2010
Endelea Kuvumilia Kidogo
Januari 2010


Ujumbe wa Urais wa Kwanza, Januari 2010

Endelea Kuvumilia Kidogo

Mojawapo ya masomo yenye kudumu ya wakati wa Kirtland ni kwamba roho zetu zinahitaji malisho ya kila mara. Tunahitajika kukaa karibu na Bwana kila siku ikiwa tutastahimili shida ambazo sisi sote ni lazima tukumbane nazo.

Msimu wa joto uliopita mke wangu pamoja nami tuliwapeleka wajukuu wetu mapacha huko Kirtland, Ohio. Ilikuwa ni nafasi maalum na muhimu kwetu kwa kukaa pamoja nao kabla ya wao kuenda kwenye misheni zao.

Wakati wa matembezi yetu kule, tulijifundisha ili kuelewa vyema hali ya Nabii Joseph Smith na Watakatifu walioishi katika Kirtland. Kipindi hicho cha historia ya Kanisa kinajulikana kama wakati wa majaribu makali lakini pia wa baraka kuu.

Katika Kirtland Bwana alipeana kati ya ishara za ajabu za mbinguni na karama za kiroho ambazo ulimwengu huu haujawahi kuona. Sehemu sitini na tano za Mafundisho na Maagano zilipokelewa katika Kirtland na maeneo jirani—ufunuo ambao ulileta nuru mpya na elimu kuhusu maswala kama Urejeo wa Pili, kuhudumia wenye mahitaji, mpango wa wokovu, mamlaka ya ukuhani, Neno la Hekima, zaka, hekalu, na amri ya kujitolea.1

Ilikuwa ni wakati wa ukuaji wa ajabu wa kiroho. Ama kweli, Roho wa Mungu kama moto alikuwa anawaka. Musa, Eliya, na viumbe wengine wengi wa mbinguni walitokezea katika wakati huu, wakiwemo Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Mwokozi wa ulimwengu, Yesu Kristo.2

Moja kati ya ufunuo mwingi ambao Joseph alipokea katika Kirtland ulikuwa ni ufunuo aliouita “jani la mzeituni … lililochunwa kutoka kwa Mti wa Paradiso, ujumbe wa Bwana wa amani kwetu” (maelezo kwa M&M 88). Ufunuo huu wa ajabu unajumuisha mwaliko wa kuvutia, “Sogeeni karibu nami na Mimi nitasogea karibu na nyinyi; nitafuteni kwa bidii nanyi mtanipata” (M&M 88:63). Jinsi Watakatifu wa Kirtland walivyosogea karibu na Bwana, Yeye pia kwa kweli alisogea karibu nao, akimwagia baraka za mbinguni vichwani mwa watakatifu.

Mbubujiko wa Kiroho

Pengine matokeo makuu ya ishara hizi za kiroho zilitendeka wakati wa kuwekwa wakfu kwa Hekalu ya Kirtland mnamo Marchi 27, 1836. Mmoja wa wale waliokuwemo alikuwa ni William Draper wa umri wa miaka ishirini na nane, aliyeelezea siku hio kama “siku ya Pentekoste.” Aliandika: “Kulikuwa na wakati wa mbubujiko wa Roho wa Bwana, ambao kalamu yangu haitoshi kuuandika yote kwa kirefu au ulimi wangu kuuelezea. Lakini hapa nitasema kwamba Roho alimwagwa na akaja kama upepo mkali unaovuma sana na kujaza hio nyumba, hata wengi waliokuwepo waliongea kwa lugha na walipata maono na kuona malaika na kutoa unabii, na walikuwa na wakati mwingi wa kufurahia kama vile haijawahi kuonekana katika kizazi hiki.”3

Hizo ishara za kiroho hazikuwa tu kwa wale waliokuwemo katika hekalu, kwani “watu wa ujirani walikuja wakikimbia pamoja (wakisikia sauti isiyo ya kawaida ndani, na wakiona nuru yenye mn’garo kama mhimili wa moto ukisimama juu ya Hekalu), na walishangazwa na kilichokuwa kikifanyika.”4

Lorenzo Snow (1814–1901), baadaye aliyepata kuwa Rais wa Kanisa, alikuwa anaishi Kirtland wakati huu uliobarikiwa. Alielezea hivi, “Mmoja angedhania kwamba baada ya kupokea ishara hizi za ajabu hakuna majaribu ambayo yangewapendua Watakatifu.”5

Lakini, ama kweli, matukio makuu ya kiroho hayatufanyi kuepukana na ushindani na majaribu. Miezi michache tu baada ya kuwekwa wakfu kwa hekalu, janga kuu la kiuchumi lilitetemesha Marekani, na Kirtland ilipata madhara zaidi. Benki ziliangamia, kuwaacha wengi katika hali ngumu ya kifedha. Kuzidisha, Watakatifu wengi ambao walikuwa wakihamia Kirtland walikuja na rasmali chache, bila kujua kile wangelifanya mara tu watakapofika au jinsi watakavyoishi.

Kabla ya kipindi kirefu, mateso yalianza na vikundi vya majambazi vikaundwa dhidi ya Watakatifu. Washiriki wa Kanisa—hata wengine waliokuwa karibu na Nabii, wengi ambao walikuwepo wakati kuwekwa wakfu kwa hekalu—waliasi na kumkashifu Joseph kama nabii aliyepotea.

Ninavyotembea karibu na Hekalu la Kirtland pamoja na mke wangu na wajukuu, nilitafakari jinsi gani ilivyohuzunisha kiasi kwamba wengine hawangebakia watiifu hata baada ya ishara za kiroho walizoshuhudia. Jinsi ilivyohuzunisha kiasi kwamba hawangevumilia fedheha na ukosoaji wa wasioamini. Jinsi gani ilivyohuzunisha kwamba, walipokumbwa na majaribu ya kifedha au mahangaiko mengine, hawangeweza kufikia ndani yao na kupata nguvu za kubakia watiifu. Jinsi gani ilivyosikitisha kwamba kwa njia nyingine walisahau mavuno ya kimiujiza ya kiroho wakati wa kuwekwa wakfu kwa hekalu.

Masomo

Ni nini tunachoweza kujifunza kutoka kwa kipindi hiki cha ajabu katika historia ya Kanisa?

Moja ya masomo makuu, yenye kudumu ya wakati wa Kirtland ni kwamba roho zetu zinahitaji malisho ya kila mara. Kama vile Rais Harold B. Lee (1899–1973) alivyofundisha: “Ushuhuda sio kitu ambacho unacho leo na kuwa nacho siku zote. Ushuhuda pengine utakua na kukua hadi kuwa uangavu wa kweli, au utadidimia kuwa bure, itategemea kile tunachofanya juu yake. Nasema, ushuhuda ambao tunaopata siku baada siku ndiyo kitu ambacho kinatuokoa kutokana na mitego ya mashimo ya adui.” Tunahitaji kukaa karibu na Bwana kila siku ikiwa tutasalimika kutokana na janga ambalo sote ni lazima tukumbane nalo.

Kwa njia zingine ulimwengu wetu unafanana na Kirtland ya miaka ya 1830. Sisi pia tunaishi katika nyakati za dhiki ya kifedha. Kuna wale wanaotesa na kushutumu Kanisa na washiriki wake. Majaribu ya kibinafsi na kijumla mara nyingine yanaweza kuonekana kuzidi.

Hapo ndipo tunapohitaji, zaidi kabisa, kusogea karibu na Bwana. Tunavyofanya hivyo, tutakuja kujua kinachomaanishwa na kumfanya Bwana kusogea karibu nasi. Tunavyomtafuta kila mara kwa bidii, kwa hakika tutampata Yeye. Tutaona wazi kwamba Bwana hatelekezi Kanisa Lake au Watakatifu Wake watiifu. Macho yetu yatafunguliwa, na tutamwona akifungua madirisha ya mbinguni na kutuosha na wingi wa nuru Yake. Tutapata nguvu ya kiroho ili kuendelea kuishi hata nyakati ya usiku wa giza nyingi.

Ingawaje wengine wa Watakatifu wa Kirtland walisahau uzoefu wa kiroho waliopata, wengi hawakusahau. Wengi wao, akiwemo William Draper, walishikilia kwa dhati elimu ya kiroho ambao Mungu aliwapatia na wakaendelea kumfuata Nabii. Njiani walipata majaribu mengi makali lakini pia ukuaji mwema wa kiroho hadi, hatimaye, wale waliovumilia hadi mwisho “walipokelewa… katika hali ya furaha isiyo na mwisho” (Mosia 2:41).

Unaweza Kuvumilia

Ikiwa utawahi kushawishiwa kuvunjika moyo au kupoteza imani, kumbuka Watakatifu hao watiifu waliobakia wa kweli katika Kirtland. Vumilia kidogo zaidi. Unaweza kufanya hii! Wewe ni sehemu ya kizazi maalum. Ulitayarishwa na kuhifadhiwa ili kuishi katika wakati huu muhimu katika maisha ya sahari maridadi ya dunia yetu. Unao uzao wa selestia na hivyo basi unazo talanta zote muhimu za kuyafanya maisha yako kuwa hadithi ya ufanisi ya milele.

Bwana amekubariki na ushuhuda wa ukweli. Umehisi mwongozo Wake na kushuhudia nguvu Zake. Na ukiendelea kumtafuta Yeye, Ataendelea kukupatia uzoefu mtakatifu kwa hizi na karama zingine za kiroho, utaweza sio tu kubadilisha maisha yako mwenyewe kwa wema lakini pia kubariki nyumba zenu, kata au matawi, jamii, miji, majimbo, na mataifa kwa wema wako.

Inaweza kuwa vigumu kuona hayo wakati mwingine, lakini vumilia kidogo zaidi, kwani “jicho halikuyaona wala sikio halikuyasikia, wala hayakuingia katika moyo wa mwanadamu, mambo ambayo Mungu aliwaandalia wampendao” na wanaomgojea Yeye (1 Wakorintho 2:9; ona pia M&M 76:10; 133:45).

Natoa ushuhuda wa ukweli wa injili rejesho ya Yesu Kristo na ukweli wa hili, Kanisa Lake. Nashuhudia kwa moyo wangu wote na nafsi yangu kwamba Mungu anaishi, kwamba Yesu Kristo ni Mwanawe na anasimama mbele mwa Kanisa hili kuu. Tunao nabii kwenye dunia tena, hata Rais Thomas S. Monson.

Tuweze kulikumbuka somo la Kirtland na kuvumilia kidogo zaidi—hata wakati mambo yanaonekana magumu. Fahamu na ukumbuke haya: Bwana anakupenda wewe. Anakukumbuka wewe. Na Atawasaidia kila mara wale wanao “vumilia katika imani hadi mwisho” (M&M 20:25).

Muhtasari

  1. Ona, kwa mfano, sehemu za 45; 56; 76; 84; 89; 97; na 104.

  2. Ona M&M 76:23; 110:2–4, 11–13.

  3. William Draper, “A Biographical Sketch of the Life and Travels and Birth and Parentage of William Draper” (1881), typescript, Church History Library, 2; spelling and capitalization standardized.

  4. Historia ya Kanisa, 4:605.

  5. Lorenzo Snow, “Discourse,” Deseret Weekly News, June 8, 1889, 26.

  6. Teachings of Presidents of the Church: Harold B. Lee (2000), 43.