UJUMBE WA URAIS WA ENEO
Njia ya Kujitegemea Inaweza kuwa Ndefu lakini Inawezekana
“Niliamua kusimamia maisha yangu na kuamua kuacha kulalamika pale nilipojua kwamba malalamiko kamwe hayabadili chochote.”
Katika Mkutano Mkuu wa Aprili 2017, Mzee M. Russell Ballard, wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alifundisha, “Kwa miaka mingi, nimegundua kwamba wale wanaofanikisha mengi katika ulimwengu huu ni wale walio na ono kwa ajili ya maisha yao, pamoja na malengo ya kuwafanya wafokasi kwenye ono lao na mipango ya muda mfupi inayotekelezeka ya jinsi ya kufanikisha hayo. Kujua wapi unaenda na jinsi ya kufika huko kunaweza kuleta maana, lengo na mafanikio kwenye maisha.”1
Mungu, Baba yetu wa Mbinguni, ametupatia mfano mkamilifu wa kuweka malengo na kufanya mipango. Yeye alitangaza kwa nabii Musa kwamba lengo Lake ni “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu”2. Tunafahamu kwamba Baba Yetu wa Mbinguni hafanyi chochote ambacho si kwa faida ya watoto Wake3.
Yeye anatupenda na anatujali. Amembariki kila mmoja wetu kwa uwezo ambao utatusaidia kufanikiwa katika kipindi hiki cha safari ya maisha ya duniani na kujiandaa kurudi kuishi Naye tena.
Safari yetu katika maisha si mbio fupi—bali mbio ndefu—na katika mbio hizi za maisha, tunafanikiwa pale tunapojifunza kupiga hatua moja mbele katika uelekeo tunaotaka kwenda—kila siku. Kwa njia sawa na hiyo, safari yetu ya kuwa wenye kujitegemea inaanza kwa hatua ya kwanza. Hakuna atakayechagua au kuamua kwa niaba yetu. Njia inaweza kuwa ndefu lakini mwisho wa safari ni wa uhakika. Inahitaji kwamba tujifunze kuchukua hatua ya kwanza ili tuweze kuona kinachofuata. Hatuwezi kuona fursa zijazo ambazo zinatungojea bila kufanya juhudi na dhabihu zinazohitajika kupiga hatua hiyo ya kwanza.
“Wakati tunapoona pengo kati ya sisi ni nani na kile tunachotamani kuwa, wengi wetu hujaribiwa kuchagua kupoteza imani na tumaini”4.
Nimejifunza somo hilo katika maisha yangu mwenyewe. Baada ya misheni yangu, nilihisi kupotea, pasipo kujua wapi pa kuanzia na nini cha kufanya. Nililalamika kuhusu maisha yangu, kana kwamba lilikuwa jukumu la mtu mwingine kutenda kwa niaba yangu. Ilinichukua miezi michache kabla ya kutambua kwamba fursa zipo kwa ajili ya kila mmoja. Jua linapochomoza asubuhi, linatoa nuru na uzima kwa kila mtu, licha ya hali zetu za kijamii, kihisia, kimwili au kiroho. Linachomoza asubuhi bila kuwa na upendeleo na kuleta tumaini kwa kila mmoja. Wale wanaofanikiwa ni wale wanaoziona fursa zikija wakati jua linapochomoza na kufanya kazi kwa bidii kuzikamata kabla ya jua kuzama. Kuna wale ambao wanaujua mwisho wa safari na wanaweka mipango kufika huko.
Baada ya kujifanyia tathmini binafsi, niliamua kufokasi kwenye vitu rahisi ambavyo vingeniruhusu kuwa na wenza wa Roho Mtakatifu kila siku. Niliacha kulalamika kuhusu kila kitu. Niliweka malengo ya kuboresha uwezo wangu binafsi wa kupokea ufunuo binafsi. Nilifahamu kwamba ikiwa ningeboresha uhusiano wangu binafsi na Baba yangu wa Mbinguni, ningeongozwa. Niliamua kuboresha sala zangu za kila siku, usomaji wangu wa maandiko wa kila siku. Nilifunga kila mwezi na kulipa matoleo yangu ya mfungo. Niliamua kulipa zaka yangu na kutumikia kwenye miito yangu na kutunza maagano yangu. Nilifahamu kwamba ikiwa ningefanya sehemu yangu ya agano, Mungu angetimiza sehemu yake—“kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu”5.
Nilifahamu kwamba ikiwa ningemrudia Bwana kwa moyo wa lengo moja, na kumwamini, na kumtumikia kwa bidii yote akilini, Yeye, kulingana na nia yake na mapenzi yake, angeniokoa kutokana na changamoto na vizuizi vyangu6. Kuwa mwenye kujitegemea ni uwezo, msimamo na juhudi ya kukimu mahitaji muhimu ya kiroho na ya kimwili ya maisha kwa ajili ya mtu mwenyewe na familia.
Nilijua pia kwamba mimi ni mwana wa Mungu na kwamba Yeye ananijali. Nilikumbuka ahadi za Bwana katika Mafundisho na Maagano 104:14–17: “Mimi, Bwana, nilizitandaza mbingu, na kuijenga dunia, kazi halisi ya mkono wangu; na vitu vyote vilivyomo ni mali yangu.
Na ni madhumuni yangu kuwa niwapatie mahitaji watakatifu wangu, kwani vitu vyote ni mali yangu.
Lakini haina budi kufanyika katika njia yangu mwenyewe; na tazama hii ndiyo njia ambayo Mimi, Bwana, nimeazimia kutoa mahitaji ya watakatifu wangu, ili maskini wapate kuinuliwa, na kwa njia hiyo matajiri hushushwa.
Kwani dunia imejaa, na viko vya kutosha na kubaki; ndiyo, nilitayarisha vitu vyote, na nikawapa wanadamu kuwa na uwezo wa kujiamulia wenyewe.”
Niliamua kusimamia maisha yangu na kuamua kuacha kulalamika pale nilipojua kwamba malalamiko kamwe hayabadili chochote.
Niliondoka nyumbani kwa wazazi wangu, nilipokuwa na miaka ishirini na moja na kwenda kuishi na mjomba wangu. Nilianza kuhudhuria chuo kilichoitwa Institut Superieur des Techniques appliquees.
Nikiwa sina pesa ya kulipia chakula au usafiri, bado nilienda shule, wakati mwingine nikisimamisha magari, ili kuomba msaada. Wakati mwingine nililia nikiwa nimesimama mtaani—nikisubiri na kusubiri. Kamwe sikukatishwa tamaa na hali yangu. Nilifanya hivyo kwa miaka mitatu. Kisha nilihudhuria chuo kikuu kingine kwa miaka mitano zaidi. Ilikuwa ngumu, lakini sikukata tamaa.
Bado nakumbuka ushauri wa baba yangu, “Mwanangu, ikiwa hutajifunza gharama ya mkate mmoja, hutajua kamwe maisha yako yana maana gani hasa.”
Nilianza kufanya vibarua hapa na pale. Nilifundisha wanafunzi. Nilifanya kila kitu ambacho kilikuwa cha heshima kufanywa. Wakati mwingine watu walinidhihaki, lakini mimi nilifahamu nilichokua nakifanya. Kilikuwa kwa ajili ya maisha yangu.
Kwa kipato changu kidogo, nililipa zaka na kuweka akiba kwa ajili ya kugharamia elimu yangu. Daima nitakuwa mwenye shukrani kwa wanasihi wangu, wazazi wangu, viongozi wangu wa ukuhani na marafiki ambao walikuwepo kunipa moyo. Uzoefu huo katika kipindi cha mwanzo cha maisha yangu ulisaidia kunifanya vile nilivyo leo.
Nilikuwa mwanafunzi wakati nilipoamua kuoa. Mke wangu alinipenda jinsi nilivyo na si kwa sababu ya kile nilichokuwa nacho. Hakika, sikuwa na mali yoyote—lakini nilikuwa na imani katika Baba yetu wa Mbinguni na Mwana Wake Yesu Kristo na nilifanya kazi kwa bidii kila siku ili kukidhi mahitaji yangu na ya familia yangu.
Kwa miaka mingi mimi na Nathalie tumefanya kazi pamoja na amenifanya niwe hivi nilivyo. Sisi hakika ni matunda ya imani yetu na ya juhudi zetu za kila siku.
Wapendwa akina kaka na Dada, ikiwa unafahamu unapokwenda na nani unataka kuwa, hata kama huoni ukomo kwa ukamilifu na yajayo kuonekana kuwa kiza, mwamini Bwana na endelea kujaribu, hatua moja baada ya nyingine. Kujua wapi unaenda na jinsi ya kufika huko kunaweza kuleta maana, lengo na mafanikio kwenye maisha.
Ninashuhudia kwamba Mungu yu hai na anatupenda. Yesu hakika ndiye Kristo. Yeye ni Mwokozi na Mkombozi wetu na kwamba kupitia Upatanisho Wake, tutaweza kushinda vikwazo vya maisha yetu. Tunaweza kufanya vizuri zaidi na kuwa bora zaidi.
Thierry K. Mutombo aliidhinishwa kama Kiongozi Mkuu mwenye Mamlaka wa Wale Sabini mnamo Aprili 2020. Amemuoa Tshayi Nathalie Sinda; wao ni wazazi wa watoto sita.