2022
Baraka za kujifunza Agano la Kale
Januari/Februari 2022


Njoo, Unifuate

Baraka za Kujifunza Agano la Kale

Tunaposoma sura na mistari ya kitabu hiki cha kale cha maandiko, tutaimarika kiroho.

Jesus Christ with stars in background

Ahadi za Rais Nelson ni kubwa na ni za kweli.

Kristo na Uumbaji, na Robert T. Barrett

Karibu kwenye ujifunzaji wa Agano la Kale kwa mwaka 2022, pamoja na nyenzo ya Njoo,Unifuate kama mwongozo! Agano la Kale ni mpangilio mtakatifu wa maandiko ambayo yamehifadhiwa kwa mkono wa Mungu kwa ajili yetu kusoma na kutafakari. Linaweza kuwa baraka na mwongozo kwetu sisi katika siku hizi za mwisho.

Agano la Kale hutupatia mtazamo wa miaka 3,500 ya imani na kujitolea kuanzia takriban miaka 4,000 KK hadi 500 KK. Kuna vitabu 39 katika Agano la Kale. Mwanzo inahusisha vipindi vinne vya maongozi ya Mungu vya Adamu, Henoko, Nuhu na Ibrahimu. Vitabu 38 vilivyosalia, Kutoka mpaka Malaki, vimejikita kwenye kipindi cha Musa.

Tunaposoma Agano la Kale, tutaweza kuwa na ufahamu mzuri wa manabii na mafundisho yao. Walifundisha injili ya Yesu Kristo. Walitoa unabii na kutazamia kuja kwa Masiya. Mafundisho yao yenye mwongozo wa kiungu yamehifadhiwa kwa ajili ya siku yetu.

Tunaposoma sura na mistari ya Agano la Kale, tutaimarika kiroho. Roho Mtakatifu ataleta kwenye umakini wetu mistari maalum ya kiroho ambayo itakuwa nguvu kwetu wakati tunapotazamia Ujio wa Pili wa Mwokozi.

Swali Lenye Mwongozo wa kiungu

Ningependa kushiriki hadithi kuhusu jinsi ambavyo mstari mmoja kutoka Agano la Kale umenishawishi katika maisha yangu yote.

Mnamo 1974, nilikuwa na miaka 17. Nilikuwa nikifurahia maisha kama kijana mdogo katika shule ya upili. Nilikuwa nikitazamia misheni yangu. Kwenye gazeti la Oktoba 1974 la Ensign , nilisoma ujumbe wenye nguvu kutoka kwa Rais Spencer W. Kimball (1895–1985) wenye kichwa cha habari “Wakati Ulimwengu Utakapoongoka.”1 Nimeusoma mara nyingi tangu hapo. Mpaka leo hii unanipa uvuvio.

Rais Kimball aliwasilisha mtazamo mpana wa ulimwengu wa ukuaji wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu. Alifundisha juu ya fursa na wajibu wetu wa kuipeleka injili ulimwenguni kote. Rais Kimball alinukuu mstari kutoka katika kitabu cha Mwanzo. Ulinipa uvuvio wakati huo na umeendelea kunipa uvuvio katika maisha yangu yote: “Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana?” (Mwanzo 18:14, ambayo ipo kwenye ratiba ya kujifunza ya Februari).

Abraham praying

Ibrahimu kwenye Nyanda za Mamre, na Grant Romney Clawson; picha ya wamisionari na Alicia Cerva; picha ya dunia kutoka Getty Images

Rais Kimball alirejea hadithi ya Ibrahimu na Sara. Sara alicheka ahadi ya Bwana kwamba yeye na Ibrahimu wangepata mtoto wa kiume. Walikuwa bado hawajabarikiwa kupata watoto. Walikuwa sasa na miaka, Sara 90 na Ibrahimu 100. Walikuwa wamepita umri wa miaka ya kupata watoto.

“Bwana akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka … ?”

“Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume” (Mwanzo 18:13–14).

Ibrahimu na Sara walionesha imani. Bwana alitunza ahadi Yake. Isaka alizaliwa. Ibrahimu akawa baba wa mataifa.

Nguvu ya Kukabiliana na Changamoto

“Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana?” Andiko hili la Agano la Kale limeniimarisha wakati nilipokabiliana na changamoto au hofu za maisha:

  • Kama mmisionari wakati nilipohisi kuzidiwa. “Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana?”

  • Baada ya misheni yangu, wakati mimi na Anne Marie tulipokuwa tunafikiria ndoa na tulikuwa na woga kuhusu jinsi ya kulipia chakula, kodi na ada ya chuo. “Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana?”

  • Kama wana ndoa wapya, tukiwakaribisha watoto na kutambua msukumo wa kifedha wa maisha. “Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana?”

  • Kukabiliana na changamoto za kuhitimu shule, familia inayoongezeka na kuanza kazi. “Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana?”

  • Wakati nilipokuwa rais wa Misheni ya Hispania Barcelona, mimi na Anne Marie mara kwa mara tulirejelea andiko hili wakati tukiwafundisha wamisionari. “Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana?” Barua kwa wamisionari wetu mara nyingi zilijumuisha rejeleo kwenye “Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda Bwana?”

Msingi wa Maandiko

reproduction of stone tablets with Ten Commandments

Musa Akigawanya Bahari ya Shamu, na Robert T. Barrett; Adamu na Hawa katika Bustani, na Lowell Bruce Bennett; uzalishaji wa bamba ya mawe kutoka Getty Images; picha ya Hekalu la San Diego California na Monica Georgina Alvarado Zarate

Mstari huu wa maandiko ni mmoja kati ya mifano mingi ya mistari yenye uvuvio inayopatikana katika Agano la Kale. Nina hakika ipo mingi ambayo tayari inakupa uvuvio. Wakati sisi kwa uangalifu na kwa sala tunasoma Agano la Kale mwaka huu, Roho Mtakatifu ataleta kwenye umakini wetu mistari maalum ya ziada ambayo itaimarisha uongofu wetu kwa Yesu Kristo na injili Yake.

Agano la Kale lina mafundisho na kanuni zenye umuhimu usiopitwa na wakati. Lina unabii ambao bado haujatimizwa. Linafundisha kuhusu ni wapi tulitoka. Na linatufundisha kuhusu agano la Ibrahimu, ambalo bado lipo kwenye matumizi leo.

Agano la Kale hutoa msingi kwa ajili ya maandiko mengine. Tunapozidi kuelewa Agano la Kale, ndivyo zaidi utakavyokua uelewa wetu wa juzuu zingine za maandiko, kwa sababu mafundisho yake yanaonekana katika vitabu hivyo vingine vya maandiko:

  • Wakati wa huduma Yake, Mwokozi alifundisha kwa kutumia maandiko kutoka Agano la Kale.

  • Lehi na familia yake walichukua bamba za shaba, ambazo zilikuwa na maandiko kutoka Agano la Kale.

  • Nefi alimfundisha Yakobo kwa kunukuu kutoka kwa Isaya katika Agano la Kale.

  • Wakati wa matembezi yake kwa Wanefi baada ya Ufufuko Wake, Yesu Kristo alinukuu kutoka kwa Isaya na Malaki katika Agano la Kale.

beings appearing to Joseph Smith and Oliver Cowdery in Kirtland Temple

Ono katika Hekalu la Kirtland, na Gary Smith; Ujio wa Pili, na Harry Anderson

Manabii na mafundisho katika Agano la Kale pia ni kiini kwenye ujumbe wa Urejesho wa injili katika siku yetu:

  • Katika matembezi yake ya mwanzo kwa Nabii Joseph Smith, Moroni alinukuu kutoka kwa Malaki.

  • Lulu ya Thamani Kuu inajumuisha vitabu vya Ibrahimu na Musa.

  • Musa, Elia, na Eliya walitoa funguo zao za ukuhani kwa Nabii Joseph Smith katika Hekalu la Kirtland.

Lengo ni Nini?

Tunaposoma vitabu katika Agano la Kale, tunapaswa kuzingatia kuwa vitabu vilichaguliwa, kutiliwa mkazo na kupangiliwa katika njia fulani kwa sababu ya theolojia. Tunaweza kujiuliza sisi wenyewe, “Kwa nini taarifa hii ilijumuishwa na inatimiza lengo lipi?”

Wakati baadhi ya vipengele vya Agano la Kale ni vigumu kueleweka, tunapaswa kukumbuka kwamba lina utajiri ambao haupaswi kupuuzwa. Kama vile Joseph Smith alivyofundisha, “Tunaamini Biblia kuwa ni neno la Mungu alimradi imetafsiriwa kwa usahihi” (Makala ya Imani 1:8). Hakika tumebarikiwa kwa kujifunza neno la Mungu!

Inaweza kusaidia katika kujifunza kwetu Agano la Kale kutafuta dhima na umaizi. Tunapaswa kutafuta njia za kuelewa vyema kwamba Mungu wa Agano la Kale ni Mungu pia wa Agano Jipya. Yehova ni Yesu Kristo. Ni jinsi gani kujifunza Agano la Kale kunatusaidia kumjua Mwokozi wetu vyema zaidi?

Dhima zingine muhimu ambazo ninazipata katika Agano la Kale hujumuisha maagano, utakatifu, manabii walio hai, dhabihu na utiifu, imani na toba, kumsifu Bwana na enzi kuu ya Mungu.

Tunapojifunza, tunapaswa kukumbuka kwamba ufunuo wa siku za mwisho hutupatia ufahamu mkamilifu zaidi wa Agano la Kale. Kwa mfano, shukrani kwa ufunuo wa siku za leo, tunajua kwamba manabii wa Agano la Kale walikuwa na Ukuhani wa Melkizedeki na kwamba manabii katika kipindi cha awali cha maongozi ya Mungu walifahamu na kufundisha injili ya Yesu Kristo.

Ahadi za Nabii

Katika kipindi hiki cha maongozi ya Mungu, tumebarikiwa kwa mara nyingine kufahamu kwamba manabii na mitume hutoa mafundisho na ushauri wenye mwongozo wa kiungu.

Mzee Quentin L. Cook wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alitambulisha kwa mara ya kwanza Njoo, Unifuate—Kwa ajili ya Watu Binafsi na Familia katika mkutano mkuu wa Oktoba 2018.2 Nyenzo hii imekuwa baraka kubwa kwetu sote. Miaka mitatu iliyopita imenipa uzoefu mkubwa na wenye maana wa kujifunza maandiko katika maisha yangu. Nina hakika baraka kama hizo zinamngoja kila mmoja wetu katika mwaka 2022.

Rais Russell M. Nelson alisema kwamba tunapopanga upya nyumba zetu kuwa mahali patakatifu pa imani na vituo vya kujifunza injili, tutapokea baraka maalum nne:

  1. “Baada ya muda siku zako za Sabato hakika zitakuwa za furaha.”

  2. “Watoto wako watafurahia kujifunza na kuishi mafundisho ya Mwokozi.”

  3. Ushawishi wa adui katika maisha yako na katika nyumba yako utapungua.”

  4. “Mabadiliko katika familia yako yatakuwa makubwa na ya kudumu.”3

Ahadi za Rais Nelson ni kubwa na ni za kweli. Baraka hizi zimekuwa za uhalisia na zitaendelea mwaka 2022 tunapojifunza na kusoma kutoka Agano la Kale

Muhtasari

  1. Ona Spencer W. Kimball, ”Wakati Ulimwengu Utapokuwa Umeongoka,” Ensign,, Oktoba 1974, 2–14.

  2. Ona Quentin L. Cook, “Uongofu wa Kina na wa Kudumu kwa Baba wa Mbinguni na Bwana Yesu Kristo,” Liahona, Nov. 2018, 8–12.

  3. Russell M. Nelson, “Kuwa Watakatifu wa Siku za Mwisho wa Mfano,” Liahona, Nov. 2018, 113.