Kumtafuta Yesu Kristo katika Agano la Kale
Kweli hizi tano zinaweza kutusaidia kuja kumjua Mwokozi wetu katika kujifunza kwetu maandiko mwaka huu.
Siku moja, Yesu Kristo alikutana na wawili kati ya wafuasi Wake kwenye njia kati ya Yerusalemu na Emau. Walipokuwa wakitembea aliwafundisha kuhusu jukumu Lake kama lilivyoelezwa katika maandiko ambayo sasa tunayarejelea kama Agano la Kale.
“Akaanza kutoka Musa na manabii wote, akawaeleza katika maandiko yote mambo yaliyomuhusu yeye mwenyewe” (Luka 24:27). Kujifunza kuhusu Mwokozi na kazi Yake ulikuwa uzoefu wa kina wa kiroho kwa wafuasi na walimsihi aendelee kukaa pamoja nao (ona Luka 24:28–32).
Kama vile wale wafuasi wa mwanzo wa Kristo, tunayo fursa ya kuja kumjua Mwokozi wetu katika njia yenye maana zaidi pale tunapotafiti Agano la Kale mwaka huu. Kumbukumbu hii, ikiambatana na vitabu vya Musa na Ibrahimu katika Lulu ya Thamani Kuu, inatupatia ufahamu kamili zaidi wa Yeye ni nani—asili Yake, kazi Yake na uhusiano Wake na Baba Yake na kila mmoja wetu. Tunahitaji ufahamu huu ili tupokee zawadi ya uzima wa milele (ona Yohana 17:3).
Hapa chini ni kweli tano zinazoweza kutusaidia kutambua na kumwelewa vyema Yesu Kristo kote katika kitabu hiki kitakatifu cha kale.
Ukweli wa 1: Yesu Kristo ni Yehova
Katika Agano Jipya, tunasoma kuhusu wakati ambapo Yesu Kristo alijitambulisha kuwa Yehova (ona Yohana 8:58, tanbihi b). Watu walikuwa na hasira na walijaribu kumpiga mawe kwa kukufuru (ona Yohana 8:59). Hawakutambua ukweli wenye thamani ambao bado unaendelea kutoeleweka kwa wengi leo: kwamba Yesu Kristo ni Yehova, Mungu wa Agano la Kale.1
Pengine sehemu ya sababu ya utambulisho wa Mwokozi katika Agano la Kale mara nyingi kutoeleweka ni kwa sababu jina “Yesu Kristo” halijatumika kwenye kitabu. Badala yake waandishi wametumia majina kadhaa kumtambulisha, kama vile “Mungu,” “Mimi Ndimi,” au “Bwana.”2 Pale tunapofahamu hili, tunaanza kumwona Yesu Kristo kwa uwazi zaidi kote katika maandiko yote. Kwa mfano:
-
Wakati Musa alipozungumza na “Mungu” katika kichaka kinachowaka moto, alikuwa akizungumza na Yesu Kristo (ona Kutoka 3:6)3
-
Hali kadhalika, Yesu Kristo alijitambulisha kama “Mimi Ndimi Mkuu” kwa Joseph Smith (Mafundisho na Maagano 29:1).
-
Yohana Mbatizaji aliitwa kutayarisha njia ya “Bwana” (Mathayo 3:3). Huu ni utimizwaji wa Isaya 40:3, ambaye alikuwa akitoa unabii wa Yesu Kristo.
-
Ona chati kwenye ukurasa wa 17 kwa ajili ya mifano mingine ya Yehova kote katika maandiko.
Ukweli wa 2: Vitu na Matukio Vinaweza Kutufunza kuhusu Mwokozi Wetu
Agano la Kale limejaa ishara na hadithi ambazo zinaweza kutukumbusha juu ya usaidizi ambao Mwokozi hutoa. Kwa mfano:
-
Maandiko mengi yanaelezea nyakati ambapo watu waaminifu waliamriwa kutoa dhabihu ya wanyama kama sehemu ya kuabudu kwao. Kwa mfano, wana wa Israeli waliambiwa kutoa dhabihu ya kondoo na kuwekea alama miimo ya milango yao kwa damu ya kondoo. Wale waliofanya hili walilindwa dhidi ya janga la kufisha la Misri. Dhabihu kama hizo hutukumbusha kwamba Yesu Kristo, Mwanakondoo wa Mungu, aliruhusu Yeye mwenyewe auwawe kama sehemu ya Upatanisho Wake. Dhabihu Yake hutuokoa kutoka kwenye kifo cha kimwili na kiroho. (Ona Kutoka 12:13.)
-
Wakati nabii Eliya alipopaswa kukimbia kuokoa maisha yake na kujificha jangwani, alihisi huzuni na kusema kwamba alitamani angekuwa amekufa. Wakati akiwa amelala, mkate na maji vilitokea kimiujiza ili kumpa virutubisho na kumfanya upya, kumuimarisha aweze kusonga mbele. Hii inaweza kutukumbusha kwamba Yesu Kristo ni Maji yaliyo Hai na Mkate wa Uzima. Yeye ni chanzo chetu kikuu cha tumaini. (Ona 1Wafalme 19:1–8.)4
-
“Neno lako ni taa ya miguu yangu,” mtunga zaburi mmoja aliandika (Zaburi 119:105; msisitizo umeongezwa). Mika alishuhudia, “nikaapo gizani, Bwana atakuwa nuru kwangu” (Mika 7:8; msisitizo umeongezwa). Maneno yao yanatukumbusha kwamba Yesu Kristo ni Nuru ya Ulimwengu, ikituongoza kurudi nyumbani kwetu mbinguni.
Unaposoma, unaweza kugundua mambo mengine ambayo yanakukumbusha juu ya Yesu Kristo na uwezo Wake wa kutuokoa—kama vile familia ya Nuhu ilivyookolewa kutokana na gharika katika safina, au wakati Yona alipopewa muda wa kutubu akiwa ndani ya nyangumi. Matukio haya yanaweza kutukumbusha kwamba Mwokozi anaweza kutubeba kupita dhoruba za maisha na kwamba Yeye daima hutupatia fursa za kurudi kwenye njia sahihi. (Ona Mwanzo 7:1; Yona 1:17.)
Ukweli wa 3: Yehova ni Mungu Binafsi
Nyakati zingine inaweza kuonekana kama vile Mungu wa Agano la Kale ana hasira na kisasi. Tunapaswa kuweka akilini kwamba waandishi wa mwanzo wa kitabu walitoka kwenye tamaduni za kale zenye mila na maelezo ambayo yanaweza kuwa magumu kwetu kuyaelewa kikamilifu leo hii. Mwongozo wa Njoo,Unifuate, mijadala ya vikundi na mwangaza kutoka kwa Roho Mtakatifu vinaweza kutusaidia kuunganisha kile tunachosoma katika Agano la Kale na kile tunachofahamu kuhusu Yesu Kristo kutoka kwenye vitabu vingine vya maandiko.
Na hapa ni moja ya sifa inayoonekana ya Yehova ambayo itakuwa yenye kufahamika kwa wanafunzi wa Mwokozi: Yeye ni Mungu binafsi . Kuingilia Kwake, kote katika njia kubwa na ndogo, ni kielelezo kwamba Yeye daima yu tayari kuwakomboa wote wale wanaomtumaini Yeye. Hapa ni baadhi ya mifano ya huduma yake ya Agano la Kale:
-
Baada ya Adamu na Hawa kufanya Kosa, Bwana aliwavisha au kuwafunika kwa mavazi ya ngozi (ona Mwanzo 3:21). Neno la Kiebrania la Upatanisho humaanisha “kufunika” au “kusamehe.”
-
Yeye alimwalika Henoko kutembea pamoja naye (ona Musa 6:34) na aliwainua watu wa Sayuni (ona Musa 7:69).
-
Yeye alimwandaa Joseph kuikomboa familia yake na wengine wengi kutokana na ukame (ona Mwanzo 37–46).
-
Yeye aliwaongoza wana wa Israeli kupitia jangwani (ona Kutoka 13:21–22).
-
Yeye aliwatembelea Haruni na Miriamu ili kuimarisha imani yao kwa nabii aliye hai (ona Hesabu 12:5).
-
Yeye alimwongoza Ruthu na kuhifadhi uzao wake kupitia familia yake (ona Ruthu 3:10–11; 4:14–17).
-
Yeye alimwita mvulana Samweli kwa jina lake (ona 1 Samweli 3:3–10).
-
Yeye alimwezesha Esta kwa ujasiri kuwaokoa watu wake (ona Esta 2:17; 8:4–11).
Ukweli wa 4: Yesu Kristo Hutusaidia Kupigana Vita Vyetu
Wakati mwingine maisha ya kila siku ni kama vita. Hakika tuko katikati ya vita vya kiroho kati ya mema na mabaya, tofauti na vita vilivyoelezewa katika Agano la Kale. Pamoja na askari wa zamani, tunapaza sauti, “Tuongoze Ee Yehova mkuu.”5 Katika maandiko haya, tunasikia jibu lake lenye hakikisho:
-
“Sitakupungukia Wala Sitakuacha”.(Yoshua 1:5).
-
“Msiogope, wala msifadhaike kwa ajili ya jeshi kubwa hili; kwani vita si yenu bali ni ya Mungu” (2 Mambo ya Nyakati 20:15).
-
“Nitakutia nguvu; … naam, nitakusaidia” (Isaya 41:10).
-
“Mimi nipo pamoja nawe nikuokoe” (Yeremia 1:8).
Ukweli wa 5: Ahadi za Bwana Zinaendelea
Tumeunganishwa zaidi na watu waaminifu wa Agano la Kale kuliko tunavyoweza kutambua. Waonaji wa kale walitazamia na kuandika kuhusu maisha ya duniani ya Yesu Kristo. Isaya, kwa mfano, alimwelezea Bwana kwa maneno yenye nguvu ambayo yalikuja kuwa sehemu ya muziki ambao mara zote tunaushiriki kwenye Pasaka na Krismasi (ona Isaya 7; 9; 40; na 53).6
Kama vile manabii hao, sisi pia tunatazamia ujio wa Kristo—wakati huu tukitazamia ujio wake wa kutawala yeye mwenyewe duniani.7 Na tunapouandaa ulimwengu kwa Ujio Wake wa Pili, tunapata nguvu kutoka kwenye kweli na ahadi zilizoandikwa mwanzo katika Agano la Kale, kama vile:
-
Baraka za patriaki, ambazo hujumuisha tamko la nyumba ya Israeli ambayo kwayo sisi ni sehemu yake. Agano Bwana alilofanya na Ibrahimu maelfu ya miaka iliyopita linahusika kwetu kama waumini wa Kanisa la agano leo, bila kujali sisi ni sehemu ya kabila gani. (Ona Mwanzo 13:14–17; Musa 2:9–11.
-
Amri ya kuitakasa siku ya Sabato, ambayo Bwana alisema ingekuwa “ishara kati ya mimi na ninyi katika vizazi vyenu vyote; ili mpate kujua ya kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi” (Kutoka 31:13).
-
Miosho mitakatifu, mipako ya mafuta, na mavazi ambavyo ni sehemu ya ibada ya hekaluni leo vilitolewa mwanzo kwa Haruni na uzao wake (ona Mambo ya Walawi 8).
Fikiria kuhusu ni wanaume na wanawake wangapi waadilifu walitoa dhabihu ili kutufikisha hapa katika historia ya mwanadamu. Tunajenga juu ya juhudi zao takatifu na kushiriki ono lao la ulimwengu linaloongozwa na Mwokozi. Kama Rais Russell M. Nelson alivyofundisha: “Baada ya miaka 4,000 ya matarajio na matayarisho, hii ndiyo siku iliyoteuliwa wakati injili itapelekwa kwa jamii za ulimwengu. Huu ndio wakati wa kusanyiko lililoahidiwa la Israeli. Na tunapata Kushiriki!”8
Mwaka wa Kipekee wa Kujifunza
Tunayo katika mikono yetu hadithi ya mwanzo wa mwanadamu—hadithi yetu kama Wakristo wa agano. Kwa sababu ya Upatanisho wa Yesu Kristo, tunafahamu jinsi safari hii ya kipekee itakavyofikia tamati. Shetani ataharibiwa, na wenye haki watakuwa washindi. Lakini ni jinsi gani hadithi yetu binafsi itajifunua?
Je tutachagua kutembea pamoja na Yesu Kristo mwaka huu? Je tutamsihi aendelee kubakia nasi, kwa umakini tukisikiliza kile anachofundisha?
Yeye ni Mwokozi mwenye upendo, mwokozi binafsi ambaye sauti yake tunaisikia katika Mafundisho na Maagano, ambaye maisha yake yameandikwa katika Agano Jipya na ambaye mafundisho yake yamefundishwa kwa uwazi ndani ya Kitabu cha Mormoni. Kwa mazoezi kidogo, tutaweza kupata huduma yake ikiwa imeenea kote katika kurasa za Agano la Kale vilevile. Yeye ni kiini cha yaliyopita, ya sasa, na ya siku za usoni za mwanadamu. Yeye amekuwa—na daima atakuwa—kando yetu katika kila hatua njiani.