Vijana Wakubwa
Kuwa Watumishi Bora wa Dunia ambayo Mungu Ameiumba kwa Ajili Yetu
Kutoka kwenye hutoba iliyotolewa katika Kongamano la Mwaka wa 18 wa Stegner Center katika Chuo Kikuu cha Utah Jijini Salt Lake, Aprili 12, 2013.
Jinsi tunavyoijali dunia, jinsi tunavyoitumia na kushiriki wingi wake, na jinsi tunavyotendea vyote vilivyo hai vilivyotolewa kwa ajili yetu ni sehemu ya jaribio letu katika maisha haya.
Shughuli zangu za ziada ni kuwa katika mazingira ya asili, iwe matembezi kwa miguu, kuteleza kwenye theluji, kusafiri kwa mtumbwi baharini, kuendesha baiskeli, au hata kwenda safari. Kama mtoto, nilipendelea kuwa msituni na kuusikiliza kwa ukimya, ushahidi wa ufasaha ambao miti mirefu ya kijani wakati wote ilitoa juu ya huyu Muumba. Na sasa nimekuwa mtu mzima, nimejua kwa kujifunza na kwa imani kwamba kama tutaelewa sisi ni akina nani, madhumuni ya maisha, na sababu ya ulimwengu kuumbwa—na kuviweka vitu hivi akilini—tutautumia ulimwengu huu, na vyote vilivyomo, kwa njia ya hali ya juu na ya utukufu zaidi.
Madhumuni ya Mungu katika Kuumba Ulimwengu
Bwana, kupitia kwa manabii Wake wote wa kale na sasa, amejaribu kutusaidia kuelewa na kufurahia zawadi ya kuishi kwenye ulimwengu mzuri. Katika Agano la Kale, Daudi alifikiria uumbaji mtukufu wa Mungu na kushangaa kwa sauti, kwa nini—miongoni mwa maajabu kama hayo—Mungu anamjali mwanadamu (ona Zaburi 8:4). Daudi alihitimisha kwamba wanadamu ni maalum, “wadogo punde kuliko malaika” (Zaburi 8:5).
Musa pia aliona katika ono dunia zisizo na idadi1 na kutangaza, “Sasa, kwa jinsi hii ninajua kwamba mwanadamu si kitu, kitu ambacho sikukidhania” (Musa 1:10).
Katika unyenyekevu wa Musa mbele za uumbaji mtukufu wa Mungu, alishindwa kutambua ukweli mkuu. Kwa hiyo Bwana alimwonyesha tena uumbaji Wake usio na kipimo na kutangaza waziwazi kwamba Yeye—Mungu—aliumba uumbaji huu “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39). Dunia hii—naam uumbaji wote—umesanifiwa ili kutusaidia sisi kupata kutokufa na uzima wa milele.
Akisema tena kuhusu madhumuni ya kuwepo kwa dunia, Bwana alisema, “Nasi tutaifanya dunia mahali ambapo hawa [akimaanisha sisi] watapata kukaa; nasi tutawajaribu kwa njia hii, ili kuona kama wao watafanya mambo yote yale ambayo Bwana Mungu wao atawaamuru” (Ibrahimu 3:24–25; ona pia mstari wa 26). Maisha katika dunia hii, yakiambatanishwa na kipawa cha maadili ya haki ya kujiamulia, hutupatia fursa ya kuchagua kutafuta na siku moja kupokea yale yote ambao Mungu anatoa.2
Wakati uumbaji wa dunia ulipokamilika, Mungu alipendezwa nao kwa sababu Yeye aliona kwamba ungetimiza madhumuni Yake kwa ajili yetu sisi, watoto Wake.3 Wana na mabinti wa Mungu na familia wanazounda sio tu wadukizi kwenye hii dunia; ila, wao ni kiini cha madhumuni yake.4
Tunapaswa Kuwa Watumishi Wema
Maisha kwenye dunia hii ni vyote, baraka na jukumu. Bwana alitamka, “Kwani, tazama, wanyama wa porini na ndege wa angani, na kile ambacho hutambaa ardhini, vimetawazwa kwa matumizi ya wanadamu kwa ajili ya chakula na mavazi, na kwamba aweze kuwa navyo vingi” (Mafundisho na Maagano 49:19). Hata hivyo, kwa sababu ulimwengu na vile vyote vilivyo ndani yake ni “kazi ya mikono [Yake]” (Mafundisho na Maagano 29:25), vyote ni mali Yake.5 Kama wakazi wa muda wa dunia hii, sisi ni watumishi—sio wamilki. Kwa hiyo, tunawajibika kwa Mungu—mmiliki mwenyewe—kwa kile tunachofanya na uumbaji Wake: “Kwani ni muhimu kwamba Mimi, Bwana, yanipasa kumfanya kila mtu awajibike, kama msimamizi juu ya baraka za kidunia, ambazo nimezifanya na kuzitayarisha kwa ajili ya viumbe vyangu” (Mafundisho na Maagano 104:13).
Jinsi tunavyoitunza dunia, jinsi tunavyoitumia na kula zawadi yake, na jinsi tunavyofanya na kile ambacho tumepatiwa ni sehemu ya jaribio letu hapa duniani. Tunapaswa kutumia kwa shukrani kile ambacho Bwana ametoa, kuepukana na uharibifu wa maisha na rasilimali, na kutumia zawadi ya duniani ili kutunza maskini.6 Bwana anajali sana maisha yote na hasa watoto Wake, na atatuwajibisha kwa kile tunachochagua kufanya au kutofanya na zawadi za uumbaji Wake.
Bwana ametuahidi kwamba kama tutamfuata Yeye na kutumia kwa busara rasilimali za ulimwengu kwa shukrani na heshima, “viijazavyo dunia ni mali yenu, wanyama wa mwituni na ndege wa angani. … Na imempendeza Mungu kwamba ametoa vitu hivi vyote kwa mwanadamu; kwani ni kwa sababu hii vilifanywa ili vitumiwe, kwa hekima, siyo ufujaji, wala siyo kwa kutumia nguvu” (Mafundisho na Maagano 59:16, 20).
Tunafaa kutumia rasilimali hizi kwa busara na shukrani, kwa nia ya kuwasaidia wengine—vizazi vya leo, jana na siku za baadaye—kupokea baraka ambazo Baba yetu wa Mbinguni anatamani watoto Wake wazipate.
Kuona Zaidi Yetu Wenyewe
Kwa huzuni leo, tunaishi katika dunia ambayo watu wanachagua kumkataa Mungu na kutendea uumbaji Wake kwa dharau. Wakati hili linatokea, Mungu na uumbaji wanaumia.
Henoko aliandika kwamba Mungu alilia kwa sababu ya chaguzi mbaya na za uchoyo za watoto Wake.7 Moroni alitoa unabii kwamba katika siku za mwisho kutakuwa na “moto, na tufani, na mivuke ya moshi … [na] kutakuweko uchafu mwingi juu ya uso wa dunia” na hali kama hizi zitaambatana na “kila aina ya machukizo; wakati kutakuwa na wengi ambao watasema, Fanya hivi, au fanya vile, na bila kujali” (Mormoni 8:29, 31). Wakati mwanadamu anapochafua ulimwengu huu kiroho au kimwili, sio tu Mungu lakini pia asili pia inaumia!8
Cha muhimu, baraka na nguvu zilizopatikana kupitia Kanisa la Bwana la urejesho na injili vina uwezo wa kupanua na kubadili nafsi ya mwanadamu kuliko kujitazama mwenyewe, kuvutia upendo wa Mungu na uumbaji Wake, na kutusaidia kufikiria ustawi wa wengine na kufikiria vizazi vijavyo.
Asili Hutuleta Karibu na Mungu
Dunia na uhai wote ni zaidi ya vitu vya kutumiwa na/au kuhifadhiwa; baadhi ya sehemu na vipande vyake pia ni muhimu vihifadhiwe! Asili ambayo haijaharibiwa na “vitu vyote vimeavyo kutoka ardhini … vimefanywa kwa faida na matumizi … ya mwanadamu, kwa kuridhisha jicho na kufurahisha moyo … na kuchangamsha nafsi” (Mafundisho na Maagano 59:18–19).
Asili katika hali yake safi kabisa hutuleta karibu na Mungu, huondoa akilini na moyoni kelele na fadhaa za kupenda vitu, hutuinua juu zaidi, hata kwenye mahali palipotukuka, na hutusaidia kumjua vyema Mungu wetu: “Dunia hubiringika kwa mabawa yake, nalo jua hutoa mwanga wake mchana, nao mwezi hutoa mwangaza wake usiku, nazo nyota pia hutoa mwanga wake. … [Mtu] yeyote aliyoiona yoyote au ndogo ya hizi amemwona Mungu akitembea katika ukuu na uweza wake” (Mafundisho na Maagano 88:45, 47).
Mimi bado napendelea kutembea juu milimani kwenye mawe na vilele vya majabali. Ingawaje ni kimya, huongelea uweza na utukufu wa Mungu—na busara Yake isiyo na kifani ya umaridadi. Alma alishuhudia, “Vitu vyote vinaonyesha kwamba kuna Mungu; ndio, hata dunia, na vitu vyote vilivyo juu yake, … vinashuhudia kwamba kuna Muumba Mkuu” (Alma 30:44).
Napenda kutazama nyota usiku, nikijaribu kuzamisha akili zangu kwenye umilele wa wakati na uwanda mpana angani katika kutazama kwangu. Daima hushangaa kuhusu maarifa ambayo huja katika hizo nyakati za ukimya ambazo, licha ya mapana ya dunia, Bwana wa ulimwengu ananijua mdhaifu mimi. Na Yeye anamjua kila mmoja wetu. Uumbaji unamshuhudia Muumba, na kama tutahifadhi hizi sehemu maalumu, bila kuziharibu, kwa ufasaha na kwa kina sana zitamshuhudia Mungu wetu na kutushawishi kusonga mbele.
Kadiri tunavyotunza dunia hii vyema na vyote vilivyo ndani yake, ndivyo itakavyohimili, vutia, imarisha, changamsha na kufurahisha mioyo yetu na roho zetu—na kutuandaa kuishi na Baba yetu wa Mbinguni katika mahali pa selestia, ambapo patakuwa ni ulimwengu huu tusimamapo leo, lakini itakuwa katika hali ya utukufu.9
Na tuitunze dunia hii kwa shukrani—nyumbani kwetu sasa na kwa siku za usoni.