2021
Jane Aliifurahia Safari Yote
Machi 2021


Wanawake wa Mwanzoni mwa Urejesho

Jane Aliifurahia Safari Yote

Je, sisi kama Jane Manning James, tumeazimia kumaliza safari yetu kwa imani?

illustration of Jane Manning James

Kielelezo na Toni Oka

Jane Manning James alikuwa amechoshwa na kutembea, lakini alikataa kusimama.

Mwanawe mkubwa, Sylvester, alikuwa mkubwa vya kutosha kutembea karibu na gari la kukokotwa na maksai. Lakini mtoto Silas, ambaye alikuwa amezaliwa safarini, bado alihitaji kubebwa. Ilikuwa mwaka 1947, familia ya James punde ingekuwa miongoni mwa waanzilishi wa kwanza kuwasili bonde Kuu la Salt Lake.

Jane hakuwa mgeni wa safari ndefu.

Miaka minne kabla, familia yake ilikuwa imeondoka nyumbani kwao katika jiji la mashariki ili kujiunga na Watakatifu katika Nauvoo, pembeni mwa mpaka wa magharibi. Safari hii ilipasa kuwachukua siku chache kwa njia ya mtoni. Kwa sababu watu wengi weusi walikuwa watumwa katika Marekani wakati huo, familia ya Jane mara nyingi ilibidi ionyeshe hati za kuonyesha uhuru wao. Na sehemu zingine zilikuwa na sheria kali za kuzuia watu wa rangi nyingine kusafiri kote katika eneo—ikijumuisha kulipishwa hadi dola $500 kwa kila mtu.

Labda kwa sababu ya hizi ada za kufedhehesha au labda kwa sababu ya ubaguzi mwingine, wafanyakazi wa chombo cha baharini walimzuia Jane na wanafamilia yake kuendelea na safari. Bila kutishika, waliacha nyuma mizigo yao mingi na wakaanza safari kwa miguu na wakibeba chochote tu ambacho wangeweza.

Jane alitembea kwa miguu kwa zaidi ya maili 800 (kilomita 1,287). Walitembea katika siku za unyevunyevu na usiku wa kiza totoro. Wakati mmoja walijikokota kupitia msituni, na kulala nje. Walipoamka, nguo zao zilikuwa nyeupe zimefunikwa kwa theluji.

“Tulitembea mpaka soli za viatu vyetu zikaisha, na miguu yetu ikawa imevimba na kupasuka na kuvuja damu,” Jane alikumbuka. “… Tulimuomba Mungu Baba wa Milele aponye miguu yetu na maombi yetu yalijibiwa.”1

Wakati wakistahimili safari hii ngumu, Jane aliimba nyimbo za dini na wazazi wake na ndugu zake, wakimsifu Mungu. Mwishowe, baada ya takribani miezi mitatu ya kutembea, waliwasili Nauvoo. Miaka kadhaa baadaye, wakati watakatifu waaminifu walipoondoka kuvuka nyanda, Jane alikuwa miongoni mwa waanzilishi wa kwanza kuanza safari ya miguu.