Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho
Mto Sakafuni
Sikuona vibaya kumsaidia mama yangu kazi zake za nyumbani, lakini kwa nini mara zote nilikuta mto sakafuni?
Kwa miaka mingi, nimetembelea nyumbani kwa mama yangu kumsaidia kazi za nyumbani. Ana miaka 80 na ni muumini mwaminifu wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.
Mama yangu ameishi peke yake tangu baba yangu alipofariki. Furaha yake kubwa ni kutembelea nyumba za kila mmoja wa watoto wake watatu, kukaa nao pamoja na wajukuu zake na kupika chakula kinachofurahisha nafsi.
Kila mara nilipotembelea nyumba ya mama yangu ili kuisafisha na kuhakikisha kila kitu kilikuwa katika mpangilio, nilikuta mto uliochakaa sakafuni. Tena na tena ningeuokota na kuuweka kwenye kiti, nikijilalamikia kuhusu kutojali kwa mama yangu.
Wakati ujao ningerudi kumtembelea na kumsaidia mama yangu, ningekuta tena mto sakafuni. Sikuwahi kusema chochote kwa mama yangu kuhusu mto, lakini asubuhi moja hatimaye niligundua kwa nini mara zote ulikuwa sakafuni.
Mama yangu alihitaji sehemu laini ambapo juu yake angepiga magoti kuomba. Alikuwa mwanamke mzee, lakini imani yake isiyotingishika ilimwongoza kwenye magoti yake katika maombi kila siku. Angeomba kwa ajili ya watoto na wajukuu zake. Angeomba kwa ajili ya rafiki zake. Angeomba kwa ajili ya wale waliokuwa kwenye uhitaji zaidi. Na angeomba kwa ajili ya wale wote ambao daima aliwapenda na hata katika umri wake wa uzee bado kwa ukarimu aliwajali.
Leo, sijilalamikii tena pale ninapoona mto sakafuni. Nyakati zingine, hata mimi hupiga magoti juu ya sehemu yake laini ili kuomba kwa Baba wa Mbinguni nikitoa shukrani kwa imani na mfano wa mama yangu.