Misingi ya Injili
Mkutano Mkuu: Mkutano wa Kanisa Ulimwenguni Kote
Tunawasikiliza manabii na viongozi wengine wa Kanisa katika mkutano mkuu. Wanatufundisha kile Mungu anataka tusikie.
Kila Aprili na Oktoba, Kanisa hufanya mfululizo wa mikutano inayoitwa mkutano mkuu. Viongozi hufundisha na kushuhudia kuhusu Yesu Kristo na injili Yake. Mkutano Mkuu hufanyika Salt Lake City, Utah,USA, na hutangazwa ulimwenguni kote katika lugha zaidi ya 90. Waumini wote na watu wote wanaopenda hualikwa kusikiliza hotuba.
Mikutano Mikuu ya Kwanza ya Kanisa
Kanisa liliundwa rasmi wakati wa mkutano mnamo Aprili 6, 1830 (ona Mafundisho na Maagano 20). Mkutano mkuu wa kwanza ulifanyika mnamo Juni 9, 1830. Tangu hapo, mikutano mikuu imekuwa ikiendeshwa chini ya uelekezi wa Rais wa Kanisa popote pale waumini wanapoweza kukusanyika. Mnamo mwaka wa1840, viongozi walianza kuendesha mikutano mara mbili kwa mwaka.
Ni Kwa Jinsi Gani Mikutano Inaandaliwa Siku Hizi
Urais Wa Kwanza, Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, na viongozi wengine wa Kanisa wanaongea katika mkutano mkuu. Kwaya ya Tarbenacle katika Temple Square na kwaya nyingine za Kanisa hutoa huduma ya muziki. Kila Mkutano una vikao vinne: viwili Jumamosi na viwili Jumapili.
Mafundisho ya Viongozi
Katika mwezi kabla ya mkutano, viongozi wa Kanisa husali juu ya kile watakachofundisha. Bwana huwaangazia kujua kile watakachosema. Wanafundisha kweli za injili na hutualika sisi kushika amri za Mungu. Pia wanashuhudia juu ya Yesu Kristo na kutuhimiza kumfuata Yeye.
Kujifunza kutoka kwenye Mkutano mkuu
Kabla ya mkutano mkuu, tunaweza kusali kusikia kile Bwana anataka tujifunze. Tunaposikiliza hotuba, Roho atatufundisha kile tunachohitaji kujua. Baada ya mkutano, mazungumzo hayo huonekana katika ChurchofJesusChrist.org, na katika Gospel Library app, na katika Liahona. Tunaweza kwa kusali kujifunza zaidi hotuba kuhusu Yesu Kristo na injili Yake.
Kutoka katika Maandiko
Yesu Kristo alifundisha kwamba tunapaswa kukusanyika pamoja mara kwa mara (ona 3 Nefi 18:22).
Waumini wa Kanisa wanapoabudu kwa pamoja, Bwana atakuwa pamoja nao (ona Mathayo 18:20).
Bwana aliwaamuru waumini wa Kanisa ”kufundishana na kuimarishana wao kwa wao” (Mafundisho na Maagano 43:8).
Kadiri waumini wa Kanisa watakavyokuwa waaminifu na kutumia imani katika Kristo, Roho Wake atakuwa pamoja nao wanapokusanyika pamoja (ona Mafundisho na Maagano 44:2).