UJUMBE WA ENEO HUSIKA
Kitabu cha Mormoni, GPS ya Kuongoza Safari zetu za Kiroho
Kama GPS inatuongoza mahali tunapotaka kufika, Kitabu cha Mormoni hutuongoza kila siku kwenye njia iletayo uhusiano wa pamoja na Baba yetu wa Mbinguni na wenza wa Roho Wake Mtakatifu.
Wakati wa kipindi changu cha hivi karibuni cha miaka miwili na miezi michache ya kukaa Afrika Kusini, nilijifunza umuhimu wa kuwa na mbinu ya kunisaidia kila nilikotaka kwenda. Ilikuwa GPS, ramani ya kielektroniki iliyoniruhusu mimi kwenda huku na kule ili kutekeleza majukumu yangu, yawe yahusianayo na familia, majukumu ya kiuweledi au majukumu yangu ya kiwito.
Kila nilipokuwa nikiweka umakini kwenye ramani hii ya kielektroniki, ningefika nilipotaka kwa muda muafaka na kwa haraka kurejea nyumbani kwa familia yangu. Lakini nilipokosea mzunguko wa barabara au kona za barabara, GPS itanipeleka kwenye barabara ndefu na wakati mwingine nitacheleweshwa kufika ninakoelekea—au kupotea kabisa barabarani na kwenda kwingineko kusikojulikana.
Kama wasafiri kwenye hii dunia—ili kutusaidia kusafiri kapita changamoto za maisha haya na kurejea katika makazi yetu ya Mbinguni—Mungu ameleta Kitabu cha Mormoni, Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo.Kinatusaidia kufikia lengo letu la kuwa na Roho Mtakatifu na hutuandaa kwa ajili ya urithi wetu wa mbinguni.
Kama GPS hutuongoza kufika mahali tunapotaka kufika, Kitabu cha Mormoni hutuongoza kila siku kwenye njia iletayo uhusiano wa pamoja na Baba yetu wa Mbinguni na wenza wa Roho Wake Mtakatifu. Ni jukumu letu kukirejelea kwa kuwa huongoza maisha yetu kila siku.
Kwa kuzingatia thamani yake na jukumu muhimu la kila nyanja za maisha ya watoto wa Mungu, Rais Russell M. Nelson aliuliza maswali kadhaa ambayo yalihitaji tafakari ya kina kutoka kwa kila mmoja wetu. Alisema, “Kaka na dada zangu, je, Kitabu cha Mormoni kina thamani kwako kiasi gani? Kama ungepewa dhahabu au rubi au Kitabu cha Mormoni, ni kipi ungechagua? Kwa dhati, ni kipi kina manufaa makubwa kwako?” 1
Maswali yake yaliniruhusu kutafakari ni jinsi gani maisha yangu yangekuwa kama nisingekuwa namjua Yesu Kristo kama Mwokozi na Mkombozi wa ulimwengu, na ningekuwaje bila ibada na maagano kama yalivyofundishwa na manabii kwenye Kitabu cha Mormoni na kama yalivyorejeshwa kupitia Nabii Joseph Smith katika kipindi chetu.
Rais Nelson aliendelea: “Kitu fulani cha dhati hutokea wakati mwana wa Mungu hutafuta kujua zaidi kumhusu Yeye na Mwanawe mpendwa. Hakuna sehemu nyingine ambapo kweli hizo hufundishwa kwa uwazi zaidi kuliko kwenye Kitabu cha Mormoni.” 2
Ningependa ufikirie kuhusu maswali matatu yafuatayo ambayo Rais Nelson aliwashauri viongozi huko Chile wayazingatie.
“Mosi, je, maisha yako yangekuwaje bila Kitabu cha Mormoni? Pili, je, usingekuwa unajua kitu gani? Na tatu, je, usingekuwa na kitu gani?”
Rais Ezra Taft Benson (1899–1994) alisema: “Kitabu cha Mormoni ni chombo ambacho Mungu amekibuni ili ‘kuifagia dunia kama vile kwa mafuriko, ili kukusanya wateule [Wake].’ Juzuu hii tukufu ya maandiko huhitaji kuwa ya muhimu zaidi katika mahubiri yetu, mafundisho yetu na katika kazi yetu ya umisionari.
“Kwa sasa, Kitabu cha Mormoni kinasomwa katika Shule yetu ya Jumapili na madarasa ya seminari kila mwaka wa nne. Mpango huu wa miaka minne, hata hivyo, haupaswi kufuatwa na waumini wa Kanisa katika masomo yao binafsi na ya familia. Tunahitaji kusoma kila siku kutoka kwenye kurasa za kitabu hicho ambacho kinamfanya mwanadamu ‘kumkaribia Mungu zaidi kwa kufuata mafundisho yake, zaidi ya kitabu kingine’.” 3
Kaka na dada zangu, Kitabu cha Mormoni kina nguvu na ushawishi halisi katika maisha ya wote wakisomao kwa nia ya dhati. Huleta amani kwa nafsi inayotafuta amani, huunganisha nyumba na familia zilizoparanganyika na hurejesha uhusiano kati ya watu wakati kinapowekwa kama kitovu cha kila uhusiano kwa sababu humleta Kristo katikati ya watu wake.
Katika Nefi wa Nne, mlango wa 1, mistari ya 15 hadi 18 tunasoma:
“Na ikawa kwamba hakukuwa na ubishi katika nchi, kwa sababu ya mapenzi ya Mungu ambayo yaliishi katika mioyo ya watu.
Na hakukuwa na wivu, wala ubishi, wala misukosuko, wala ukahaba, wala uwongo, wala mauaji, wala uzinifu wa aina yoyote; na kwa kweli hakujakuwa na watu ambao wangekuwa na furaha zaidi miongoni mwa watu wote ambao waliumbwa na mkono wa Mungu.
Hakukuwa na wanyangʼanyi, wala wauaji, wala hakukuwa na Walamani, wala aina yoyote ya vikundi; lakini walikuwa kitu kimoja, watoto wa Kristo, na warithi wa ufalme wa Mungu.
Na jinsi gani walibarikiwa! Kwani Bwana aliwabariki kwa matendo yao yote; ndiyo, hata walibarikiwa na kufanikiwa mpaka miaka mia moja na kumi ikapita; na kizazi cha kwanza kutoka Kristo kilikuwa kimepita, na hakukuwa na ubishi katika nchi yote.”
Tangu mara ya kwanza nilipokijua Kitabu cha Mormoni zaidi ya miaka 35 iliyopita nimeendelea kukisoma kila siku na maisha yangu yamekuwa na maana zaidi kama mfuasi wa Kristo. Nina uelewa dhahiri wa uhusiano wangu na Baba yangu wa Mbinguni na binadamu wenzangu.
Katika familia yangu tunao mpango wa kujifunza Kitabu cha Mormoni pamoja na watoto wetu. Ushawisi ambao kitabu hiki kinaendelea kuwa nao kwenye maisha yao ni wa thamani na tunayo furaha tuwaonapo wakitumia kanuni za Injili ambazo wanazielewa kwa uwazi sana.
Elie K. Monga aliitwa kama Sabini wa Eneo mnamo Aprili 2017. Anakaa Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Amemuoa Vianney Mwenze na ni wazazi wa watoto wanne.