wa mtu binafsi na kupoteza maisha ya mtu kama njia ya kupata uzima tele na wa milele, Mwenyewe akiwa mfano kamili. Hebu tuangalie onyesho la tukio hili katika mojawapo ya video za Biblia iliyotengenezwa na Kanisa.
Yesu: Imempasa Mwana wa Adamu kupatikana na mateso mengi, na kukataliwa na wazee, na wakuu wa makuhani, na waandishi, na kuuawa, na baada ya siku tatu kufufuka.
Petro: Hasha, Bwana, hayo hayatakupata.
Yesu: Nenda nyuma yangu, Shetani; u kikwazo kwangu; maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu. Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate. Kwa kuwa mtu atakaye kuiokoa nafsi yake, ataipoteza; na mtu atakayepoteza nafsi yake kwa ajili yangu, ataiona. Kwani atafaidiwa nini mtu akiupata ulimwengu wote, na kupata hasara ya nafsi yake? Au mtu atatoa nini badala ya nafsi yake? Kwa sababu Mwana wa Adamu atakuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika zake; ndipo atakapomlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake. 5
Nataka kuzungumza nanyi juu ya tamko la Bwana linaloonekana kana kwamba ni kinyume kuwa “Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona.” 6Linafundisha fundisho la nguvu, la kina ambalo tunahitaji kuelewa na kutumia.
Profesa mwangalifu alitoa umaizi huu: “Kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kazi ya Mungu katika maisha yako ni kubwa kuliko hadithi ungependa maisha hayo yaseme. Maisha yake ni makubwa kuliko mipango yako, malengo, au hofu. Kuokoa maisha yako, itabidi uweke chini hadithi zako na, dakika kwa dakika, siku kwa siku, urudishe maisha yako Kwake.”7
Zaidi ninavyofikiria juu ya jambo hili, ndivyo zaidi ninashangazwa na jinsi mara kwa mara Yesu alitoa maisha yake kwa Baba, jinsi gani kikamilifu alipoteza maisha yake katika mapenzi ya Baba---katika maisha na kifo. Hii hasa ni kinyume cha mtazamo na mbinu za Shetani, ambazo zimekubaliwa sana katika dunia ya ubinafsi ya leo. Katika baraza la maisha kabla ya maisha duniani, katika kujitolea kujaza nafasi ya Mwokozi katika mpango wa kiungu wa Baba, Yesu alisema, “Baba, mapenzi yako yafanyike, na utukufu uwe wako milele.” 8 Lusiferi, kwa upande mwingine, alisema, “Tazama, mimi hapa, nitume, mimi nitakuwa mwanao, nami nitawakomboa watu wote, ili nafsi moja haitapotea, na hakika mimi nitafanya hivyo; kwa hivyo nipemimi heshima yako.” 9
Amri ya Kristo ya kumfuata ni amri ya kukataa kwa mara nyingine tena mfano wa Kishetani na kupoteza maisha yetu,, badala ya maisha ya kweli, maisha halisi, maisha yanayoelekeza ufalme wa selestia ambayo Mungu amempangia kila mmoja wetu. Maisha hayo yatabariki kila mtu tumgusaye na yatatufanya tuwe watakatifu. Na uono wetu wa sasa, uliopungukiwa, na ufahamu, ni maisha ambayo yanazidi ufahamu. Hakika “jicho halijapata kuyaona, wala sikio kuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao.” 10
Natamani tunagekuwa na mazungumzo zaidi kati ya Yesu na wanafunzi Wake. Ingekuwa na msaada kuwa na umaizi kuhusu kile inamaanisha, kwa kutenda, kupoteza maisha yako kwa ajili Yake na kwa hivyo kuipata. Lakini nilipotafakati juu yake, nilitambua kwamba maneno ya Mwokozi tu kabla na baada ya tamko Lake linatoa miongozo ya dhamani. Tuzingatie vipengele vitatu.
Ajikane Mwenyewe, Ajitwike Msalaba Wake Kila Siku
Kwanza ni maneno ya Bwana yaliyosemwa mara tu kabla Yeye kusema, “Mtu yeyote akitaka kuokoa maisha yake, atayapoteza.” 11 Kama ilivyoandikwa katika kila moja ya muhtasari wa injili, Yesu alisema, “Mtu yeyote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake, anifuate.” 12 Luka anaongeza neno kila siku---“basi ... ajitwike msalaba wake kila siku.” 13 Katika Mathayo, Tafsiri ya Joseph Smith inaongezea kauli hii na ufafanuzi wa Bwana wa kile kinachomaanisha kujitwika maslaba wako mwenyewe: “Na sasa kwa mtu kujitwika msalaba wake, ni kujikana mwenyewe uasi wote, na kila tamaa ya kidunia, na kuzishika amri zangu.” 14
Hii inaambatana na tamko la Yakobo: “Dini iliyo safi, isiyo na taka mbele za Mungu Baba ni hii, Kwenda kuwatazama yatima na wajane katika dhiki yao, na kujilinda na dunia pasipo mawaa.” 15 Ni maisha ya kila siku ya kuepuka yote yaliyo machafu kwa uamuzi ukiweka amri mbili kubwa---upendo wa Mungu na jirani---ambapo amri zingine zote zimo. 16 Hivyo basi, moja ya kipengele cha kupoteza maisha yetu badala ya maisha makuu Bwana ametupangia yamo katika kujutwika msalaba Wake siku baada ya siku.
Mtu Atakayenikiri, Nami Nitamkiri mbele za Baba
Kauli inayoandamana ya pili inapendekeza kwamba kupata maisha yetu kwa kuyapoteza kwa ajili Yake kunajumuisha kutaka kufanya uanafunzi wetu kuwa wazi na hadharani: “Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu.” 17
Kwingineko katika Mathayo, tunapata kauli ambatanishi:
“Kila mtu atakayenikiri mbele ya watu, nami nitamkiri mbele za Baba yangu aliye mbinguni.
Bali mtu ye yote atakayenikana mbele ya watu, nami nitamkana mbele za Baba yangu aliye mbinguni.” 18
Maana moja ya wazi, na ya kutisha ya kupoteza maisha yako kwa kumkiri Kristo ni kuyapoteza kwa kweli, kimwili, katika kuendeleza na kutetea imani yako Kwake. Tumezoea kufikiria juu ya mahitaji haya yaliokithiri kama kutumika katika historia tunaposoma kuhusu wafa mashahidi wa siku za nyuma, ikiwa ni pamoja na wengi wa Mitume wa kale. Sasa tunaona, hata hivyo, kwamba kile kilichokuwa ni cha kihistoria kinasonga kwa wakati wa sasa. Taarifa za habari kutoka Iraq na Syria zinazungumzia mamia ya Wakristo na wachache wengine wakiondolewa kutoka makazi yao ama kuuawa na Waislamu wenye msimamo mkali katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita. Magaidi hudai kwamba Wakristo hawa wabadilishe kuwa wa muundo wa imani yao yaUislamu ama wahame vijiji vyao ama wafe. Itakuwa vigumu kwa wakristo kumkana Yule, wengi wamekimbia na baadhi wameuliwa. 19 Hakika nafsi kama hizo zitakuwa kati ya zile ambazo Mwokozi hataaibika kukiri mbele za Baba yake katika siku ya baadaye. Hatujui kile huenda kikaja katika siku zijazo, lakini ikiwa yeyote kati yetu atalazimika kukumbana na kiwewe ya kupoteza maisha yetu kwa kweli katika shughuli ya Mwalimu, naamini tunafaa kuonyesha ujasiri huo huo na uaminifu.
Matumizi ya kawaida (na wakati mwingine yaliyomagumu zaidi) ya mafundisho ya Mwokozi, hata hivyo, yanahusiana na jinsi tunavyoishi siku baada siku. Yanahusiana na maneno sisi husema, mfano sisi huweka. Maisha yetu yanapaswa kumkiri Kristo, na pamoja na maneno yetu yashuhudie imani Kwake na kujitolea Kwake. Na ushuhuda huu lazima utetewe kwa ujasiri mbele ya kejeli, ubaguzi, ama kashfa kwa upande wa wale ambao wanampinga Yeye “katika kizazi hiki kiovu.” 20
Kwa wakati tofauti Bwana aliongeza kauli hii ya ajabu kuhusu uaminifu wetu Kwake:
“Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.
“Kwa maana nilikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu.
“Na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.
“Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.
“Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.” 21
Akisema kwamba hakuja kuleta amani, lakini badala yake upanga, inaonekana katika hisia ya kwanza kinyume na maandiko yanayomzungumzia Kristo kama “Mkuu wa Amani,” 22 na tangazo katika kuzaliwa Kwake, “Utukufu kwa Mungu juu mbinguni, na amani duniani, watu aliopendezwa nao,” 23 na marejeo mengine yanayojulikana vyema, kama vile, “Amani nawaachieni, amani yangu nawapa.” 24 “Ni kweli kwamba Kristo alikuja kuleta amani---amani kati ya muumini na Mungu, na amani miongoni mwa binadamu. Hata hivyo matokeo yasiyoepukika ya kuja kwa Kristo ni vita---kati ya Kristo na mpinga Kristo, kati ya nuru na giza, kati ya watoto wa Kristo na watoto wa ibilisi. Mgogoro huu unaweza kutokea hata kati ya wanafamilia moja.” 25
Nina uhakika kwamba idadi ya ninyi mlio miongoni mwa watazamaji wetu duniani kote jioni hii mmepitia kibinafsi kile Bwana anaelezea katika mistari hii. Mlikataliwa na kutengwa na baba na mama zenu, ndugu na dada mlipokubali injili ya Yesu Kristo na kuingia katika agano Lake. Katika njia moja au nyingine, upendo wako mkuu wa Kristo umehitaji dhabihu ya mahusiano ambayo yalikuwa muhimu kwenu, na mmemwaga machozi mengi. Hata hivyo pamoja na upendo wenu wenyewe usiopunguka, mmeshikilia kwa nguvu chini ya msalaba huu, mkijionyesha kutokuaibisha na Mwana wa Mungu.
Karibu miaka mitatu iliyopita mshiriki wa Kanisa alishiriki nakala ya Kitabu cha Mormoni pamoja na rafiki aliyekuwa Muamishi kule Ohio. Rafiki alianza kusoma kitabu na hakuweza kukiweka chini. Kwa siku tatu hakuwa na tamaa nyingine ila kukisoma Kitabu cha Mormoni. Yeye na mke wake walibatizwa, na kwa muda wa miezi saba kulikuwa na wanandoa watatu wa Kiamishi waongofu na wanachama wa Kanisa waliobatizwa. Watoto wao walibatizwa miezi kadhaa iliyofuata. Familia hizi tatu ziliamua kubaki katika jamii yao na kuendelea maisha yao ya Kiamishi ingawa walikuwa wameiacha imani ya Kiamishi. Hata hivyo, kwa sababu ya kubatizwa, walikabiliwa na “kuepukwa” na majirani wao wa karibu. Kuepukwa kunamaanisha kwamba hakuna yeyote katika jamii yao ya Kiamishi angezungumza nao, angefanya kazi pamoja nao, angefanya biashara pamoja nao, au kushiriki pamoja nao kwa njia yoyote. Hii inajumuisha si tu marafiki, lakini wanafamilia---kina ndugu na dada, wazazi na mababu.
Awali, Watakatifu hawa wa Kiamishi walihisi upweke na kutengwa kwani hata watoto wao walikuwa wanakabiliwa na uepukwaji na kuondolewa kutoka shule zao za Kiamishi kwa sababu ya ubatizo wao na ushiriki katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Watoto wao wamevumilia kuepukwa na mababu na binamu na majirani wa karibu. Hata baadhi ya watoto wakubwa wa familia hii ya Kiamishi ambao hawakukubali injili hawangezungumza, kushirikiana, au hata kuwatambua wazazi wao. Familia hizi zimesumbuka kutokana na athari za kijamii na kiuchumi za kuepukwa, lakini zimefanikiwa.
Imani yao imebaki imara. Shida na upinzani wa kutengwa zimewasababisha kuwa imara na kutotingisika. Mwaka baada ya kubatizwa, familia hizi zilifunganishwa katika hekalu na wanaendelea kwa uaminifu kuhudhuria hekalu kila wiki. Wamepata nguvu kwa kupokea maagizo na kuingia katika maagano na kuheshimu maagano. Wote wanashughulika kikamilifu katika kundi lao la Kanisa na wanaendelea kutafuta njia za kushiriki nuru na maarifa ya Injili na familia zao na jamii kupitia vitendo vya wema na huduma.
Ndiyo, gharama ya kujiunga na Kanisa la Yesu Kristo inaweza kuwa ya juu sana, lakini mawaidha kupendelea Kristo juu ya wengine wote, hata wanafamilia wetu wa karibu, yanatumika pia kwa wale ambao huenda walizaliwa katika agano. Wengi wetu huwa washiriki wa Kanisa bila upinzani, labda kama watoto. Changamoto tunayoweza kukabiliana nayo ni kubaki kuwa waaminifu kwa Mwokozi na Kanisa Lake mbele ya wazazi, wakwe, ndugu, au dada, au hata watoto wetu ambao maadili, imani, au uchaguzi wao unafanya kuwa vigumu kumsaadia Yeye na wao. Si suala la upendo. Tunaweza na lazima tupendane kama Yesu anavyotupenda. Kama alivyosema Yeye, “Hivyo watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu, mkiwa na upendo moja kwa mwingine” 26 Lakini, Bwana anatukumbusha, “Ampendaye baba au mama yake kuliko anipendavyo mimi hanistahili; naye ampendaye mwana au binti kuliko anipendavyo mimi hanistahili.” 27 Hivyo, ingawa upendo wa kifamilia unaendelea, mahusiano yanaweza kukatizwa na, kulingana na mazingira, hata msaada au kuvumiliana wakati mwingine kusimamishwa kwa ajili ya upendo wetu mkuu.
Kwa kweli, njia bora ya kuwasaidia wale tunaowapenda---njia bora ya kuwapenda---ni kuendelea kumweka Mwokozi kwanza. Tukijitupa mbali kutoka kwa Bwana kwa ajili ya huruma kwa wapendwa ambao wanateseka au kufadhaika basi tunapoteza njia ambayo tungeweza kuwasaidia. Tukibaki, hata hivyo, imara katika imani katika Yesu, tuko katika nafasi kupokea na kutoa msaada wa Mungu. Ikiwa (au niseme wakati) wakati unakuja ambapo mpendwa mwanafamilia anataka mno kurejea kwa chanzo cha kweli na cha kudumu, yeye atajua nani wa kuamini kama mwongozo na rafiki. Kwa sasa, pamoja na karama ya Roho Mtakatifu kuongoza, tunaweza kufanya huduma ya kutosha kupunguza maumivu ya chaguo baya na kumfunga majeraha kadiri tunavyoruhusiwa. Vinginevyo, hatutumikii wale tunaowapenda wala sisi wenyewe.
Kwa Kuwa Itamfaidi Mtu Nini Kuupata Ulimwengu Wote, Akipata Hasara ya Nafsi Yake?
Sehemu ya tatu ya kupoteza maisha yetu kwa ajili ya Bwana ambayo nataka kutaja inapatikana katika maneno ya Bwana,
“Na atakayeyapoteza maisha yake katika ulimwengu huu, kwa ajili yangu, atayapata katika ulimwengu ujao.
Kwa hivyo, acheni dunia, na okoeni nafsi zenu; kwa nini, mtu atafaidi yeye kuupata ulimwengu wote na kuyapoteza maisha yake mwenyewe? Au mtu atatoa kitu gani badala ya maisha yake” 28
Au ilivyo katika Tafsiri ya Joseph Smith Kwani yamfaa mtu nini kama atapata ulimwengu wote, na bado hampokei yule Mungu amemtakasa, na apoteza nafsi yake, naye mwenyewe kuwa mtengwa?” 29
Kusema kwamba kuacha dunia katika neema ya kumpokea “yeye ambaye Mungu aliyemteua” ni kinyume cha kile kilicho wazi katika dunia ya leo ni hakika upungufu wa himizo. Vipaumbele na maslahi mara nyingi tunayoona karibu nasi (na wakati mwingine ndani yetu) ni ya kibinafsi sana: tamaa ya kutambuliwa; sisitizo kwamba haki za mtu fulani ziheshimiwe (ikiwa ni pamoja na haki inayodhaniwa kamwe usikasirishwe); hamu inayoangamiza ya fedha, vitu, na uwezo; hisia ya haki kwa maisha ya faraja na furaha; lengo la kupunguza wajibu na kuepuka kabisa dhabihu yoyote ya binafsi kwa ajili ya mema ya mwingine; kutaja machache tu.
Hii si kusema kwamba hatupaswi kutafuta kufanikiwa, hata kuhitimu katika juhudi za kustahili, ikiwa ni pamoja na elimu na kazi ya heshima. Mapema mwaka huu, Jed Rubenfeld na Amy Chua, ambao ni mume na mke maprofesa katika Yale Law School, walichapishwa kitabu chenye jina The Triple Package: How Three Unlikely Traits Explain the Rise and Fall of Cultural Groups in America. Tasnifu yao ni kwamba baadhi ya vikundi katika Amerika vinafanya vizuri zaidi kuliko vingine kulingana na sifa tatu za kitamaduni, zikielezwa katika kitabu, vitu vinavyopatia vikundi hivi . Chua na Rubenfeld wanatambua Wamormoni, Wayahudi, Waasia, wahamiaji kutoka Afrika Magharibi, Wahindi---Wamarekani, na Wakuba---Wamarekani kama vikundi katika Amerika vilivyo na sifa hizi leo.30
Wakilinganisha vikundi hivi na jamii ya Marekani kwa ujumla juu ya vitu kama vile “kipato, elimu, uongozi wa kampuni, ustaarabu, na viwango vingine vya kawaida," Chua na Rubenfeld wanasema,
“Kama kuna kikundi kimoja katika Marekani ambacho kina fuzu kwa uwazi na mafanikio ya kawaida, ni Wamormoni. …
Wakati Waprotestanti wanafikia asilimia 51 ya idadi ya watu Marekani, Wamormoni wa Amerika walio kati ya milioni 5 na 6 wanawakilisha asilimia 1.7 tu. Hata hivyo idadi kubwa ya kushangaza imepanda juu ya nyanja za mashirika na siasa Amerika.”31
Hakika mafanikio hayo yanafaa kupongezwa, lakini ikiwa tutaokoa maisha yetu, ni lazima daima tukumbuke kwamba mafanikio hayo si hitimisho lenyewe, bali njia ya kufikia maana ya mwisho ya juu. Katika imani yetu, lazima tuone mafanikio ya kisiasa, kibiashara, kielimu, na ya aina sawa si kama yanatubainisha bali yanawezesha utumishi wetu kwa Mungu na jirani---kuanzia nyumbani na kuendelea mbali iwezakanavyo duniani. Maendeleo ya kibinafsi yana thamani kwa vile yanachangia katika kukuza sifa za kama Kristo. Katika kupima mafanikio, tunatambua ukweli wa kushangaza ulio msingi wa yote---kwamba maisha yetu ni mali ya Mungu, Baba yetu wa Mbinguni, na Yesu Kristo, Mkombozi wetu. Mafanikio yanamaanisha kuishi kwa amani na mapenzi Yao.
Kinyume na maisha ya ubinafsi, Rais Spencer W. Kimball alitoa elezo rahisi la njia bora zaidi:
“Huduma kwa wengine inaongeza maana na uzuri wa maisha haya wakati tunajiandaa kuishi katika ulimwengu bora. …Tunaposhiriki katika huduma ya wanadamu wenzetu, matendo yetu hayawasaidii tu, lakini tunaweka matatizo yetu wenyewe katika mtazamo mpya zaidi. Tunapowajali wengine zaidi, kuna muda kidogo kujijali wenyewe! Katikati mwa muujiza wa kuhudumu, kuna ahadi ya Yesu kwamba kwa kujipoteza wenyewe, tunajipata wenyewe! [Ona Mathayo 10:39]
“Hatujipati tu wenyewe kwa njia ya kutambua mwongozo wa kiungu katika maisha yetu, lakini zaidi tunavyowatumika wenzetu katika njia sahihi, ndipo tunapata maana zaidi katika nafsi zetu.Tunapata maana zaidi maishani mwetu tunapowatumikia wengine---kweli, ni rahisi 'kujipata' wenyewe kwa sababu kuna mengi zaidi ya sisi kupata!” 32
Mifano ya Kupoteza Maisha Yako katika Kristo na Injili Yake
Acha nifunge na mifano michache ya kile kinachomaanisha kwa maisha ya kila siku kupoteza maisha yako katika Kristo na injili Yake na hivyo basi kupata maisha ya maana na (hatimaye uzima wa milele).
Rais Henry B. Eyring alikuwa rais wa Ricks College, iitwayo Chuo Kikuu cha Brigham Young---Idaho kwa sasa, mnamo Juni 1976, wakati Bwawa la Teton lilikamillika, si mbali na Rexburg, lilibomoka. “Galoni bilioni themanini ya maji zilivuma kuelekea Rexburg kwa kasi ya maili arobaini kwa saa, yakisomba mbali kila kitu katika njia.” 33 Watu wengi katika jamii walijibu kwa ushujaa, kuwasaidia wengine hata wakati nyumba zao wenyewe na mali zilikuwa zinaharibiwa na mafuriko. Wachache, hata hivyo, walitekeleza hata wapendwa wao na kuwaacha na kujitunza wenyewe.
Rais Eyring, ambaye yeye mwenyewe alisaidia kuongoza juhudi kuu za msaada, alitaka kuelewa ni nini kilichangia tofauti kati ya vitendo vya kishujaa wa baadhi ya watu na usaliti wa wengine. “Alianzisha utafiti mdogo wa kisayansi lakini wa muhimu. ‘Kulikuwa na jambo moja tu tugeweza kupata,’ baadaye aliliambia darasa la kufuzu shule ya upili.
“Wale ambao walikuwa mashujaa walikuwa watu ambao daima walikumbuka na kuweka ahadi katika mambo madogo, mambo ya kila siku … ahadi ya kubakia baada ya chakula cha jioni kanisani ili kusafisha, au kuja kufanya kazi katika mradi Jumamosi kusaidia jirani.
‘“Wale ambao walitoroka familia zao wakati kulikuwa na shida walikuwa mara nyingi wametoroka majukumu yao wakati hayakuwa magumu sana. Walikuwa na muundo wa kushindwa kuweka neno lao kufanya mambo madogo wakati dhabihu kwao ingekuwa kidogo na kufanya yale waliyosema wangefanya ingekuwa rahisi. Wakati gharama ilikuwa juu, hawangeweza kuilipa. ’”34
Dada Christofferson nami tulikuwa na rafiki tuliyekutana wakati wa siku za shule ya sheria, mshiriki wa kata yetu katika Durham, North Carolina. Yeye na mume wake walikuwa wenzi bora vijana wenye watoto wadogo. Alibarikiwa na akili, urembo, na utu wa kung’aa. Kila mtu alimpenda na kufurahia kuwa karibu naye. Miaka 25 baadaye, hata hivyo, wakati alikuwa bado katika miaka yake ya 40, alishambuliwa na saratani ya tumbo iliyoenea kwa haraka ambayo haikuwa na tiba, iliyoenea pia kwenye maini na mapafu yake. Licha ya mshtuko na maumivu maisha yake yalipokaribia ukingoni, aliandika maneno haya kwa familia yake na marafiki, ambao alijuta sana kuwaacha: Mpango wa [Mungu] ni wa kiuungu na unaendelea alivyopanga. Kwa vile nimeteule kupitia jaribio hili, najua kwamba lazima liwe ni nufaa kuu kwangu na furaha kuu. Tayari, baraka za kiroho zaja, na ninahisi kwamba kabla ya mwisho nitapitia yale yote ninayohitaji ili kujiandaa kukutana na Mwokozi wangu. Nguvu zake ziko duniani. Hakuna makosa. … Majaribio ni mengi na mazito kwa sasa. Kila mmoja anaonekana kuteseka kutoka mateso yake mwenyewe. Mtazamieni Bwana na mpokee msaada wake. Kubalini yale mambo ambayo ni yenu na maumivu yatachukuliwa kutoka kwenu, na amani itakuja.”
Dada fulani kijana mzima aliamua kuhudumu misheni ya muda baada ya kuhitimu shahada ya kwanza na ya pili na baada ya kushiriki katika kazi za kifahari na masomo nyumbani na ng’ambo. Yeye alikuwa amekuza uwezo wa kuungana na kuhusiana na watu kutoka karibu kila mfumo wa imani, ushawishi wa kisiasa, na utaifa, na yeye akiwa na wasiwasi kwamba akivaa tagi ya jina ya mmisionari siku nzima, kila siku ingeweza kuwa kitambulisho ambacho kinaweza kuzorotesha uwezo wake wa kipekee kwa kuanzisha mahusiano. Wiki chache tu ndani ya misheni yake, yeye aliandika nyumbani juu ya uzoefu rahisi lakini wa maana: "Dada Lee nami tulimsugua dawa ya kupaka kwenye mikono ya mwanamke mzee yenye baridi yabisi---mmoja wetu kila upande---wakati sisi tumeketi katika sebule yake. Yeye hakutaka kusikiliza ujumbe wowote alisema, lakini hebu tuimbe, alipenda tukiimba. Asante tagi nyeusi ya jina ya mmisionari kwa kunipa leseni ya kuwa na uzoefu wa karibu sana na wageni kabisa.”
Kupitia mateso yaliyompata, Nabii Joseph Smith alijifunza kupoteza maisha yake katika huduma ya Bwana wake na Rafiki yake. Yeye wakati mmoja alisema, “Nilifanya hii iwe sheria yangu: Bwana akiamuru, tenda.”35Nadhani sote tungefurahia kujaribu kufikia kiwango cha Ndugu Joseph cha uaminifu. Hata hivyo, alilazimishwa wakati mmoja kufungwa kwa muda kwa miezi katika jela Liberty, Missouri, akiteseka kimwili lakini pengine zaidi kihisia na kiroho kwa vile hakuweza kumsaidia mke mpenzi wake, watoto wake, na Watakatifu walipokuwa wananyanyaswa na kuteswa. Ufunuo wake na maelekezo yake yalikuwa yamewaleta Missouri kuanzisha Sayuni, na sasa walikuwa wanafukuzwa kutoka makao yao katika majira ya baridi katika wilaya nzima. Licha ya hayo yote, katika hali hiyo katika jela hiyo, alitunga barua yenye maongozi kwa Kanisa ya ufasaha mwingi na kuinua nathari, sehemu ambayo sasa inajumuisha sehemu za 121, 122, na 123 za Mafundisho na Maagano, ikihitimisha na haya maneno, “Kwa furaha na tufanye mambo yote yaliyo katika uwezo wetu; na ndipo tusimame imara, kwa uhakika mkubwa, kuuona wokovu wa Mungu, na kwa mkono wake kufunuliwa.” 36
Bila shaka, mfano mkubwa wa kuokoa maisha ya mtu na kupoteza ni hii, “Baba yangu, ikiwa haiwezekani kikombe hiki kiniepuke nisipokunywa, mapenzi yako yatimizwe. " 37Kwa kutoa maisha yake, Kristo hakujiokoa Mwenyewe---Yeye aliokoa maisha ya kila mmoja wetu. Alifanya iwezekane kwetu kubadilishana kile ambacho bila hivyo kingekuwa hatimaye ni bure, kwa uzima wa milele.
Ushuhuda
Mandhari ya maisha ya Mwokozi yalikuwa “Nafanya siku zote yale yampendezayo [Baba]" 38Naomba kwamba mtaifanya kuwa mandhari ya maisha yenu.Mkifanya hivyo, mtaokoa maisha yenu.
Rafiki zangu wapendwa mtosheke na juhudi na mafanikio yenu yote kuweka matakwa Yake mbele. Msiaibike kwa ajili ya Kristo au injili Yake, na kuweni tayari kuweka chini vitu mnavyovipenda, mahusiano mnayoyapenda, na hata maisha yenyewe kwa ajili Yake. Lakini wakati mnaishi, acheni maisha yenu yawe sadaka. Jitwikeni msalaba wake kila siku katika utii, na huduma. Hizi ni athari na matunda ya imani yetu, katika jina la Yesu Kristo, Amina.
© 2014 na Intellectual Reserve, Inc. Haki zote zimehifadhiwa. Kingereza kiliidhinishwa: 1/14. Tafsiri iliidhinishwa : 1/14. Tafsiri ya “Saving Your Life.” Language. PD10051044 743