Kushinda Shughuli za Ulimwengu
Shughuli za ulimwengu hazipaswi kunivuruga katika kutii neno la Mungu.
Hata kama tumeahidiwa baraka kubwa, kama tunahangaika na shughuli za ulimwengu badala ya mapenzi ya Bwana, tutapoteza baraka hizo. Hii inaonekana wazi kupitia uzoefu wa mwanaume mmoja katika siku za mwanzo za Urejesho.
James Covel alikuwa amekuwa mtumishi katika imani nyingine kwa miaka 40, lakini baada ya kusikia injili ya urejesho, yeye “alifanya agano na Bwana kuwa angetii amri yoyote ambayo Bwana angempatia kupitia Joseph Nabii” (Mafundisho na Maagano 39, kichwa cha sehemu). Kupitia kwa Joseph, Bwana alimwambia Covel, “Sikiliza sauti yangu, ambayo yasema kwako wewe: Simama na ubatizwe, na ukaoshe dhambi zako, ukililingana jina langu, nawe utampokea Roho wangu, na baraka kubwa namna hii ambayo kamwe hujazijua” (Mafundisho na Maagano 39:10).
Hata hivyo, Covel punde “alikataa neno la Bwana, na kurudi kwenye kanuni zake za zamani na watu wa awali” (Mafundisho na Maagano 40, kichwa cha sehemu). Kuongelea juu ya Covel, Bwana alisema kwamba “akalipokea neno kwa furaha, na moja kwa moja shetani akamjaribu; na woga na mateso na shughuli za ulimwengu zikamsababisha yeye kulikataa neno” (Mafundisho na Maagano 40:2). Kwa sababu ya wasiwasi juu ya shughuli za ulimwengu, Covel alipoteza baraka alizokuwa ameahidiwa na Bwana.
Je, Nibaki au Niende?
Katika maisha yangu mwenyewe, nimejifunza kwamba sharti tusiache shughuli za ulimwengu zituvuruge tusimtii Bwana. Nilikulia katika nyumba nzuri na yenye upendo ambapo wazazi wangu walitufundisha vyema katika injili, na upendo wao kwetu uliakisi upendo wa Baba wa Mbinguni kwa watoto Wake.
Katika umri wa miaka 16, nilialikwa kufanya kazi katika shamba la mifugo huko Marekani, kukiwa na uwezekano wa siku moja na mimi kujenga nyumba yangu hapo. Hii ilinipendeza, kwa vile nyumbani kwetu, Uholanzi, ni nchi ndogo tu, yenye mlundikano wa wakazi wengi.
Kwa kweli, mababu zangu upande wa baba yangu wote walikuwa na hamu ya kuishi mahali pengine. waliishi Indonesia, ambayo ilikuwa koloni ya Uholanzi. Niliweza kuelewa kwa nini. Katika indonesia, hali ya hewa ilikuwa nzuri, mandhari nzuri, na nafasi kubwa. Vinasaba vyangu vilikuwa na shauku za kusafiri ambavyo viliwasukuma mababu zangu. Je, mimi pia niache nchi yangu ya kuzaliwa na kutafuta mafanikio na matukio yasiyo ya kawaida?
Wakati wa muda wa kufanya maamuzi, baba yangu alinipatia nakala ya barua iliyoandikwa kwake na dada zake miaka mingi awali na rais wao wa misheni, Donavan van Dam. Rais van Dam aliwaomba wabakie Uholanzi na kujenga Kanisa hapo. Baba yangu aliniambia kwamba aliamua kufanya hivyo kabisa. Kwa vile jina la familia ya Boom lilikuwa kwenye barua, sasa ilikuwa zamu yangu kuangalia kile nitakachofanya.
Katika miaka ya baada ya Vita vya II vya Dunia, waumini wengi wa Kanisa ilibidi wahamie Amerika na Kanada. Hiyo bado ilikuwa inaendelea katika miaka ya 1970, licha ya kusisitiziwa na viongozi wa Kanisa waumini wabaki katika nchi zao wenyewe na kuimarisha Kanisa hapo walipokuwa wanaishi. Kwa maombi, mimi pia nilifanya uamuzi wa kubaki na kujenga Kanisa katika Uholanzi, bila kuelewa vyema kabisa kile ambacho hii ingemaanisha siku za usoni.
Maamuzi, Maamuzi
Nilipomaliza shule ya upili miaka ya mwishoni mwa 1970, uchumi wa Uholanzi ulikuwa umedorora. Viwango vya kutokuwa na ajira vilikuwa juu. Kwa jumla, mambo yalionekana ya kusikitisha sana. Ilikuwa vigumu kwa waliohitimu digrii kuamua nini cha kufanya.
Baba yangu alikuwa anatumikia kama rais wa tawi. Mara moja moja alizungumza nami juu ya uwezekano wa kuhudumu misheni. Bila shaka, hilo lilikuwa jambo zuri kufanya. Nilikuwa ninatazamia hilo maishani mwangu mwote.
Lakini sikuona jinsi gani kuhudumu misheni kungenisaidia kukidhi mahitaji ya familia yangu ya baadaye. Tangu utotoni daima nilikuwa na shauku kubwa ya siku moja kupata kipenzi cha maisha yangu na kujenga familia yetu pamoja.
Nilikuwa na umri wa miaka 17 wakati huo, na sikujua cha kufanya, nikaanza ngazi iliyofuata ya elimu. Lakini baada ya majuma kadhaa niligundua kwamba fani hii ya masomo haingeweza kunipatia furaha. Nilikuwa na maswali kuhusu kama ingeweza kunipatia ajira ya kutegemewa. Nikafikiria kuacha chuo.
Wazazi wangu hawakufurahishwa na jambo hili. Waliniambia ningeacha chuo tu kama ningekuwa nimepata ajira. Labda walifikiria kwamba nisingepata kamwe kwa sababu ya mdororo wa kifiedha. Nilitumia mchana mzima kwenye baiskeli, nikienda sehemu moja ya biashara hadi nyingine. Mwishowe kampuni moja iliniajiri kufanya kazi katika bohari lao.
Mpango Wangu
Hata ingawa nilichukua hii ajira ya muda, nilkuwa na mpango. Nitakuwa polisi. Kufanya kazi serikalini ingekuwa njia thabiti ya kukidhi mahitaji ya familia yangu ya baadaye na kila kitu kingekuwa sawa.
Nakumbuka siku nilipoenda kufanya mtihani wa kuingia shule ya polisi. Nilipanda gari moshi mapema asubuhi na kutumia siku nzima nikifanya kila aina ya mtihani. Mwisho wa siku niliitwa ofisini. Waliniambia nimepita mithani yote na wangependa kunichukua, lakini kwa sababu nilikuwa na umri wa miaka 17, nilikuwa mdogo sana. Waliniambia nijaribu tena baada ya mwaka mmoja.
Ulimwengu wangu uliporomoka, na njiani kwenda nyumbani nilikuwa nikifikiri, “Nini kitafuata?” Nyumbani baba yangu alisikiliza kuvunjika moyo kwangu na akaomba anipatie baraka. Nilitarajia kwamba Bwana ataniambia kwamba kila kitu kitakuwa sawa na ningekubaliwa katika chuo cha polisi katika njia ya kimiujiza. Badala yake Bwana aliniambia kwamba kama ningemweka Yeye kwanza, ningepata mkate kwenye meza yangu na uwezo wa kuitunza familia yangu ya baadaye.
Mpango Bora
Katika majibu ya maombi yangu, nilipokea jibu ambalo, kwangu mimi, kumweka Bwana kwanza kulimaanisha kwenda kuhudumu misheni. Daima nilidhamiria kufanya hivyo lakini nilikuwa sijaona jinsi hatua moja ingeongoza kwenye hatua nyingine. Sasa nilijua kwamba kuhudumu misheni ndiyo kitu ambacho ningefanya, na nilitaka kufanya hivyo upesi iwezekanavyo.
Wakati huo, gharama ya misheni ilikuwa gilda 10,000 katika fedha za zamani za Uholanzi, au mshahara wa mwaka mzima. Niliendela kufanya kazi katika bohari na kufikia msimu wa kiangazi wa 1981, nilikuwa na gilda 10,000. Na pia nilitimiza miaka 18. Baba yangu, rais wa tawi, aliniambia nilikuwa mdogo sana kwenda misheni, pia rais wa wilaya na rais wa misheni. Wakati huo, ulihitajika kuwa na umri wa miaka 19. Lakini siku yangu ya kuzaliwa ya 18 nilienda kwa daktari na daktari wa meno peke yangu na wakajaza sehemu zao katika fomu yangu ya maombi ya umisionari.
Kwa njia fulani, niliweza kuwashawishi viongozi wangu kunisahili na kutuma maombi yangu. Kisha tukangojea. Mimi sikujua kwamba baba yangu, kama rais wa tawi, alikuwa amepokea barua. Maombi yalirudishwa kwake na taarifa kwamba nilikuwa mdogo sana. Lakini hakutaka kushiriki hii nami, kwa hiyo alitembea nayo kwenye mfuko wa koti lake kwa majuma mengi bila kunijulisha. Kwa bahati nzuri, wakati ule ule alikuwa amepokea taarifa nyingine. Ilisema kwamba katika hali fulani Ndugu viongozi wa ukuhani walikuwa radhi kuwaacha wavulana kwenda mapema kama wameandaliwa vyema. Punde niliitwa kuhudumu na kutumwa Misheni ya England London East. Misheni yangu ikawa baraka ya maisha yote.
Baraka kutoka kwa Bwana
Miezi mitatu baada ya kurudi kutoka kwenye misheni yangu, nilikutana na kipenzi cha maisha yangu. Mwaka mmoja baadaye tulifunga ndoa na kuunganishwa katika Hekalu la London England. Uchumi ulikuwa bado si imara, lakini niliweza kupata ajira na kukidhi mahitaji ya familia yangu. Daima kuna mkate kwenye meza na paa juu ya vichwa vyetu.
Kama mmisonari, haya yamekuwa maandiko yangu pendwa: “Kadiri utakavyoshika amri za Mungu utafanikiwa katika nchi” (Alma 36:1). Kwa mwongozo huu, niliamua kufanya kile baba yangu alichofanya—kubaki Uholanzi na kujenga Kanisa katika nchi yangu ya asili.
Leo lile tawi dogo ambapo nilikulia sasa ni kata kubwa ya kupendeza ambapo wajukuu wetu wanafurahia wenza wa marafiki wengi, wanakusanyika katika darasa pana la Msingi. Wana wetu wana kazi nzuri na wamebarikiwa kuwa na mkate kwenye meza. Ninaona kwamba maamuzi yangu yamekuwa na matokeo kwa kizazi kijacho, ambao pia wana hamu ya kumweka Bwana kwanza katika maisha yao.
Nina shukrani kwamba nilijifunza mapema katika maisha yangu kwamba maamuzi sahihi ni kuzishinda shughuli za ulimwengu na kumweka Baba wa Mbinguni kwanza. Yeye amenipatia baraka ambazo vinginevyo kamwe nisingezijua.