2022
Kuwa Shujaa Kihisia
Januari/Februari 2022


Vijana Wakubwa

Kuwa Shujaa Kihisia

Mwandishi anaishi Seville, Hispania.

Kamwe sikuwahi kupitia wasiwasi hadi niliporejea nyumbani kutoka kwenye misheni yangu, hivyo sikuwa na uhakika wa jinsi gani nisonge mbele.

smiling young woman

Picha imewekwa tayari na mwana mitindo

Maisha yalikuwa yakienda kama ilivyopangwa.

Nilikuwa karibu kumaliza misheni yangu. Kipindi cha miezi 18 iliyopita, ushuhuda wangu ulikuwa umeimarika na ono langu la mpango wa wokovu lilikuwa limekua. Nilikuwa sijawahi kuhisi kuwa karibu na Mwokozi wangu na Baba yangu wa Mbinguni kama hivi. Maisha yalionekana yenye furaha kamili.

Hakika, mimi na familia yangu tulikuwa tukipitia kipindi chetu cha majaribu, lakini kwa ujumla, nilikuwa nimefurahishwa na nilikuwa na mipango mingi kwa kile kitakachokuja mbeleni. Lakini kisha nilirejea nyumbani. Na mshtuko ulikuwa wa kuumiza sana. Nilihangaika kujizoeza tena maisha ya kila siku. Nilikuwa na hofu iliyofululiza kuhusu kufanya chaguzi nzuri na kuwa mkamilifu katika utiifu wangu. Niliweka nguvu kubwa kwangu mwenyewe kubaki kwenye kiwango cha juu kiroho ambacho nilikuwa nacho kote katika misheni yangu kwa sababu nilihofu kwamba ikiwa nisingefanya hivyo, ningerudi nyuma kiroho.

Kadiri shinikizo nililojiwekea lilivyoongezeka, nilianza kupata wasiwasi na mashambulio ya hofu. Likawa likitokea mara kwa mara, na hatimaye nilihisi kama nilikuwa nikizama.

Kwa bahati mbaya, nilificha hisia zangu kwa familia na marafiki. Nilifahamu kwamba shinikizo na msongo wa mawazo havikuwa vitu vya kuonea aibu, lakini nilihisi kutoweza kuhimili na niliyepotea kiasi kwamba sikujua hata jinsi ya kuelezea kile nilichokua nakipitia ili kupata msaada.

Kwa shukrani, Bwana daima yupo pale kutuongoza wakati tunapomgeukia Yeye. Baada ya kutafakari na kuomba mara kadhaa, nilihisi msukumo wa kuzungumza na kaka yangu pamoja na mke wake. Walinisaidia kutambua kwamba sikuwa “nimerukwa na akili” kama nilivyodhani na kwamba changamoto za kihisia zinaweza kutokea kwa mtu yeyote.

Dada Reyna I. Aburto, Mshauri wa Pili katika Urais Mkuu wa Kikundi cha Usaidizi alishuhudia juu ya ukweli huu: “Rafiki zangu wapendwa, inaweza kutokea kwa yeyote kati yetu—hususani wakati, kama waaminio katika mpango wa furaha, tunajiwekea mizigo isiyo ya lazima juu yetu kwa kudhani tunapaswa kuwa wakamilifu sasa. Mawazo kama hayo yanaweza kuwa ya kuchosha. Kufikia ukamilifu ni mchakato ambao utatokea kote katika maisha yetu ya duniani na ya baadaye—na kupitia tu neema ya Yesu Kristo.1

Kozi Yenye Mwongozo wa Kiungu

Nilipoomba kwa Baba wa Mbinguni kwa ajili ya mwongozo, nilitambua kwamba nilihitajika kutoa nafasi kwa rasilimali ambazo Yeye ametupatia na nilihitajika kujifunza na kubadilika daima. Kwa shukrani, kwa wakati ule nilipata nafasi ya kuhudhuria kozi ya Kanisa ya kuwa shujaa kihisia. Fursa ilionekana kuja wakati muafaka na siamini kama ilikuwa bahati mbaya.

Katika mwongozo wa kozi, ushujaa kihisia umefafanuliwa kama ifuatavyo:

  • “Uwezo wa kukabiliana na changamoto za kihisia kwa ujasiri na imani iliyojikita katika Yesu Kristo.

  • “Kuwasaidia wengine pamoja na wewe mwenyewe vizuri kadiri unavyoweza.

  • “Kutafuta msaada wa ziada pale inapohitajika.”2

Kwa maneno mengine, ushujaa kihisia ni jambo ambalo sote tunalihitaji.

Kwangu mimi, kozi hii yenye mwongozo wa kiungu ni ishara ya wazi kwamba Baba wa Mbinguni anafahamu majaribu tunayokabiliana nayo katika siku za leo kama waumini wa Kanisa la Yesu Kristo. Yeye anataka aweze kutusaidia tuendelee kusonga mbele kwenye njia ya kurudi Kwake. Kuona vipengele vingi vizuri vya kozi hii kulinisaidia kutambua jinsi kwa kina Baba wa Mbinguni anavyomfahamu kila mmoja wetu na mahitaji yetu binafsi na mara moja nilihisi amani pale nilipoanza kujifunza. Kozi inafundisha kweli za wazi na zenye nguvu za milele ambazo zinaweza kutumika kwenye maisha yetu wakati tunapokabiliwa na maswala ya afya ya akili, iwe ni sisi wenyewe au mtu fulani tunayempenda.

Moja ya mafundisho yaliyoniingia sana yanapatikana katika sura ya tisa, “Kuwapa Nguvu Wengine.” Sura hii ndiyo iliyonisaidia mimi hatimaye kutoka kuomba usaidizi. Inafundisha kanuni ya kuhudumiana. Nilijifunza jinsi ilivyo muhimu kuwahudumia wengine kwa kuhalalisha hisia zao na mihemko na maoni na kuwafikia kwa huruma na uelewa. Nilitambua pia kwamba nilihitajika kuwaamini watu wengine kunisaidia katika mapambano yangu.

Nilipoweza kuweka mawazo haya katika vitendo na kuwa muwazi kwa familia na rafiki zangu kuhusu mapambano yangu ya afya ya akili, nilishangazwa kwamba walikuwa na huruma sana na hawakunihukumu. Nilipokea usaidizi mwingi kutoka kwao.

Ninahisi kama wasiwasi wangu ungeongezeka na ungeongoza kwenye giza kama nisingeshiriki changamoto zangu kwa wapendwa wangu. Na uzoefu huu ulinisaidia kufikia na kuonesha huruma kwa wengine kuhusu hofu zao na matatizo pia.

Tunaweza Kukabiliana na Siku za Baadaye kwa Tumaini

Naona ni ya kuchekesha jinsi wakati niliporejea kutoka kwenye misheni yangu, nilikuwa na hofu nyingi kuhusu kupoteza “msimamo wa kiroho” ambao nilikuwa nimeupata kipindi cha misheni yangu, kwa sababu sasa ninatambua kwamba kurejea nyumbani ilikuwa mwanzo tu wa ukurasa mpya ambapo ningeweza kupata njia za kukuza imani yangu.

Mahusiano yangu binafsi na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo yamekua na kuongezeka kwa kina tangu nirejee nyumbani hususani kwa sababu ya kanuni nilizojifunza katika kozi ya ushujaa kihisia na kupitia kumtegemea Baba wa Mbinguni na Mwokozi kwa ajili ya usaidizi. Yanaonekana halisi zaidi na kuwepo katika maisha yangu ya kila siku.

Nimejifunza na kukubali kwamba kama watoto wa Mungu, daima tunabadilika, tunajifunza na tunakua. Na bado kupitia mabadiliko yetu ya maisha, Baba wa Mbunguni habadiliki. Yeye hakunitarajia mimi niwe mkamilifu kwenye misheni yangu na hatarajii hilo sasa. Yeye ananipenda tu na ananitaka niendelee kujitahidi kuelekea Kwake na kufanya vizuri kadiri niwezavyo katika safari yangu ya kurudi Kwake.

Sasa, kwa sababu tu nilisoma kozi hii ya ushujaa kihisia, hiyo haina maana kwamba sina tena wasiwasi au mashambulizi ya kushindwa kufikiri au nyakati ambapo nahisi kuzidiwa na hofu ya wakati ujao. Bado wakati mwingine napitia hayo. lakini sasa natambua mipangilio hii na nimejifunza nyenzo za kusaidia kuikabili katika njia nzuri, nikiboresha kiwango cha maisha yangu ya kila siku.

Mwishoni, kozi hii imenifunza mbinu za kuendana na mazingira kwa nyakati ambapo napitia wasiwasi na changamoto. Ilinifundisha kuwa na uvumilivu na huruma kwangu mwenyewe na kwa mapungufu yangu. Na nilijifunza kuelewa jinsi Mungu anavyoniona na kutoshambuliwa kwa yasiyojulikana ya siku zijazo.

Kupitia vyote, weledi na usaidizi wa kimbingu, nimetambua kwamba tunazo nyenzo muhimu za kujua jinsi gani ya “kujitendea wenyewe … na sio kutendewa” (2 Nefi 2:26) na hisia na mihemko yetu pale tunapoendelea kutembea kuelekea kwa Kristo.

Muhtasari

  1. Reyna I. Aburto, “Katika Mawingu na Jua, Bwana, Kaa Nami!,” Liahona, Nov. 2019, 58.

  2. Kupata Nguvu katika Bwana: Ushujaa Kihisia (2021), 8, ChurchofJesusChrist.org.